Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, July 30, 2010

Dk Wilbrod Slaa ahutubia Musoma leo

Dk. Wilbrod Slaa, mgombea urais aliyejitokeza kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo hii alihutubia Musoma, akiwa katika ziara fupi ya kupata wadhamini wa kutimiza masharti ya kupitishwa na Tume ya Uchaguzi kama mgombea urais wa chama chake.



Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema:
Mwalimu [Nyerere] aliwahi kusema: Ikulu si mahali pa kukimbilia....
Na mara nyingi nimesema, uraisi wa Tanzania hata nikipewa bure, siutaki kwa sababu najua uzito ulioko. Kwa sababu natambua uzito wa maneno ya Mwalimu kuwa hakuna bisahara ya kukimbilia Ikulu. Kwa sababu natambua Ikulu ni dhamana ya kuwabeba Watanzania, kuwasaidia Watanzania walala hoi, wanyonge wasiyo na sauti, kuwanyanyua na kuwapeleka kwenye neema...
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kulia, akimtambulisha mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa
Kwenye mkutano huohuo, mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema:

Watanzania wote wamepigika, na umasikini wenu umaskini wetu ndiyo umekuwa mtaji wa Chama cha Mapinduzi. Chama cha Mapinduzi kina wenyewe, na mwenyewe siyo wewe. Ni kikundi kidogo cha walaji ambao wanatumia utawala wa nchi hii kama neema kwa familia zao, na Watanzania wengine wa kawaida wakiendelea kupigika.

Dk. Slaa, kulia, akimtambulisha mgombea ubunge wa CHADEMA kwa jimbo la Musoma Mjini, Vincent Nyerere





Mabere Marando, akihutubia wakazi wa Musoma
Naye Mabare Marando aliyejiunga na CHADEMA hivi karibuni alisema:

Mwalimu [Nyerere] alituachia maadui watatu: ujinga, maradhi, na umaskini. Sasa ameongezeka adui wa nne: Chama cha Mapinduzi.

Naye Wilfred Rwakatare, mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera, ambaye alikuwa kwenye mkutano huo alisema:
Kuna mwana-CCM anaweza akanibishia kwamba kichwa kimoja cha Dk. Slaa ni sawa sawa na wabunge mia moja wa CCM?
Huu ni uchokozi, lakini hatujawasikia CCM nao kujibu mapigo. Bila shaka tutawasikia katika siku zijazo.

Thursday, July 29, 2010

Kaburi la mbaguzi nambari wani: Cecil Rhodes

Juu ya vilima vya Matopo, jirani ya mji wa Bulawayo nchini Zimbabwe, lipo kaburi la Cecil Rhodes. Anajulikana kwa sifa nyingi kwa wanaompenda, lakini anajulikana pia kama mbaguzi wa rangi wa kiwango cha juu kabisa.

Alienda kwanza Afrika ya Kusini kulima pamba lakini baadaye akavutiwa na almasi na mwaka 1871 akaachana na kilimo na kuanza kusaka almasi na ardhi. Alianza kukamata vitalu na kufanya manunuzi ya ardhi, na baadaye akaanzisha De Beers Mining Company.

Alijiingiza kwenye siasa kupitia koloni la Waingereza la Cape na alikuwa kinara wa kununua ardhi zilizosababisha kupatikana kwa maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa Waafrika kwa ajili ya shughuli zake za uchimbaji madini. Mwaka 1888, Rhodes alipeleka mawakala wake kwa Mfalme Lobengula wa Matebele (sasa sehemu ya Zimbabwe) ambao walimrubuni akaamini alikuwa akiweka sahihi mkataba wa uchimbaji wa madini wakati ukweli ukiwa alikuwa ameuza himaya yake yote kwa Rhodes.

Kwa nguvu ya Serikali ya Uingereza Rhodes aliruhusiwa kuendeleza maeneo aliyoyamiliki kwa kutumia British South African Company. Akitumia eneo alilopora kwa Mfalme Lobengula, Rhodes aliongeza udhibiti kuelekea kaskazini mpaka Rhodesia ya Kaskazini (Sasa Zambia), Nyasalaand (sasa Malawi), na Bechuanaland Protectorate (sasa Botswana). Maeneo yote haya baadaye yakawa makoloni ya Uingereza.

Uporaji wake wa ardhi ulileta shida kwa mamilioni ya Waafrika na athari zake zinaendelea mpaka leo hii kwenye baadhi ya maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na Zimbabwe.

Inasemekana kuwa mavetarani wa vita vya ukombozi vya Zimbabwe wanapinga kuwepo kwa kaburi la Rhodes na wamewahi kujaribu kulilipua kwa mabomu.

Tuesday, July 20, 2010

Makazi ya Mwalimu Nyerere Butiama (3)

Baada ya kwisha vita vya Kagera mwaka 1979, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliamua kumjengea Mwalimu Nyerere nyumba ya kuishi, ikiwa kama zawadi kwake kwa ushindi wa vita hivyo, akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa wakati huo. Nyumba hiyo, ambayo ilijengwa Butiama ilijengwa na kitengo cha ujenzi cha JWTZ.

Nyumba iliyojengwa na JWTZ inavyoonekana kwa nje

Imejengwa katika eneo la Mwitongo, karibu na eneo ilipojengwa nyumba nyingine ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na Chama cha Mapinduzi.

Sehemu ya ndani ya nyumba iliyojengwa na JWTZ

Ujenzi wa nyumba hii ulipoanza, wanajeshi walikatwa mishahara yao kuchangia gharama za ujenzi. Hata hivyo baadaye Serikali ya awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilichukuwa jukumu la kuendeleza ujenzi ambao uliisha wakati wa Serikali ya awamu ya tatu ya Rais. Benjamin Mkapa, na kukabidhiwa kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1999.

Aliishi kwenye nyumba hiii kwa siku 14 tu kabla ya kwenda kwenye matibabu Uingereza ambako alifariki tarehe 14 Oktoba, 1999.

Sunday, July 18, 2010

Makazi ya Mwalimu Nyerere Butiama (2)

Hii ni nyumba ambayo Chama cha Mapinduzi (CCM) ilimjengea Mwalimu katika miaka ya themanini. Nyumba hii ilijengwa kwenye eneo la mwinuko la Mwitongo kijijini Butiama.


Ni nyumba ambayo Mwalimu Nyerere aliishi kwa kipindi kirefu baada ya kustaafu uongozi wa Serikali akiwa kijijini Butiama.

Msanifu wa jengo hili ni mwanamama ambaye jina lake sijaweza kulipata, ambaye aliandaa pia michoro ya hoteli maarufu ya Lobo iliyopo kwenye mbuga za hifadhi za Serengeti.

Saturday, July 17, 2010

Makazi ya Mwalimu Nyerere Butiama

Hii ndiyo nyumba ya Mwalimu Nyerere aliyokuwa akifikia alipokuwa akisafiri kwenda Butiama akiwa kama Rais wa Tanzania kati ya miaka ya sitini hadi miaka ya themanini mwanzoni.

Ni nyumba ambayo ina vyumba vinne. Viongozi wenzake wa wakati huo walipomtembelea Butiama walistaajabishwa na udogo wa nyumba yake, na ndiyo wakafikia uamuzi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kumjengea nyumba nyingine kubwa zaidi ambayo ilijengwa miaka ya themanini katika eneo la Mwitongo.

Wednesday, July 7, 2010

Mada yangu ya leo: Ni nani ataibuka bingwa Kombe la Dunia?

Ni dhahiri kuwa matarajio ya mashabiki wengi wa soka Ulimwenguni, hususani juu ya matokeo ya baadhi ya mechi za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Afrika Kusini sasa hivi, hayajatimia.

Niliweka swali kwenye wavuti hii: "Timu ipi itashinda Kombe la Dunia?" Na ingawa majibu ni machache, yanaakisi yaliyokuwa matarajio ya wengi wanaofuatilia Kombe la Dunia.

Kati ya wasomaji watano wa wavuti hii, wawili walitabiri ushindi kwa Argentina, mmoja kwa Brazil, mmoja kwa Uingereza, na mmoja kwa Hispania. Timu zote hizo nne zimeshafungishwa virago kurudi makwao baada ya kufungwa na timu nyingine zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia. Timu ambazo washabiki wengi hawakuzifikiria zimebaki kwenye mashindano. Leo hii, wakati Ujerumani ikijiandaa kupambana na Hispania, ni Uholanzi peke yake iliyopata nafasi ya kuingia kwenye fainali ikisubiri mshindi wa pambano la leo.

Hoja yangu ya leo ni kuwa: utabiri wa nani anaweza kushinda mashindano ya Kombe la Dunia ni jambo gumu sana. Maradona na Argentina walikuwa wanatisha, na Brazil walipoisambaratisha Taifa Stars, tusiokuwa na uzoefu wa soka tuliamini kuwa ndugu zake Marcio Maximo wanaelekea kwenye kutwaa taji.

Lakini, kama ambavyo wataalamu wanasema, matokeo ni baada ya dakika tisini (au mia ishirini, pamoja na penalti).

Nikiulizwa sasa hivi, naitabiria Ujerumani ushindi baada ya kuona ilivyoiadabisha Argentina kwa 4-0. Nimeangalia kumbukumbu niliyonukuu miaka minne iliyopita wakati wa Kombe la Dunia. Inasema kuwa timu ya Ujerumani (ya wakati huo) bado haina wachezaji wenye uzoefu wa kutosha, lakini baada ya miaka minne itakuwa timu moja hatari sana. Hili Diego Maradona analitambua kuliko mtu yoyote.