Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, May 22, 2013

Tatizo la ziara ya Rais Obama Tanzania

Rais Barack Obama akija Tanzania sina hakika kama atafika Dar es Salaam, lakini iwapo atafika huko mimi nitafanya jitihada niwe sehemu nyingine ya Tanzania. Nakumbuka Rais George Bush alipotembelea Dar es salaam na sitaki yanikute ya wakati huo.

Kero kubwa ilikuwa kufungwa kwa barabara kuu za Dar es Salaam kwa muda mrefu kupisha msafara wa Rais Bush na mwenyeji wake kuelekea Ikulu. Yaliyojiri Ikulu sifahamu lakini nakumbuka kuona picha moja ikionyesha wanajeshi wa Marekani wakiwa juu ya paa la Ikulu wakipiga doria kali kumlinda Rais wao kwenye eneo la Ikulu yetu.

Bila hata kutembelewa na rais wa Marekani, jiji la Dar es salaam linafikiwa na waheshimiwa wengi tu wazalendo ambao kila wanapopita kwenye barabara zake basi husimamisha matumizi ya barabara zake kwa wakazi wa Dar es Salaam. Atakapofika Mheshimiwa Obama ni dhahiri kuwa yatatokea yale yale ya aliyemtangulia au hata zaidi.

Ilipotua ndege ya George Bush kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ndege nyingine hazikuruhusiwa kutumia uwanja huo mpaka ilipoondoka. Watanzania ambao kawaida huongoza ndege zinazotumia uwanja wa ndege wa Dar es Salaam walipewa likizo ya muda na kazi yao ilikasimiwa na wageni mpaka ndege ya rais wao ilipopaa. Rais Bush alipokwenda Arusha mawasiliano ya simu za viganjani yalikatwa kabisa mpaka alipoondoka.

Ninegombwa ushauri ningesema Rais Obama asifikie Dar es Salaam ambako ataathiri shughuli za watu zaidi ya milioni 4. Afadhali aende hata Dodoma. Au aje Butiama, ambako kuna wakazi wasiozidi 20,000.

Tuesday, May 21, 2013

Nkrumah bado anakumbukwa


Mwaka 2008 mimi na baadhi ya wadau kutoka nchi wanachama za Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) tulialikwa nchini Zimbabwe kuandika kuhusu uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Baada ya kura kupigwa tulitembelea kituo kikuu cha kutoa taarifa za uchaguzi cha Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) jijini Harare ili kupokea taarifa zilizoendelea kufika hapo toka sehemu mbalimbali za Zimbabwe.
Maafisa wa Tume ya Uchaguzi wa Zimbabwe wakitangaza matokeo ya uchaguzi wa Zimbabwe.
Wadau ambao walikuwa waandishi wa habari walikuwa ni pamoja na Bayano Valy kutoka  Msumbiji (aliyesimama, kushoto), na Penny Kamanga (aliyesimama, kulia) kutoka Malawi.
Nimewahi kuandika kwenye blogu yangu ya Kiingereza kuhusu tofauti za kimtazamo kati ya Dk. Kwame Nkrumah, na Mwalimu Julius Nyerere. Kwenye picha ya hapo juu, nukuu iliyopo kwenye fulana aliyovaa huyo mwanahabari aliyekaa kulia inatanabahisha kufanana kwa baadhi ya mitazamo yao. Tafsiri ya nukuu:

Uhuru wa Ghana hauna maana iwapo hautahusishwa na ukombozi kamili wa Afrika.

Ni msimamo ambao Mwalimu Nyerere naye alikuwa nao. Wakati wa uongozi wake, Tanzania ilitoa msaada mkubwa wa hali na mali kuunga mkono vyama vya ukombozi kutoka nchi za Kiafrika ambazo zilibaki chini ya utawala wa kikoloni na kibaguzi, ikiwa ni pamoja na Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini, na Namibia.

Saturday, May 11, 2013

Desturi ya Wazanaki ya kupokea mahari

Siku chache zilizopita nimehudhuria sherehe ya kupokea mahari ya kitukuu wa Mtemi Edward Wanzagi wa Butiama.
Wageni wanajitambulisha.

Wageni (waliosimama), wanawasalimia wenyeji.
 Desturi inaelekeza kuwa mahari lazima ipokelewe kabla ya saa sita mchana, yaani kabla jua halijavuka na kuwa upande wa magharibi.
Kukagua mahari.
Kuna mlolongo mfupi wa matukio yanayohusiana na sherehe hiyo. Wageni wanaoleta mahari wanatambulishwa kwa wenyeji wao, na wao wanatambulisha upande wao. Halafu, wageni wanajongea walipoketi wenyeji na "kuwaamkia." Na kama ishara ya heshima wageni wote wanaamkia "shimakoo" hata kwa wale wageni ambao wanaostahili "shikamoo" zao kutoka kwa baadhi ya wenyeji. Wakati wa kusalimia wenyeji huketi wakati wageni wanasimama mbele ya wenyeji.
Kukagua mahari.
Baada ya salamu ndiyo unawadia wakati wa kukabidhiwa mahari. Mahari iliyoafikiwa ni ng'ombe sita, na mbuzi wanne. Wenyeji hukagua mahari kuhakikisha kuwa ng'ombe na mbuzi wako kwenye hali nzuri. Na hapo ilitokea mmoja wa wazee kwa upande wa wenyeji kutamka kuwa mmoja wa ng'ombe alikuwa na homa, hakuwa mzima. Na desturi ingelazimisha yule ng'ombe kurudishwa na kuletwa mwingine ambaye hana tatizo. Lakini ikaamuliwa kuwa pengine hali hiyo ya ng'ombe ilisababishwa na safari ndefu ya kuwafikisha pale Butiama na kuwa baada ya muda hali ya kawaida ya ng'ombe yule itarejea.
"Ng'ombe mmoja ana homa," alisema mzee mmoja baada ya kuwakagua ng'ombe.
Baada ya hapo msemaji wa wenyeji anatamka kuwa mahari imekamilika na kina mama wanapiga vigelegele.  Inafuata hatua ya kukabidhi zawadi ndogo kwa wazee (blanketi), na kwa mama wa bibi harusi (kitenge na sufuria). Mwisho kwenye ratiba ni chakula na baadaye wageni kuondoka.
Mzee Joseph Muhunda Nyerere anapokea blanketi kutoka kwa mwakilishi wa Bwana Harusi.
Baada ya hapo inasubiriwa siku ya kufunga ndoa. Kwa mila na destru za zamani, ndoa ingekuwa imekamilika baada ya kupokelewa mahari.

Maharusi watarajiwa hawahudhurii sherehe hii.

Monday, May 6, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Neno jipya nililojifunza leo ni ajari. Siyo ajali, bali ajari.

Ajari ni muda wa ziada ambao mfanyakazi anabaki kazini akifanya kazi kwa muda wa ziada, zaidi ya muda aliopangiwa kwa mujibu wa mkataba wake wa kazi. Ajali ni ni tukio lenye athari mbaya linalotokea ghafla; ni neno ambalo linafahamika kwa watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili, hata wale ambao ni mbumbumbu wa lugha hiyo.

Wednesday, May 1, 2013

Ukarimu wa Watanzania unatoweka

Enzi zilizopita utamaduni wa Mtanzania ulihusisha pia ukarimu. Leo hii utamaduni huo unatoweka.

Nianze kwa tukio lililonitokea yapata miaka 27 iliyopita. Nilikuwa nasafiri kutoka Arusha kuelekea Butiama nikiendesha gari nikiwa peke yangu. Nilitoka kwenye lango la Ikoma la Hifadhi ya Serengeti jioni na mvua kubwa ilikuwa inanyesha. Kwa sababu kiza kilikuwa kimeingia na kwa sababu barabara ilikuwa mbaya sana kutokana na mvua na ilikuwa dhahiri gari ingeweza kuzama kwenye matope na kusababisha nilale porini, nilipofika Fort Ikoma niliamua kuelekea Mugumu ili niweze kulala huko na kuendelea na safari kesho yake.

Kutokana na mvua kubwa iliyoendelea kunyesha, barabara kati ya Fort Ikoma na Mugumu nayo ilikuwa mbaya sana lakini Landrover 109 niliokuwa naendesha ilimudu kukabiliana na hali mbaya ya barabara ingawa mara kadhaa ilielekea kunasa kwenye matope. Katikati ya safari yangu kuelekea Mugumu, ikiwa imepita saa 3:00 usiku na nikiwa katikati ya pori, nilikutana na mtu mmoja akitembea kwa mguu ambaye aliashiria kunisimamisha na kuomba nimchukue. Nilisimamisha gari kumchukua. Alikuwa anaelekea Mugumu.
File:Land Rover Series III 109.JPG
Aina ya gari niliyoendesha siku hiyo. Picha: Buckers.
Nakumbuka tulifika Mugumu baada ya saa 5:00 usiku na sikufanikiwa kupata chumba kwenye hoteli za Mugumu. Zote zilikuwa zimejaa. Yule mtu niliyemchukua porini alinuchukua mpaka anakoishi akanipisha chumba chake nikalala mpaka asubuhi na kuendelea na safari yangu ya kuelekea Butiama. Bila yeye ningelala ndani ya gari.

Hiyo ndiyo Tanzania ya zamani. Ya watu wenye kuaminiana na wenye ukarimu ambao leo hii ni vigumu kuuona. 

Pamoja na kuwa miaka 27 iliyopita nilisimamisha gari katikati ya pori na kumpa msaada mtembea kwa miguu ambaye sikuwa namfahamu, nakiri kuwa leo hii nitasita kusimamisha gari mchana kumchukuwa mtu nisiyemfahamu katika eneo lolote la Tanzania. Na hata yule mtu aliyenipisha kitanda chake sidhani kama leo hii atathubutu kukaribisha mtu asiyemfahamu alale chumbani kwake bila kuwa na hofu kuwa mgeni wake atahama na baadhi ya mali zake.

Imani inatoweka na ukarimu unafifia kutokana na mabadiliko ndani ya jamii ambayo yameleta Watanzania wasiyothamini uhai wa binadamu wenzao na hivyo kusababisha kubadilika kwa mila na desturi ambazo tulizoea zamani.