Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, April 27, 2010

Kumbukumbu ya Karume

Mapema mwezi huu Katibu Mkuu wa chama cha Wananchi (CUF) Seif Shariff Hamad alihudhuria khitma ya Marehemu Rais Abeid Karume, aliyeuwawa tareke 7 Aprili 1972.

Picha mbili za juu: Kaburi la Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyezikwa makao makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui, Zanzibar.

Khitma hiyo iliyofanyika kwenye makao makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui, Zanzibar, na ambayo ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Karume inayoadhimishwa tarehe 7 Aprili kila mwaka, ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Tanzania ikiwa ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, Rais Amani Karume wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa Rais Dk. Mohamed Shein, pamoja na Waziri Kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha.

Kabla na baada ya khitma nilishuhudia Maalim Seif akiongea kwa uchangamfu na viongozi wenzake waliyohudhuria (sehemu kubwa ya vingozi hao ikiwa ni viongozi wa CCM), kitendo ambacho kingeonekana cha kawaida kwa mgeni wa siasa za miaka ya hivi karibuni zilizosheheni uhasama mkubwa kati ya viongozi na wanachama wa CCM na CUF.

Hakikuwa kitendo cha kawaida na vichwa vya habari kuhusu siku hiyo vilizungumzia kitendo hicho cha kihistoria na ambacho kinaonekana kuashiria kufungua ukurasa mpya wa maridhiano kati ya CCM na CUF kwa upande wa Zanzibar.

Jitihada za hivi karibuni za Rais Aman Karume na za Maalim Seif kutafuta suluhu ya kipindi kirefu cha kutoelewana kati ya CCM na CUF, pamoja na jitihada za awali za kutafuta muafaka, zitaonekana kuwa ndiyo chimbuko la Maalim Seif kuonekana kwenye mkusanyiko ambao zamani ungeonekana kuwa ni wa wana CCM tu. Leo hii, Baraza la Wawakilishi limesharidhia uundwaji wa serikali ya mseto kwa Zanzibar, jambo ambalo linaweza kupunguza uhasama na kuimarisha maridhiano.

Picha: Baada ya shughuli rasmi Maalim Seif 'alivamiwa' na waandishi wa habari na kujibu maswali kadhaa.

Sunday, April 18, 2010

Wanyama waliyopo Butiama


Aina hii ya tumbili wanapatikana kwa wingi kwenye maeneo kadhaa ya kijiji cha Butiama. Makazi yao ni kwenye msitu wa Muhunda. Kila kunapopambazuka wanasambaa kwenye maeneo mbalimbali ya kijiji kutafuta chakula.


Butiama pia ni eneo ambalo lina wanyama aina ya pimbi ambao huishi kwenye maeneo yenye miamba. Pimbi ni mnyama ambaye hulia anapokabiliwa na hatari au anaposhuhudia tukio lisilo la kawaida. Miaka iliyopita kuna mtu alianguka chini baada ya kupatwa na kiharusi. Sehemu alipoanguka huyo mtu hapakuweko mtu, lakini pimbi wengi walijitokeza wakipiga makelele mpaka watu waliokuwa karibu walifuatilia chanzo cha zile kelele za wale pimbi na kumkuta yule mtu amezirai, na kumchukuwa na kumpeleka hospitali.

Halafu kuna nyoka wa kumwaga...nitaleta habari za nyoka kwenye taarifa zijazo.


Tuesday, April 13, 2010

Uchaguzi Mkuu 2010


Wageni wanaotembelea maeneo ya jimbo la uchaguzi la Musoma Vijijini wataona mabango yanayofanana na hili lililopo kwenye picha ambalo lipo karibu na kijiji cha Butiama. Kwa upande mmoja lina picha ya Mbunge wa sasa, Mh. Nimrod Mkono, na upande wa pili lina picha yake na ya Rais Jakaya Kikwete.

Mh. Mkono anatarajiwa kugombea nafasi hiyo ya ubunge kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, nafasi ambayo taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa inawaniwa pia na wagombea wawili ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa CHADEMA.

Sunday, April 11, 2010

Boti za Mwanza zinatumia barabara


Kwa watu wenye taaluma ya uandishi wa habari kuna msemo kuwa mbwa anapomuuma binadamu hiyo siyo habari, lakini binadamu anapomuuma mbwa hiyo inakuwa habari ambayo watu wanastahili kufahamishwa.

Katika pitapita zangu jijini Mwanza niliwahi kuona boti imebewa juu ya gari na hii nikaona ni habari ambayo siyo ya kawaida. Kwa hali ya kawaida ni vyombo vinavyopita kwenye maji, kama meli na pantoni, ambavyo hubeba magari.

Tuesday, April 6, 2010

Mali za Wajerumani

Kuna maeneo mengi ya Tanzania, kama hii hapa kwenye picha iliyopo karibu na kijiji cha Butiama, unapoweza kuona alama ambazo hazijulikani ni za nini. Maelezo yasiyo na uthibitisho yatolewayo na baadhi ya watu ni kuwa hizi ni alama ambazo ziliwekwa na Wakoloni wa Kijerumani waliokuwa nchini kati ya mwaka 1891 na 1919. Inasemekana waliweka hizi alama maeneo ambako walichimbia madini yenye thamani.

Alama hizi zilizopo Butiama zinaonekana ni za muda mrefu sana uliyopita. Ni alama zenye msalaba, na zinakaribiana kwa futi chache tu. Miaka michache iliyopita kwenye sehemu inayofanana na hii, ndani ya pango, watu kadhaa walikufa wakijaribu kuchimba ndani ya hilo pango baada ya kufukiwa na mawe na kifusi.

Nakumbuka kuonana na mtu mmoja jijini Dar es Salaam miaka mingi iliyopita aliyeniomba nigharamie ununuzi wa baruti kwa ajili ya kwenda kulipua eneo lililopo Kondoa ambalo yeye aliamini lilikuwa na shehena ya madini ya Wajerumani. Kama ambavyo huwa sipendi kucheza bahati nasibu, mimi sikukubali ombi lake.

Saturday, April 3, 2010

Takwimu

Iwapo dunia ingekuwa ina watu 100, tungepata matokeo yafuatayo:

Jinsia:
50 wanawake
50 wanaume

Watoto/watu wazima:
20 watoto
80 watu wazima
14 kati ya hao watu wazima watakuwa na umri wa miaka 65 na kupita

Mgawanyiko wa kijiografia:
61 watakuwa kutoka Asia
12 toka Bara Ulaya
13 toka Afrika

Dini:
31 Wakristu
21 Waislamu
14 Wahindu
6 wa dini ya Buddha
12 wa dini nyinginezo
16 wasiyo na dini yoyote

Lugha wanazoongea:
17 Lugha mojawapo ya Kichina (kichina kina michepuo kadhaa)
8 Kihindi
8 Kiingereza
7 Kihispania
4 Kiarabu
4 Kirusi
52 Lugha nyingine (pamoja na Kiswahili)

Elimu:
82 watajua kusoma na kuandika; 18 hawatafahamu

Njaa/lishe:
1 atakuwa anakufa kutokana na njaa
17 watakuwa na utapiamlo
15 watakuwa na uzito uliopindukia

Maji:
83 watakuwa na uwezo wa kupata maji safi na salama ya kunywa
17 hawatakuwa na uwezo huo

Mengineyo:
1 atakuwa na shahada ya chuo; 1 atakuwa na kompyuta; 75 watakuwa na uwezo kiasi wa kupata chakula na sehemu ya kuijikinga kutokana na upepo na mvua, wakati 25 hawatakuwa na fursa hiyo.

Taarufa kamili ipo hapa.