Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, December 28, 2012

Lugha yetu Kiswahili: Kamusi ya Kiswahili kwenye mtandao

Hivi karibuni nililazimika kutafuta maana ya Kiswahili ya neno la Kiingereza dilemma na tafsiri iliyopo kwenye Kamusi ya Kiingereza - Kiswahili iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tole la 2006, imetoa neno "mtanziko."

Lakini TUKI hao hao kwenye Kamusi yao ya Kiswahili - Kiingereza, toleo la 2001, hawajatoa maana ya neno hilo kwa lugha ya Kiingereza. Inawezekana kuna toleo lijalo ambalo litaweka maana ya "mtanziko" kwa lugha ya Kiingereza.
Hali kadhalika toleo la mwaka 2004 la Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Oxford University Press nalo halina neno hilo.

Nilifanya utafiti kidogo kwenye mtandao na kugundua wavuti inayoitwa The Kamusi Project ambayo inayo kamusi ya Kiingereza - Kiswahili - Kiingereza inayoruhusu watumiaji kutafuta maana ya maneno na inaruhusu pia hata mtumiaji kuongeza maneno ambayo hayapo kwenye kamusi hiyo. Nyongeza ya maneno hupitiwa na mtaalamu na inapoonekana ni sahihi basi inaorodheshwa rasmi kwa matumizi na watumiaji wengine.

Tuesday, December 25, 2012

Mkutano wangu na Jaffar Idi Amin

Taarifa ifuatayo ni ya siku nyingi kidogo, na awali niliitoa kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza From Butiama and Beyond tarehe 15 Mei 2009. Nairudia hapa katika mfululizo wa taarifa ambazo niliwahi kuzitoa kwenye From Butiama and Beyond na ambazo naamini wasomanji wangependa kuzirudia kusoma na vilevile kutoa fursa kwa wale ambao bado hawajazisoma kuweza kutafakari niliyoyaandika wakati huo.
***************************************
Mapema mwezi Aprili mimi pamoja na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tulikuwa wenyeji kijijini Butiama wa Jaffar Amin, mmojawapo wa watoto wa kiume wa zaidi ya watoto 50 wa kiongozi wa zamani wa Uganda Idi Amin Dada.

Nakiri kuwa kabla ya ujio wake nilijikuta kwenye mtanziko mkubwa ambao ulinifanya nisite kwa muda kuendelea kuandikia kwenye blogu yangu. Sikuwa na hakika wasomaji wangu wangechukuliaje mkutano wangu na Jaffar. Unapotamka tu 'Idi Amin' basi siku zote utaibua hisia kali, na mimi niligundua hizo hisia zilikinzana na sababu nilizoona zinaafikiana na uamuzi wangu wa kukubali wazo la BBC la kuonana na Jaffar.
Karibu Butiama: Jaffar Amin (kushoto), pamoja na mimi tukiwa Butiama ndani ya nyumba ambayo Mwalimu Nyerere alijengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kumalizika kwa vita kati ya Uganda na Tanzania.
 Nilieleza sababu zangu kwenye makala niliyoandika kwenye safu yangu iitwayo Letter from Butiama. Kwa kifupi niliwjenga hoja kuwa matukio ya kale tuyaache yabakie ya kale na umuhimu wa matukio hayo unajitokeza pale tu ambapo tunahitaji kijufunza jambo kutokana na matukio yaliyopita ili tusirudie makosa ya zamani. Matukio yaliyopita yasitumike kama rungu la kuwapiga wale wa sasa ambao hawahusiki kabisa na matukio ya zamani.

Mkutano wetu na Jaffar ulijikita kwenye wazo la BBC la kuadhimisha, kwa kupitia vipindi kadhaa vya redio vilivyorushwa mwezi Aprili, kumbukumbu ya miaka 30 ya vita vya Kagera, vita kati ya Uganda na Tanzania vya 1979 - 1980. Solomon Mugera, mkuu wa Idara ya Kiswahili ya BBC, alieleza kuwa awali wazo lilikuwa mkutano wetu ufanyike Nairobi. Alibainisha ni Jaffar aliyependekeza kuwa mkutano uhamishiwe Butiama, badala ya Nairobi.

Kwa hiyo katikati ya mwezi Machi nlijiandaa kuonana na Jaffar jijini Nairobi lakini nikafahamu mwishoni kabisa kuwa mkutano ulihamishiwa Butiama pasipo kufahamishwa mapema hayo mabadiliko. Ninahisi kuwa BBC waliendelea na mipango ya kukutana Butiama bila kunifahamisha kwa kuhofu kuwa ningakataa wazo lao.

Nilipata shida kubwa sana kuorodhesha waalikwa. Ilikuwa rahisi kuamua nani kati ya marafiki zangu kuwaalika. Baadhi yao walinirahisishia kazi kwa kuniomba niwaalike. Orodha ngumu ilikuwa ile ya viongozi wa serikali wa mkoa. Sikuwa na hakika iwapo wangehudhuria ingawa hutembelea Butiama mara kwa mara. Niliwatumia mialiko na baadhi yao walihudhuria mkutano ule pamoja na Jaffar.

Mwisho wa yote inaelekea kuwa wale waliofuatilia matangazo ya maadhimisho yaliyorushwa na BBC pamoja na mkutano na Jaffar walibaki na maoni chanya tu kuhusu mkutano wangu na Jaffar. Mtoa maoni mmoja alipendekeza kuwa mtu aliyeibua wazo la kuwakutanisha watoto wa Idi Amin na Julius Nyerere alipaswa kupendekezwa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.
Solomon Mugera wa BBC akihutubia waalikwa.
Ni matumaini yangu kuwa siku Solomon Mugera atakapoinuka akiwa amevalia vazi rasmi kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mjini Oslo (pamoja na kupokea hundi ya dola milioni moja) basi atakumbuka kuniorodhesha mimi pia kwenye orodha yake ya waalikwa.w

Monday, December 24, 2012

Kuzima simu ndani ya benki ni usumbufu tu

Ukiingia benki nyingi za Tanzania utakutana na tangazo linalozuwia kutumia simu ukiwa ndani ya benki na inawezekana kuambiwa kuzima simu yako ya kiganjani ukijaribu kuitumia.

Sijaelewa mantiki ya kanuni hii. Naamini kuwa wenye mabenki wana hofu kuwa mtu mwenye kusudio la kutenda uhalifu ndani ya benki anaweza kutumia simu kurahisisha uhalifu huo. Na hii inawezekana kuwa ni kweli lakini mtu aliyekusudia kufanya uhalifu atafanya hivyo katika mazingira yoyote yale.

Hapa inaleta maana kuwa jambazi asiye na simu hawezi kutenda uhalifu. Nimewahi kumueleza mfanyakazi wa benki aliyenizuwia nisiongee na simu kuwa kuna wahalifu wengi wapo nje ya nchi ambao wanaibia mabenki kwa njia ya mtandao. Wao wameambiwa nao wazime kompyuta zao? Na yule askari mwenye silaha ambaye yuko nje ya benki kazi yake nini? Kuelekeza wateja kuegesha magari tu na kutumia mashine za ATM?

Mimi imenitokea mara kadhaa simu yangu kuita nikiwa ndani ya benki lakini mara zote hujitahidi kumaliza mazungumzo haraka ili nimalize yaliyonipeleka benki kwanza halafu ndiyo, kwa wakati wangu, nimtafute huyo aliyenipigia kumalizia mazungumzo iwapo hayakuisha.

Ingeleta maana zaidi kwa wenye mabenki kusema kuwa mteja anapoingia benki amalize yaliyompeleka benki kwanza halafu ndiyo aanze kuongea na simu kwa sababu mshika mawili moja humponyoka, lakini hoja kuwa mtu siye na simu hawezi kufanya ujambazi haina uzito wowote.

Saturday, December 22, 2012

Dk. Antipas Massawe anasema Muungano umepitwa na wakati (sehemu ya pili kati ya sehemu mbili)

Katika awamu hii ya pili ya makala yake, Dk. Antipas Massawe anaendeleza na kuhitimisha hoja kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umepitwa na wakati. Ni mawazo yake, si yangu.
*************************************
Muungano wa Tanzania umepitwa na wakati demokrasia ya vyama vingi ilipozaliwa (sehemu ya pili kati ya sehemu mbili).

Na Dk. Antipas Massawe

(inaendelea)

Kwa sehemu ya kwanza ya makala hii soma hapa:Athari ya tatu kubwa itarajiwe kujitokeza pia pale ambapo muundo wa muungano unaojumuisha serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) utakapokataliwa kama mfano wa kuigwa na hivyo kuwa hata kikwazo kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa  Bara la Afrika unaoshirikisha Zanzibar na Tanganyika. Muundo wa muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ilibidi uwe ni ule unaotarajiwa utakubalika kama mfano wa kuigwa na wengine wote kama msingi kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na hatimaye muungano wa Bara la Afrika tarajiwa. 

Vinginevyo huu muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulioundwa kwa mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) utaishia kuwa kikwazo kwa ushiriki wake kamilifu na wenye manufaa makubwa ndani ya Shirikisho la Afrika ya Mashariki  na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mfumo wa serikali moja ya Muungano ni mzuri kwani ndio wenye gharama ndogo lakini kwa Wazanzibari ambao karibu wote ni Waisilamu na Wabara ambao karibu wote ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu mfumo huu bado sio mzuri kwani utatujengea agenda za udini ndani ya demokrasia yetu ya vyama vingi na matokeo yake ni pande zote za Muungano zikijikuta kulazimishiwa serikali dhaifu na kunyimwa ile imara na kuandamwa na chuki na migogoro ya kidini kama illivyoshuhudiwa huko Zanzibar hivi karibuni. 

Mfumo huu pia sio mzuri kwani kila pande ndani ya Muungano utashindwa kubuni na kuendeleza fursa zake nyingi muhimu kwa maendeleo yake binafsi ambazo hazitaonekana muhimu katika ngazi ya Muungano. Nadhani hili ni mojawapo ya yaliyopelekea muungano wa nchi za Kisovieti kusambaratika. Ni sababu hii inaoufanya mfumo huu wa serikali moja ya Muungano kutoweza kuwa msingi mzuri wa kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mifumo ya serikali mbili kwenye muungano (ya Zanzibar na ya Muungano) na mbili (ya Tanganyika na ya Muungano) sio mizuri kwa Wazanzibari ambao karibu wote ni Waisilamu na Wabara ambao karibu wote ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu kwani katika mazingira kama hayo utakuwa ukitujengea agenda za udini ndani ya demokrasia yetu ya vyama vingi na kutuletea athari zake mbaya. Mfumo huu pia sio mzuri kwani hakuna sababu zozote za msingi na zinazokubalika na pande zote mbili husika ndani ya Muungano pale ambapo upande mmoja ukiruhusiwa kuendelea kuwa na serikali yake binafsi na upande mwingine ukinyimwa fursa kama hiyo. Ni sababu hii inaoyoifanya mifumo hii ya serikali mbili za muungano kutoweza kuwa misingi mizuri ya kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mfumo wa serikali tatu kwenye muungano (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano) sio nzuri kwani haitakuwa rahisi kujenga hoja za msingi kudhihirisha manufaa  ya kuwa na serikali ya tatu ya Muungano yenye gharama kubwa kati ya Zanzibar ambayo ni kisiwa kidogo sana ndani ya bahari ya Hindi na Tanganyika ambayo ni nchi kubwa sana ndani ya Bara la Afrika. Hata hivyo mfumo huu wa kila mhusika ndani ya Muunngano kuendelea kuwa na serikali yake ndani ya serikali ya muungano unaonekana ndio mfumo mzuri wa kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa kwani kutokana na wingi wa mataifa shiriki ndani ya muungano, ajenda za udini zitakosa fursa ya kujijenga na kukua ndani yake na kila taifa shiriki na serikali yake litaendelea kuwa na fursa ya kubuni na kuendeleza zile ajenda na sera zake binafsi za maendeleo ambazo hazionekani muhimu katika ngazi ya serikali ya muungano.

Mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Tanganyika bila ya muungano) inaonekana ndiyo  unaofaa kuzijengea Zanzibar na Tanganyika uhusiano na ushirikiano mzuri na endelevu na uliojengeka kwenye misingi imara, urafiki na ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa mawili huru na jirani. Mfumo huu wa serikali mbili bila ya muungano utazipa pande zote mbili husika fursa nzuri kwa kila moja kushiriki kikamilifu kwenye mchakato mzima wa ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa ikizingatia maslahi yake binafsi na ya wote kwa ujumla.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unaohusisha mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) umepitwa na wakati pale ilipozaliwa demokrasia ya vyama vingi na ni budi ujadiliwe upya kwa kina na mapana kuendana na nyakati tulizo nazo na mazingara ya demokrasia ya vyama vingi tuliyo nayo hivi sasa ili athari na faida zake ziweze kuonekana bayana na kuwawezesha Wazanzibari  na Wabara wengi kuweza kuamua ni mfumo upi wa ushirikiano unaowafaa kuendelea nao badala ya huu uliopitwa na wakati.

Makala inayohusiana na hii hapa:
Sehemu ya kwanza ya makala hii:
http://muhunda.blogspot.com/2012/12/dk-antipas-massawe-anasema-muungano.html
Makala nyingine juu ya Muungano:
http://muhunda.blogspot.com/2012/08/mada-yangu-ya-leo-muungano-una-manufaa_24.html

Friday, December 21, 2012

Dk. Antipas Massawe anasema Muungano umepitwa na wakati (sehemu ya kwanza kati ya sehemu mbili)


Katika makala hii ambayo nitaitoa hapa kwa awamu mbili, Dk. Antipas Massawe anatoa hoja kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umepitwa na wakati. Ni mawazo yake, si yangu.
*************************************
Muungano wa Tanzania umepitwa na wakati demokrasia ya vyama vingi ilipozaliwa (Sehemu ya Kwanza kati ya sehemu mbili).

Na Dk. Antipas Massawe

Muungano wa kisiasa kati ya Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa tarehe 26 April, 1964. Sababu kubwa iliyopelekea kuzaliwa kwake ni moyo waliokuwa nao waasisi wake (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume) wa kuunda muungano wa kisiasa baina ya nchi huru za Bara la Afrika wakianzia na shirikisho la Afrika ya Mashariki. Lengo lilikuwa kulinda na kudumisha mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 dhidi ya utawala wa wachache wa kisultani ulioondolewa madarakani na kuanzisha ujenzi wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika kisiasa.

Kuzaliwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar kulitokana na matakwa binafsi ya waasisi wake na wananchi wa kawaida kutoka pande mbili husika hawakushirikishwa kikamilifu katika zoezi zima la kufanya maamuzi kuhusu kuundwa kwake na haionekani mahali popote upembuzi yakinifu ulifanyika kubaini faida na athari za muungano wenyewe kwa wahusika (ukijumuisha mifumo ya serikali zake zote mbadala: moja (ya Muungano), mbili (ya Zanzibar na ya Muungano), tatu (ya Tanganyika na ya Muungano), nne (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano) na tano (ya Zanzibar na ya Tanganyika bila ya Muunngano). Kwa kifupi muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulizaliwa wakati wa kipindi cha udikteta wa chama kimoja tawala ndani ya pande zote mbili husika kwenye Muungano.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ni wa pekee na haujawahi kuigwa na wengine mahali popote duniani na umedumu chini ya utwala wa mfumo wa udikteta wa chama kimoja na sasa uko chini ya utawala wa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

Athari  kubwa kutokana na Muungano hazikuweza kuonekana kwenye kipindi chake cha  awamu ya kwanza chini ya mfumo wa udikteta wa chama kimoja kwani kwenye kipindi hiki chama tawala ndicho kimekuwa kikiamua yote kuhusu maswala ya Muungano kitaifa na jukumu la wengine wote kutoka bara na visiwani lilikuwa ni kubariki maamuzi hayo ya chama kimoja tawala. Kwa mfano, chama kimoja tawala kikishaamua huyu ndiye atakaeyekuwa rais wa Muungano, basi jukumu la wengine wote kutoka pande mbili za Muungano limekuwa ni kupiga kura moja ya ndio kuashiria kubariki kwao chaguo la chama hicho kimoja tawala.

Kwa hiyo kutokuwepo upinzani kutoka vyama vingine vya siasa dhidi ya udikteta wa chama kimoja tawala kuhusu maswala ya Muungano na rais mteule wa chama tawala kutokuwa na ushindani wa wagombea kutoka vyama vya upinzani imekuwa ndiyo sababu ya athari kubwa tarajiwa kushindwa kujitokeza kutokana na utekelezaji wa Muungano huu baina ya Wazanzibari (ambao karibu wote ni Waisilamu) na Wabara (ambao karibu wote ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu) na fursa iliyopewa Zanzibar ya kuendelea kuwa na serkali yake ya Zanzibar wakati Tanganyika ikinyimwa fursa kama hiyo ya kuendelea kuwa na serikali yake ya Tanganyika bila sababu zozote za msingi.

Athari ya kwanza kubwa kutokana na huu Muungano wa kisiasa baina ya Wazanzibari na Wabara inatarajiwa kujitokeza kwa nguvu kwenye kipindi chake cha awamu ya pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Kwa mfano itakapojitokeza kwamba miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais mmoja ni Mkristu na mwingine ni Mwisilamu basi itarajiwe kwamba karibu Wazanzibari wote ambao ni Waisilamu watajitokeza na kumpigia mgombea Muislamu kura ya ndio bila kuzingatia vigezo vingine vya ubora. Athari ni kwamba Muungano huu utakuwa unatujengea ubinafsi unaoambatana na agenda zenye lengo la kutujengea na kutuimarishia udini ndani ya demokrasia ya vyama vingi na matokeo yake ni Muungano kunyimwa utawala bora pale matakwa ya udini yatakapotawala chaguzi kuu za uongozi ndani ya Muungano na chuki za kidini na migogoro yake na athari zake kuanza kujitokeza  kama ilivyoshuhudiwa huko Zanzibar hivi karibuni.

Athari ya pili kubwa kutokana na huu Muungano uliowapa Wanzanzibari fursa ya kuendelea kuwa na serikali yao ya Zanzibar wakati Wabara wakinyimwa fursa kama hiyo ya kuendelea kuwa na serikali yao ya Tanganyika itarajiwe pia kujitokeza kwenye awamu yake ya pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwani sio haki Wazanzibari kufaidi kushiriki ndani ya serikali ya Tanganyika na bunge lake kupitia serikali ya Muungano na bunge lake wakati Wabara hawana fursa kama hiyo kutokana na kutoshirikishwa ndani ya serikali ya Zanzibar na bunge lake na uwezekano mkubwa wa mgongano wa maamuzi na utekelezaji wa sera za serikali ile ya Zanzibar na za ile ya Muungano.

(itaendelea...)

Ushauri wa bure kuhusu uendeshaji wa gari

Hii makala ni tafsiri ya makala yangu ya Kiingereza ambayo ilichapishwa tarehe 1 Mei 2005 kwenye makala zangu "Letter from Butiama" nilizoandika kwenye gazeti la Daily News kati ya mwaka 2005 na 20011.
*************************************************
Ikiwa habari za siasa na hususan mkutano wa wiki ijayo wa uteuzi wa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi kushamiri kwenye kinywa cha kila mtu mimi nageukia mada ambayo haihusiani kabisa na siasa, uendeshaji gari. Huu ni ushauri ambao unaweza kuutumia kukuwezesha kuendesha gari kwa usalama zaidi na kukuepusha na hali za kushtukiza, hasa pale unapokuwa kwenye masafa marefu.

Huu siyo ushauri wa juu juu kama ule wa kukutaka ukague maji ya rejeta kabla hujaanza safari. Ni ushauri ambao pengine hutafundishwa kwenye vyuo vya udereva. Huu ushauri unatolewa na mtu ambaye ameendesha gari kwa karibia miaka 25 akiwa na ajali moja tu ndogo.

Bado sijakutana na dereva ambaye anakiri kuwa yeye ni dereva asiye wa viwango. Kwa hiyo kanuni ya kwanza ya uendeshaji gari ni: kabla hata hujawasha gari ni muhimu kujiamini; usipojiamini hakuna mtu mwingine atakayekuamini. Jichukulie kama ni mwendeshaji bora kuliko wote duniani; kile unachopungukiwa utakipata kutokana na uzoefu. Lakini usichukulie huu ushauri kwa maana yake halisi, yaani neno kwa neno kwa sababu pamoja na kuwa unajiamini bado utahitaji mafunzo ya msingi ya udereva, pamoja na kuwepo ukweli kuwa kuna watu ambao wameweza kujifunza kuendesha gari baada ya kupata leseni zao.

Kanuni ya pili ni usitoe lifti kwa watu usiowafahamu, hasa wanaume. Kuna wanaume wengi zaidi wenye makusudio ya kutenda uhalifu kuliko wanawake wenye tabia za aina hiyo. Matokeo ya tafiti ulimwenguni yanaonyesha kuwa kuna wanaume wengi zaidi wanaokutwa na hatia za jinai zaidi ya wanawake. Kwa Uingereza kwa mwaka 1984 idadi ilikuwa 86%. Kama moyo wako unakutuma kuwasaidia wenye shida nashauri utoe lifti kwa wanawake tu, lakini kuwa mwangalifu na warembo. Mara nyingine, nyuma ya mwanamke mrembo anayeomba lifti hujificha mwanaume mwenye sura mbaya mwenye nia mbaya.

Ni maoni yangu kuwa mtu ambaye ni salama kabisa kumsaidia ni mwanamke mzee. Au bora zaidi, mwanamke mwenye watoto. Yumkini kuwa hata mwanamke mwenye kusudio la kutenda kosa la jinai atawaacha watoto wake nyumbani kabla ya kujaribu kuteka nyara gari.


Kanuni ya tatu: epuka kusimamisha gari kusaidia mtu ambaye anaonekana kama amejeruhiwa na umemkuta kalala barabarani. Mwezi Novemba mwaka jana, nikiwa safarini kutoka Mwanza kwenda Dodoma, nilikuta kizuizi barabarani usiku na mtu mmoja ambaye alikuwa amevaa kiraia alijitokeza akiwa na silaha ya kijeshi. Nilihisi kuwa na polisi kwa sababu hakuelekeza silaha dhidi yangu kudai nimpe pesa. Kabla sijaondoka alinitahadharisha kuwa kilomita 40 zilizobaki kuelekea Dodoma lilikuwa ni eneo la hatari na akaniuliza, "Unafahamu kanuni za kuendesha gari usiku?"

Nilimuuliza: "Kwa mfano?"
Akasema: "Kwa mfano, ukikuta mtu kalala barabarani utafanya nini?
Nikamwambia: "Nitamkwepa halafu nitarudi kesho asubuhi kuangalia kama bado yuko pale."
Akaniambia: "Endelea na safari. Unafahamu kanuni za uendeshaji usiku."

Kanuni ya nne: Endesha kwa kasi kubwa unayataka ukiwa mwenyewe. Unayo haki ya kusitisha maisha yako kama hiyo inakupendezesha lakini pindi unapokuwa na abiria kwenye gari yako basi onyesha staha kidogo kwa hulka ya kila mwanadamu ya kutaka kuishi milele. Nilivunja hiyo kanuni mara moja na sikujuta kufanya hivyo. Niliendesha gari toka Songea hadi Dar es Salaam nikiwa na abiria kwa mwendo wa kasi wakati wa ile safari. Tulipofika nusu ya safari tulifika tulisimama kwenye milima ya Kitonga kwa dakika chache kununua mahindi ya kuchoma njiani. Dakika 20 kabla ya kufika hapo tulikuwa tumepita mabasi mawili ya abiria ambayo yalipofika eneo lile lile (wakati sisi tulikuwa tumeshaondoka) yalivamiwa na majambazi yenye silaha ambayo yalimjeruhi kwa risasi aliyefika kwenye eneo wakati tukio la utekaji linaendelea.

Siku iliyofuata tuliposikia habari za lile tukio la ujambazi tuliafikiana kuwa jambo lililonisukuma niendeshe gari kwa kasi kubwa lilituokoa kuwepo kwenye shambulio lile la ujambazi.


Ni bora pengine kuongezea kuwa, wakati mwingine, uendeshaji wa kasi unaweza kutumika kuepukana na hali ya hatari (nakumbuka hii kanuni kutoka kwenye mafunzo yangu ya udereva miaka 25 iliyopita).

Thursday, December 20, 2012

Bondia Fadhili Majia kupambana kwenye mchujo wa kuwania ubingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola


Taarifa kutoka kwa Onesmo Ngowi, Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC), inaarifu kuwa bondia Fadhili Majia amepewa nafasi ya kupambana na bondia wa Ghana Isaac Quaye katika mpambano utakaoamua bondia atakayepata fursa ya kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola kwenye uzito wa Flyweight.

Taarifa kamili hii hapa:

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) imepiga kura kumruhusu bondia wa Tanzania Fadhili Majia apambane na bondia Isaac Quaye wa Ghana katika mchujo (Elimination) wa kutafuta mpinzani atakayekutana na bingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola katika uzito wa Flyweight Kevin Satchell wa Uingereza. Mpambano wa Fadhili Majia na Isaac Quaye utafanyika jijini Accra, Ghana tarehe 22, Februari 2013.

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Onesmo Ngowi ni mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola na alikuwa wa kwanza kumpigia bondia Fadhili Majia kura ili acheze na Quaye.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa bondia Fadhili Majia kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola ambayo inaziunganisha nchi zote zilizokuwa zinatawaliwa na himaya ya Uingereza.

Wakati huo huo Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola imepitisha azimio la kuruhusu ubingwa wa baraza hilo katika bara la Afrika. Ubingwa huo utakuwa unajulikana kama “CBC Africa Zone” na tayari wapo mabondia kadhaa wa nchi za Afrika ya Magharibi ambao wameshandaa mapambano mwakani.

Napenda kuwahamasisha mapromota wa Kitanzania kuchangamkia fursa hizi adimu na kuandaa mapambano ya ubingwa wa "CBC Africa Zone" kwa manufaa ya mabondia wetu.

TPBC imejiandaa kuwatafutia mabondia wa Kitanzania mapambano mengi ya nje ili waweze kujijenga kimchezo na pia kuweza kupata kipato kizuri.

Imetumwa na mimi:

Onesmo Ngowi
Rais, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC)
Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC)

Bondia Fadhili Majia kupambana kwenye mchujo wa kuwania ubingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola


Taarifa kutoka kwa Onesmo Ngowi, Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC), inaarifu kuwa bondia Fadhili Majia amepewa nafasi ya kupambana na bondia wa Ghana Isaac Quaye katika mpambano utakaoamua bondia atakayepata fursa ya kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola kwenye uzito wa Flyweight.

Taarifa kamili hii hapa:

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) imepiga kura kumruhusu bondia wa Tanzania Fadhili Majia apambane na bondia Isaac Quaye wa Ghana katika mchujo (Elimination) wa kutafuta mpinzani atakayekutana na bingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola katika uzito wa Flyweight Kevin Satchell wa Uingereza. Mpambano wa Fadhili Majia na Isaac Quaye utafanyika jijini Accra, Ghana tarehe 22, Februari 2013.

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Onesmo Ngowi ni mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola na alikuwa wa kwanza kumpigia bondia Fadhili Majia kura ili acheze na Quaye.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa bondia Fadhili Majia kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola ambayo inaziunganisha nchi zote zilizokuwa zinatawaliwa na himaya ya Uingereza.

Wakati huo huo Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola imepitisha azimio la kuruhusu ubingwa wa baraza hilo katika bara la Afrika. Ubingwa huo utakuwa unajulikana kama “CBC Africa Zone” na tayari wapo mabondia kadhaa wa nchi za Afrika ya Magharibi ambao wameshandaa mapambano mwakani.

Napenda kuwahamasisha mapromota wa Kitanzania kuchangamkia fursa hizi adimu na kuandaa mapambano ya ubingwa wa "CBC Africa Zone" kwa manufaa ya mabondia wetu.

TPBC imejiandaa kuwatafutia mabondia wa Kitanzania mapambano mengi ya nje ili waweze kujijenga kimchezo na pia kuweza kupata kipato kizuri.

Imetumwa na mimi:

Onesmo Ngowi
Rais, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC)
Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC)

Naibu Waziri atembelea Butiama, achangia utalii wa utamaduni

Naibu Waziri wa Viwanda na Bisahara, Mhe. Gregory Teu, ametembelea Butiama hivi karibuni na kutoa Shs.160,000/- kuchangia shughuli za utalii wa utamaduni zinazoratibiwa na Butiama Cultural Tourism Enterprise (BCTE).
Kutoka kushoto kwenda kulia: Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Gregory Teu, msaidizi wake ambaye jina lake haliweza kupatikana mara moja, na mimi, wakati nilipokuwa natoa maelezo ndani ya Maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo kwenye nyumba ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), eneo la Mwitongo, Butiama.
Katika ziara yake fupi aliyofanya akiwa safarini kutoka Tarime kuelekea Mwanza, Mhe. Teu alizuru eneo la Mwitongo ambalo lenye makazi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kaburi la Mwalimu Nyerere, maktaba ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, na vivutio vingine vilivyopo Mwitongo.

Friday, December 14, 2012

Francis Cheka avuliwa ubingwa wa mabara wa IBF

Kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa  International Boxing Federation (IBF), bondia Francis Cheka ambaye alitwaa unbingwa wa mabara wa IBF wa uzito wa middleweight tarehe 28 Aprili 2012 baada ya kumshinda bondia Mada Maugo, amevuliwa ubingwa huo baada ya kushiriki kwenye pambano ambalo halikupata idhini ya IBF.

Pambano lililomvua ubingwa Cheka ni aliloshiriki dhidi ya Karama Nyilawila tarehe 29 Septemba 2012.
Francis Cheka alipotwaa ubingwa wa mabara wa IBF, tarehe 28 Aprili 2012.
Taarifa fupi ya Lindsay Tucker, ambaye ni mwenyekiti wa ubingwa wa IBF/USBA imeeleza kuwa kutokana na kanuni 5.H iwapo bingwa anashiriki katika pambano ambalo halijaidhinishwa na IBF katika uzito wake, basi ubingwa wake utatangazwa kuwa wazi pasipo kuzingatia iwapo bingwa huyo ameshinda au ameshindwa hilo pambano.

Wednesday, December 5, 2012

Mtanzania Mariagoreth Ndangio afariki Uingereza, mwili wasafirishwa nyumbani kwa mazishi

Jana, tarehe 4 Desemba 2012, muda wa saa tano Watanzania waishio Luton Uingereza, ndugu na marafiki kwa ujumla walijumuika katika kanisa la Kikatoliki la Holy Ghost Westbourne, Luton, Uingereza, katika ibada ya kumuaga MariaGoreth Ndangio tayari kwa safari ya mazishi kuelekea nyumbani Tanzania.
Marehemu Mariagoreth Ndangio
Katika ibada hiyo mama mzazi wa marehemu aliwashukuru watu wote waliojitoa kwa kila hali wakati wa kumuuguza mwanae mpaka mauti ilipomkuta. Pia kaka wa marehemu alisoma historia fupi ya marehemu na kueleza upendo na ushirikiano aliokuwa nao na watu wote.

Mwili wa marehemu unatarajiwa umesafirishwa leo Jumatano kuelekea Tanzania kwa ajili ya mazishi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Luton ( Luton Tanzanian Community ) Bw. John Mbwete kwa niaba ya familia ya marehemu na Jumuiya ametoa shukurani kubwa kwa watu wote waliojitoa kwa hali na mali, Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na Tanzania Association kwa ushirikiano waliotoa katika kufanikisha safari ya mwisho ya Mariagoreth kuelekea Tanzania.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu.
Shukrani.
*******************************
Taarifa imetolewa na:
Abraham Sangiwa
Katibu – Luton Tanzanian Community ( TLC )