Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, April 26, 2012

Zawadi ya gari kwa mshindi wa pambano la ngumi za kulipwa kati Francis Cheka na Mada Maugo

Pamoja na zawadi ya fedha taslimu ambazo zitalipwa na promota wa pambano la Jumamosi tarehe 28 Aprili 2012 kati ya Francis Cheka na Mada Maugo, zawadi ya ziada ya gari imeongezwa kwa msindi wa pambano hilo.
Kushoto ni Johannes Lugenge, na kulia ni promota wa pambano, Lucas Rutainurwa, wakionyesha gari atakalozawadiwa mshindi pamoja na mkanda wa ubingwa wa IBF.

Pambano hilo la ubingwa wa mabara wa Afrika ni la raundi 12 na litafanyika kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam katika uzito wa kilo 75. Kwa mujibu wa taarifa toka kwa promota wa pambano, Lucas Rutainurwa, maandalizi yote yanaenda vizuri.

Wednesday, April 25, 2012

Mila na tamaduni

Kwa kabila la Wazanaki ilikuwa desturi kuzika kwenye eneo la nyumbani, mbele ya nyumba anayoishi mfiwa. Ni kwa kufuata mila ndiyo Mtemi Nyerere Burito alizikwa mbele ya nyumbe yake mwezi Aprili 1942. Nyumba ya mviringo inayoonekana kwenye picha ndipo ilipokuwa nyumba yake.
Kaburi la kushoto ni lake, la kulia ni la mke wake wa tano, Christina Mgaya wa Nyang'ombe na mama mzazi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hata hivyo kwa kufuata mila hizo hizo, mara tu baada ya kuzikwa wakazi wote wa makazi ya mfiwa, hasa kama ni kiongozi wa familia, huhama na kueleka kwenye makazi ambako warithi wa mfiwa waliishi. Hii ni kwa sababu kila mrithi alichukua mali alizorithi na kuhama nazo. Wakati huo, wake za mfiwa pia walirithiwa. Mtemi Nyerere Burito alikuwa na wake 22.

Mila hii ya kuzika eneo la nyumbani inaanza kupotea na kijijini Butiama yapo maeneo ya kuzika.

Sunday, April 22, 2012

Bondia Francis Miyeyusho kuzipiga Uingereza 27 Aprili

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBC) imetoa kibali kwa bondia wa kimataifa wa Tanzania Francis Miyeyusho kucheza pambano la ngumi nchini Uingereza. Miyeyusho atazipiga na bondia Luke Wilton wa Uingereza tarehe 27 mwezi huu katika hoteli ya Holiday Inn iliyo katika mtaa wa jijini Belfast, Ireland ya Kaskazini. Mpambano huo ni wa kugombea mkanda wa kimataifa wa Masters katika uzito wa Super Fly.
Miyeyusho anatarajia kuondoka nchini tarehe 22 mwezi huu siku ya Jumapili na shirika la ndege la Uingereza (British Airways).
Francis Miyeyusho ni bondia wa kimataifa aliye kwenye viwango vya mashirikisho / vyama mbalimbali ya vya ngumi duniani. Shirikisho la ngumi la Kimataifa IBF limemweka kwenye nafasi ya 5 katika orodha ya mabondia 15 bora wa mabara duniani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Francis Miyeyusho kucheza nchini Uingereza na mabondia wa huko na anatagemea kuonyesha umahiri mkubwa katika mpambano huo.
TPBC inamtakia safari njema Miyeyusho katika safari yake ya kuitangaza Tanzania katika medani ya michezo ya kimataifa.
Ikumbukwe kwamba ni Ngumi za Kulipwa pekee ambazo zimekuwa zinaig’arisha na kuitangaza vyema Tanzania katika miaka ya karibuni.
Katika mpambano huo, wimbo wa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia utapigwa mbele ya maelfu ya watazamaji pamoja na mamilioni wengine ambao watakuwa wanaangalia kwenye luninga.
TPBC imeanzisha rasmi mkakati wa kutumia mchezo wa ngumi za kulipwa kuitangaza Tanzania kama sehemu salama ya kufikia kwa watalii na wawekezaji (destination market for tourism and direct investments) "Sports Tourism" kwa maana ya "Utalii wa Michezo"
Aidha tunamuombea Mungu Miyeyusho aende salama na afanikiwe kurejea na mkanda wa International Masters nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Onesmo A.M.Ngowi
Rais,
Tanzania Professional Boxing Commission (TPBC)

Wednesday, April 18, 2012

Usafiri wa Bajaji


Hakuna ubishi kuwa usafiri wa Bajaji kwenye Jiji la Dar es Salaam ndiyo unaomuwezesha msafiri kusafiri kwa haraka zaidi kati ya sehemu moja na nyingine ya Jiji hilo.

Lakini ni usafiri wenye adha zake. Inasemekana kuwa madereva wa teksi hawafurahii hata kidogo ukweli kuwa Bajaji zimewapoka abiria kwa kiwango kikubwa kutokana na unafuu wa gharama zake na uwezo wake wa kumfikisha mteja anapokwenda kwa haraka zaidi. Kwa hiyo mteja wa Bajaji hayuko salama sana na inasemekana mara kwa mara Bajaji zinagongwa na teksi.

Aidha, inaponyesha mvua Bajaji haina kinga ya kuridhisha kwa msafiri. Hivi karibuni nikiwa Dar wakati mvua ikinyesha nilijikunyata katikati ya kiti cha Bajaji nikijaribu kujikinga na mvua iliyokuwa ikipenya pande zote mbili. Isitoshe, maji ya mvua yalianza kupenya kwenye turubai nikawa kama nimefungulia bomba kwenye bafu manyunyu. Tulipopita kwenye dimbwi la maji gari iliyotupita kwa kasi ilitumwagia maji.

Kila kizuri kina kasoro yake.
posted from Bloggeroid

Monday, April 16, 2012

Mada yangu ya leo

Nilikuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam tarehe 14 Aprili 2012 niliposikia taarifa kuwa tetemeko kubwa la ardhi lilitokea nchini Indonesia na limesababisha kuzuka kwa wimbi la Tsunami kwenye Bahari ya Hindi na kuwa wimbi hilo lilitarajiwa kufika kwenye fukwe za Afrika Mashariki jioni ya siku hiyo hiyo.

Wakazi wa Dar es Salaam walitahadharishwa kuhama maeneo yaliyo karibu na bahari, na nilishuhudia wengi wao ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa maofisini kwenye majengo yaliyopo katikati ya Jiji wakiondoka kwa wingi kwenye majengo hayo na kuelekea maeneo ambayo yangewaepusha na janga la kukumbwa na Tsunami.

Ilikuwa ni siku ya mvua kubwa, na kama ilivyo kawaida jijini Dar es Salaam inaponyesha mvua kubwa, kulikuwa na msongamano mkubwa sana wa magari katikati ya Jiji na maeneo ya Upanga, maeneo ambayo nilipita nikitembea kwa mguu. Naamini hali ya msongamano ilikuwa hivyo hivyo kwenye maeneo karibu yote ya Jiji ikiwa ni pamoja na kwenye barabara kuu zinazopita kandokando ya Bahari ya Hindi, sehemu ambayo ilikuwa na hatari kubwa zaidi kukumbwa na Tsunami.

Baadaye siku hiyo niliamini kuwa Mwenyezi Mungu ana upendeleo mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam baada ya kusikia taarifa kuwa tishio la Tsunami halikuwa kubwa kama ilivyotabiriwa awali na hatari yoyote kwa maisha ya watu na mali ilitoweka.

Ukweli ni kuwa wimbi hilo lingefika Dar es Salaam kwa kishindo kile kile tulichoshuhudia nchini Japan basi kwa hakika tungeshuhudia maafa makubwa sana. Wakazi wengi wa Jiji hilo wangekutwa ndani ya magari yao au ndani ya daladala kutokana na msongamano mkubwa wa magari ambayo yalikuwa yakisogea hatua chache tu baada ya muda mrefu.
posted from Bloggeroid

Wednesday, April 4, 2012

Pimbi wa Butiama

Mnyama anayepatikana Butiama kwa wingi ni pimbi.
Huyu mnyama ana ukubwa wa sungura na anapenda kukaa kwenye miamba.

Siyo kawaida ya wenyeji wa Butiama kula huyu mnyama lakini wachache waliowahi kumla wanasema nyama yake ina ladha ya kuku.

Ni kawaida kukuta mkusanyiko mkubwa wa kinyesi chake kwenye eneo moja, jambo linaloashiria kuwa pimbi wanayo tabia ya kutumia sehemu moja kumalizia haja kubwa.

Sent from Samsung Mobile


Tuesday, April 3, 2012

Chama cha Mapinduzi ukingoni?

Katika miaka ya hivi kariubuni Chama cha Mapinduzi (CCM) kimejikuta kikaangoni mara kwa mara kutokana na mpambano mkali wa kisiasa ambao unaletwa kwake na vyama vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Sasa dalili zinaonyesha CCM inaelekea ukingoni.

Kwenye kura zilizopigwa tarehe 1 Aprili 2012, CCM kimeshindwa kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru lililoachwa wazi kutokana na kifo cha mbunge wake, Jeremiah Sumari, ambaye alikuwa mwanachama wa CCM.

Kwamba wapiga kura walewale waliyomchagua mwanachama wa CCM kuwa mbunge wao mwaka 2010 wameamua sasa kuchagua mgombea wa CHADEMA ni ishara dhahiri kuwa CCM inaendelea kupoteza imani ya Watanzania wengi.

Ni mwanzo wa mwisho wa CCM kama chama tawala? Tuanze mazoezi ya kumwita mwanachama wa chama cha upinzani “Mheshimiwa Rais”? Jibu litategemea iwapo CCM kitajiangalia upya na kuirejesha misingi ambayo ilikifanya kuwa chama kilichopigania maslahi ya wakulima na wafanyakazi. Baada ya hilo, itategemea kwa kiasi kikubwa nani atateuliwa na CCM kuwa mgombea wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2015.

CCM wakiendelea na muenendo wao wa sasa, muda si mrefu watahamia kwenye benchi za upinzani bungeni.

Sunday, April 1, 2012

Wageni wa Butiama

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Rwamkoma, kijiji kilichopo jirani na Butiama, walitembela Butiama hivi karibuni na kuzuru kaburi la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililopo kwenye makazi yake eneo la Mwitongo.
Picha inaonyesha wanafunzi hao wakiwa mbele ya hilo kaburi.