Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, April 30, 2013

Bara la Afrika lapewa sauti kwenye tamasha la filamu la nchini Ubelgiji, Afrika Filmfestival

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu nilihudhuria tamasha la filamu nchini Ubelgiji linalojulikana kama Afrika Filmfestival.

Ni tamasha linalofanyika kila mwaka na huhusisha kuonyeshwa filamu nyingi kuhusu bara la Afrika zinazoonyeshwa ndani ya kumbi mbalimbali zilizopo kwenye miji kadhaa ya nchini Ubelgiji.
Bango la Afrika Filmfestival la mwaka huu. Picha: Lilian Nabora. Picha zaidi za Afrkia Filmfestival zinapatikana hapa:  https://www.facebook.com/media/set/?set=a.440201782735019.1073741834.199073470181186&type=1
Madhumuni ya tamasha hilo ni kutoa fursa kwa Waafrika wenyewe kuizungumzia Afrika kwa njia ya filamu za kubuni na zisizo za kubuni. Ni dhahiri kuwa watengeneza filamu wasio Waafrika hawalioni bara la Afrika kwa mtazamo ule ule ambao mzaliwa wa bara hili anaweza kuwa nao. Na aghalabu, mtazamo wa wasiyo Waafrika kuhusu bara la Afrika huwa mara nyingi unatoa taswira ya bara lenye matatizo mengi pasipo mafanikio, jambo ambalo siyo kweli.

Kwenye tamasha la mwaka huu baadhi ya filamu kutoka Tanzania zilizoonyeshwa ni pamoja na The Teacher's Country, filamu isiyo ya kubuni na ambayo nimeshiriki kama mmojawapo wa Watanzania wanne wanaotoa maoni yao kuhusu miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.

Bara la Afrika linapata fursa ya kujisemea nchini Ubelgiji kila mwaka kupitia Afrika Filmfestival.

Thursday, April 25, 2013

Wageni wa Butiama: Selma James

Miaka kadhaa iliyopita, Selma James, mkazi wa London Uingereza, alitembelea Tanzania. Yeye na wenzake walipofika Butiama niliwauliza sababu iliyowafanya waamue kutembelea Butiama. Walisema walisoma maandishi mablimbali ya viongozi wa dunia lakini hawakuwahi kusikia kiongozi hata mmoja akitamka umuhimu wa wanawake katika maendeleo ya nchi, kwa hiyo walikuwa na shauku kubwa ya kutembelea sehemu alikotoka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwenye Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere alisema haya kuhusu wanawake:
Ingefaa kuwauliza wakulima wetu, hasa wanaume, ni saa ngapi za juma na majuma mangapi kwa mwaka wanafanya kazi. Wengi hawafanyi kazi hata kwa nusu ya saa ambazo mpokea mshahara anafanya. Ukweli ni kuwa kwenye vijiji wanawake wanafanya kazi ngumu sana. Nyakati nyingine wanafanya kazi kwa saa 12 au 14 kwa siku. Wanafanya kazi hata siku za Jumapili na za sikukuu. Wanawake wanaoishi vijijini wanafanya kazi ngumu kuliko mtu mwingine yeyote Tanzania.  Lakini wanaume wanaoishi vijijini (na baadhi ya wanawake mijini) wako likizo kwa nusu ya maisha yao. Nguvu ya mamilioni ya wanaume kwenye vijiji na maelfu ya wanawake mijini ambazo kwa sasa zinapotezwa kwenye udaku, dansi na kunywa, ni hazina kubwa ya nchi ambayo inaweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu zaidi ya ambavyo tunaweza kupata kutoka mataifa tajiri.
Haya ndiyo maneno yaliyomvutia Selma na wenzake kutembelea Butiama.

Selma James ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake, ni mwandishi mwenza wa kitabu The Power of Women and the Subversion of the Community, ni mmoja wa waasisi wa International Wages for Housework Campaign, na ni mratibu wa Global Women's Strike.

Selma ni mke wa mwanaharakati mashuhuri kutoka Trinidad, C.L.R. James, ambaye aliandika vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na The Black Jacobins.

Baada ya ziara yao ya Butiama, mwaka 2007, nilipata mualiko kutoka kwao kuhudhuria hafla jijini London ya uzinduzi wa Azimio la Arusha, tukio lililohusisha pia kuchapishwa kijitabu kidogo kuhusu Azimio la Arusha kikiwa na makala yangu na ya Selma James, pamoja na Azimio la Arusha lenyewe.
Selma James, kushoto, na mimi jijini London, Uingereza, mwaka 2007.
Baada ya kustaafu urais Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa inahitaji wendawazimu kidogo kulizungumzia Azimio la Arusha kwa wale wanaoamini kuwa bado lina manufaa. Selma na kundi lake waliamini kuwa Azimio la Arusha bado lina umuhimu mkubwa na linapaswa kufahamika kwa walimwengu.

Na kwa machache niliyoyasikia kutoka kwenye Tamasha la Tano la Kigoda cha Taalum cha Mwalimu Nyerere mapema mwezi huu, yaelekea kuwa kuna wengi ambao wanaamini kuwa Azimio linayo misingi muhimu ambayo yapaswa kuzingatiwa leo hii.

Wednesday, April 24, 2013

Mada yangu ya leo: Ukiritimba wa Tanzania ni kikwazo kwa maendeleo

Mojawapo wa vikwazo vikubwa kwa utendaji kazi Tanzania ni ukiritimba. Ni janga la Taifa, nadiriki kusema. Nimeshuhudia katika siku chache zilizopita tatizo hili kwenye taasisi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Nilimsindikiza mwekezaji mmoja kwenye ofisi ya kanda ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuwasilisha maombi ya kusamehewa malipo ya kodi ya nyongeza ya thamani kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji. Taratibu zinataka muombaji afuate hatua hizi:

1.       Achukue ankara kwa muuzaji wa bidhaa ambazo zinaombewa msamaha
2.       Ajaze fomu maalumu ya maombi ya kusamehewa kodi ya nyongeza ya thamani
3.       Awasilishe katika ofisi ya Mamlaya ya Mapato Tanzania fomu (kwenye mkoa ambako mradi unaendelezwa) ili idhini ya kusamehewa kodi itolewe; na
4.       Arudi kwa muuzaji na kulipia bidhaa bila kodi na kuchukuwa hivyo vifaa

Tatizo liko katika ngazi nyingi. Kwanza, taratibu zote za kuomba misamaha ya kodi au zinafanyika Dar es Salaam au kwenye makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania, au kwenye ofisi za kanda za kituo cha uwekezaji. Ofisi hizi za kanda siyo nyingi kwa hiyo, kwa mwekezaji ambaye hayuko Dar es salaam au jirani na ofisi za kanda,  inamlazimu aingie gharama kubwa ya kusafiri mara kwa mara kati ya eneo la mradi kwenda kwenye maeneo hayo ambapo maamuzi ya kusamehewa kodi yanachukuliwa.

Si hivyo tu, lakini kwa mwekezaji ambaye hayuko Dar es salaam au jirani na mji mkubwa hulazimika mara kwa mara kupata mahitaji ya vifaa vya ujenzi kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania. Mathalani, kwa mwekezaji aliyeko Butiama, anahitaji kusafiri mara kwa mara kwenda nje ya mkoa wa Mara kununua vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mwanza na Dar es Salaam.

Tatizo la ukiritimba, ambalo wapanga taratibu wa Dar es Salaam (na watunga sheria wa Dodoma) huwa hawalioni, ni hili na linaonekana vizuri kwa mfano halisi wa namna ambavyo mwekezaji wa Butiama anapaswa kupata msamaha wake wa VAT:

1.       Anasafiri kwenda Mwanza au Dar es Salaam kupata ankara ya vifaa ambavyo anataka kununua. Nasisitiza kuwa analazimika kusafiri kwa kuwa tunafahamu kuwa, tofauti na nchi zilizoendelea, kwetu ni muhimu kuona vifaa kabla ya kuvinunua.
2.       Anajaza fomu ya kuomba msamaha wa kodi na kuiwasilisha kwenye ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya Mkoa wa Mara, na kupewa idhini. Ofisi ya mkoa pia ina jukumu la kukagua mradi na kuhakikisha kuwa unaendelezwa.
3.       Anarudi Dar es Salaam au Mwanza kulipia vifaa bila malipo ya kodi, na kuchukuwa vifaa.

Jambo ambalo nimejifunza ni kuwa hali ya kutoaminiana kati ya ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ngazi mbalimbali (makao makuu na mikoani) ndiyo inayosababisha hizi taratibu za ajabu za kufanya muombaji alazimike kwenda Dar es Salaam au Mwanza mara mbili ili kukamlisha mzunguko wa manunuzi na kupata msamaha wa kodi.

Nilimuuliza Meneja wa Mkoa wa TRA Mwanza: “Hivi usingeweza kumpigia simu meneja mwenzako Musoma na kupata uthibitisho kuwa mradi huu ni halali na unaendelezwa Butiama?”

Alinijubu kuwa, kwanza, sheria na kanuni haziruhusu. Mwekezaji anatakiwa apate barua ya Mkuu wa Wilaya alipo (kutihibitisha uwepo wa mradi katika wilaya yake) ambayo inapaswa kuwasilishwa kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato ya Mkoa, na jalada la mwekezaji kufunguliwa likiwa na orodha ya vifaa vilivyoruhusiwa msamaha wa kodi. Halafu, kila mwekezaji anapofanya manunuzi ofisi ya TRA Mkoa itapunguza vile vilivyonunuliwa. Aidha, ofisi hiyo tu ndiyo yenye mamlaka ya kufanya ukaguzi wa mradi kuhakiki vifaa visitumike tofauti na ilivyoombwa na mwekezaji.

Meneja huyo wa Mwanza alinitolea mifano kadhaa ya wawekezaji wasiyo waaminifu ambao walipewa misamaha ya kodi lakini hawakuwa na miradi yoyote ya uwekezaji waliyoendeleza, na badala yake wakatumia vifaa vilivyosamehewa kodi kwa matumizi mengine. Alimalizia kwa kusema: “Unajua watu wamekuwa wadanganyigu sana siku hizi kwa hiyo lazima kuchukuwa tahadhari.”

Nilimuuliza iwapo taratibu zote zimekamilishwa, kwanini ofisi yoyote ya TRA katika mkoa wowote wa Tanzania isiweze kuwasiliana na ofisi ya TRA iliyopo kwenye mkoa wenye mradi ili kutihibitisha  uwepo wa mradi ili kumpunguzia mwekezaji ambaye ni mwaminifu safari ya nenda rudi ili kukamilisha mzunguko. Bado hakuona kuwa ni tatizo ambalo mamlaka inapaswa kusumbuliwa nalo na kwake yeye tatizo la msingi lilikuwa kudhibiti wasiyo waaminifu bila kujali athari kwa wale waliyo waaminifu.

Kwa maoni yangu tatizo la kudhibiti uhalifu linagubikwa pia na uvivu wa kufikiri mbinu za kudhibiti wahalifu. Kwa hiyo linapoonekana tatizo, uamuzi unakuwa kudhibiti utendaji badala ya kurahisisha utendaji. Sasa hivi Tanzania ina Mkongo wa Taifa ambao ungeweza kutumika vizuri kufanya mawasiliano kati ya ofisi za TRA za mikoa ili taarifa muhimu za wawekezaji ziweze kupatikana kwenye ofisi yoyote ya TRA nchini.

Si hivyo tu, kompyuta zimejaa kwenye maofisi ya Tanzania. Zinatumia kwa ajili ya nini? Nimeshuhudia kwenye maofisi kadhaa hutumika kisikilizia nyimbo za kwenye CD na kuangalia televisheni. Nina hakika pia hutumika kwa ajili ya Facebook, Twitter, na shughuli nyingine za mtandao ambazo kamwe haziwezi kumpunguzi bugdha mwekezaji anayejaribu kuomba msamaha wa kodi ya nyongeza ya thamani.

Nilimwambia yule meneja wa Mwanza kuwa iwapo polisi wa Tanzania wangekuwa wanafanya kazi kama TRA, basi hali ya uhalifu ingekuwa mbaya kuliko ambavyo ilivyo sasa. Kwa sababu Mtanzania angetenda uhalifu Butiama akahamia Kibondo akiwa na uhakika kuwa polisi wa Kigoma wakimwona watasema kuwa siyo kazi yao kumkamata kwa sababu kosa limefanyika kwenye Mkoa wa Mara. Kwangu mimi  TRA ni chombo cha kitaifa na huduma yao haiwezi kuishia ndani ya mipaka ya mikoa. Ama sivyo tuambiwe sasa kuwa Chama cha Mapinduzi kinaanza kutekeleza sera za CHADEMA kwa kupitia njia za panya.

Nilijaribu kueleza kwa meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwenye ofisi yao ya kanda iliyopo Mwanza adha hii ya ukiritimba, na hasa kufanyika Dar es Salaam kwa maamuzi ya masuala mbali mbali. Kwa maoni yake (na baadhi ya sheria zinaelekeza hivyo) kuna maamuzi mengi ambayo yanaweza kuidhinishwa na maafisa mahususi tu ambao wako Dar es Salaam.

Nilimkumbusha kuwa kuna maelfu wa maafisa hapa nchini wanaotekeleza majukumu kwa niaba ya rais kwa hiyo labda umefika wakati kupitia upya sheria na kuangalia uwezekano wa kukaimishwa kwa baadhi ya maamuzi yanayokwamisha utendaji.

Kuacha Mamlaka ya Mapato, ipo mifano mingine mingi kwenye taasisi nyingine ambayo nayo inaathiri utendaji katika sehemu mbalimbali za nchi. Mfano mmojawapo ni huduma za kampuni za simu. Ni mara kadhaa nimepiga simu kwenye kitengo cha huduma kwa wateja katika mojawapo ya kampuni za simu kulalamikia huduma fulani nikaambiwa: “njoo ofisini.” Hawa waliyoniambia “njoo ofisini” hawakuwa na ofisi Musoma, kwa hiyo “njoo ofisi” kwangu inamaanisha “njoo/nenda Mwanza”, safari ya kilomita 190.

Tatizo la vitengo vya huduma kwa wateja kwenye kampuni hizi za simu ni kuwa wanapaswa kuwa na watu wenye uwezo wa kutoa maelekezo kutatua tatizo kwa njia ya simu, lakini labda kwa kutokuwa na watu ambao wamepewa mafunzo ya kutosha, wanaposhindwa kumaliza tatizo lako wanasema: “njoo ofisini.”

Tanzania ina watu wengi kuliko wanaoishi Dar es Salaam. Hili likizingatiwa, matatizo mengi ya ukiritimba yatapungua.

Taarifa nyingine zinazofanana na hii:

Monday, April 22, 2013

Safari hii Bunge limepata wabunge

Yaliyotokea bungeni hivi karibuni yanashangaza kidogo. Hapana, yanashangaza sana.

Baadhi ya wabunge wameamua kuvua majoho ya staha na heshima kati yao na kujitwika majoho ya kejeli, na lugha ambazo hazina ustaarabu hata kidogo. Inaelekea kuwa wanasahau kuwa mamilioni ya Watanzania wanawasikia na kuyaona wanayotenda.

Aliyetoa wazo kuwa majadiliano ya bungeni yasionyeshwe moja kwa moja kwenye televisheni anaweza kuwa ana hoja nzuri. Kwa kuona malumbano na mabishano yanayoendelea bungeni wapiga kura tunaona kama vile baadhi ya kura zetu zilikwenda kusikostahili.

Wakati mwingine ukisikiliza majadiliano yanayoendelea ndani ya bunge unaweza kufikiri siyo bunge bali ni mkutano ambao hauna kanuni wala taratibu. Huyu anabishana na mbunge mwenzake, wakati mwingine anabishana na Naibu wa Spika.

Nikiwa ndani ya gari nilisikia mbunge mmoja akiongea bungeni na kushauri serikali iidhinishe ulimaji wa bangi. Mwingine tena katika majadiliano akaporomosha tusi la nguoni kwa lugha ya Kiingereza ambalo sidhani kama limewahi kutamkwa kwenye mabunge yanayotumia lugha ya Kiingereza. Mwingine (lakini huyu aliomba radhi) akamwambia mheshimiwa mwenzake kuwa yeye haongei na mbwa, bali anaongea na mwenye mbwa.

Siyo wabunge wote wanaojihusisha na hii sura mpya ya bunge lakini mtiririko huu wa matukio na matamshi yanayotoka bungeni unatishia kushusha hadhi ya bunge kama chombo kimoja muhimu katika jamii.

Baadhi ya wabunge wanapaswa kukumbushwa kuwa wanao wajibu wa kuonekana kuwa na tabia ambazo jamii inatarajia kiongozi kuwa nayo. Nayo ni pamoja na kuonyesha ustahamilivu kwa wale wanaoweza kuwa na mawazo tofauti, na hata pale ambapo mawazo yanatofautiana basi kupingana bila ya kuonyesha dharau na kejeli. Kama tutaendelea na lugha hizi bungeni basi bado kidogo tutashuhudia bunge letu linakuwa ulingo wa ngumi.

Monday, April 15, 2013

Muhunda 'aonekana' tena Butiama

Mzimu wa kabila la Wazanaki wa Butiama unaojulikana kama Muhunda 'umeonekana' Butiama siku chache zilizopita.

Taarifa kuhusu Muhunda ambazo nilizitoa kwenye makala zilizopita hizi hapa:


Kwa mujibu wa mtoa habari, Muhunda 'alionekana' jioni ya tarehe 11 Aprili 2013 jirani na eneo la msitu wa Muhunda. 'Alionekana' Butiama mara ya mwisho Julai 2011.

Sunday, April 14, 2013

Jifunze Kiswahili kwa njia ya mtandao

Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Georgia inatoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa njia ya mtandao.

Maelezo yaliyopo kwenye tovuti inayoitwa Kiswahili kwa Komputa yanaonyesha kuwa kozi hiyo ya Kiswahili inaendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu na inaelekea kuwa hufundishwa darasani pamoja na nyongeza ya masomo yaliyopo kwenye tovuti hiyo.

Mbali na kuwa Kiswahili sahihi ni "kompyuta" na siyo "komputa" na kuwa baadhi ya matamshi yaliyorekodiwa kwa njia ya sauti yanatofautiana na matamshi niliyozowea kusikia (mfano "redio" inatamkwa "radio"), tovuti hiyo bado inaweza kuwa ya manufaa makubwa na inaweza kumsaidia mwanafunzi yoyote wa lugha ya Kiswahili ambaye anafahamu vyema Kiingereza na anaweza kujifunza mwenyewe kutokana na maelezo yaliyopo.

Anwani ya tovuti hii hapa: http://www.africa.uga.edu/Kiswahili/doe/index.html

Kila mwaka wa masomo una sura sita, na kozi inakamilika kwa sura 18. Mwisho wa kila sura mwanafunzi anapaswa kufanya mtihani ambao unaweza kutumwa kwa njia ya mtandao kwa mwalimu kwa masahihisho.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/02/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2013/01/lugha-yetu-kiswahili.html

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya nne kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya nne kati ya sehemu nne)

Ikiwa kulikuwa na mchango wa serikali katika muziki, basi ulikuwa mdogo au ulikuwa ni kwa shughuli maalumu lakini si kwa kutengeneza mazingira ya kuwezesha unafuu kwa wanamuziki kwa ujumla. Idara ya Utamaduni imeendelea kupata bajeti ndogo ambayo imefanya Baraza La Sanaa La Taifa kuendelea kubaki Dar es Salaam tu, likibangaiza kuweko kwa kutegemea kutoa vibali mbalimbali kwa wasanii, na nguvu zake kuonekana Dar es Salaam tu. Na kwa kuwa hakuna Maafisa Utamaduni Mkoa, na Maafisa Utamaduni Wilaya na Manispaa wako chini ya serikali za mitaa hivyo kuwa wizara tofauti na Waziri wa Utamaduni, nguvu za serikali katika utamaduni ni 0.

COSOTA, chombo ambacho shughuli yake ilikuwa ni kulinda hakimiliki za wasanii na ambacho kilikuwa chini ya wasanii, kwa kinyemela kabisa kimerudishwa katika mikono ya serikali, lakini bado kinakusanya mirabaha 'kwa niaba ya wasanii' huku kukiwa na bodi isiyo na uwakilishi wa wasanii kuanzia 2007. Swali: utakusanyaje pesa kwa niaba yangu lakini huniruhusu kujua ni kiasi gani umekusanya, unazitumiaje na ukiulizwa unakuwa mkali!!!!!!? Kuna wasanii wamekuwa wakidai kurudishiwa COSOTA, ushauri wangu wasanii wakae wajipange  na kuelewa vizuri sheria ya Hakimiliki kabla ya kujitwishwa zigo hilo la miba.

Katika miezi sita ya mwisho ya 2012 kumejitokeza spidi kali ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato kutengeneza mazingira ya kukusanya mapato kutokana na mauzo ya kazi za muziki na filamu. Kimsingi kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi na wasanii ni wananchi pia, lakini taratibu zake ndiyo zinanipa utata, hasa pale ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa njia hii itasaidia wasanii kwa kupunguza kuibiwa. 

Sentensi hii inaonyesha wazi anayeiongelea au hajui mfumo wa biashara ya kazi muziki, au kwa makusudi anapotosha ili kuficha kitu. Wasanii wengi huwa wamekwishalipwa kwa kazi ambazo zimesambaa na ziko barabarani zinaibiwa, wanaoibiwa ni wasambazaji. Hivyo kulinda kazi hizo unamlinda msambazaji si msanii. Pia kuanza kukusanya kodi kwa kazi hizi kumepewa jina ‘kurasimishwa  kwa kazi ya usanii’. 

Kuna mabilioni wasanii wanatakiwa walipwe na watumiaji wa kazi za sanaa, kama redio na TV, mapromota, waajiri na kadhalika lakini hakuna anaeliongelea hilo wala hakuna anaetamka takwimu hizo. Kuna kazi ya kurudisha mitaala ya masomo ya sanaa mashuleni, kurudisha vyuo vya walimu wa sanaa, kurudisha maafisa utamaduni kuwa chini ya Wizara ya Utamaduni kuwawezesha kufanya kazi zao kadiri ya Sera ya Utamaduni, na mengine mengi ya aina hiyo ndiyo ningeona kurasimisha kazi za sanaa. Lakini kukusanya kodi tu kwa kazi ambazo hata hivyo mikataba yake mingi inautata na kuita urasimishaji si sahihi.

Katika nchi nyingi critics au watu ninaoweza kuwaita Kiswahili wakosoaji, huwa ni muhimu katika maendeleo ya sanaa. Watu hawa hupata heshima kutokana na kuweza kuangalia mapungufu katika kazi za sanaa na kuyasema, jambo ambalo hupelekea wasanii kujirekibisha na kutengeneza kazi bora zaidi. Hapa kwetu kutoa ushauri ni kutafuta matusi, toka kwa wasanii wenye kazi husika, vyombo vya habari na hata sehemu ya jamii. Umefika muda wahusika kuchukua uchambuzi kama changamoto za kuboresha kazi.

Niliyoyataja hapa yote yako wazi. Ninachotegemea ni kuona 2013 hatua zinaanza kupigwa kurekebisha ili wanamuziki wa nchi hii nao wapate nafasi sawa na wengine wa nchi nyingine.

John Kitime
31.12.2012
Sinza, Dar es Salaam 

Taarifa zinazohusiana na hii: