Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, July 22, 2011

Maana sahihi ya neno 'fisadi'

Leo hii wakati nikisikiliza kipindi cha Kipima Joto cha ITV kinachoongozwa na Rainfred Masako, nimemsikia Profesa Tigiti Sengo akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi sahihi ya neno 'fisadi'. Alisema:
Fisidi ndiyo mwizi; fisadi ni malaya na mlevi.
Huyu ni gwiji wa lugha ya Kiswahili. Natabiri kuwa miaka 20 tangu leo hii, Watanzania wataendelea kutumia neno ‘fisadi’ kama ambavyo linavyotumika sasa hivi kwa makosa. Au inawezekana mafisidi hawatakuwepo wakati huo.

Tuesday, July 19, 2011

Takwimu: Viwango vya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi Ulimwenguni


Kwa wachumi, kipimo kimojawapo cha hali ya uchumi ni kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma. Kwa ujumla, kasi kubwa ya ongezeko haileti manufaa kwa uchumi na kazi mojawapo muhimu ya Serikali yoyote ni kudhibiti ongezeko la bei kwa kupitia sera zake. Aidha, ongezeko la bei linapunguza uwezo wa wafanyakazi kumudu gharama za maisha na linaweza kuwa chachu ya migomo ya wafanyakazi na ukosefu wa amani kwenye nchi.

Sifa mojawapo ya Serikali ya Awamu ya Tatu ya Tanzania ya Rais Benjamin Mkapa ilikuwa mafanikio yake ya kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei.

Zipo nchi kadhaa duniani ambazo takwimu zake zinaonyesha kuanguka kwa mfumuko wa bei. Maana yake, ni kuwa bei za bidhaa na huduma zinapungua badala ya kupanda. Hizi, kwa mujibu wa wavuti ya Wikipedia ni pamoja na Seychelles, Ireland, na Gabon.

Orodha kamili ya Wikipedia inapatikana hapa. Baadhi ya nchi zilizopo kwenye orodha hiyo na kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei ni kama ifuatavyo:

Nafasi Duniani
Nchi
Kasi ya Mfumuko wa Bei (%)
1
Seychelles
-2.2
2
Ireland
-1.6
3
Gabon
-1.3
7
Japan
-0.7
24
Ujerumani
1.1
27
Senegal
1.2
34
Burkina Faso
1.4
34
Marekani
1.4
40
Canada
1.6
50
Cameroon
1.9
55
Umoja wa Falme za Imarati
2.2
84
Libya
3.0
92
Uingereza
3.3
121
Kenya
4.2
130
Afrika ya Kusini
4.5
140
China
5
142
Zimbabwe
5.03
166
Rwanda
6.4
179
Tanzania
7.2*

*Hizi ni takwimu za 2010

Friday, July 15, 2011

Wageni wa Butiama: Dk. Thomas Molony


Mtafiti mwandamizi wa Kituo cha Masomo ya Afrika kilichopo Chuo Kikuu cha Edinburgh, Dk. Thomas Molony, yuko kijijini Butiama mwezi huu wa Julai akiandika kitabu juu ya muasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922 – 1999).
Dk. Thomas Molony
Kitabu hicho kitahusu sehemu ya maisha ya Mwalimu kati ya mwaka 1922 alipozaliwa hadi mwaka 1952, baada tu ya kuhitimu masomo yake kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh na kabla hajajitupa kwenye harakati za kudai uhuru toka kwa Waingereza. 

Kwa kujiandaa na uandishi wa kitabu hiki, Dk. Molony amefanya utafiti nchini Uingereza na Tanzania na ni mara yake ya pili kutembelea Butiama. Anatarajia kitabu chake kitachapishwa kabla ya mwisho wa mwaka, kuwahi maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru tarehe 9 Desemba.

Thursday, July 14, 2011

Mbio za Mwenge wa Uhuru kuanzia Butiama mwaka huu

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa muda mrefu kidogo uliyopita, mbio za Mwenge wa Uhuru zitaanza kijijini Butiama tarehe 14 Oktoba mwaka huu, na kumalizika Dar es Salaam. Tarehe 14 Oktoba ni maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Nyerere, siku aliyofariki Mwalimu Nyerere mwaka 1999.
Dk. Nassoro Matuzya, kiongozi wa mbio za mwenge 2010 akipandisha Mwenge wa Uhuru eneo la Mwitongo wakati wa mbio za mwenge mwaka jana.
Vyanzo vyangu vya habari vinaniambia kuwa awali sherehe hizi zilikuwa zifanyike Mbeya na pesa za maandalizi zilishatumwa huko. Baada ya uamuzi wa kuhamishia sherehe kuja Butiama taarifa zinaeleza kuwa pesa zilizokwishatumwa Mbeya hazikuweza kupatikana kwa sababu, kwa mujibu wa Serikali mkoani Mbeya, pesa hizo tayari zilikuwa zimeshatumika kwa maandalizi. Hii imeilazimu Serikali kutafuta upya pesa za kugharamia sherehe za Butiama.

'Muhunda' aonekana Butiama


Hivi karibuni, siku chache baada ya mazishi ya mwanafamilia, alionekana nyani mkubwa akikatisha kwenye baadhi ya maeneo ya kijiji cha Butiama.

Nilipata taarifa za kuonekana kwa nyani huyo baada ya kuulizwa: “Umemuona Muhunda?”

“Muhunda?”

“Ndiyo, ametutembelea.”

Wakati napokea taarifa hiyo, mbwa walikuwa wakibweka ovyo, mithili ya mbwa mwitu.

Kuna Muhunda wawili tu ninaowafahamu. Mmoja ni baba yangu mdogo, Joseph Muhunda. Na mwingine ni mzimu wa kabila la Wazanaki, kiumbe asiye wa kawaida anayeaminika kuishi ndani ya msitu wa nasaba wa Muhunda uliyopo jirani na Mwitongo, sehemu yalipokuwa makazi ya babu yangu. Ni marufuku kuingia ndani ya msitu huo ila kwa watu maalumu tu, kwa mfano rika la wazee, au wanyikura ambao ndiyo wasimamizi wa msitu. Aidha kukata miti ya huo msitu pia ni marufuku ingawa kuokota matawi makavu yalioanguka inaruhusiwa.

Mwalimu mstaafu, Jack Nyamwaga, anakumbuka kuwa wakati wa utoto wake kuna nyani mkubwa alifika kwenye makazi ya babu yangu, Mtemi Nyerere Burito. Yule nyani alisogelea na kuanza kula mihogo iliyokuwa imeanikwa nje, na watoto walipojaribu kumfukuza Mtemi Nyerere aliwazuwia na kusema wamwache yule nyani aendelee kula ile mihogo.

Inaaminika kuwa mzimu huu hujibadilisha katika maumbile mbalimbali ikiwa ni pamoja na chui, nyoka, mbuzi, au nyani. Ni nadra kuona nyani Butiama na ingawa nimewahi kuwaona kwenye milima ya jirani na Butiama huwa hawafiki eneo la Butiama. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 11 kwa nyani kuonekana hapa Butiama.

Wanaoamini kuwepo kwa mzimu huu wanaamini kuwa umefika kufuatia msiba tuliyopata hivi karibuni. Mashuhuda wanasema kuwa huyu nyani aliyeonekana hivi karibuni alitokea upande wa kaskazini, akavuka eneo lenye makazi, akipuuzia watoto waliokuwa wanamrushia mawe, na alifika kwenye kaburi la ndugu tuliyemzika hivi karibuni na akabaki pale kwa dakika chache halafu akaelekea Mwitongo.
Wakati wa msiba wa ndugu yangu, Mazembe Joseph Nyerere.
Siyo mbwa tu walikuwa wamekosa amani, inasemekana kuwa hata tumbili ‘waliingia mitini’ na hawakuonekana kabisa, ingawa kwa kawaida eneo la Mwitongo lina makundi mengi ya tumbili.
Tumbili 'waliingia mitini.'
Katika miaka iliyopita kila nyani mkubwa alipojitokeza eneo la Butiama wanyikura walikutana na kutuma wawakilishi kwa mpiga ramli mashuhuri aliye eneo la Mto Kirumi kupata ufafanuzi juu ya ujumbe au tafsiri ya kuonekana ‘Muhunda’. Iwapo ‘Muhunda’ alikuwa amekasirishwa na tukio fulani ndani ya jamii, basi ujumbe uliwasilishwa kwa jamii na tambiko lilifanyika.