Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, June 22, 2015

Utamaduni wa utoaji majina miongoni mwa kabila la walango wa Uganda

Nimepata fursa hivi karibuni ya kuonana tena na mmoja wa watoto wa kiume wa rais wa zamani wa Uganda, Apollo Milton Obote na tuliongelea utamaduni wa kutoa majina kwa kabila lao la walango.

Nilipenda kufahamu kwa nini jina lake halina ubini wa baba yake, Obote. Yeye anaitwa Eddy Engena-Maitum, na ni askofu wa kanisa la Bright Morningstar Ministry. Alinijibu kuwa kwa mila na desturi za kabila lao, kila mtoto anayezaliwa anapewa majina yake bila kuweka jina la baba mzazi. Alifafanua kuwa majina yote ya baba yake ni yake, hakutumia ya baba yake (babu yake Eddy).

Mdogo wake naye anafuata utaratibu huo huo: ni Jimmy Akena, ambaye ni mwanasiasa na rais wa chama cha Uganda Peoples' Congress. Aidha, ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika 2017. Alipomuoa mbunge mwenzake Betty Amongi mwaka 2013 Rais Yoweri Museveni alihudhuria harusi hiyo.

Mimi (kulia), nikiwa pamoja na Askofu Eddy Engena-Maitum jijini Kampala hivi karibuni.
Eddy anafafanua kuwa zipo faida na hasara za kutotumia ubini wa baba yao. Wakati mwingine akijitambulisha kama mtoto wa Milton Obote wale wasiomfahamu humtilia shaka wanapoona kuwa jina lake kamili halina jina la baba yake. Faida ni kuwa pale inapokuwa siyo lazima kujitambulisha hivyo inampa fursa ya kubaki bila utambulisho huo ambao, kwa watoto ambao wazazi ni wanasiasa inaweza kuwa ni jambo linalozua hisia tofauti kwa wanaobaini hali hiyo. Inaweza kutokea kubebeshwa kesi ambayo siyo yako.