Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, September 20, 2011

Mada yangu ya leo: Kumekucha


Wakati majadiliano ya madai ya katiba mpya yanaanza niliwahi kuandika makala kwenye safu yangu ya Letter from Butiama, iliyopo kwenye gazeti la Serikali, Daily News, nikitabiri kuwa yatatokea makundi tusiyoyatarajia katika mchakato huu wa kudai haki ndani ya katiba mpya.

Baadhi ya makundi hayo yameanza kuibuka, gazeti la Majira linaripoti. Toleo lake la Septemba 16, 2011 linanmnukuu mwakilishi wa kundi la mashoga akidai nao watambuliwe ndani ya katiba mpya ili kulinda haki zao kama raia. Alinukuliwa akisema kuwa hubaguliwa wanapoomba kazi na kwa kukosa ajira wanaendelea na tabia ambazo hazikubaliki ndani ya jamii.

Hoja yangu, ambayo niliitoa kwenye makala yangu ya Kiingereza kwenye gazeti la Daily News ni kuwa suala zima la mabadiliko ya kikatiba linajikita kwenye kumpa fursa kila raia kufurahia uraia wake bila bugudha toka kwa mtu, taasisi, au kundi lingine lolote la raia. Katiba pia inaainisha wajibu wa raia katika masuala mbalimbali.

Lakini tatizo ni kuwa kwenye nchi nyingi huwa hakuna makubaliano ya mipaka ya haki hizi, na wakati nchi nyingine zinaainisha haki kwa makundi fulani ya raia wake, nchi nyingine zinaweza kuweka marufuku kwa haki hizo hizo kwa makundi ya aina hiyo.

Mfano niliotoa kwenye makala yangu ni kuwa baadhi ya nchi zimepitisha sheria zinazoruhusu ndoa za jinsia moja wakati suala hilo ni ukiukwaji wa sheria kwenye nchi nyingi duniani. Rais Robert Mugabe, ambaye ni mpinzani mkubwa wa sera hizi akihutubia nchini Zimbabwe alisema kuwa sheria hizi zinataka kuruhusu "bibi yangu (nyanya) mzazi kuona na bibi yako."

Kwetu sisi migongano hiyo sasa imefika. Raia shoga anadai haki za kikatiba. Kwa misingi ya wale wanaotufundisha kuwa kila raia anapaswa kuwa na haki chini ya katiba ya nchi ni dhahiri kuwa raia huyu anapaswa kupewa haki zake ndani ya mabadiliko mapya ya katiba.

Iko hoja itakayotolewa na waumini wa dini kadhaa, kuwa suala la ushoga ni kinyume na mafundisho ya dini. Lakini misingi ya kikatiba na haki kwa raia inakinzana na maadili kama haya ya kidini. Kwa mitazamo hiyo hiyo ya haki kwa kila raia, raia wote – wenye dini na wasiyo nayo – wanapaswa kupata haki ile ile ya msingi chini ya katiba.

Kwa mantiki hiyo, yoyote anayepinga ushoga kwa misingi ya dini anaweza kujibiwa kuwa suala la dini haliwezi kuwa kigezo kwa raia ambaye hana dini na anayedai haki zake chini ya katiba.

Maadili, mila na desturi, na tamaduni vimekuwa vigezo vinavyoongoza jamii zetu tangu enzi za mababu na bado zinaongoza jamii katika sehemu nyingi za Tanzania ambapo vigezo hivi vinatumika. Lakini maingiliano na wageni yameleta na yanazidi kuleta vigezo vipya ambavyo vitaleta mkanganyiko mkubwa ndani ya jamii kwa ujumla, na hususani ndani ya huu mjadala wa katiba mpya.

Ni dhahiri kuwa kuna mengi yatapingwa kuhusu hivi vigezo vipya na kuna uwezekano mkubwa kuwa Watanzania wengi hawatakubali kuingizwa kwa haki za mashoga kwenye katiba. Lakini litakapokataliwa ina maana kuwa tutakuwa tumeamua kuchagua 'yanayotufaa' na 'yasiyotufaa'. Na uamuzi kuwa hili linafaa na hili halifai unakinzana na azma ya kumpa kila raia uhuru wa kuwa kile anachotaka kuwa. Kwa maana nyingine, kuna mipaka ya kitamaduni inayoshinikiiza kuwa siyo kila uhuru utakubalika ndani ya jamii ya Kitanzania.

Siyo kazi rahisi kuongoza Serikali katika nyakati hizi za sasa. Zamani ilikuwa rahisi kusema hili halifai, na hili linafaa. Siku hizi kila mtu ana haki. Siku hizi tunaambiwa hata watoto ambao bado wanajikojolea kitandani wanapaswa kupewa uhuru wa kuamua wanayoyataka wao.

Ni mkanganyiko usio mdogo. Ndio maana nasema, kumekucha.

Saturday, September 17, 2011

Mwanaharakati Brian Haw wa Uingereza amefariki

Nilivyotembelea Uingereza mwaka 2006 nilipata fursa ya kumtembelea mwanaharakati Brian Haw, aliyeweka hema mbele ya viwanja vya bunge la Uingereza kwa muda unaokaribia miaka kumi akiishi hapo na kutumia kipaza sauti chake kuendeleza kampeni yake dhidi ya vita vya Irak.
Brian Haw, kushoto, mimi, na mke wake Kay, kulia.
Taarifa ambazo nimechelewa kuzipata zinaeleza kuwa alifariki jijini Berlin, Ujerumani, tarehe 18 Juni, 2011 kutokana na ugonjwa wa saratani ya mapafu.

Nilipomtembelea alinieleza kuhusu kusudio lake la kumfikisha aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kwenye mahakama ya makosa ya kivita kwa kuiingiza Uingereza kwenye vita vya Irak.

Jim Becket, Jaffar Amin, na Andrea Wobmann watarajia kupanda Mlima Kilimanjaro wiki ijayo


Niko njiani kuelekea Moshi kwa ajili ya maandalizi ya kupanda Mlima Kilimanjaro chini ya The Mwalimu Nyerere/Mt. Kilimanjaro Charity Climb

Nilikusudia kusafiri moja kwa moja hadi Moshi kupitia njia ya Serengeti lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa. Hivi sasa niko Mwanza na natarajia kufika Moshi kesho kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kutokana na maandalizi hafifu ya uchangishaji wa pesa za hisani ambao nafanya kila mwaka ninapokwea Mlima Kilimanjaro, yawezekana kuwa azma ya kuchangisha pesa za hisani haitafana sana mwaka huu. Katika siku chache zijazo na kabla ya kuanza msafara nitafanya uamuzi iwapo itawezekana kufanikisha kuchangisha pesa za hisani au iwapo nitalazimika kuahirisha uchangishaji huu mpaka msafara ujao wa kukwea Mlima Kilimanaro.

Suala lingine katika msafara wa mwaka huu ni kuwa muongozaji mashuhuri wa filamu toka nchini Marekani, Jim Becket, anakusudia kupiga picha za filamu wakati wa msafara huu. Jaffar Amin naye anatarajia kuungana nami katika msafara huu kutokana na makubaliano yetu wakati wa msafara wa mwaka jana kuwa tutaendeleza jitihada za kuchangisha pesa za hisani.

Kwa kuwa Jaffar atakuwa nasi, Jim anakusudia kujumuisha ndani ya filamu yake historia ya mahusiano kati ya Tanzania na Uganda na jinsi gani haya mahusiano yamebadilika, akijikita juu ya malengo ambayo mimi na Jaffar tunayo katika masuala ya hisani.

Mwanadada Andrea Wobmann ambaye amewahi kufanya kazi ya kujitolea jijini Mwanza naye pia anajiunga nasi kuukwea Mlima Kilimanjaro

Wednesday, September 14, 2011

Wageni wa Butiama: Kelvin Bernard


Muda si mrefu uliyopita, Kelvin Bernard, wa pili toka kulia kwenye picha hii hapa chini,
pamoja na wanafunzi wenzake Benedicto David, Raphael Nenebwa, and Kelvin Ryoba toka Mwanza walitembelea Butiama kwa ajili ya kukamilisha somo lao kuhusu Mwalimu Nyerere.

Walifanya utafiti wao kwenye Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, kwenye maktaba ya Mwalimu Nyerere, na kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Mwitongo, Butiama.

Sunday, September 11, 2011

Mashambulizi ya Septemba 11: Marekani imeelewa somo?


Leo ni miaka kumi tangu kutokea mashambulizi ya Septemba 11 2011 yaliyofanyika katika miji ya Washington na New York nchini Marekani na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000.

Katika maadhimisho hayo vyombo kadhaa vya habari na taarifa nyingi zilizopo kwenye mtandao zimejikita kwenye kuwauliza walioshuhudia mashambulizi hayo kukumbuka hali ilivyokuwa kwao siku ya shambulio.

Lakini ni sehemu ndogo ya vyombo hivyo vya habari vinavyohoji kwanini shambulio lilitokea, na iwapo sababu ambazo zilisababisha shambulio hilo bado zipo, na ni hatua gani zimechukuliwa kuepuka kutokea tena shambulio kama hilo ambalo lilihusishwa na Osama Bin Laden, ambaye aliuwawa hivi karibuni.

Kama ni kweli kuwa shamubilizi hilo liliongozwa na Osama na wafuasi wake, kuna maswali ya kuuliza. Tofauti za kiitikadi na kidini zinazosemekana zilisukuma mashambulizi hayo bado zipo? Kama zipo, jitihada gani zimefanyika na Serikali ya Marekani na washirika kuziondoa? Kuna uwezekano wa kufikia muafaka utakaoweza kufuta hizo tofauti, na kuzifanya pande zote mbili kusitisha mapambano kati yao?

Afisa mwandamizi wa shirika la ujasusi la Uingereza MI5 alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa uwezekano wa kupambana na kuwashinda wafuasi wa makundi ya Kiislamu kama lile linaolomuunga mkono Osama ni ndogo sana, na nchi za Magharibi sasa zinaangalia uwezekano wa kukubali yaishe, yaani kukaa meza moja na upande wa pili kutafuta suluhisho lisilohusisha matumizi ya nguvu.

Mwandishi mmoja wa Marekani akihojiwa hivi karibuni alisema anaona kama bado Marekani haijajifunza kutokana na mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Anaeleza kuwa badala ya kuwa ingefanyika jitihada kubwa ya kujaribu kuelewa tamaduni na desturi za watu wengine duniani, inaonekana kama vile Wamarekani bado wanajiona kuwa wanachoona sawa wao ndiyo sawa kwa binadamu wengine wote na wanaonekana hawajali sana yanayotokea sehemu nyingine ya dunia.

Thursday, September 8, 2011

Mimea ya Mlima Kilimanjaro


Mlima Kilimanjaro una mimea ambayo haipatikani sehemu nyingine yoyote duniani. Mmea huu unaitwa Giant Groundsel (jina la kisayansi ni Senecio 
keniodendron) na hustawi kwenye maeneo ambayo kwa kawaida yana ukungu mwingi. Kwenye picha ya hapo juu ni eneo lililopo karibu na kambi ya Barranco iliyopo mita 3,900 juu ya usawa wa bahari.

Tuesday, September 6, 2011

Matunda ya Nyamisisi

Ukifika Nyamisisi, eneo liliopo karibu ya Butiama, kwenye barabara kuu ya Mwanza - Musoma, utakuta harakati hizi za wafanyabiashara wanaouza matunda kwa abiria wa mabasi na gari ndogo zinazosimama eneo hilo.
Matunda mengi yanatokea Tarime na kuletwa Nyamisisi na wafanyabiashara.

Lugha yetu Kiswahili


Taswira ya lugha ya Kiswahili na ya wale wanaotumia lugha hiyo ni masuala ambayo yanaleta mitazamo na maana mbalimbali.

Nina rafiki yangu toka Kagera alinisimulia kuwa kwa baadhi ya Wahaya katika nyakati ambazo wenye uwezo wa kuongea Kiswahili fasaha walikuwa wachache, hasa kwenye maeneo ya vijijini, mtu yoyote aliyeongea lugha Kiswahili vizuri alionekana ni mtu mmoja mjanja mjanja ambaye hakuwa mtu wa kuaminika kwa urahisi.

Nakumbuka simulizi nyingine pia toka Uganda zinazoeleza kuwa kwa sababu lugha ya Kiswahili ilikuwa inatumika na wanajeshi (na inaendelea kutumika mpaka sasa) basi lugha hiyo imehusishwa katika historia ya Uganda na nyakati ambapo jeshi lilionekana kama kinara wa ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Katika matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili, mtu anayeitwa Mswahili, pamoja na kuwa na maana nyingine, ni mtu mwenye maneno mengi, na mjanja.