Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, November 18, 2017

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao ni adhabu ya sheria, na kukutana uso kwa uso na unayemtukana.

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ni sheria ambayo inaainisha matusi kama mojawapo ya makosa ambayo yanaweza kumtia mtu hatiani kwa yale anayoyaandika au kwa picha anazoweka mtandaoni. Kuna baadhi ya watu, au kwa kutokujua sheria au kwa makusudi, tayari wametiwa hatiani na maandiko ambayo yanaainishwa kuwa makosa kwenye sheria hii.

Na sina shaka kuna wengi wengine watakumbwa na tatizo hilo kwa sababu inaelekea kuna watu wanaamini kuwa akiwa kajibanza pembezoni mwa nchi akarusha matusi kwenye mtandao basi siyo rahisi kupatikana.

Tatizo la kuonana uso kwa uso limenitokea leo baada ya kutembelewa Butiama na Fabian Zegge, "rafiki" wa mtandao ambaye sikutarajia kuonana naye hata siku moja. Alifika Musoma kwenye shughuli zake na akaamua kunitembelea Butiama.

Mara baada ya kusalimiana naye nilimwambia kuwa angekuwa ni mtu ambaye tulirushiana maneno yasiyo na ustaarabu katika mawasiliano yetu kwenye mtandano, leo hii ningeona aibu kujitokeza kusalimiana naye. Ningemwambia amekosea namba ya simu aliponipigia awali kutaka kufahamu iwapo nipo nyumbani.
Kutoka kushoto kwenda kulia: mimi, Fabian Zegge, na mwenyeji wake.
Nimejifunza mambo mawili ya msingi leo: kwanza, hawa "marafiki" wa ndani ya mtandao ambao wengi wetu tunaamini hatutaonana nao hata siku moja ni watu ambao tunaweza kuonana nao wakati wowote. Sikutarajia kuonana na Fabian Butiama.

Pili, na kwa kutambua ukweli huo, nimeone umuhimu kwamba tunapowasiliana na watu mbalimbali kwenye majukwaa kwenye mtandao tunapaswa kuongozwa na ustaarabu kwenye kauli zetu.

Bila kuzingatia hayo tutaumbuliwa na sheria au aibu ya kukutana na tunaowatukana.

Saturday, November 11, 2017

Mimba zisizoisha za Chausiku Suleiman

Zaidi ya miaka sita iliyopita nilipata fursa ya kumtembelea mama mmoja, Chausiku Suleiman, anayeishi Maji Chai, jirani na Tengeru kwenye barabara kuu ya kutoka Moshi kwenda Arusha. Alinipa simulizi za ajabu. Yeye anapata ujauzito kila anapojifungua, bila hata kukutana na mume wake.

Nilipoonana naye alikuwa na umri wa miaka 47 na alikuwa na watoto 16 aliyewazaa ndani ya kipindi cha miaka 30. Tatizo lake lilianza alipopata ujauzito wa mtoto wa tano. Majuma matatu baada kujifungua alihisi kuwa alikuwa mjamzito tena. Nilipoonana naye mwaka 2011 alisema kuwa mimba yake wakati huo ilikuwa ina zaidi ya miaka mitatu.

Chausiku Suleiman akiwa na baadhi ya watoto wake, Maji Chai, Arusha.
Nilipomuuliza iwapo ametafuta ushauri wa daktari aliniambia kuwa madaktari wameshindwa kubaini tatizo lake na wameshindwa kuona kama ana kichanga tumboni.

Alisema anahisi kuwa madaktari wanaamini kuwa ana imani kuwa na tatizo ambalo halipo.