Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, January 27, 2012

TPBC yaingia makubaliano na Chuo cha Polisi Moshi

Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) na Chuo cha Polisi cha Kimataifa cha Moshi (CCP) wameingia makubaliano ya kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo vya vijana.

Katika Makubaliano hayo yaliyofikiwa mwezi August, 2011, TPBC na CCP watashirikiana kuchagua vijana wenye vipaji vya mchezo wa ngumi na kuwaendeleza ili waweze kucheza michezo ya majeshi pamoja na mashindano mengine ndani na nje ya Tanzania.

Makubaliano haya yamekuja wakati ambapo Tanzania inahitaji msukumo mkubwa kwenye medani ya michezo ili kuweza kufufua ari na moyo wa michezo kama ilivyokuwa katika miaka ya 70 na 80.

Aidha, Makubaliano haya yana lengo la kuandaa jeshi zuri la wanamichezo hodari watakaoleta sifa jeshi la Polisi pamoja na Tanzania kwa ujumla. Tayari vijana wengi wanafanya mazoezi katika kambi (Gym) ya ngumi ambayo imewekwa katika viwanja vya michezo vya CCP. Kambi hiyo inawashirikisha pia vijana kutoka maeneo mengine mkoani Kilimanjaro ambao sio Polisi.

Katika kusimamia hili, Rais wa TPBC Onesmo Ngowi akishirikiana na Afisa Mipango na Utawala wa CCP Superintendent of Police, Lutusyo Mwakyusa watahakikisha kuwa vifaa muhimu vinapatikana pamoja na mazingira ya kufanyika mazoezi na upatikanaji wa wataalam wanaotakiwa wanapatikana.

Naye Superintendent of Police, Yahya Mdogo ambaye ni Afisa wa Michezo katika Chuo cha Polisi cha Kimataifa Moshi ataangalia kwa karibu mwendendo mzima wa mahitaji ya kila siku ya mazoezi.

Tayari TPBC imeshatoa vifaa muhimu vya mazoezi pamoja na wataalam (Makocha) wa kuwafundisha mabondia hao wako katika sehemu ya mazoezi.  Vijana wengi ambao walikuwa hawana kazi au mahala pa kwenda wakati wa saa za jioni kwa sasa wanafanya mazoezi na wenzao katika uwanja wa CCP.

Aidha, baadhi ya mabondia kutoka katika mkoa wa Kilimanjaro ambao walikuwa wameweka kambi katika jiji la Nairobi nchini Kenya na Arusha wamejumuika katika kambi hii mpya. Mabondia hao ni pamoja na Pascal Bruno anayejulikana na wengi kama "Prince Kilimanjaro", Emilio Norfat, Charles Damas, Alibaba Ramadhani, Robert Mrosso, Bernard Simon na wengine wengi

Baadhi ya wataalam waliojitokeza kuwafundisha vijana hawa ni pamoja na Felix Joseph na Pius Msele ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kuwa wachezaji na makocha wa timu ya ngumi ya taifa.

Makubaliano haya ni baadhi tu ya mikakati mipya za TPBC za kuamsha ari ya mchezo wa ngumi kwa kuzisambaza mikoani kuliko ilivyozoeleka ngumi kufanyika katika mkoa wa Dar -Es-Salaam peke yake.

"Kwa sasa kazi kubwa tulivyo nayo ni kuzipeleka ngumi mikoani ambako tunaamini kuna vijana wengi sana wenye moyo pamoja na vipaji vikubwa" alisema Ngowi.

Thursday, January 5, 2012

Ingekuwa unaishi kwenye sayari ya Mercury...

Sayari inayojulikana kama Mercury ndiyo iliyo karibu zaidi na jua miongoni mwa sayari zinazojumuishwa ndani ya mfumo wa Jua na sayari zake inayojulikana kwa Kiingereza kama Solar System. Mercury ina umbali wa wastani wa kilomita 58 milioni kati yake na Jua.

Dunia inachukuwa mwaka mzima, siku 365, kulizunguka jua. Mwaka mzima wa Mercury unachukuwa siku 88 tu. Lakini siku moja ya Mercury ni suala lingine. Siku nzima hapa duniani (au mzunguko mmoja wa dunia) inachukuwa saa 24. Siku nzima, au mzunguko mmoja, kwenye sayari ya Mercury unachukuwa siku 59 za hapa duniani.
Mercury: sayari ndogo kuliko zote kwenye mfumo wa Jua na sayari zake. Picha kwa hisani ya NASA.
Wanasayansi wanatumia muda mwingi kuchunguza uwezekano wa kuwepo uhai wa aina fulani kwenye sayari mbalimbali. Mpaka sasa bado hawajafanikiwa kupata viumbe hai vya aina yoyote sehemu nyingine zaidi ya hapa duniani. Na pengine vyema hali hiyo kubaki hivyo.

Wazo kuwa kuna viumbe kama binadamu wanaweza kuishi kwenye mazingira ambapo mawio mpaka machweo ni siku 59 inaibua changamoto za aina yake.

Wednesday, January 4, 2012

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya nne kati ya nne

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya nne kati ya nne

Funzo
Mafuriko haya yanatupa funzo la kuhakikisha kuwa tunavyo vyombo na vifaa vya kukabiliana na hali kama hii isitokee siku nyingine. Lakini pia tunakuwa wepesi wa kuchukua hatua za kuokoa maisha ya watu na si kusubiri hali inapokuwa mbaya ndipo tunaleta msaada kwa watu. Maisha ya watu wengi yangepotea kama si hatua za haraka na za makusudi zilizofanywa na mbunge wa Mafia za kukodi boti na kuipeleka eneo la mafuriko. Vyombo vya uokozi vya serikali vilikuwa wapi?

Miaka 50 ya Uhuru, changamoto bado ni nyingi na kubwa sana lakini la kusikitisha zaidi ni kwamba mafunzo ya kuthamini utu wa watu ambayo tuliyarithi kutoka kwa hayati Baba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yametoweka katika nyoyo zetu na leo hii tunasisitiza waathirika "wahame" tena bila fidia. Tumewaona wanawake wajawazito na watoto wakiwa hawana chakula; tumewaona majeruhi hawapati matibabu katika muda muafaka; tumewaona wazee hawana nguo za kujisitiri. Ndugu zangu Watanzania, ama kwa hakika tumeuona umaskini ukitembea. Ni uchungu ulioje.

Mungu Ibariki Tanzania

Tuesday, January 3, 2012

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya tatu kati ya nne 

Kuhama si suluhisho pekee la kukabiliana na maafa. Suluhisho ni kujenga miundombinu inayoweza kuhimili maafa hayo ingawa naamini nguvu ya Mungu ndiyo kinga kuu. Zipo nchi kama Japan na New Zealand ziko kwenye ukanda wa tetemeko la ardhi. Indonesia takriban kila mwaka inakumbwa na tetemeko la ardhi, milipuko ya volkano na mafuriko. Uturuki, Pakistani na hata Marekani huwa zinakumbwa na athari za mitetemeko ya ardhi na mafuriko.

Ujumbe katika nchi hizi si kuhamisha watu bali ni kujenga miundombinu imara inayoweza kukabiliana na nguvu hizi za asili na walau kupunguza makali yake. Kwa Dar es Salaam sijasikia hoja ya kujenga kingo katika mto uliofurika ili kupunguza makali ya mafuriko siku zijazo. Kwa nini hatuoni hili la miundombinu na tunakimbilia kuwahamisha waathirika?


Ni ukweli uliowazi kwamba maeneo yalikotokea mafuriko ni maeneo mazuri kwa biashara na ujenzi wa majumba makubwa ya kisasa. Je, wakishahama hawa waathirika maeneo haya yatabaki kuwa wazi tu au yatagawiwa kwa matajiri na "wawekezaji" kujenga vitega uchumi vyao? Kama serikali au jiji litayagawa haya maeneo kwa wawekezaji kwa nini tunataka kuwahamisha watu hawa bila kuwapa fidia inayolingana na thamani ya maeneo yao?

Najua fika kuwa wakati huo waja, ambao serikali au jiji litasema 'maeneo haya ni mazuri kwa biashara na kwamba wawekezaji watajenga nyumba imara za kuhimili mafuriko na kujenga kingo kwenye mto na miundo mbinu ya kuzuia mafuriko'. Tutaipokea hoja hiyo kwa mikono miwili na kusahau kwamba ilifanyika dhuluma ya kuwahamisha waathirika bila kuwapa malipo. Naungana na waathirika kuidai fidia kabla ya kuhamishwa kwa haki katika maeneo yao. Natoa wito kwa serikali kuwalipa fidia waathirika. Pili natoa wito kwa Watanzania kuhakikisha kuwa waathirika wanapata haki yao. Natoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuliangalia suala hili kwa kina na mapana yake.


Itaendelea.