Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, May 28, 2012

Maandalizi ya kupanda Mlima Kilimanjaro mwezi ujao

Kuna maandalizi mengi muhimu katika kujiandaa kupanda mlima Kilimanjaro. Suala moja muhimu sana ni kufanya mazoezi ya kutosha kabla ya kwenda mlimani, mazoezi yanayopaswa kufanywa kwa muda wa miezi mitatu kabla ya msafara.
Kuna viatu maalum kwa ajili ya kukwea milima mirefu. Wataalamu wanashauri kuwa viatu hivyo vitumike kwanza kabla ya kuanza msafara na vivaliwe kwa muda ili mtumiaji avizowee. Kutumia viatu kabla ya msafara kunasaidia pia kufahamu iwapo havibani sana na vinamtosha mtumiaji barabara.
Nikiwa najiandaa kueleka tena Mlima Kilimanjaro mwezi ujao kwa mara ya tano nikiwa na kundi la wageni toka Marekani ambao pamoja nao tunachangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya shule ya Sekondari ya Nyegina iliyopo jirani na Musoma, nimeanza kutumia viatu hivi juma moja kabla ya kuanza msafara wa kupanda Mlima Kilimanjaro. Viatu hivi nimeshavitumia mara kadhaa kwenye misafara iliyopita ya Mlima Kilimanjaro.

Saturday, May 19, 2012

Dimpoz kuzindua 'single' yake mpya Bilicanas Dar Jumapili 20 Mei 2012

Taarifa toka Mroki Mroki zinasema kuwa msanii Omy Dimpoz atazindua 'single' yake mpya leo kwenye Klabu ya Bilicanasa ya Jijini Dar es Salaam. Picha na habari kwa hisani ya Mroki Mroki wa Digital Company & FK Blog.
BAADA ya kutamba na wimbo wake wa Nai Nai, msanii anaekuja juu kwa kasi na mshindi wa Tuzo mbili za Kili Music Award 2012, Omy Dimpoz, anataraji kuzindua 'single' yake mpya ya Baadae katika ukumbi wa Club Bilicanas jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mtandao huu wa Kijamii, meneja wa msanii huyo, Mbaruku Issa ‘Mubenga’ alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika na show itakuwa ya uhakika na ya kuvutia.

Mubenga amesema Ommy Dimpoz anataraji kuzindua wimbo huo alioufanyiwa kazi na mwandaaji wa muziki Man Water huku akkimba pamoja na mwanadada Angel.

Aidha Mubenga amesema Dimpoz atasindikizwa na wakali wa Bongo Fleva, Diamond, Ben Pol pamoja na msanii Alawi Jr pamoja na Ma DJ wakali wa Bongo kutoka kundi la Super Deejayz.

Tayari Dimpoz ameshaanza kuwasikilizisha wimbo huo baadhi ya mashabiki wake wa mikoa ya Mwanza na Moshi wakati wa Ziara ya Wakali wa Kili Music Awartd 2012 inayoendelea ambapo leo atakuwa Mbeya chini ya udhamini wa bia ya Kilimanjaro.

“Wimbo ni mkali na mashabiki wanaukubali vilivyo na tunaomba mashabiki wa Bongo Fleva make tayari kwa singo hiyo mpya itakayoanza sasa kuchezwa katika vituo vya redio na kumbi za burudani nchini kote baada ya uzinduzi huo,” alisema Mubenga.

Mubenga amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambao ni mashabiki na wapenzi wa muziki wa kizazi kipya kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Dimpoz katika uzinduzi huo wa aina yake katika Klabu ya Bilicanas katikati ya jiji la Dar es Salaam Jumapili.

Wednesday, May 16, 2012

HakiElimu yatoa zawadi ya vitabu kwa maktaba ya Mwalimu J.K. Nyerere

Asasi ya HakiElimu hivi karibuni imetoa zawadi ya vitabu kadhaa kwa maktaba ya Mwalimu J.K. Nyerere iliyopo Butiama.

Maktaba ya Mwalimu J.K. Nyerere inatunza mkusanyiko wa vitabu binafsi zaidi ya 8,000 vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambavyo alivikusanya katika kipindi chote cha maisha yake, na ipo kwenye makazi yake yaliyopo kijijini Butiama.
Zawadi ya vitabu iliyotolewa na HakiElimu katika maktaba ya Mwalimu J.K. Nyerere, kijijini Butiama.
Vitabu zaidi ya 50 vilivyotolewa na HakiElimu vitatunzwa kwenye maktaba hiyo, ambayo ni kivutio kimojawapo kati ya vivutio kya wageni wanaotembelea kijiji cha Butiama, sehemu alipozaliwa Mwalimu Nyerere tarehe 13 Aprili 1922, na ambapo alizikwa tarehe 23 Oktoba 1999.

Sunday, May 13, 2012

Timu ya waTanzania DMV yatoka sare na Ethiopia B

Timu ya waTanzania DMV imetoka sare, bila kufungana, na timu ya Ethiopia B katika mchezo uliochezwa jana huko Burtonsville, Maryland, nchini Marekani katika ligi ya Diaspora World Cup.
Kikosi kamili cha timu ya waTanzania DMV wakiwa na mdhamini mpya wa timu hiyo, mbunifu wa mitindo ya Kwetu, Missy Temeke, akiwa na na shabiki Didi Vava, katika uwanja wa Greencastle, uliopo Burtonsville, Maryland.
Mchezaji wa timu ya Ethiopia akipambana vikali na Yousouf Godson Liuzinho, kipindi cha kwanza, katika ligi ya 2011 Diaspora World Cup kwenye kiwanja cha Greencastle, kilichopo Burtonsville, Maryland.
Wachezaji wa wa timu ya Ethiopia wakiwania freekick katika dakika ya 62 ya mchezo huo.
Didi Vava, kushoto, akiwa na Sharif Qullatein, Dogo Hudhaifa Shatry, na mmiliki wa blog ya swahilivilla Abou Shatry, wakiwa katika jukwaa la wapenzi wa timu ya waTanzania DMV.
Mdhamini wa timu ya waTanzania DMV ambaye ni mwanamitindo na mbunifu wa mitindo ya Kwetu Fashion Design, Missy Temeke, akiwa na Bendera ya Taifa.

Picha na habari kutoka kwa mwana blog Abou Shatry wa http://swahilivilla.blogspot.com/

Saturday, May 12, 2012

Timu ya Tanzania DMV kuchuana na Ethiopia (B) leo

Katika mchezo wa ligi ya 2011 Diaspora World Cup unaoendelea katika viwanja vya Hyattsville na Germantown, jijini Maryland nchini Marekani, timu ya Tanzania DMV itachuana vikali na timu ya Ethiopia leo hii Jumamosi May 12, 2012 saa 6:00 mchana katika kiwanja cha Greencastle, kilichopo Burtonsville, Maryland.
Kundi (B) Timu ya wa Ethiopia katika mchezo wa awali walifungwa mabao 3-0 na timu ya Malawi ndani ya uwanja cha Greencastle, Burtonsville, Maryland. Leo Ethiopia watajiandaa vikali ili kutaka kurudisha nguvu zao kwa mchezo waliopoteza dhidi ya timu hiyo ya Malawi, ambayo leo itapambana na Armenia saa 7:00 mchana. Katika mechi ya awali Armenia waliwabamiza Nigeria bao 4-1.

Tanzania DMV katika mchezo wa kwanza siku ya Jumapili 29 April 2012 walifanikiwa kuwabamiza Ghana mabao 3-2 ndani ya uwanja wa SoccerPlex Stadium uliyopo Ager Road Hyattsville Maryland.

Kama kawaida yao timu ya Tanzania DMV inawaomba Watanzania wote ushirikiano wenu ili kuipa changamoto timu ya Watanzania DMV. Mnaombwa pia kufika mapema saa 5:00 kuzowea mazingira kabla ya mchezo huo kuanza.

Sehemu ya mchezo utakaochezwa leo hii ni Fairland Field 3928 Greencastle Rd. Burtonsville, Maryland 20866 Habari na http://swahilivilla.blogspot.com/

Habari na picha kutoka http://swahilivilla.blogspot.com/ na Abou Shatry.

Wednesday, May 9, 2012

Bondia Selemani Kidunda afuzu kushiriki michezo ya Olimpiki ya London

Pichani, mwenyekiti wa chama cha ngumi za ridhaa Tanzania, Michael Changarawe, kushoto, akimpongeza bondia Selemani Kidunda kwa kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki ya London Uingereza akiiwakilisha Tanzania.

Michezo ya Olimpiki itachezwa jijini London kuanzia tarehe 27 Julai hadi 12 Agosti, 2012.

Picha na habari kwa hisani ya superboxingcoach.

Lugha yetu Kiswahili

Kwa Kiswahili sanifu, kofia ya rangi nyekundu anayovaa Mhe. Nimrod Mkono, mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, inaitwa tarabushi. Aidha, huitwa pia tarbushi.
Bango la barabarani lenye picha ya Mhe. Nimrod Mkono akiwa amevaa tarabushi, akiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kulia.
Asili ya tarabushi ni eneo la Ugiriki ya kale lakini ni kofia ambayo huvaliwa sana na Waislamu wa eneo la mashariki la Bahari ya Mediterenia. Mpaka mwaka 1925 kofia hii ilikuwa sehemu ya vazi rasmi nchini Uturuki.

Tuesday, May 8, 2012

Ngowi kusimamia pambano la ubingwa wa IBF nchini Ghana


Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) limemteua Rais wa Shirikisho hilo katika bara la Afrika, Onesmo Alfred Ngowi kusimamia pambano la ubingwa wa mabara linalotambuliwa na IBF.



Mpambano huo utafanyika katika jiji la Accra nchini Ghana tarehe 26 Mei kati ya bingwa wa mabara wa IBF Emmanuel Tagoe wa Ghana na mpinzani wake Antonio De Vitis wa Italy katika uzito wa Junior Lightweight.
Katika mpambano huo wa kutetea mkanda wa ubingwa wa IBF ambao unashikiliwa na Tagoe Ngowi atasaidiwa na waamuzi wengine kama ifuatavyo: Refarii: Roger Barnor (Ghana). Majaji: Francisco de Ruvo, (Italy), Andre Pasquier (France) na Shadrack Acquaye (Ghana).

Mpambano huo uliopewa jina la “Ni Sasa au Hakuna Tena”, bondia Joseph Agbeko wa Ghana atagombea mkanda wa dunia wa Organizesheni ya Ngumi ya Kimataifa (IBO) akichuana na bondia Michael Domingo wa Ufilipino katika uzito wa Bantam.

Bondia Joseph Agbeko anayeishi katika mji wa Bronx katika jiji la New York nchini Marekani atakumbukwa kwenye mpambano wake mkali wa kugombea ubingwa wa IBF katika uzito wa Bantam kati yake na bondia Abner Mares wa Mexico tarehe 3 mwezi Agosti 2011 katika jiji la Las Vegas, Nevada, nchini Marekani ambako ilibidi warudiane mara ya pili baada ya kutokea malalamiko ya kuonewa kwa Agbeko.

Hata hivyo bondia Abner Mares alimshinda tena Joseph Agbeko waliporudiana tarehe 18 Novemba 2011 katika jiji la California, nchini Marekani.

Naye bondia Joshua Okine wa Ghana ambaye alikuwa bingwa wa mabara wa IBF katika uzito wa Middle kabla ya kupoteza ubingwa wake kwa kupandisha uzito atapambana na bondia Theofiilus Teteh pia wa Ghana kugombea mkanda wa WBO Africa.

Bondia Sammuel Amaoko, anayejulikana pia kama Bruno wa Ghana, atapambana na bondia Sidney Siqueira wa 
Brazil kugombea mkanda wa WBO Africa katika uzito wa Heavyweight.   

Mapambano haya yaliyoandaliwa na Golden Mike Boxing Promotions ya Ghana yatafanyika katika uwanja wa kimataifa wa El-Wak, jijini Accra nchini Ghana chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Ngumi za Kulipwa ya Ghana (Ghana Boxing Authority, GBA).

Usimamizi wa Ngowi katika mpambano huu unakuja kipindi kifupi baada ya Francis Cheka wa Tanzania kuunyakua mkanda wa IBF Continental Africa Title katika uzito wa Super Middle tarehe 28 April mwaka huu.

Thursday, May 3, 2012

Harusi za siku hizi

Bwana Harusi akitambulisha familia yake katika mojawapo ya harusi za miaka ya hivi karibuni.
Harusi za siku hizi ni tofauti sana na zile za zamani.

Katika miaka iliyopita maharusi walikaa pamoja (kwa zile harusi ambazo maharusi hukaa pamoja) na walielekezwa na Msimamizi Mkuu wa Sherehe wakati wa kusimama, wakati wa kukaa, wakati wa kukata keki, na wakati wa kuingia ukumbini kufungua dansi.
Leo hii, Msimamizi Mkuu wa Sherehe anayo kauli ile ile juu ya maharusi, lakini maharusi wanao uhuru mkubwa zaidi kuzunguka ukumbini. Jambo jipya ambalo linaonekana kwenye harusi za siku hizi ni utambulisho wa familia wa pande zote mbili unaofanywa na bwana harusi, na bibi harusi, jambo ambalo halikuonekana kwenye harusi za miaka ya zamani.

Kwenye harusi za zamani maharusi walikaa kimya na kujionyesha kama watu wataratibu sana, hata kama ukweli ulikuwa tofauti na taswira iliyoonekana. Leo hii kwenye harusi maharusi huonyesha hisia zao waziwazi na wanacheza muziki katika kila hatua ya sherehe: kuanzia kupokea zawadi toka kwa wageni, mpaka wakati wa kusogelea meza wakati wa kukata keki ya harusi.