Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, May 20, 2010

Lugha yetu Kiswahili


Picha hii inaonyesha pikipiki ambayo haijapata namba ya usajili yenye maandishi ya lugha isiyokuwepo duniani. Neno "chassis" ni la asili ya lugha ya Kifaransa. Lakini mwenye pikipiki hii, au mwandika namba, ameandika "chasess" neno ambalo haliko kwenye Kiingereza, Kifaransa, wala Kiswahili.

Neno sahihi la Kiswahili lingekuwa "chesisi" kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza, toleo la pili la mwaka 2000, iliyochapishwa na Taasisi ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa vile msamiati wa Kiswahili unakuwa kila mara, inawezekana limejitokeza neno jingine mbadala linalofanana na lugha yetu. "Chesisi" bado ni neno linalofanana kimatamshi na asili ya lile la Kifaransa.

Ukweli unabaki kuwa katika maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, kuendeleza ushabiki wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye maandishi na mazungumzo ni jambo linalokuwa gumu kila siku zinavyozidi kupita.

Lakini pamoja na hayo bado ni muhimu kuunga mkono jitihada za Serikali kuamua kutumia lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zote rasmi za Serikali. Matumaini ni kuwa huu utaratibu utatumika pia bungeni ambapo tabia ya kuchanganya Kiingereza na Kiswahili imekuwa jambo la kawaida.

Sunday, May 16, 2010

Teknolojia ya ujenzi wa nyumba ya Hydraform

Kwa miaka kadhaa sasa nchini Tanzania, baadhi ya wajenzi wa nyumba wamekuwa wakitumia mashine za Hydraform kufyatulia matofali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.


Ujenzi kwa kutumia matofali ya Hydrafom unapunguza matumizi ya saruji inayotumika kwenye ujenzi wa kuta za nyumba kwa sababu matofali hayo yanashikana yenyewe na kuondoa haja ya kuwepo saruji kati ya tofali na tofali. Saruji inatumika kwenye kozi ya kwanza tu ya ujenzi wa ukuta, na kozi tatu za mwisho za ukuta. Kwa sababu hii, matumizi ya saruji ni madogo kuliko kwenye ujenzi wa kutumia matofali ya kawaida.

Aidha. baada ya kumaliza ujenzi wa ukuta, hakuna ulazima wa kupiga ripu kwenye ukuta wa nje. Ripu inapigwa ndani tu na hivyo kupunguza matumizi ya gharama ya saruji kwa ajili ya ripu.


Mashine ya Hydraform inafyatua kati ya matofali 1,300 - 1,500 kwa siku kutegemea na uzoefu wa wafyatuaji. Hata hivyo inawezekana kufyatua hadi matofali 2,ooo kwa siku kwa wafyatuaji wazoefu. Mfuko mmoja wa saruji wa kilo hamsini unatoa matofali kati ya 77 -90, na mchangayniko wa udongo na saruji unatumia maji kidogo sana.

Mchanganyiko hutumbukizwa ndani ya mashine na kushindiliwa kwa nguvu za haidroliki. Matofali yanapotoka kwenye mashine yanapangwa matano matano na kufunikwa kwa siku tatu yakimwagiliwa maji asubuhi na jioni kwa siku hizo tatu. Kuanzia siku ya nne matofali yanaweza kutumika kwa ujenzi.Kutokana na ujenzi wa Hydraform kutotumia saruji kati ya matofali, ujenzi wake ni wa haraka kuliko kawaida.

Tuesday, May 11, 2010

Barabara ya zamani ya Mwanza

Siku moja nikiwa ndani ya basi kutoka Arusha kuja Butiama ulizuka ubishi mkali wa kisiasa kati ya abiria na dereva wa basi kuhusu iwapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeleta maendeleo yoyote nchini tangu kuondoka wakoloni. Abiria wawili kina mama walisema hakuna maendeleo yoyote, wakati dereva wa basi alisema yapo maendeleo.

Siku hiyo basi liliwahi kufika Mugumu, kituo kimojawapo katika safari ya kuelekea Musoma, na wale abiria wakasema kuwa tulikuwa tumewahi sana kufika kwa kuwa barabara ilikuwa nzuri wakilinganisha na hali ya barabara ilivyokuwa vipindi vya nyuma. Niliwakumbusha kuwa usemi kuwa CCM haijaleta maendeleo itaonekana kutokuwa na nguvu kwa wao kusifia kuwa barabara ilikuwa nzuri kuliko zamani.

Labda ukweli ni kuwa serikali yoyote ambayo ingekuwa madarakani baada ya uhuru ingelazimika kujenga barabara sehemu mbalimbali za Tanzania.

Barabara mojawapo ambayo imebadilika sana kwa sasa ni ile ya Mwanza hadi Musoma. Nakumbuka kuwa barabara ya zamani ilipita Butiama, na likuwa ni barabara ya vumbi ambayo


hii leo (pichani, juu) bado inatumika kwa safari za gari kwenda Arusha kupitia mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Barabara hiyo ilikuwa ikichepukia Nyamuswa kuelekea Bunda na Mwanza.

Kati ya mwaka 1977 na 1983 Serikali ilijenga barabara mpya ya lami ambayo haukupita tena Butiama, lakini ikasogezwa kiasi cha kilomita 11 mashariki ya Butiama na sasa inapita karibu na mji wa Kiabakari.

Hata hivyo barabara hiyo ilikamilika na kasoro kidogo. Daraja mojawapo lililoopo karibu na kijiji cha Sabasaba halina upana ule ule wa barabara na gari zinapokutana hapo, hasa zikiwa gari
kubwa, haziwezi kupishana katikati ya daraja na inabidi dereva kutoa nafasi kwa dereva mwenzake apite.
Picha: Kasoro kwenye barabara ya Mwanza hadi Musoma, daraja jembamba.

Monday, May 10, 2010

Mada yangu ya leo: Kuchelewa kufika kwenye ahadi imekuwa desturi

Mada yangu ya leo siyo ndefu, lakini naamini ni ya muhimu sana.

Ni kwanini watu wengi huwa wagumu sana kutimiza ahadi za muda? Ni kwanini hawawahi kwenye ahadi wanazopanga na watu wengine? Nakiri kuwa tatizo hili hata mimi hunikuta mara moja moja, nikiwa mmojawapo wa watu wanaochelewa kwenye ahadi. Lakini nikijilinganisha na wengine, naona kuna tofauti mkubwa.

Mimi nimeishi kijijini Butiama kwa muda mrefu sasa, na nimeshuhudia kuwa suala la muda halipewi kipaumbele hata kidogo. Nimewahi kupanga mikutano na wanakijiji wenzangu mara kadhaa na pale tulipokubaliana kuwa mkutano utakuwa saa kumi jioni, watu wachache ambao unaweza kusema waliwahi kufika walianza kuingia kwenye ukumbi saa 10:45. Nilipolalamika kwanini wamechelewa kwenye kikao, waliniambia kuwa saa kumi ilimaanisha ni muda wote kati ya saa 10:01 had saa 10:59. Aidha, waliniambia kuwa ningetaka kikao kianze saa kumi basi ningewaarifu watu kuwa kikao ni saa 9:00.

Mimi sikubaliani na wanaosema kuwa hili ni tatizo la Waafrika. Ni Uafrika gani huo ambao hujitokeza siku moja na kujificha siku nyingine? Mwaafrika huyo huyo ukimwambia kuwa basi la kwenda Arusha litapita Butiama saa 11:30 alfajiri atawahi kituoni nusu saa kabla, lakini kwenye ahadi nyingine anachelewa.

Kuwahi katika vikao ni muhimu sana kwa sababu muda ule unaopotezwa kwa kusubiri wachelewaji ungeweza kutumika kufanya mambo kadhaa ya uzalishaji na maendeleo. Nina hakika kuwa hizo dakika ambazo tunazipoteza Tanzania katika mwaka mmoja zinaleta hasara kubwa sana kwenye uchumi.

Sunday, May 2, 2010

Watemi na nyoka


Umbali wa kilomita 20 toka Butiama kwenye barabara inayoelekea Fort Ikoma na kwenye mbuga za Serengeti kipo kijiji cha Nyamuswa, makazi ya aliyekuwa Mtemi wa Ikizu, Chifu Mohamed Makongoro Matutu aliyefariki mwana 1958.

Nimetembela makazi ya Mtemi Makongoro mara kadhaa na kufahamishwa kuwa kuna nyoka mkubwa katika eneo la mawe lililopo karibu na makazi yake. Mwanae mmoja ambaye alinizungusha kwenye eneo hilo kumsaka huyo nyoka anasema ni nyoka wa siku nyingi sana na yeye anakumbukua kuwepo huyo nyoka hapo nyumbani wakati wa utoto wake, yeye mwenyewe kwa sasa nikikadiria ana miaka karibu 60.

Ingawa hatukufanikiwa kumuona huyo nyoka mkubwa na mkongwe niliambiwa ni nyoka ambaye yuko eneo hilo la Mtemi Makongoro kwa ridhaa ya Mtemi mwenyewe na kwa sababu hiyo wanaoendelea kuishi pale hawamdhuru. Mara moja moja hujitokeza kutoka eneo la kilima na mawe na kuota jua nyakati za asubuhi, lakini wakati mwingine hutoka eneo hilo ambalo liko mwendo mfupi kutoka makazi ya watu na kupitapita wanakoishi watu. Inasemekana kuwa ni nyoka wa miaka mingi sana mpaka ameota majani sehemu ya juu ya kichwa chake.

Hapa Butiama, eneo ambalo aliishi Mtemi Nyerere Burito ni eneo lenye nyoka mkubwa ingawa hata huyo bado sijapata fursa ya kumuona. Huyo nyoka huishi ndani ya nyumba mojawapo ambayo alikuwa akiishi Mwalimu Nyerere, nyumba ambayo haitumiki kwa muda mrefu sasa. Nyoka huyo huhama kwenye nyumba hiyo watu wanapoitumia, lakini hurudi ndani wanapoondoka.

Imani za Wazanaki kuhusu wanyama na nyoka zinaweza kuwa zinafanana kidogo na zile za Waikizu wa Nyamuswa. Wazanaki hawadhuru wanyama, hasa wale wanaoishi katika maeneo alipoishi mtemi. Kuna imani wanyama hao wanaweza kuwa ni mizimu.

Katika chumba kimojawapo cha nyumba inayosemekana ina nyoka huyo mkubwa nimekumbana na nyoka wadogo mara kwa mara kwenye meza ninayotumia kufanya kazi zangu, pamoja na kuwashuhudia wakipita kwenye sakafu. Inaelekea ni nyoka ambao huzaliwa ndani ya nyumba lakini wakikua hutoka nje ya nyumba. Hivi karibuni nimewatoa nje nyoka wadogo watatu, na kwa kuwa muda kidogo umepita bila kuwaona nahisi uwepo wangu ndani ya nyumba ile unawafanya waanze kuihama.
Kwa muda mrefu nilikuwa nahisi kuwa aina ya nyoka ambao nimewona na kuwatoa nje ni wenye sumu kali, lakini sikuweza kuthibitisha mpaka hivi karibuni. Kitabu cha aina mbalimbali ya nyoka kinaainisha kuwa nyoka aliye kwenye picha (juu) ambaye nilimtoa nje anajulikana kama Mamba Mweusi (Black Mamba). Anaitwa Mamba Mweusi kwa sababu akifungua mdomo eneo lote la ndani ya mdomo pamoja na ulimi wake una rangi nyeusi. Anapokua anafikia urefu wa zaidi ya mita 2.