Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, December 13, 2014

Mwisho wa kampeni Butiama za uchaguzi wa serikali za mitaa

Viongozi na wagombea wa Chama cha Mapinduzi wa kijijini Butiama wakiomba kura mbele ya wakazi wa Butiama siku moja kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika nchini kote kesho tarehe 14 Desemba 2014.
Mkutano huu (picha ya juu) ulifanyika eneo la stendi, Butiama. Wapinzani wao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walifanya mkutano wa mwisho wa kampeni kwenye kitongoji cha Mtuzu, Butiama.

Friday, December 12, 2014

Mabondia na unga (sehemu ya tatu ya awamu tatu)

Promota wa ndondi za kulipwa, Ibrahim Kamwe, anaeleza kwa nini baadhi ya mabondia wanajiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Ibrahim Kamwe
Ukiangalia umbumbumbu na maskini tulionao mabondia, hapo wajanja wenye pesa zao, wafanyabiashara, na baadhi ya viongozi wanatumia udhaifu tulionao mabondia kutuhadaa kwa kutupatia safari za nje za kimichezo au matembezi ya kwenda kufanya mazoezi ughaibuni na hatimaye kutubebesha mihadarati (madawa ya kulevya) bila kujua kwa kutuwekea katika mizigo tunayosafiri nayo. Wakati mwingine kuna baadhi ya wafanya biashara hao wenye pesa zao hukuweka wazi wakati unaenda pigana umbebee mzigo wake na atakulipa pesa nyingi. Hapo ndipo tunapobanwa ukiangalia nyumbani tunalalia telemka tukaze, tunashindia tembele mlo mmoja, msosi wa kengele tena kwa masimango, mfukoni huna kitu na wala huna kazi itakayokupatia pesa ya kula kwa wakati huo. Hapo sijaingiza mambo ya kodi, na demu wangu namlinda vipi.

Hii njaa na umaskini tulio nao mabondia ndiyo inawapa nguvu vigogo kututumia kwa kutubebesha madawa ya kulevya kusafirisha nje wakijua wazi hatuwezi kataa kutokana na dhiki tuliyo nayo. Tutakubali tu kwani hakuna apendae kulala njaa, kulala pachafu, au kuvaa midabwada.

“Siwezi acha dili la pesa kama hili wakati jina langu kubwa kila kona linatajwa mitaani na vyombo vya habari lakini mimi binafsi nauli ya daladala sina. Siku ya tatu leo nakula mlo mmoja kwa siku, watoto hawapo katika hali nzuri, mazoezi yenyewe sifanyi kwa raha nafikiria nitapata wapi mshiko. Leo unaniletea ishu ya pesa niikatae si nitakuwa kichaa?”


“Wadau wenzangu wa ngumi ,wapambe wao, na walio karibu na sisi mabondia wana nguo za bei kubwa wanapendeza, wana magari. Ukiangalia mimi bondia ndiye mtendaji wao mkuu nipo ovyo sina kitu mfukoni wala tumboni, madeni kibao yaani majanga matupu.”

Ushauri wangu kwa serikali au taasisi zinazohusika na wanaolichukia jambo hili kiukweli - maana wengine hujifanya kulichukia mdomoni pembeni ndiyo watendaji wakuu wa kuwatumia wanamichezo au wasanii kwa faida zao - mabondia au wanamichezo tuboreshewe maeneo yetu ya michezo ikiwemo katika vilabu vyetu na maeneo ya mazoezi, na vifaa viongezwe. Ikiwezekana kodi ya vifaa vya michezo ipunguzwe ili viwe vingi nchini mabondia wasibabaike na vya kuazima au kuangalia katika TV vifaa vya wenzetu.


Serikali iwajali mabondia, isaidie kudhamini semina za walimu wa ngumi ili wawaongoze vyema vijana wao. Magym ya makusudi yajengwe na maeneo ya wazi wasigawane wenye pesa na viongozi kwa faida zao. Wajenge sehemu za michezo ya ndani, na kama pia itatumika njia ya kutoa madarasa matupu katika mashule yetu kwa ajili ya kutuachia sehemu ya mazoezi ya jioni itasaidia sana kukuza mchezo na walimu wenye taaluma kufundisha vizuri kuliko mabondia kufundishana vichochoroni na kutokuwa na nidhamu ya mchezo wala maisha.

Sunday, December 7, 2014

Mabondia na unga (sehemu ya pili ya awamu tatu)

Promota wa ndondi za kulipwa, Ibrahim Kamwe, anaeleza kwa nini baadhi ya mabondia wanajiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Siku za hivi karibuni kuna vimaendeleo kidogo kwa baadhi ya mabondia; tunafanya mazoezi katika vilabu vya pombe kwa kuwalipa kodi ya mazoezi wenye baa. Naweza kusema Tanzania hakuna sehemu rasmi za kufanyia mazoezi ya ndani zilizotengwa na serikali kwa ajili ya raia wake wapenda michezo na kama zipo ni chache na ziko katika makambi ya jeshi kwa masharti magumu kwa raia wa kawaida. 

Siku za nyuma wakazi wa mjini kama vile Kisutu, Gerezani na Kariakoo walikuwa wanafanya mazoezi pale Arnatoglou. Siku hizi huwezi kusikia kuna mwanamichezo katokea Gerezani au Kariakoo. Iliyobaki kwao ni kuuza na kutumia madawa ya kulevya na kukimbizana na wafanyabiashara wa maeneo hayo. Naweza kuilaumu serikali kwa kutoendeleza michezo bali ilishiriki kuuwa kabisa michezo maeneo hayo na mengineyo zaidi.

Kwa sisi tulioanza kukua kimichezo pambano la ngumi likiandaliwa huwa tunalipwa kuanzia shilingi 5,000/- mpaka 20,000/- kwa mapambano haya madogomadogo na iwapo kutakuwa na pambano kubwa na kupata bahati ya kucheza unaweza kulipwa shilingi 40,000/- mpaka 100,000/-. Mapambano makubwa yanaweza kuwa moja, mawili, au matatu kwa mwaka; hayazidi hapo. Haya mapambano madogo tunaweza pata mawili mpaka sita kwa mwaka.

Msiwaone mabondia wakicheza mkadhani wana kipato kikubwa. La hasha! Ni wale tu wachache waliobahatika kupata wadhamini au waratibu wenye uwezo wa kipesa ndiyo kidogo hutoka.

Kwa sisi wengine ukiangalia elimu ya kusoma hatuna, kazi hakuna, na mchezo wa ngumi tunaupenda na pengine tuna vipaji na kufanya vizuri katika mapambano yetu. Hivyo mchezo ndiyo huwa kama ajira yetu kwa sababu tunapata chochote kidogo kupitia mchezo huo kuliko kuiba au kukimbizana na mapolisi katika kamari na kuishia jela.

Kwetu sisi mabondia huona ni jambo la kifahari na hufurahi mno pale tu tunapopata pambano la nje ya nchi na hufurahia kupanda ndege na vile vimisosimisosi tunavyopata tukiwa mahotelini ugenini. Tukihadithiana mambo ya safari uswahilini kwetu tunahisi tunakosa mambo mengi ya raha.

Hapo ndipo mawakala wa ngumi hutupata na mabondia huwa wanadiriki kukubali kwenda kucheza popote tukijua tutapanda ndege, tunakula raha bila kujali  na wala kuhoji tuendako tutalipwa kiasi gani cha pambano nitakalocheza wala kujua usalama wangu.


(itaendelea na sehemu ya tatu)

Tuesday, November 25, 2014

Mabondia na unga (sehemu ya kwanza ya awamu tatu)

Promota wa ndondi za kulipwa, Ibrahim Kamwe, anaeleza kwa nini baadhi ya mabondia wanajiingiza kwenye biashara ya madawa ya kulevya.
Ibrahim Kamwe
Asili ya mabondia wengi  duniani wanatoka katika familia duni. Kwa mfano hapa kwetu ni nadra kumkuta bondia ametoka Upanga, Oysterbay, au Masaki ushuwani, nikiwa na maana  mabondia wengi wanatoka uswahilini. Ni watu wa hali duni. Wengi wetu hatujakalia madawati ya shule na wengine tuliojitahidi tumefika darasa la tano au sita. Kama wazazi walikomaa ndiyo tunamaliza la saba.

Baadhi yetu tukiwa na umri wa kuanzia miaka sita nyumbani huwa tunaanza kupewa uzowefu wa kuuza visheti, maandazi, vitumbua, karanga n.k. na vikibaki nyumbani hauli chakula mpaka viishe. Shuleni mwalimu mkali, darasani hafundishi mpaka usome tuisheni ndiyo unapata kufundishwa kidogo, na ukishindwa maswali yake unapata viboko vya ghadhabu. Hapo ndipo tunapoamua kuachana na shule na kutinga mitaani. Michezo yetu ni katika madampo na vichochoroni na tukifikia umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea tunajua jinsi ya kutafuta pesa kwa kuuza njiwa, kucheza kamari, malani, kuiba kuku na bata, na kwa wale walio watukutu zaidi kuuza na kuvuta bangi ni sehemu ya maisha ya kawaida tu huku mitaani kwetu.

Mara nyingi mlo kwetu ni mmoja tu kiubishoo au kuwa wageni ndiyo tunakula milo miwili. Katika maisha yetu muda mwingi tupo huru na michezo kuliko kusoma, hasa kolokolo, ngoma, mpira, na ngumi. Mpira tunacheza mabarabarani, vichochoroni, na kwenye madampo, wakati ngumi tunajifundisha katika makamali, vichochoroni, au uwani kwa kina masta. Begi au tairi linafungwa juu ya mti, tizi linaendelea bila vifanyio vya mazoezi vilivyo rasmi. Mwendo mdundo tunasonga na tunashinda au kufanya vizuri katika mashindano yetu tunayoshiriki na hali yetu duni hii hii ya kimaisha, na majina yetu kutangazwa sana katika vyombo vya habari na kupata umaarufu mkubwa nchini, nchi jirani na hata nchi za Ulaya.

Lakini ukibahatika kututembelea na kuangalia tunapoishi na familia zetu na umaarufu tuliyonao, utakuta maisha yetu mabovu na yanasikitisha.

(itaendelea na sehemu ya pili)

sehemu ya pili ya makala hii

Friday, November 21, 2014

Wazanaki na dini

Simulizi hii nimepewa na Mwalimu Jack Nyamwaga, kiongozi mstaafu wa kijiji cha Butiama ambaye pia anafahamu vyema baadhi ya matukio ya historia ya kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama. Ni simulizi inayotoa picha kuhusu baadhi ya mila na desturi za Wazanaki.
Mwalimu Jack Nyamwaga, kulia, akiongea na Dk. Thomas Molony, mtafiti na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh.
"Wamisionari wa kwanza waliofika hapa Butiama walikuwa Waprotestanti. Wakati huo Roman Catholic walikuwa wameshafika Nyegina [karibu na Musoma]. Hata hivyo Waprotestanti hawakuingia ndani sana kueneza dini miongoni mwa Wazanaki.

Halafu wakaja Seventh Day Adventist (SDA) na wakasema kuwa masharti ya madhehebu yao ni pamoja na wanaume kuoa mwanamke mmoja tu na waumini wao kukatazwa kunywa pombe. Hayo masharti hayakuwa rahisi kukubaliwa na Wazanaki ambao siyo tu walikuwa na desturi ya kuoa mke zaidi ya mmoja, lakini walikuwa na asili ya kunywa pombe na hata kuitumia katika mitambiko. Mwaka 1938 SDA wakahamia Busegwe [kijiji cha jirani] ambako kulikuwa na mchanganyiko wa makabila mengine zaidi ya Wazanaki. 
Halafu wakaja Mennonite na wao pia walikuwa na marufuku ya kunywa pombe. Hawa wakashauriwa kwenda Bumangi [kijiji cha jirani]. Mtemi Nyerere Burito alipoambiwa kuwa anapaswa kuwa na mke mmoja akauliza: "Hawa wake zangu 13 nitawapeleka wapi?"

Walipofika wamisionari wa madhehebu ya Roman Catholic Wazanaki wa Butiama wakapendekeza kanisa lao lijengwe Magorombe, kijiji kilicho mbali na Butiama kwenye ardhi inayotitia ikitarajiwa kuwa kanisa likijengwa hapo lintaanguka. Mmisionari aliyekwenda huko alipanda mikaratusi iliyofyonza maji na akajenga kanisa imara.

Waislamu walipokuja nao walikuwa na marufuku ya kunywa pombe. Wao wakashauriwa waende Nyamuswa kwa Mtemi Makongoro Matutu, ambaye alikuwa rafiki wa Mtemi Edward Wanzagi. Yeye aliwapokea na akasilimu. 
Kizingiti kikubwa cha kuwahi kuenea kwa dini miongoni mwa Wazanaki wa Butiama ilikuwa suala la marufuku ya kuoa mke zaidi ya mmoja na marufuku ya kunywa pombe."

Tuesday, October 14, 2014

Huduma kwa mteja mkoani Mara

Hili ni tukio la kweli na nimelishuhudia.

Siku moja nilikuwa abiria kutoka Nyamisisi kwenda Mwanza ndani ya basi lililoanza safari yake Tarime.

Baada ya muda kondakta alimsogelea abiria aliyekaa karibu yangu na mazungumzo yakawa hivi:

Konda: Nipe hizo hela!
Abiria: Ngapi?
Konda: Kwani hujui?!?!?!

Baada ya muda abiria akatoa nauli kamili halafu wakaendelea:

Abiria: Nifahamishe nauli sahihi kwa ustaarabu.
Konda: Kwani wewe nani? Usiniletee mambo yenu ya Kikurya!

Sehemu nyingine Tanzania watu wangekunjiana ngumi. Mkoa wa Mara ni mazungumzo ya kawaida tu kati ya mtoa huduma na mteja wake.

Saturday, October 11, 2014

Uongo wa waandishi wa habari: sikuikataa noti ya Mwalimu Nyerere

Juzi nilipewa fursa ya kutoa neno la shukurani kijijini Butiama kwenye hafla ya kuzindua onyesho la noti na sarafu kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere.

Mgeni rasmi alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Juma Reli. Katika kumalizia neno la shukurani niliomba uongozi wa Benki Kuu kuangalia uwezekano wa kubadilisha picha ya Mwalimu Julius Nyerere waliyotumia kwenye noti ya shilingi elfu moja. Kwa maoni yangu ile picha haifanani kwa karibu sana na sura ya Mwalimu Nyerere. Sikuamuru wala sikuikataa noti, ila niliomba tena kwa unyenyekevu mkubwa. Lakini ukifuatilia habari zilizoandikwa juu ya ombi langu utapata picha tofauti.

ITV walifungua dimba la upotoshaji kwa kusema kuwa nilitamka kuwa picha ile inamdhalilisha Mwalimu (au familia yake?). Huu ni uongo wa mchana na siyo kweli kabisa kuwa nilitumia neno “kudhalilisha.” Nikisoma baadhi ya vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti yaliyoandika habari hizo navyo vinapotosha.

The Citizen wameandika kuwa nimeitaka serikali kuiondoa hiyo noti. Huo nao ni uongo mwingine. Gazeti lingine limeandika kuwa familia ya Mwalimu Nyerere imeikataa noti ya shilingi elfu moja. Ni uongo juu ya uongo. Naamini orodha ni ndefu zaidi lakini sijapata fursa ya kufuatilia kwa muda mrefu.

Sikusema kuwa familia imeikataa noti. Nilichosema ni hayo niliyoandika mwanzo wa taarifa hii.

Ninayo bahati mbaya ya kutungiwa maneno ambayo sijayasema kwenye taarifa zinazonihusu. Mwanzo nilikuwa napuuzia nikiamini kuwa tatizo hili litaisha lakini kila muda unavyozidi kupita naona hali ni ile ile.

Nimekuwa nawashauri waandishi wa habari waache kutumia mtindo wa kuandika “Madaraka alisema….” na badala yake watumie maneno yangu mwenyewe na kuandika habari kwa njia ya kuninukuu. Naamini njia hii inapunguza kuweka maneno ambayo hayakutamkwa.


Naanza kufikia kuamini kuwa maneno yangu mwenyewe huwa hayauzi magazeti na inalazimika mwandishi kuweka chumvi kidogo ili magazeti mengi zaidi yatoke. Kama hii ni kweli basi hali hii inadhirihisha kuwa sifa ya weledi kwenye sekta ya habari inaanguka, na inahitaji kufanyika jitihada ya kuirekebisha.  

Saturday, October 4, 2014

Hiki ni kielelezo cha utu uzima

Leo nimetembelea kituo cha polisi kutoa taarifa ya kupotelewa vitu vyangu. Nimegundua umri umepiga hatua kubwa.

Afisa aliyechukuwa maelezo yangu aliponiuliza umri wangu nilijibu: 54.

Akauliza: miaka? Nikamjibu: ndiyo, miaka. Au naonekana nimezidisha?

Nilitamani kumwambia: Hapana. Maandazi.

Ningejibu hivyo labda saa hizi ningekuwa rumande kwa kosa la kudhalilisha Jeshi la Polisi.

Lakini nilitambua kuwa kwake yule afisa miaka 54 haikuwa kidogo.

Tuesday, September 30, 2014

Mila na tamaduni: Watanzania ni wakarimu (sehemu ya tano)

Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.

Jiunge nami kwenye sehemu ya tano na ya mwisho ya msafara huu...

Agosti 5
Ni zaidi ya kilomita 40 toka Bunda kuelekea Butiama na safari inaenda vizuri tu nikiwa nimejaa shauku ya kumaliza hili zoezi.
Hata hivyo adui mkubwa wa masafa marefu kwa baiskeli ni njaa na suala la kupata chakula cha mchana ni muhimu kabisa ili kuweza kuendesha baiskeli kwa saa zaidi ya tano kwa siku ya leo. Naenda kwa wastani wa kilomita kama 11 kwa saa. Kwa hiyo nalazimika kusimama tena Nyamisisi kukamilisha mlo wangu wa mchana kabla ya kuendeela na safari hadi Butiama. Nyamisisi ni sehemu ambayo siyo mashuhuri tu kwa matunda ila ina sifa ya kuwepo wataalamu juu ya taarifa za wanasoka na wasanii maarufu.

Napumzika sehemu ambayo nilikaa na Elvis Lelo Munis miezi kadhaa iliyopita alipopita hapa akielekea Nairobi na baadaye Moshi. Elvis ni Mtanzania ambaye alizunguka nchi zaidi ya mia moja za dunia akitumia baiskeli na alimaliza ziara yake hiyo ya maelfu ya kilomita mwezi Julai 2014. Nimekula chipsi mayai na baadaye naanza ngwe ya mwisho ya mzunguko wangu.
Mimi namalizia ziara yangu ya kilomita zaidi ya 170 lakini nahisi nahitaji mapumziko baada ya safari yangu ya kutoka Ukerewe mpaka Butiama.

Saturday, September 27, 2014

Mila na tamaduni: Watanzania ni wakarimu (sehemu ya nne)

Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.

Jiunge nami kwenye sehemu ya nne ya msafara huu...

Agosti 4
Sijaendesha baiskeli kwa masafa marefu kwa muda mrefu kwa hiyo leo naanza kusikia mwili unapanga njama za kuanzisha mgomo wa kutoendelea na safari. Hata hivyo hii ni njia ambayo nimeshawahi kupita kwa baiskeli kuelekea Ukerewe na muda si mrefu najikuta nimefika kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Bulamba.

Inanipa matumaini kuwa safari ya kwenda Bunda imepungua kwa kiasi kikubwa. Nilipokaribia Bunda nilikimbiliwa na mtoto wa miaka sita hivi akaniomba pesa. Huwa nawakanya watoto wasiwe na tabia ya kuomba pesa kwa wapita njia ili kulinda usalama wao. Hata hivyo kwa leo ninakiuka taratibu zangu mwenyewe na kufanya naye majadiliano yafuatayo:

"Unataka pesa za nini?"
"Za kununulia pipi."

Hapo nilifungua mfuko wangu na kutoa kipande cha chokoleti kilichochanganywa na karanga. Alipofungua kifungio naamini ile taswira ya alichokiona ilimfanya asite kidogo akaniuliza:

"Hiki ni nini?"
"Kula tu ni tamu sana."

Alivyoonja alicheka ghafla akiwa na furaha isiyo na kifani halafu akaniambia: "Uwe unapita hapa kila siku!"
Alipofungua chokoleti alisita kuila.
Alinisababisha mimi pia kucheka.

Taarifa inayofuata: Naagiza chipsi mayai

sehemu ya tatu ya makala hii

Wednesday, September 24, 2014

Mila na tamaduni: Watanzania ni wakarimu (sehemu ya tatu)

Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.

Jiunge nami kwenye sehemu ya tatu ya msafara huu...

Agosti 3
Mapema asubuhi nilianza safari yangu ya baiskeli ya kurudi Butiama kwa kuelekea kwenye kivuko cha Rugezi na ni leo ndiyo iliyodhihirisha kwangu kuwa Watanzania bado watu wakarimu. Nilipovuka upande wa pili kwenye mji mdogo wa Kisorya, nilisimama kwa muda kwenye mgahawa kuongeza mlo wa asubuhi wa chapati mbili na chai, ingawa ilikuwa inakaribia saa tano asubuhi.

Nikiwa na uhakika kidogo wa kuendelea na safari yangu mpaka njaa itakaponilazimisha kusimama na kula chakula cha mchana, nilianza safari ya kuelekea Kibara. Hata hivyo haikuchukuwa muda nikalazimika kusimama kutafuta chakula kwenye kijiji kilicho njiani.

Pembeni yangu niliona jengo linafanana na mgahawa. Alitokeza binti mmoja na mazungumzo yakawa hivi:

"Una chakula?"
"Ndiyo"
"Chakula gani?"
"Chai na chapati"
"Mimi nimeulizia chakula, siyo chai."
"Samahani, nina chai na chapati tu."

Niliendelea kudadisi:

"Kwani wewe mchana huli chakula?"
"Nitakula.
"Unapika nini?"
"Ugali na dagaa."
"Basi ongeza na cha kwangu halafu nitakulipa."

Akakubali. Chakula kilipokuwa tayari akanikaribisha kwenye mgahawa wake, akanipa maji ninawe na yeye akanawa tukakaa pamoja kula.
Niliegesha usafiri wangu, nikapiga picha, halafu nikaingia kusubiri chakula.
Wakati nakaribia kushiba nikapata nguvu za kuongea kidogo na kumwomba radhi kuwa nimempunguzia chakula chake kwa siku hiyo. Aliniambia nisijali, na kuwa labda kuna siku na yeye atanitembelea na mimi nitamkaribisha chakula.

Nikijiandaa kuondoka nilimuuliza nimlipe kiasi gani kwa kile chakula. Alinishangaa na kuniambia: "Wewe si nilikwambia kuwa hakuna tatizo? Pesa za nini?"

Nikabaki hoi. Lakini nilifungua mfuko wa baiskeli yangu na kutoa pakiti ya biskuti nikampa na kusema ni zawadi kwa watoto wake. Alifurahi sana na kuniuliza bei ya biskuti zile. Nilimwambia shilingi elfu tatu nikapanda basikeli na kuanza safari ya kuelekea Kibara.

Vijijini wema huu bado upo. Sina hakika kama mijini hali imebakia hivi.

Taarifa ijayo: Hiki ni nini?

Sehemu ya pili ya makala hii

Saturday, September 6, 2014

Mila na tamaduni: Watanzania ni wakarimu (sehemu ya pili)

Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.

Jiunge nami kwenye sehemu ya pili ya msafara huu...

Agosti 2
Tulitembelea makazi ya kwanza walipofikia Wakristu wa kwanza kutua kwenye kisiwa cha Ukerewe zaidi ya miaka 100 iliyopita. Hakuna maelezo mengi sana kuhusu eneo hili ila simulizi za mauaji yaliyofanyika hapo dhidi ya baadhi ya wageni hao na mtawala wa eneo hilo wa wakati huo. Ni eneo ambalo liko kwenye kilima chenye mwinuko mkubwa unaowezesha kuona umbali mkubwa juu ya Ziwa Viktoria. Mwenyeji wangu aliniambia kuwa nyakati ambapo hakuna ukungu yawezekana kuona ndege zikipaa na kutua kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza.
Ukerewe ni kisiwa chenye mandhari za kuvutia na visiwa vingi vinavyokizunguka. Upande wa kulia wa picha kinaonekana kisiwa cha Bwiru.
Baada ya hapo tulitembelea eneo la ufukweni wa ziwa ambapo mjasiria mali mmoja wa Nansio, makao makuu ya wilaya ya Ukerewe, anajenga hoteli itakayozingatia utunzwaji wa mazingira wa eneo hilo.

Taarifa ijayo: Watanzania ni watu wakarimu

sehemu ya kwanza ya makala hii
sehemu ya tatu ya makala hii

Saturday, August 23, 2014

Mila na Tamaduni: Watanzania ni wakarimu (sehemu ya kwanza)

Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.

Jiunge nami kwenye msafara huu...

Agosti 1
Safari yangu ilianzia Mwanza kwa kuvuka na meli iitwayo MV Clarias kuelekea Nansio, Ukerewe. Huko nilipokelewa na muongozaji wageni maarufu wa kisiwa cha Ukerewe, Tumaini Yohana Ladislaus ambaye ni mmiliki wa Tumaini Tours.
Muda mchache kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ukerewe kutokea Mwanza.
Siku ya kwanza alinipeleka kwenye makazi ya Mtemi Gabriel Ruhumbika, kwenye kijiji cha Bukindo ambako tulipata maelezo mafupi ya historia ya eneo hilo kutoka kwa mmoja wa waongozaji anayepokea wageni katika makazi hayo. Mtemi Ruhumbika ni baba mzazi wa Mtemi Michael Lukumbuzya ambaye alishika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwa ni pamoja na kuwa balozi wa Tanzania nchini Canada.
Muongozaji wageni akitoa maelezo ya picha mbili za Mtemi Michael Lukumbuzya.
Tulipotoka hapo tulielekea kwenye kijiji cha Murutunguru. Hapa ilikuwa sawasawa na kufungua kurasa za kitabu cha watu mashuhuri. Niliambiwa hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa mkuu wa walinzi binafsi wa Rais Julius Kambarage Nyerere; hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Gertrude Mongella; hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania, Pius Msekwa, na kadhalika, na kadhalika. Na ni hivyo hivyo katika sehemu nyingi ya kisiwa cha Ukerewe.

Inasemekana Ukerewe ndiyo eneo lenye mkusanyiko mkubwa zaidi kwa kilomita za mraba za wasomi wa shahada za uzamivu kuliko sehemu yoyote ile Tanzania, na pengine hata Afrika.

Itaendela na: Mjasiriamali wa Ukerewe

sehemu ya pili ya makala hii

Tuesday, July 29, 2014

Mwisho wa Tanzania siyo Kibaha

Kuna watumishi wengi katika sekta ya umma na ya binafsi ambao kwao Tanzania ni Dar es Salaam. Sisi tunaoishi bara hatuna tofauti na kuwa wakazi wa Kandahar nchini Afghanistan.

Nitatoa mifano. Jana nilitaka kukamilisha usajili wangu wa shahada mojawapo ya chuo kikuu kimojawapo cha Tanzania. Waliopitia zoezi hili wanafahamu kuwa maombi yote yanafanyika kwenye mtandao. Ukikwama wakati wa kujaza maombi zimetolewa namba za simu ambazo unaweza kupiga kupewa maelekezo. Nilikwama mapema kwa sababu nina stashahada ya nje ya nchi ambayo mchakato wa maombi hauitambui. Nilipiga simu hizo kwa muda mrefu lakini au hazipokelewi au haziko hewani.

Bahati nzuri nilipata namba nyingine ya Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU) ambayo nilipiga na kuunganishwa na mama mmoja. Nilimueleza tatizo langu. Akaniambia kuwa TCU bado haijakamilisha tathmini ya shahada za nje na kwa hiyo nilipaswa kupeleka shahada yangu “ofisini” ili ihakikiwe.

Nilimwambia kuwa mimi niko Musoma. Akanijibu: “Sasa mimi nifanyeje?” Ilikuwa ni kama vile ananieleza: “Nani kakutuma kuishi bara?”

Sifahamu kama watu wanaopanga taratibu mbovu kama hizi wanatambua kuwa safari kutoka baadhi ya sehemu za Tanzania ni zaidi ya kilomita 1,000 hadi Dar es Salaam na inagharimu pesa. Hawa wanatoa majibu kama vile Watanzania wote milioni 45 wanaishi Dar. Naamini kuna makumi ya maelfu ya waombaji wa kusoma kwenye vyuo vikuu ambao hawako Dar. Kwanini inashindikana kuwepo mwakilishi wa Kanda ili mimi niliye Butiama nisilazimike, mathalani, kusafiri hadi Dar kuhakiki cheti changfu? Ingetosha kusafiri hadi Mwanza tu, ingawa wakati mwingine hata Mwanza pia naona ni mbali ambako ingewezekana kupanga muda maalumu wa kuonana na huyu mhakiki na gharama yake kujunuishwa kwenye gharama ya maombi. Ongezeko la gharama hii haitazidi gharama za kusafiri kwenda Dar.

Ukweli ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa raia wake wote wanapata huduma kwa haki na usawa ule ule. Ningekuwa na muda (na pesa) ningefungua kesi mahakamani kudai kukiukwa kwa haki zangu za msingi kama raia ambaye anastahili kupata huduma ile ile ya umma kama raia anayeishi Dar es Salaam.

Mfano mwingine, na hapa nasisitiza kwa nini nimesema kuwa hata Mwanza ni mbali, unahusu kampuni za simu. Kuna aina nyingi za matatizo ambayo yanaweza kumalizwa kwenye simu, lakini baadhi ya watoa huduma za kampuni za simu watakwambia unapaswa kwenda kwenye ofisi zao ili kutatua shida fulani.

Nagombana mara kadhaa na watoa huduma wa kampuni ya simu ya Voda. Watoa huduma wa Voda wanayo sentensi wanayopenda sana kutumia kumaliza tatizo: “Nenda Voda Shop.” Mimi kwenda Voda shop iliyo karibu ni kilomita 80 (kwenda na kurudi). Mimi nilifikiri maana ya kuwa na simu ni kupunguza ulazima wa kufunga safari zisizo za lazima, na kuongeza ufanisi katika kazi. Ukiniambia niende Voda Shop napoteza siku nzima ya kazi bila sababu ya msingi.

Halafu siku ukitoa takwimu kuwa una wateja milioni 10 na mimi pia utanihesbau katika usawa ule ule na mteja wa Dar es Salaam wakati mimi nalazimika kulipia gharama za ziada ili kutumia huduma yako?

Nasema haya siyo kwa kukosoa tu bila sababu ila kwa kutoa hoja kuwa kuna baadhi ya taratibu zinapaswa kupitiwa upya ili kutoa huduma sawa kwa mteja wa Butiama kama ambavyo anafaidika mteja wa Dar. Kuna ukweli kuwa foleni za Dar zinaweza kusababisha hata mkazi wa Dar kuona kuwa safari ya kwenda Voda Shop badi ni kero kwake. Kama hii ni kweli, basi hata yeye ana haki ya kulalamika.

Teknolojia ina manufaa ni na ingerahisisha sana shughuli za utawala na biashara nchini lakini bado ziko hitilafu nyingi za kurekebisha. La msingi ni kuwa Tanzania ni nchi kubwa na inahitaji mtazamo huo mpana kupanga mipango ya kuhudumia raia na wateja.

Saturday, July 26, 2014

Mada yangu ya leo: siyo kila aliye chumbani amelala usingizi

Siyo kweli kuwa kila aliye chumbani amelala usingizi. Nitafafanua.

Ninapokuwa kijijini Butiama sehemu kubwa ya kazi yangu inahusu kutangaza kijiji hiki kama kivutio cha utalii wa kihistoria na kiutamaduni. Nafanya kazi hiyo kwa taarifa ninazoweka mtandaoni na kwa mawasiliano ya moja kwa moja (kwa simu na barua pepe) na wale wanaopanga safari za kutembelea Butiama.Vitendea kazi vyangu ni kompyuta ambayo ninayo chumbani kwangu, na simu. Chumba changu ni ofisi yangu. Mimi nikisema naenda ofisini inanichukua chini ya dakika moja kufika kazini, kwa sababu ni safari ya kutoka kitandani kwangu mpaka kwenye meza yenye kompyuta.

Nafahamu wataalamu wanasema zipo athari za kuweka ofisi nyumbani lakini hiyo siyo mada yangu ya leo. Ninachosisitiza sasa ni kuwa mabadiliko ya teknolojia yamerahisisha kuhama na ofisi sehemu yoyote tunayotaka. Kompyuta na simu zimepunguza ulazima wa aina fulani za wafanyakazi kuwepo ndani ya jengo mahususi ili kutekeleza majukumu yao.
Ofisini kwangu.
Kwa bahati mbaya mabadiliko haya ya teknolojia hayako wazi kwa kila mtu. Kwa wengi kazi halisi ni inayofanyika katika sehemu mahususi, mathalani shambani, kiwandani, au ofisini, na kwa kijijini inaonekana kuwa ni kazi iwapo tu inamtoa mtu jasho.

Ukijifungia chumbani (kwangu ni ofisini) kuanzia asubuhi mpaka jioni unadhaniwa kuwa umelala usingizi. Kuna siku nilisikia mgeni anaambiwa kuwa nimelala na nikalazimika kutoka ndani kumkaribisha chumbani aliyetamka maneno hayo na kumuonyesha kuwa chumbani kwangu ni ofisini kwangu.

Kama nilvyosema siyo kila aliyekuwa chumbani amelala usingizi.

Wednesday, July 16, 2014

Tujisahihishe

Watanzania tuna sifa ya kuwa waoga sana kuwasahihisha wenzetu wanapokosea. Naomba kuwa tofauti kwa leo. Na ni kwa nia nzuri tu.

Kombe la Dunia la FIFA limeisha hivi karibuni na nilisikia (kwenye redio na runinga) na kuona kwenye maandishi, haswa kwenye mitandao ya jamii, matumizi yasiyo sahihi ya majina ya baadhi ya timu zilizoshiriki kwenye mashindano hayo.

"Ujerumani" iliandikwa "Ujeruman." Na kwa Kiingereza badala ya kuandika "Germany", baadhi ya watu waliandika "German." Tatizo hili la matumizi ya lugha lisichukuliwe kuwa ni kwa lugha au majina ya kigeni pekee. Jana nikiwa kwenye ndege nilisikia mfanyakazi wa ndani ya ndege akitutangazia abiria kuwa "tumetua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerele." Huyo ni Mtanzania anashindwa kutamka "Nyerere." Na haikuwa mara yangu ya kwanza kusikia "Nyerere" kuitwa Nyerele." Kama ungeondoa muktadha ungefikiri alikuwa anazungumzia nyenyere.

Lakini jambo la kushangaza zaidi ni kuwa baada ya kutamka hivyo alianza kuongea kwa Kiingereza kutoa taarifa hiyo hiyo kwa abiria tuliokuwa ndani ya ndege, lakini alipoongea kwa Kiingereza alitamka "Nyerere" kwa usahihi.
Nilipanda ndege ya shiriki hili. Safari ilikuwa nzuri, lakini lugha ilikuwa na walakini.
Hii mifano inaashiria matatizo mawili. Kwa mfano wa kwanza ni kutojuwa matumizi sahihi ya majina au lugha ("Germany" ni nchi; "German" ni Mjerumani) au kutojali kuwa makini tunatamkaje majina au maneno (huyo huyo aliyetamka "Nyerele" anatamka "Nyerere" baada ya sekunde chache).

Nawasilisha hoja.

Sunday, July 13, 2014

Wakati mwingine picha zinadanganya

Hii (chini) ni picha ya eneo la Dar es Salaam, katika makutano ya barabara ya Bibi Titi na Mtaa wa Zanaki, ambalo kwa miaka mingi nimekuwa napita kwa mguu na ni eneo ambalo limebadilika sana katika kipindi hicho cha karibia miaka 30. 

Kushoto mwa picha hii (hapaonekani) kuna jengo kubwa lenye ofisi na maduka kwenye ghorofa za chini na nyumba za kuishi kwenye ghorofa za juu. Ni sehemu ambayo zamani waliishi Watanzania wa jamii ya Kiasia . Jengo lililojengwa hapo lilibadilisha kabisa taswira ya eneo hilo na liliongeza idadi ya majengo mapya ambayo yanachipuka Dar es Salaam kila kukicha. Majengo mengi ya zamani na ya kihistoria yanaendelea kubomolewa.


Lakini pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea kwenye baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam ninahisi kuwa picha hii haiakisi ukweli wa hali ilivyo katika eneo hilo. Ukweli ni kuwa picha hii inapamba zaidi hali halisi.

Nimeshapita kwenye eneo hili mara mia kadhaa lakini sijaona hali hiyo nzuri ambayo naiona kwenye picha hii. Kwa hakika teknolojia ya kamera imefanikiwa kupamba ukweli kwa sifa bandia.

Saturday, July 12, 2014

Wageni wa Butiama: Urmila Jhaveri

Ni Watanzania wachache wa kizazi kipya wanatambua mchango wa baadhi ya Watanzania wenye asili ya Kiasia kwenye harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Mmoja wa wanaharakati hawa ni Urmila Jhaveri ambaye hivi karibuni alitembelea Butiama.
Mama Urmila Jhaveri akiwa Butiama kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere. 
Mama Jhaveri, mwenye umri wa miaka 83 na ambaye alizaliwa kwenye kisiwa cha Pemba, ni mjane wa Kantilal Jhaveri aliyekuwa miongoni mwa wanasheria watatu wa upande wa utetezi kwenye kesi ya kashfa ya jinai ya mwaka 1958 iliyomkabili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa harakati za kudai uhuru iliyofunguliwa dhidi yake na serikali ya kikoloni ya Uingereza. Kantilal Jhaveri alifariki nchini India Januari 2014.

Wakati wa kudai uhuru wakati mume wake akiwa mmoja wa viongozi wa chama cha Waasia, Indian Association, kilichoshirikiana na kuunga mkono sera za Tanganyika African National Union (TANU), Urmila alishiriki kwenye harakati hizo akiwa mwanachama wa kitengo cha wanawake cha TANU ambacho kilijulikana kama TANU Women's Section.

Hivi karibuni amechapisha kitabu juu ya maisha yake kiitwacho Dancing with Destiny ambacho atakizindua tarehe 19 Julai  2014 jijini Dar es Salaam.

Itakuwa fursa nzuri kwa wote kukumbuka mchango muhimu wa makundi mbali mbali ya Watanzania kwenye harakati za kudai uhuru.

Sunday, May 18, 2014

Mwanza, juzi

Juzi nikiwa jijini Mwanza, mtu mmoja nisiyemfamu aliniomba pesa. Nilimjibu kuwa sikuwa na pesa za kumpa. Aliendelea kuniomba. Nilisisitiza sikuwa na pesa.

Akasema: "Du! Sasa mheshimiwa unaniacha na hali mbaya sana."

Mimi: "Vumilia. Leo huna, kesho utapata."

Yeye: "Tutafika kweli? Eti wanasema tusubiri mpaka mwaka 2025 ndiyo mambo yatakuwa mazuri kwetu sisi maskini? Tutakuwa bado tunaishi kweli?

Mimi: "Vumilia. Tutafika."

Niliondoka nikiwaza kuhusu matarajio ya raia mwenzangu kuhusiana  na Visheni ya Maendeleo ya 2025 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Ikifika tarehe 1 Januari 2026 na hali yake iko vile vile patachimbika.

Tuesday, May 13, 2014

Uandishi ni kazi kweli kweli!

Ni muda mrefu sasa sijachapisha habari zozote hapa kwenye blogu yangu. Uandishi wa mara kwa mara siyo kazi ndogo, hasa pale mwandishi anapotarajiwa kuongea jambo la maana kila wakati, na kufanya hivyo mara kwa mara.

Tatizo mojawapo linalonizuwia kuandika mara kwa mara ni kusafiri huku na kule kwa shughuli mbali mbali. Nimejenga mazowea ya kuandika nikiwa sehemu moja tu: nyumbani. Ninaposafiri sipati utulivu wa kutosha kuniwezesha kuandika vyema.

Hata hivyo naweka kando hivyo visingizio na natarajia kuanza tena kuhuisha blogu hii kwa kuweka habari hapa na maoni yangu ya masuala kadha wa kadha.