Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, September 14, 2013

Asikwambie mtu, Mtanzania mwenye simu siyo maskini

Baadhi ya matumizi ya simu yanaashiria kuwa Watanzania wanao uwezo mkubwa.

Nimekuwa msikilizaji wa mazungumzo ya simu ninapokuwa mitaani au safarini na katika utafiti usiyo rasmi ambao nimefanya, watu wengi wanaotumia simu hawazitumii kama nyenzo za kuongeza ufanisi katika shughuli zao, bali huzitumia kama chombo cha kupiga porojo zisizo na manufaa kwao au kwa wanaoongea nao.

Sina mamlaka kuhoji ambavyo mtu aliye huru anaamuaje kutumia salio lako kwenye simu, lakini kukosa mamlaka hayo hakufuti ukweli kuwa Watanzania wengi tunapoteza pesa zetu za mawasiliano kupiga porojo na kutuma ujumbe wa maandishi ambao hauleti maendeleo yoyote kwetu na kwa Taifa. Wanaochekelea ni wamiliki wa kampuni za simu ambao bila shaka wanatunisha mifuko yao kwa kila sekunde inayopita.

Chukua mfano huu: nimeketi ndani ya ndege iliyowasili kwenye uwanja wa ndege halafu abiria kadhaa wanawasha simu zao na kuwapigia simu watu ambao wamefika kuwapokea uwanjani wakiwaambia kuwa kuwa ndege imeshatua. Hii nimeshuhudia mara nyingi. "Vipi, umeshafika? Na sisi ndiyo tumetua."

Kwangu ingekuwa inaleta maana zaidi iwapo baada ya kutoka uwanjani na asimuone aliyempokea ndiyo apige simu kumuuliza kilichomsibu mwenyeji wake mpaka asifike uwanjani.

Siku za hivi karibuni nimeshuhudia mtu anayeongea kwenye simu karibu siku nzima. Akimaliza simu moja anapiga na kuongea na nyingine. Sijui anaongea nini kwa sababu anaongea Kizanaki (lugha ambayo siifahamu vizuri) lakini pamoja na kutofahamu lugha hiyo bado sipati picha ya suala ambalo litanifanya niongee kwa siku nzima. Hoja yangu hapa ni kuwa siyo rahisi kuongea mfululizo kwa karibu siku nzima na ukawa unapanga masuala ya kuleta maendeleo kwako au kwa jamii inayokuzunguka. Asilimia kubwa ya mazungumzo itakuwa porojo ambayo matokeo yake itakufanya kupungukiwa tu pesa ambazo ungeweza kuzitumia kwa jambo la maana zaaidi na lenye manufaa. Dakika chache kwenye simu kila siku zinafikia pesa nyingi baada ya muda mrefu.

Naweza kuwa nitatofautiana na wengi lakini ule woga wa serikali hivi karibuni kutoza shiling elfu moja kwa mwezi kwa kila mtumiaji wa simu ulikuwa woga wa kisiasa kwa sababu baadhi ya makundi ya jamii yalilivalia njuga suala hilo na kodi hiyo ya mawasiliano ilionekana kuwa ingeipunguzia serikali ushawishi kwa Watanzania. Inawezekana kuwa serikali inayo matatizo mengi 

Ukweli ni kuwa watumiaji wengi wa simu wanatumia pesa nyingi kwa mwezi kuongea na kuandika ujumbe wa maandishi usiyo na manufaa yoyote lakini ambao unawagharimu kiasi kikubwa kuliko hiyo shilingi elfu moja.

Friday, September 13, 2013

Hatari ya kuamini kila unachoambiwa

Miaka arubaini iliyopita taarifa ya kutua kwenye mwezi kwa chombo cha anga cha Marekani, Apollo 11, na kutembea kwenye mwezi kwa wanaanga wawili kutoka chombo hicho kulizua maswali mengi kutoka kwa mwanafunzi mwenzangu, Richard. Yeye hakuamini iliwezekana kwa binadamu kufika kwenye mwezi. Umri wangu ulikuwa miaka tisa na naamini Richard alikuwa na umri huo huo. Alisema, "Wanatudanganya hao!"

Mimi niliamini kuwa wale wanaanga wawili walifika kwenye mwezi. Sijui kwa sababu ipi sikuwaza kuwa ni uongo, lakini nakumbuka tu kuwa niliamini taarifa tulizosikia na kusoma bila kuhoji. Kwa umri wetu maoni yetu, ya kuamini au kutoamini, hayakutokana na ushahidi wowote tuliokuwa nao lakini ajabu ni kuwa tulikuwa na maoni tofauti.
Mwanaanga Edwin "Buzz" E. Adrin akionekana kwenye mwezi pembeni ya chombo kilichotua kwenye mwezi tarehe 20 Julai 1969. Picha ya National Space Agency (NASA).
Ukweli ni kuwa nilifikia maamuzi ambayo watu wengi hufikia katika mazingira ya aina hiyo. Tunayoambiwa tunaamini. Tatizo ya hali kama hii ni uwezekano wa kupokea taarifa za uongo kutoka mamlaka na serikali mbalimbali na kutumika kwa manufaa ya hao watoa taarifa za uongo.

Niligundua hivi karibuni kuwa wasiwasi wa taarifa zile kwa Richard za mwaka 1969 haukutokea Tanzania tu; hata baadhi ya Wamarekani hadi hii leo hawaamini kuwa Wamarekani wenzao walifika kwenye mwezi na wanasema kuwa mandhari ya mwezi ambayo tunaiona kwenye baadhi ya picha ilibuniwa na kutengenezwa hapa hapa duniani kwenye jengo moja kubwa linalohifadhi ndege kwenye uwanja mmojawapo wa ndege wa nchini Marekani.

Inawezekana kuwa tofauti ya sasa na mwaka 1969 ni kuwa watu wengi zaidi wamejenga desturi ya kutoamini taarifa za serikali na mamlaka mbalimbali. Serikali na mamlaka zimebainika mara nyingi kutoa taarifa za uongo na watu sasa wanaposikia taarifa hizo huanza kwa kutoamini hizo taarifa mpaka pale watakapopata taarifa kutoka vyanzo tofauti zinazothibitisha ukweli wa hizo taarifa za awali.

Taarifa inayofanana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2012/01/ingekuwa-unaishi-kwenye-sayari-ya.html

Tuesday, September 10, 2013

Enzi za Mwalimu

Baada ya kutangazwa Azimio la Arusha, mwaka 1967, baadhi ya makundi ya Watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania yalianza kutembea kwa mguu kutoka sehemu moja hadi nyingine ya nchi kuunga mkono Azimio la Arusha.
Picha ya Idara ya Habari Maelezo
Kwenye picha ni vijana kutoka mkoa wa Mara ambao walitembea hadi Dar es Salaam kuunga mkono sera ambayo iliweka umuhimu kwa serikali kumiliki njia kuu za uchumi na kutumia rasilimali ya Taifa kwa manufaa ya wananchi.

Ikulu, Dar es Salaam, walipokelewa na Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.