Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, June 29, 2013

Maandalizi ya kukwea Mlima Kilimanjaro mwezi Septemba yameanza

Juzi nimeanza rasmi maandalizi (ya mazoezi) ya kukwea tena Mlima Kilimjaro mwezi Septemba mwaka huu, kuanzia tarehe 23 hadi 30 Septemba. Safari hii nitakuwa nachangisha pesa kuchangia ujenzi wa shule ya msingi iliyopo kijiji cha Kichalikani, mkoa wa Tanga. Yanahitajika mazoezi ya siyo chini ya miezi mitatu kujiandaa vyema kukabiliana na changamoto ya kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, mita 5,895 juu ya usawa wa bahari.

Hii ni safari ambayo awali nilipanga ifanyike mapema mwaka huu lakini nililazimika kuiahirisha kutokana na majukumu mengine yaliyonikabili.
Mandhari mwanana kwenye njia ya Marangu ya Mlima Kilimanjaro.
Moses Kusotera, raia wa Zimbabwe anayeishi na kufanya kazi nchini Uingereza, ataungana nami kukwea mlima huu maarufu pamoja na kuchagnisha pesa za shule ya Kichalikani.

Ukitaka kujiunga nami niandikie barua pepe kwa kubofya hapa.

Taarifa nyingine zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/01/kunguru-wa-mlima-kilimanjaro.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wagumu-wa-mlima-kilimanjaro.html

Ziara ya Rais Barack Obama Tanzania: yale yale!

Kama nilivyoandika kwenye blogu hii hivi karibuni, ziara ya rais wa marekani nchini Tanzania huwa inakuja na usumbufu wa kiwango cha juu kwa raia.

Kuna taarifa kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utafungwa kwa vipindi virefu tarehe 1 na 2 Julai 2013, siku ambazo Rais Barack Obama atakuwa ziarani Tanzania. Sehemu ya taarifa niliyoiona inasema:
Please be advised due to VVIP movement (US Presidential delegation) scheduled visit to DAR on 1st July, JNIA will be closed as per below:
 Monday 1st July from 02:20 to 03:25 pm
Tuesday 2nd July from 10:40 to 11:45 am
 Kindly ensure your travel arrangements are in order to avoid any disruption to your trip.
Taarifa inaeleza kuwa tarehe 1 Julai, uwanja utafungwa kati ya saa 8:20 usiku wa manane mpaka saa 9:25 alasiri na tarehe 2 Julai uwanja utafungwa saa 4:40 hadi saa 5:45 asubuhi.

Mimi nilipendekeza kupunguza usumbufu kwa raia huyu mgeni mashuhuri angefanyia mazungumzo yake na wenyeji wake Butiama. Ziara hii Dar es Salaam inasumbua watu zaidi ya milioni nne; Butiama itasumbua watu kama 20,000 tu. Lakini nani atanisikiliza?

Friday, June 7, 2013

Lugha yetu Kiswahili: Ulemavu wa ngozi?

Imezuka desturi ya miaka ya hivi karibuni ya kubadilisha baadhi ya matumizi ya lugha na kutunga matumizi ambayo yanakuwa mbadala ya mazoea yaliyopo. Mojawapo wa mabadiliko ya lugha ya aina hii ni kuacha kutumia neno "zeruzeru" na badala yake kutumia "mlemavu wa ngozi."

Mabadiliko haya yanaiga desturi iliyoanzia Marekani ya kuacha kutumia maneno, misemo, au majina ambayo matumizi yake yalionekana kudhalilisha au kuudhi makundi kadhaa ya jamii ambayo yalibaguliwa kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na jinsia, dini, rangi ya ngozi, na kadhalika.

Mathalani, kwa mantiki hiyo, baadhi ya Wamarekani hutumia physically challenged (mwenye changamoto za kimaumbile) badala ya maneno invalid (asiyejiweza), handicapped (kilema), au disabled (mlemavu).

Mimi naafiki ubunifu wa misemo mipya mbadala na kuacha matumizi ya misemo ambayo inadhalilisha. Lakini bado sijaona mantiki ya matumizi ya "mlemavu wa ngozi" badala ya "zeruzeru." Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford, toleo la pili 2004) inaeleza zeruzeru kuwa ni "...mtu ambaye nywele na ngozi yake imekosa rangi yake kamili na badala yake kuwa nyeupe sana na ambaye macho yake hayawezi kuvumilia mwangaza mwingi; albino."

Haya maelezo yanadhalilisha?