Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, November 29, 2013

Maajabu ya mapishi [imefanyiwa masahihisho]

Hii ni tafsiri ya makala ya lugha ya Kiingereza niliyoandika na ikachapishwa kwenye gazeti la Daily News kwenye safu yangu iliyoitwa Letter from Butiama, makala nilizoandika kati ya mwaka 2005 na 2011. Makala hiyo ilichapishwa tarehe 26 Juni 2005.
*****************************************************
Inasemekana kuwa biashara zote zinazohusu nyama ndani ya mkoa wa Mara zinadhibitiwa na Wazanaki. Utawakuta kwenye kila ngazi ya biashara hiyo kama wamiliki, kama wafanyabiashara wa kununua na kuuza ng'ombe, na muhimu zaidi, kama wamiliki wa bucha. Aidha wamepata mafanikio wakubwa kwenye biashara hiyo kwenye jiji la Mwanza.

Somo kubwa linalojitokeza katika kuchunguza masuala yanayobainisha kampuni zenye mafanikio makubwa na zile zenye mafanikio duni ni ukweli kuwa mameneja wa kampuni zenye mafanikio wamejikita kwenye shughuli za bidhaa na huduma ambazo wanazielewa vyema. Inaelekea kuwa mmoja wa wafanyabiashara wa ng'ombe niliyeonana naye anaelewa vyema ukweli huu. Alinipa somo kuhusu hali mbali mbali za nyama kutoka sehemu tofauti za mwili wa ng'ombe na kuhitimisha kuwa nyama ya ng'ombe yenye ladha bora kuliko zote ni inayopatikana sehemu ya ndani ya paja la ng'ombe. Uelewa usiyo wa kawaida kama huu pengine ndiyo chanzo cha Wazanaki kutawala biashara ya ng'ombe na nyama ndani ya mkoa wa Mara. Napata picha ya matajiri wa Kizanaki wakimiliki biashara ya nyama ya bara la Afrika kama ambavyo Wajapani wamedhibiti biashara ya magari.

Pamoja na hii hamasa ya Wazanaki juu ya ng'ombe na nyama, ukweli unabaki kuwa hisia kali ya mtu mmoja inaweza kuwa mwiko kwa mtu mwingine. Migongano mikubwa ya kitamaduni inaweza kupatikana kwenye chaguzi ambazo watu toka tamaduni mbalimbali wanafanya kuhusu chakula wanachokula na kile wasichokula. Kwa baadhi ya dini kula nyama ni mwiko. Mboga na nafaka ndiyo hutumika kama vyakula vya msingi kwa jamii hizi.

Suala la chakula lilizua taharuki kwenye ziara mojawapo ya Rais Nyerere katika miaka ya sabini kwenye nchi mojawapo ya Ulaya. Kama ilivyo desturi kwenye misafara ya viongozi wa nchi, kiongozi mwenyeji wa nchi ile aliandaa dhifa ya taifa kwa mgeni wake, na baada ya juma moja Rais Nyerere akaandaa dhifa kwa mwenyeji wake. Wakati wa dhifa ya pili, mmoja wa Watanzania waliokuwa kwenye msafara ule alimdanganya Mtanzania mwenzake kuwa miongoni mwa vyakula vilivyoandaliwa kwenye dhifa ya kwanza ilikuwa ni pamoja na vyura na kuwa yule mwenzake alikula hao vyura bila kufahamu.

Aliyetoa taarifa hiyo alikusudia yawe mazungumzo kati yao tu, lakini aliyepewa taarifa ya kula miguu ya vyura alianza kujisikia vibaya hapo hapo na akaanza kutapika wakati dhifa ikiendelea.

Nilipokuwa mwanafunzi nchini Italia mimi na rafiki yangu George kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo tulialikwa chakula cha jioni na mwenyeji wetu Mtaliani. Baada ya kutuagizia chakula alisema kuwa alikuwa ametuchagulia chakula mahususi kwa ajili yetu ambacho huandaliwa marafiki wa karibu kabisa au wageni mashuhuri. Ukweli ni kuwa alikuwa ametuagizia miguu ya vyura. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kula miguu ya vyura na nakumbuka ladha ilikuwa kama ya samaki. Mara tulipowekewa sahani zetu mezani na mhudumu, George alishituka na alitaka kuhama kabisa ile meza tuliyokaa. Mimi na mwenyeji wetu tulipoanza kushambulia ile miguu nakumbuka George alipata shida kubwa kubaki kwenye meza moja na sisi na kuangalia kitendo ambacho ni dhahiri kilimfadhaisha sana.

Mwenyeji wetu, ambaye aliwahi kutembelea nchi kadhaa za Afrika, alishangaa sana George. Alimuuliza anawezaje kuona kinyaa kula miguu ya vyura wakati yeye ameshuhudia Waafrika wakila wale wadudu ambao hutokeza baada ya mvua kunyesha. Alikuwa anazungumzia senene. George naye alishindwa kumuelewa Giuseppe. Mtu anawezaje kulinganisha kula senene na miguu ya vyura? Alisema Giuseppe alikuwa analinganisha vitu ambavyo havipaswi kulinganishwa kabisa.

Kuacha mimi, hamna kati yao ambaye alikuwa ameshakula miguu ya vyura pamoja na senene. Kimya kimya niliwashangaa hao wawili ambao walikuwa wanabishana ubishi ambao hawakuwa na mamlaka hata kidogo ya kuuendeleza. Jambo ambalo sikuweza kulibainisha wakati ule ni chakula kipi, kati ya chura na senene, kilikuwa na ladha nzuri zaidi.

Ukweli ni kuwa yawezekana kufikia usemi kuwa ladha ya chakula ni uamuzi ambao uko kichwani mwa mtu mmoja mmoja. Nimewahi kujitwika ujasiri usiyo na mfano na nikala chakula ambacho machoni kilikuwa kinatisha kuangalia lakini nikajikuta nimeweka mdomoni chakula chenye ladha nzuri kuliko maelezo. Tofauti na mwananchi mwenzangu ambaye alikuwa kwenye ziara ya Rais Nyerere, mimi nilifahamu chakula nilichokula siku ile kwenye ule mgahawa nchini Italia, kwa hiyo jambo la kushangaza ambalo naweza kulizungumzia ni ladha nzuri tu ya miguu ya vyura.

Monday, November 25, 2013

Hatua kumi za mauaji ya kimbari: 3 na 4

Nimetembelea Rwanda hivi karibuni na nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea mojawapo ya vituo vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Jambo moja la msingi ambalo Watanzania tunaweza kijufunza ni kuwa maafa yaliyotokea Rwanda yanaweza kutokea pia Tanzania. Kwa mujibu wa wachunguzi wa sababu zinozogeuza binadamu mmoja kuwa adui wa binadamu mwenzake na hata kufikia hatua ya kumaliza uhai wa mwenzake ziko duniani kote.

Sababu hizi zinaanza na mchakato wenye hatua nyingi ambao hufikia mauaji kama yale yaliyotokea Rwanda. Kinachozuwia maafa kama hayo kutokea ni hatua mahususi zinazopaswa kuchukulia na jamii za kukatisha uendelezwaji wa huo mchakato.

Kwa mujibu wa Dr. Gregory Stanton wa Genocide Watch, hatua za viashiria vya kuwepo kwa mchakato na za kuzuwia maafa kama ya Rwanda ziko kumi.

Hatua ya Tatu: Ubaguzi

Hatua hii inaanza kutenga makundi kwa mujibu wa uainishaji wa hatua ya kwanza. Mfano mashuhuri wa ubaguzi huu ni sera za kibaguzi za Afrika ya Kusini, apartheid. Kwenye hatua hii pia ndoa kati ya mtu wa kundi moja na jingine inapigwa marufuku na wale wanaoendeleza dhana hii. Yawezekana pia hata watu wa kundi linalobaguliwa kuanza kufukuzwa kwenye kazi, kama ambavyo ilifanyika dhidi ya Wayahudi wakati wa utawala wa Hitler huko Ujerumani.

Wakati mwingine zinatolewa hoja za kutenga nafasi za kazi kwa makundi mahususi ndani ya jamii. 

Mifano: Katika kukoleza ubaguzi zinaweza kuchukuliwa hatua za kubagua watu wa kundi moja kutonunua bidhaa za watu wa kundi jingine.

Hatua za kuepuka ubaguzi: Kuweka sheria zinazozuwia ubaguzi kwa misingi ya rangi, dini, kabila, utaifa, jinsia, tabaka, au chama.

Kuwezesha watu binafsi, na siyo waendesha mashtaka wa serikali pekee, kufungua mashitaka dhidi ya watu wanaotuhumiwa kufanya ubaguzi.

Hatua ya Nne: Udhalilishaji wa Kibinadamu

Kwenye hatua hii kundi moja linajipambanua kuwa ni bora kuliko lingine na kufanya kundi linalonyanyaswa kuonekana kama siyo binadamu kamili. Udhalilishaji wa kibinadamau unaondoa kusita kwa binadamu mmoja kuchukua hatua ya kumuua binadamu mwenzake.

Mifano: Nchini Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari, Watutsi waliitwa mende na majina mengine ya kudhalilisha.

Hatua za kuepuka udhalilishaji: Kupinga kwa nguvu zote matumizi ya maneno ya kudhalilisha binadamu mwingine, pamoja na kuzuwia watu wa aina hii visa za kusafiria kwenda nchi nyingine na kueneza chuki.

Kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu au makundi ya watu yanayochochea madhara dhidi ya makundi mengine.

Serikali ichukue hatua za kufungia vituo vya redio na televisheni ambavyo vinachochea uhasama baina ya makundi mbali mbali. Tanzania tumeshuhudia vituo kadhaa kufungiwa kwa muda tu na kuruhusiwa kuendelea na matangazo.

Zitolewe fursa za kuleta maridhiano kwa njia zifuatazo:
  • kuanzisha vipindi kwenye vyombo vya habari vya kitaifa vyenye maudhui yanayokusudia kupunguza au kuondoa uhasama
  • kushirikisha viongozi wa kisiasa na dini kuongea na kukemea ubaguzi na kuhubiri kustamihiliana
  • kuhimiza madhehebu na dini mbalimbali kufanya kazi pamoja dhidi ya makundi ya chuki
  • kujenga makundi yanayofanya kazi pamoja kuepusha mauaji ya kimbari  
Muongozaji wageni katika mojawapo ya vituo vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 akitoa maelezo kwa wageni.
Itaendelea na:
  • Hatua ya Tano: Uratibu
  • Hatua ya Sita: Kingamizi

Wednesday, November 20, 2013

John Kitime aelezea historia yake

Zamani, kwenye miaka ya tisini, niliwahi kumiliki gazeti lliloitwa Sanaa na Michezo ambalo lilichapisha makala kuhusu maisha ya mwanamuziki John Kitime, ambaye sasa hivi yuko na Kilimanjaro Band, Wananjenje.

Wakati huo aliwasilisha maelezo yake ambayo yalitumika kuandika makala fupi iliyochapishwa kwenye gazeti hilo.

Huyu hapa tena, John Kitime, akielezea maisha yake ndani ya muziki.
"Nilianza kwanza kupiga gitaa mwaka 1968 nikiwa kwenye mwaka wangu wa kwanza wa shule ya sekondari. Tangu napata kumbukukumbu tulikuwa na gitaa nyumbani wakati wote. Baba yangu alipiga gitaa tangu alivyokuwa mdogo. Yeye ni mtaalamu wa nyimbo za asili na ana mamia ya tunzi ambazo kwa bahati mbaya hazijarekodiwa.

Mwaka 1968 nilianza masomo yangu ya sekondari na baba yangu aliniruhusu kupiga gitaa. Alikuwa ni mtu aliyesisitiza masomo kwanza.

Mwaka 1975 niliunda bendi ndogo kwetu Iringa na baadhi ya wanachama wa bendi hiyo waliendelea kimuziki na kupata umashuhuri mkubwa. Wawili kati yao, Ally Makunguru na Nicholas Mlapone, wako nje ya nchi. Makunguru yuko Mombasa, Kenya na Mlapone yuko Ujerumani.Kundi hili hili ndiyo lilikuwa chimbuko  ya bendi kubwa, Tancut Almasi Orchestra.

Mwaka 1980 niliondoka Iringa na kuelekea Dar es Salaam na nilianza kufanya kazi kama msomaji wa prufu wa gazeti la Daily News. Wakati wa ziada nilikuwa mwanamuziki wa bendi ya Osheka, bendi ambayo ilivunjika mwaka 1981. Lakini ilikuwa bendi ambayo ilikuwa na wanamuziki wazuri sana kama Martin Ubwe ambaye sasa hivi ni kiongozi wa bendi ya Mionzi ambayo iko Mbeya, na Sammy Mhina ambayo ni mpiga ngoma wa Heart Strings Band.

Mwaka 1983 nilipata fursa ya kuigiza kwenye sehemu ndogo ya filamu inayoitwa Wimbo wa Mianzi iliyotolewa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Filamu Tanzania na One World Production (OUP), kampuni ya Uholanzi. Nilipewa pia mkataba wa kutunga nyimbo kwa ajili ya filamu hiyo.

Ilikuwa wakati natafuta wanamuziki wa kurekodi muziki wa filamu hiyo ndipo nilikutana na Tchimanga Assosa, mwanamuziki mashuhuri wa Congo ambaye aliwahi kupiga muziki na bendi ya Lipua Lipua na Orchestra Kamale, ambaye alikuwa anakusudia kuunda bendi na tukaunda bendi iliyoitwa Orchestra Mambo Bado. Nillikuwa na bendi hiyo kwa miaka miwili.

Baada ya hapo nikajiunga na Orchestra Makassy iliyomilikiwa na Mzee Makassy. Bendi hii wakati huo ilikuwa na mwanamuziki Fan Fan Mosesengo (aliyekuwa na Marehemu Lwambo Luanzo Makiadi} na pia Remmy Ongala, ambaye sasa amejijengea jina kubwa akiwa na Orchestra Super Matimila. Sasa hivi Fan Fan yuko London (Uingereza) akiongoza bendi yake mwenyewe, Somo Somo. Pia mwanamuziki mwingine aliyeunda Orchestra Makassy alikuwa Kinguti ambaye sasa yuko na Bicco Stars.

Baada ya hapo nikaunda bendi yangu mwenyewe, TX Seleleka. Nilipata vyombo kutoka kwa rafiki yangu Mholanzi Kick Van den Hevel ambaye baadaye tena alichukua vyombo hivyo hivyo na kuanzisha bendi ya Tatunane. TX Seleleka ilipiga muziki hoteli ya New Africa kama bendi ya hoteli kwa mwaka mmoja halafu ikavunjika baada ya Kick kuchukua vyombo vyake.

Mwaka 1986 nilirudi Iringa nikawa mwanamuziki mwanzilishi wa Tancut Almasi Orchestra bendi ambayo ilikuwa inaundwa na wanamuziki miongoni wa waliyo bora kuliko wote nchini: Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, mapacha wa Ki-Congo waimbaji; wapiga gitaa wawili Shaban Yohana, ambaye sasa hivi ni kiongozi wa Vijana Orchestra, na Kawelee Mutimwana, kiongozi msaidizi wa MK Group; Mafumu Bilali, mpiga saksafoni mahiri ambaye sasa yuko Japani na Zanzibar Sound;kinanda wakati huo kilipigwa na Abdul Salvador, kiongozi wa Washirika Stars, na wanamuziki wengine wengi ambao wameendelea kuwa na sifa kila walipoenda.

Mwaka 1990 nyimbo zangu mbili nilizotunga nikiwa na Tancut, Lungulye na Afrika Nakulilia, zilishinda mashindano ya Top Ten Show zikichukua nafasi ya kwanza na na pili. Nilishinda zawadi ya redio kaseti ya National ambayo nasikitika nililazimika kuiuza ili kupata pesa za kurekodi hii kaseti yangu ya sasa.

Nyimbo nane kwenye hizi ninazorekodi sasa ni uzoefu wangu kutoka kwenye hii miaka yote, bila kusahau ushawishi wa baba yangu. Hii nyimbo Ifipwepo ni utunzi wa baba yangu, nikiwa nimeupangilia kwenye muziki.

Ningekuwa na nafasi nzuri ningeweza kurekodi vizuri zaidi, na kutoa aina nyingi zaidi za muziki. Nakiri kuwa kaseti hii nimeirekodi kwa madhumuni ya kuiza kwa hadhira ya Watanzania ili niweze kurudisha pesa na kununua redio kaseti nyingine."
Taarifa nyingine zinazohusiana na hii:

Saturday, November 16, 2013

Hatua kumi za mauaji ya kimbari: 1 na 2

Nimetembelea Rwanda hivi karibuni na nikiwa huko nilipata fursa ya kutembelea mojawapo ya vituo vya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Jambo moja la msingi ambalo Watanzania tunaweza kijufunza ni kuwa maafa yaliyotokea Rwanda yanaweza kutokea pia Tanzania. Kwa mujibu wa wachunguzi wa sababu zinozogeuza binadamu mmoja kuwa adui wa binadamu mwenzake na hata kufikia hatua ya kumaliza uhai wa mwenzake ziko duniani kote.

Sababu hizi zinaanza na mchakato wenye hatua nyingi ambao hufikia mauaji kama yale yaliyotokea Rwanda. Kinachozuwia maafa kama hayo kutokea ni hatua mahususi zinazopaswa kuchukulia na jamii za kukatisha uendelezwaji wa huo mchakato.

Kwa mujibu wa Dr. Gregory Stanton wa Genocide Watch, hatua za viashiria vya kuwepo kwa mchakato na za kuzuwia maafa kama ya Rwanda ziko kumi.

Hatua ya Kwanza: Uainishaji

Hapa inafanyika jitihada ya kuainisha makundi ndani ya jamii, "sisi na wao." Ubaguzi unaweza kuchukua njia mbalimbali kama vile dini, kabila, utaifa, na hata matabaka ya jamii.

Uainishaji unasaidia kuwagawa watu na kurahisisha kampeni za mapambano dhidi ya kundi mojawapo ndani ya jamii.

Mifano: Tanzania tumeshaanza kujipambanua kwa dini zetu kwa muda mrefu sasa, pamoja na kwa maeneo tunayotoka. Aidha, "wa bara na wa visiwani" umekuwa wimbo mashuhuri wa miaka ya hivi karibuni.

Hatua za kuepuka uainishaji: Kusisitiza utaifa zaidi kuliko makundi. Kuweka mkazo kwenye matumizi ya lugha moja inayounganisha wote, mfano Kiswahili. Kupinga kwa nguvu zote wanasiasa na vyama vya siasa vinavyoendeleza siasa za kibaguzi.

Hatua ya Pili: Uashiriaji

Hapa zinatumika alama au ishara zinazoweka mkazo wa kubainisha makundi yaliyoainishwa katika hatua ya kwanza.

Mifano: Wakristu dhidi ya Waislamu, Wazanzibari dhidi ya Watanzania bara; Itikadi nazo zinaweza kutumika kama nyenzo za kubaguana: walalahoi dhidi wa wala nchi, Wadanganyika dhidi ya Wadanganyaji, n.k.

Hata nguo zinaweza kutumika kubaguana: magwanda dhidi ya wale wa kijani na njano. Nimeshuhudia picha ya makada wa chama kimoja cha siasa wakimshambulia mwanachama wa chama tofauti kwa mawe na matofali.

Hatua za kuepuka uashiriaji: ni pamoja na kuondoa uainishaji wa kidini au kikabila kwenye vitambulisho vya aina zote. Mpaka leo hii Mtanzania yoyote anayetoa taarifa kwenye kituo cha polisi anapaswa kutaja dini na kabila lake.
Vitambulisho vya Rwanda vilitoa taarifa za kabila la mwenye kitambulisho na vilitumika kuwasaka wahanga wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Aidha, kupinga matumizi ya maneno au majina yanayodhalilisha kundi lolote ndani ya jamii.

Itaendelea na:
  • Hatua ya Tatu: Ubaguzi
  • Hatua ya Nne: Udhalilishaji wa Binadamu
Taarifa nyingine inayohusiana na hii:

Friday, November 1, 2013

Mtwara sawa lakini Loliondo hapana?

Nimekuwa na msimamo unaofanana kidogo na sera ya serikali juu ya rasilimali za Tanzania; kwamba ni mali ya Watanzania wote, na siyo ya wale walio karibu na hiyo rasilimali. Sikubaliani na hoja kuwa wale wananchi walio karibu na rasilimali ndiyo wapewe upendeleo zaidi juu ya kufaidika na rasilimali hiyo.

Sababu yangu ya msingi ni kuwa kufanya upendeleo wa aina hiyo kutajenga ubaguzi dhidi ya Watanzania wengine. Watanzania wengine wataonekana kuwa "wanaingilia" rasilimali inayopaswa kutumika na wale wazawa wa eneo husika tu. Na ndiyo maana napata shida kuunga mkono hoja ya baadhi ya Watanzania, kama wale wananchi wa Mtwara, wanaodai rasilimali ya gesi ni yao kwanza.

Lakini hatuwezi kusema hatuelewi kwanini kuna madai kama yao. Unaweza kujenga hoja nzuri kuzungumzia kwanini wananchi wa Mtwara wanaamua kuwa gesi ya Mtwara ni yao. Ni ubovu wa sera za muda mrefu za serikali zilizopuuza umuhimu wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanafaidika na rasilimali yao. Haya ni matokeo ya muendelezo ule wa sera zinaotoa vipengele vya upendeleo kwa wawekezaji na ulipaji wa mrahaba pekee. Mwekezaji aliweza kumiliki asilimia 100 ya mradi wa rasilimali muhimu na kuilipa serikali au kodi kidogo au kusamehewa kabisa na kiwango cha mrahaba ambacho, kimsingi, kilikuwa kidogo sana.

Wananchi waliofundishwa miaka nenda rudi kuwa yatosha kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji na malipo ya mrahaba wa chini ya asilimia tano hawakuelewa hilo somo na hawataweza kulielewa hata kwa karne nzima. Matokeo yake ni kupoteza imani kabisa kwa serikali na maamuzi yoyote inayoyafanya kwenye eneo la uwekezaji. Tunachoshuhudia sasa ni wananchi "kuchukua chao mapema"; kwamba rasilimali ambazo ziko jirani nao ni lazima ziwape faida wao. Watanzania wengine wahangaike na mali zilizopo maeneo yao. 

Huu ni mwanzao wa kuparaganyika kwa nchi. Wale wasio na rasilimali watakula wapi? Watapata ajira wapi? CHADEMA wamejaribu kuelezea namna utaratibu wa kila mtu na chake (majimbo) na kidogo kilichopo kipelekwe kwenye serikali kuu lakini kwangu mimi sera hii ina walakini kuwa itaanza kupandikiza hisia kuwa Mlima Kilimanjaro una wenyewe. Hali kadhalika Serengeti, Selous, na mbuga nyingine ambazo zinaliingizia Taifa mabilioni ya shilingi kila mwaka. Vivyo hivyo kwa gesi na mafuta yanayosubiriwa kwa hamu.

Badala ya kuitaka serikali iwajibike zaidi katika kuwanufaisha wananchi wake, tunaanza kugawana kile kidogo kilicho jirani yetu. Ni sawasawa na wenyeji kugombania makombo baada ya chakula kutengewa wageni.

Kutegemea kuwa jambo litatokea (ubaguzi wa watu kutokana na maeneo yao ya asili) hakuthibitishi kuwa jambo hilo kweli litatokea. Lakini binadamu wote tunaishi kwa kufanya maamuzi kuhusu yaliyokwisha tokea zamani, ya sasa, na matarajio yetu ya yale yanayoweza kutokea. Ndiyo msingi wa mipango yote thabiti, kwa hiyo siyo rahisi kujenga hoja kupuuza hoja za aina hii.

Sasa basi tugeukie Loliondo. Wakati siungi mkono madai ya wananchi wa Mtwara naunga mkono madai ya wale wa Loliondo ambao wanapinga kusudio la serikali la kutenga kilomita za mraba 1,500 kwa wawekezaji kwa shughuli za utalii, pamoja na serikali kutaka watu hao wahame kupisha shughuli za uwekezaji. Wamasai wapatao 30,000 na ng'ombe zao wahamishwe ili kupisha shughuli za utalii.

Bado nina msimamo kuwa Tanzania ni ya wote lakini kwa wakazi wa tarafa ya Loliondo, ambao wengi wao ni wafugaji na wanaoishi maisha yanayotegemea sana ardhi wanayokalia kwa ustawi wao na wa mifugo yao, kugawa hayo maeneo kwa matumizi ya wawekezaji ni kuwanyima Watanzania hawa chanzo cha msingi kinachobeba mfumo wao wa maisha.

Hii ni sawa na kuhatarisha uhai wao. Hasara atayopata mkazi wa Loliondo atakayehamishwa haiwezi kamwe kufidiwa na kiasi chcochote cha pesa, hata kama pesa hizo zisingieishia serikalini na zikagawiwa kwa wakazi hao.

Mkazi wa Mtwara ana haki kuhoji serikali ionyeshe faida kwake (na kwa Watanzania wengine) ya sera ya muda mrefu ya uwekezaji, lakini hata kama madai ya kuweka Mtwara viwanda muhimu vya sekta ya gesi haitatimizwa, maisha ya mwana-Mtwara hayatabadilika kwa kiasi kikubwa kulinganishwa na athari na matatizo makubwa ambayo atayapata mkazi wa Loliondo ambaye maisha yake yataathrikia kutokana na kuhamishwa kwenye ardhi ambayo anaitegemea kila siku kwa maisha yake na kwa mifugo yake.

Katika mazingira haya, madai ya wananchi hawa wa Loliondo ni sahihi kabisa, kwa maoni yangu. Ya Mtwara bado yanahitaji kujengewa hoja zaidi.

Taarifa nyingine zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/09/john-mnyika-wa-chadema-anajibu-hoja.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/amani-millanga-bado-anahoji-sera-ya.html