Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, January 29, 2013

Wageni wa Butiama: Jaji Augustino Ramadhani

Kati ya wageni ambao wametembelea Butiama ni pamoja na aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani. Alitembelea Butiama wakati akiwa Jaji Mkuu.
Jaji Augustino Ramadhani akipata maelezo toka kwa muongozaji wageni wa Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere ya Butiama wakati wa ziara yake ya Butiama.
Mapema mwaka 2012 Jaji Ramadhani aliteuliwa kuongoza jopo la majaji waliochunguza tukio la Naibu Jaji Mkuu wa Kenya, Nancy Baraza, aliyetuhumiwa kumtishia kwa silaha mlinzi mmoja wa duka moja la jijini Nairobi.

Amani Millanga ahoji ukodishwaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji (sehemu ya pili kati ya sehemu tatu)


Katika sehemu ya pili ya makala yake hii ambayo nitaitoa katika sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.
**********************************************************
Mali ya Taifa (sehemu ya pili)

Na Amani Millanga

Hoja ya pili kwamba “ardhi bado ipo” ni hoja ambayo inatolewa bila kuangalia kwa mapana na kina athari za ukodishaji ardhi kwa wageni. Mwaka 1961 idadi ya watu ilikuwa ni milioni kumi. Miaka 50 baadaye Tanzania ilikuwa na watu milioni 45. Hii ina maana kwamba idadi ya watu imeongezeka mara 4.5 toka milioni kumi hadi milioni 45 mwaka 2011.

Kwa msingi wa hesabu hii ina maana kwamba katika miaka 50 ijayo  (mwaka 2061) Tanzania itakuwa na watu milioni 45 x 4.5 = watu milioni 202.5. Je watu hawa wataishi wapi? Watajimudu vipi? Watapata wapi ardhi ilhali sehemu kubwa ya ardhi yetu itakuwa imekodishwa kwa wageni kwa miaka 99?

Hapo ina maana kwamba utakuwa na miaka 49 ya wawekezaji kumaliza muda wao. Katika hii miaka 49 (yaani mwaka 2110) idadi ya Watanzania itakuwa imeongezeka tena mara 4.5 (tukitumia msingi wa hesabu yetu wa ongezeko la watu wa mara 4.5) kwa maana kwamba watu milioni 202.5 x 4.5 = Tanzania itakuwa watu milioni 911.25 Hadi idadi ya watu inafikia kiwango hiki cha milioni 202.5 katika miaka 50 ijayo (mwaka 2061) au milioni 911.25 katika miaka 99 ijayo (mwaka 2110) tufahamu kwamba itakuwepo vita kali sana ya wananchi kuidai ardhi yao. Wengi watakufa bure kwa sababu ya maamuzi yasiyo ya kizalendo yanayotolewa hivi sasa ya kukodisha ardhi.

Mtu anaweza kusema ni jambo ambalo haliingii akilini kwamba Tanzania katika miaka 99 ijayo itakuwa na watu milioni 911.25. Lakini hili ni jambo ambalo linawezekana tukidurusu historia ya ongezeko la watu duniani. Ukiziangalia takwimu za ongezeko la idadi ya watu duniani katika miaka 2000 iliyopita utaona kwamba ongezeko kubwa la watu limekuwepo katika miaka 200 tu iliyopita. Mwaka 1800 dunia ilikadiriwa kuwa na idadi ya watu bilioni moja na mwaka 1900 idadi ya watu iliongezeka na kufikia bilioni moja na nusu. Tokea mwaka 1800 hadi mwaka 2000 idadi ya watu iliongezeka mara sita kufikia watu bilioni 6.1. 

Katika kipindi cha miaka 12 tu yaani mwaka 2000 hadi mwaka 2012, idadi ya watu duniani imeongezeka kwa kasi kubwa sana na imefikia watu zaidi ya bilioni 7.1 kwa mujibu wa tovuti http://www.worldometers.info/world-population/. Umoja wa Mataifa unakadiria idadi ya watu itakuwa bilioni 9 ifikapo mwaka 2050 na ongezeko kubwa la watu liko Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo itakuwa na watu bilioni 2.756 mwaka 2050, likiwa ni ongezeko la watu bilioni 1.9 kutoka watu milioni 856 mwaka 2010 (ongezeko la watu zaidi ya mara mbili katika miaka 40) na 39% ya watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 duniani watakuwa Waafrika ifikapo mwaka 2100 kutoka 14% mwaka 2010.

Kwa hiyo upo ushahidi wa kutosha kwamba katika miaka 50 ijayo Tanzania itakuwa na watu milioni 202.5. Ardhi haiongezeki. Sasa katika hizo hekta milioni 44 tulizonazo ambazo kwa idadi ya watu ya milioni 45 ya mwaka 2011 ni sawa na hekta 0.977 kwa kila Mtanzania (kwa maana ya hekta milioni 44 gawa kwa watu milioni 45). Je hamuoni kwamba wastani huo wa ardhi kwa kila mtanzania utakuwa umeshuka sana katika miaka 50 ijayo?

Hesabu hii itatupa mwanga: hekta milioni 44 gawa kwa watu milioni 202.5 utapata hekta 0.217 kwa kila mtanzania. Je katika kasi hii ya kukodisha ardhi kwa wageni wastani huu wa hekta 0.217 utakuwepo kwa kila mtanzania? Ardhi itapatikana wapi? Bila shaka vijana watasimama kuidai ardhi tena kwa mabavu.

Ni ukweli usio na shaka kwamba idadi ya watu wanaohama vijijini kwenda mijini inaongezeka lakini hii haina maana kwamba katika miaka 50 ijayo 80% ya Watanzania itakuwa inaishi mijini na 20% itakuwa inaishi vijijini. Katika miaka 50 iliyopita yamekuwepo mabadiliko madogo sana ya watu kuhamia mijini ingawa kasi ya kuhamia mijini inaongezeka lakini bado 80% na huenda hata zaidi wanaishi vijijini hivi sasa. Kama hali itaendelea kuwa hivi, basi katika kujenga taswira ya hali ya mambo itavyokuwa tunaweza kukadiria kwamba 50% ya Watanzania watakuwa wanaishi mijini mwaka 2061. Hii ina maana kwamba watu milioni 202.5 gawa kwa mbili utapata idadi ya watu 101.25 watakuwa bado wanaishi vijijini wakitegemea kilimo kama ajira yao kuu.

Je tutakuwa na ardhi ya kukidhi mahitaji ya watu hawa kwa mnasaba wa kasi ya ukodishaji ardhi iliyopo? Hapa ndipo unahitajika umakini wa hali ya juu sana katika kuangalia hatima ya Tanzania na watu wake. Kwa mtizamo uliopo sasa Tanzania ya 2061 itakuwa na mgogoro mkubwa sana wa ardhi zaidi ya ule wa Zimbabwe. 

Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html

Sunday, January 27, 2013

Kwenye soka huwa nashangilia wanyonge siku zote


Makala hii niliandika zaidi ya miaka mitatu iliyopita kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza. Nairudia hapa kwa wale ambao hawakupata fursa kuisoma wakati huo, tarehe 30 Juni 2009. Nimekosa kuangalia mapambano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanayoendelea sasa hivi nchini afrika Kusini lakini ningekuwa nafuatilia mashindano hayo ningekuwa nawapigia debe wanyonge, timu ambayo hakuna shabiki anatarajia itashinda.
*********************************************
Mimi siku zote hushangilia wanyonge, hususani kwenye michezo. Kwa hiyo nilifurahishwa Jumapili iliyopita nilipowasha televisheni na kushuhudia hali isiyo ya kawaida ambapo timu ya taifa ya Marekani ikiwa inaongoza kwa goli moja bila majibu na, kabla ya kipenga cha nusu ya kwanza kusikika, ikiongoza kwa magoli mawili dhidi ya miamba ya soka Brazil kwenye pambano la fainali za mabara la FIFA nchini Afrika ya Kusini.

Katika ulimwengu wa soka Brazil inatisha, ni taifa kubwa wakati Marekani ni bwana wadogo. Katika lugha ya vita na silaha Brazil ni mzinga wa upana wa milimita 130 wakati Marekani ni kama bastola ndogo isiyojaza hata mfuko wa shati. Kwa hiyo si ajabu kumsikia kocha wa Marekani Bob Bradely akisema baada ya timu yake kushindwa: "Ni matarajio yangu kuwa watu katika sehemu mbalimbali duniani wataona kuwa tunayo timu na wachezaji wazuri. Ni hatua kubwa kwetu."
Timu ya Taifa ya Brazil iliyoshinda Kombe la Dunia mwaka 1970 nchini Mexico.
Timu nilizozishabikia kwenye mashindano zilikuwa mlolongo wa timu zilizoorodheshwa na FIFA kwa ubora lakini orodha ile ikiwa imewekwa kichwa chini miguu juu, yaani zile za mwisho ndiyo nilipendelea zaidi zishinde.

Katika kipindi cha pili Brazil walisawazisha mabao yote mawili na kuongeza bao la tatu la ushindi ambalo lilikuwa uthibitisho kuwa Brazil itabaki inatawala ulimwengu wa soka, angalau kwa sasa.

Habari njema kwa timu nyingine ambazo zitapambana na Brazil kwenye Kombe la Dunia la FIFA mwakani nchini Afrika ya Kusini ni kuwa bingwa wa FIFA wa mabara - ambapo mabingwa wa mabara wanapambana dhidi yao - hajawahi kutwaa ubingwa wa dunia mwaka unaofuata.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/mada-yangu-ya-leo-ni-nani-ataibuka.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/06/hii-kali.html

Wednesday, January 9, 2013

Wageni wa Butiama: Mhe. Benjamin William Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ametembelea Butiama mara nyingi, kabla na baada ya kustaafu kwake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Kwenye picha hii ilikuwa mara yake ya mwisho kutembelea Butiama alipohudhuria mazishi ya Mzee Josephat Kiboko Nyerere, mdogo wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mzee Kiboko ni baba mzazi wa mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA).

Amani Millanga ahoji ukodishwaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji (sehemu ya kwanza kati ya sehemu tatu)


Katika makala yake hii ambayo nitaitoa katika sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.
 ******************************************

Mali ya Taifa (sehemu ya kwanza)
Na Amani Millanga

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, Tanzania inazo hekta 44 milioni za ardhi nzuri ya kilimo. Kwa sasa ni asilimia 23 tu ya ardhi hiyo inatumika kwa kilimo, ambayo ni sawa na hekta 10,120,000.  Hii ina maana kwamba tuna ziada ya hekta 33,880,000 (yaani hekta 44,000,000 kutoa hekta 10,120,000). Ziada hii ya ardhi ambayo haitumiki kwa lolote inaonekana ni kubwa sana. Hoja iliyoko mezani ni kuikodisha ardhi kwa wakulima wakubwa wa kigeni kwa ajili kilimo cha mashamba makubwa ili serikali na wananchi wanufaike na ardhi hii ambayo “haizalishi”.

Zinatolewa hoja kwamba wakulima wa kigeni wataleta teknolojia ya kisasa na mitaji mikubwa itakayohuisha kilimo na kutoa ajira kwa Watanzania. Kwamba “kupitia ukodishaji wa ardhi kwa wageni Tanzania itafanya mapinduzi makubwa ya kijani na hatimaye kupunguza umaskini”.

Ni hoja tamu, na zimeongeza kasi zaidi katika ukodishaji ardhi ili “tunufaike na kilimo cha kibiashara” ambacho kimsingi kipo tokea tupate uhuru. Zinatolewa hoja kwamba “Watanzania wasiwe na wasiwasi kwani ardhi ni mali ya taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria.” Kwamba “mwekezaji atakodishwa ardhi kwa muda wa miaka 33, 66 au 99 na baada ya hapo ardhi itarejeshwa serikalini.” Hivyo basi “tuwapokee wakodishaji ardhi kwa mikono miwili kwani wanaleta neema.”

Hoja hizi hazina mashiko kwani zinahalalisha  kurejeshwa kwa ukoloni kwa mgongo laini wa ukodishaji ardhi jambo ambalo ni hatari sana kwa Tanzania ya leo na kesho na nitaeleza kwa nini.

Ukoloni unazo sura nyingi sana na mbinu kila aina za kuliteka taifa. Ukodishaji ardhi ni njia mojawapo ya kuukaribisha ukoloni mpya wa kutawaliwa na makampuni ya kibeberu. Ukisema hili wanajibu kwamba “hizo ni fikira za kale -Tanzania ni nchi huru.”

Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba taifa-nchi (nation-state) ni ardhi. Hivi taifa-nchi linakaa wapi? Unapoikodisha ardhi kwa miaka 99 ina maana umeifanya ardhi hiyo kuwa ni koloni kwa miaka 99. Wajerumani na Waingereza walitutawala jumla ya miaka 77. Katika miaka 99 na nguvu ya pesa, mlowezi atafanya atakavyo. Na kwa kufanya hivi atakavyo Watanzania watageuzwa watumwa ndani ya nchi yao. Watanyanyaswa na kupigwa viboko. Tunayashuhudia haya yakifayika katika migodi ya dhahabu hadi Watanzania kuuwawa. Na katika Tanzania inayokumbatia rushwa na ufisadi mwekezaji anakingiwa kifua.

Je Mtanzania kibarua katika shamba la mlowezi atapata haki yake? Zipo taarifa nyingi kwamba kwa kutumia rushwa wageni wanapewa ardhi bwerere. Na kwa mchakato uliopo wa uraia wa nchi mbili (kama utapitishwa) katika siku si nyingi walowezi watapewa uraia na Tanzania ya kesho itageuka kuwa Zimbabwe ya sasa. Watanzania wataidai ardhi yao na walowezi wataiweka Tanzania katika msukosuko mkubwa. 

Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html

Tuesday, January 8, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Miaka mingi iliyopita wakati nafanya kazi Dar es Salaam nilikuwa natoa huduma ya kufasiri lugha ya Kitaliani kutoka kwenye nyaraka mbalimbali zenye maandishi ya Kiingereza na Kiswahili. Nilipata kusoma nchini Italia miaka mingi iliyopita ambako nilijifunza lugha ya huko.

Kwa kuwa mimi siyo mtaalamu wa lugha mara kadhaa nilitembelea ofisi ya Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ambayo ilikuwa jirani na ofisi yangu ili kupata ufafanuzi wa maneno ambayo sikuwa na hakika niliyatumia kwa usahihi kwenye ile kazi ya tafsiri.

Wakati mmoja mtaalamu mmoja wa lugha huko BAKITA alinifahamisha kuwa maana sahihi kwa Kiingereza ya neno "tafsiri" ni translation na kuwa "kufasiri" ilikuwa na maana to translate. Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa maelezo yake, haikuwa sahihi kutamka: "Leo nimetafsiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza. Ilikuwa sahihi kusema: "Leo nimefasiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza. Hii ndiyo hoja yangu niliyokusudia kuiwasilisha leo hapa ambayo nimelazimika kuibadili baada ya kufungua kamusi ili kuhakikisha kuwa ninayotaka kuandika ni sahihi.
Nilichogundua ni tofauti kidogo na yale niliyoambiwa kule BAKITA. Ni kweli kuwa neno lina maana ile niliyofafanuliwa na yule mtaalamu. Lakini nimegundua sasa, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza toleo la 2001 iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni sahihi pia kusema: "Leo nimetafsiri aya mbili kutoka kwenye kitabu cha lugha ya Kiingereza."

Hisia zangi ni kuwa matumizi yasiyo sahihi yaliendelea kwa muda mrefu na kwa watumiaji wengi sana wa lugha ya Kiswahili na kuwafanya waandaaji wa Kamusi kuhalalisha matumizi mapya ya neno hilo.

Taarifa zinazohusiana na taarifa hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/10/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2012/11/lugha-yetu-kiswahili.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/04/lugha-yetu-kiswahili.html

Monday, January 7, 2013

Miraji Mrisho Kikwete ateuliwa Makamu wa Rais wa IBF/Afrika Maendeleo ya Vijana

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JANUARY 6, 2012

Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Afrika (IBF/Africa) limemteua Bw. Miraji Mrisho Kikwete kuwa Makamu wa Rais anayeshughulikia maendeleo ya vijana katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati. Uteuzi wa Miraji unaanza January mwaka mpya 2013.

Katika kumteua Miraji,  Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Bw.  Onesmo Ngowi alisema kuwa Miraji ana uwezo wa kuwahamasisha na kuwaunganisha vijana katika shughuli za maendeleo.

Aliendelea kusema kuwa Miraji atakuwa anawahamasisha vijana, kuwaunganisha, kuwajengea uwezo wa kimaendeleo yatakayoratibiwa na IBF.

Aidha, Rais huyo alisema kuwa Miraji atakuwa anabuni njia mbalimbali za kuwaunganisha vijana wa Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati ili waweze kufaidika na miradi ya IBF ambayo inalenga kwenye elimu, kujenga vipaji pamoja na kuwaunganisha kwenye biashara ya utalii wa michezo.

Katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika katika jiji la Honolulu, jimbo la Hawaii, nchini Marekani hivi karibuni IBF iliupokea mradi wa “Utalii wa Michezo” uliobuniwa na kuwakilishwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtazania Onesmo Ngowi.

Lengo kuu la mradi huo ni kulifanya bara la Afrika, hususan Tanzania, kuwa kitovu kikuu cha “Utalii Michezo” hivyo kujenga uchumi imara. Nchi za Tanzania na Ghana ziliteuliwa kuwa nchi za mfano kwenye mradi huo.

Katika mradi huo, IBF itatumia mtandao ilionao katika nchi zaidi ya 203 duniani kuhamasisha wanachama wake na famlia zao, wapenzi pamoja na marafiki zao kuja Afrika/Tanzania kutalii pamoja na kuwekeza katika miradi mbalimbali.

Uteuzi wa Miraji utasaidia kuwaunganisha vijana ili waweze kuchangia na kufaidika na biashara ya utalii kwenye mradi huo na umefanywa wakati muafaka.

Miraji ambaye ni mjasiriamali amejipambanua katika maendeleo ya jamii na ana mchango mkubwa sana katika kuendeleza vijana nchini Tanzania.

Rais Ngowi alimwelezea Miraji kama tegemeo ambalo vijana wanalihitaji kwani wanahitaji uhamasishaji wa hali ya juu na Miraji ana uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa kwani alishawahi kuifanya kwa kipindi kirefu.

Miraji Mrisho Kikwete ni msomi wa Chuo Kikuu cha nchini Oman ambako amesomea elimu ya utawala wa biashara ambayo ndiyo lengo kuu la uteuzi wake. Ana haiba ya kupendwa na vijana pamoja na uwezo wa kujichanganya nao.

Imetolewa na:


Makao makuu
IBF Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati
Dar-Es-Salaam, Tanzania

Thursday, January 3, 2013

Taarifa ya Serikali kufafanua kuhusu miradi ya utafutaji na uvunaji wa gesi asilia nchini


****************************************************
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUFAFANUA KUHUSU MIRADI YA
UTAFUTAJI NA UVUNAJI WA GESI ASILIA NCHINI

1.0   UTANGULIZI

Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi Asilia ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa  yatakayopatikana kwa wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi.

Siku ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara, wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya  maandamano ya kudai raslimali ya Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara ya  Nishati  na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania wote kwa kupitia vyombo vya habari.

Tokea Uhuru, uchumi wa Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile katani (Tanga na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa (Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma  na Mara),  chai (Iringa) na tumbaku (Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya nchi yetu   bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka       mikoa    hiyo     hawajawahi     kufanya        maandamano  wakidai
upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania wengine) wa aina yo yote ile.

1

Mapato   yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga  na  Tabora),  almasi  (Shinyanga)  na  tanzanite   (Manyara) yamewanufaisha Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule! Minofu ya samaki wa Ziwa Victoria (Mara, Mwanza na  Kagera) imeliingizia Taifa letu fedha nyingi ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wo wote.

Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote. Mahindi kutoka Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu bila kujali eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi hayo ni kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na Kagera inatumiwa na wakazi  wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya mikoa inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa  aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam bila manunguniko yo  yote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo cha Mto Ruvu.

Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya  wenyeji  wa sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo yote ile kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya      Upinzani         kupanga,  kuhamasisha,                     kushabikia   na    kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara Mjini.

2.0   RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA

Gesi Asilia ilianza kugundulika hapa nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa  cha  Songo  Songo,  Mkoani  Lindi.  Baada  ya  hapo  Gesi  Asilia imegundulika maeneo ya Mtwara Vijijini, yaani Mnazi  Bay (1982) na Ntorya (2012), Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha
Gesi Asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa Futi za

2

Ujazo  Trilioni   4.5   –  8.  Katika  kipindi  cha  miaka  mitatu  iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia uliojikita zaidi  kwenye  maji  ya  kina  kirefu  cha  bahari.  Kiasi  cha  Gesi  Asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji inafikia  takribani Futi za Ujazo Trilioni 27. Kiasi cha wingi wa Gesi Asilia yote iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 35.

Kufuatana  na  Sheria  za  nchi  yetu  zinazotumiwa  kugawa mipaka  ya mikoa iliyopo kando  kando mwa bahari (isivuke 12 nautical miles au
22.22 km kuingia baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika
Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14 tu ya gesi yote iliyogundulika nchini. Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa yetu, Lindi inayo 7% ya gesi yote, Pwani 1% na huku Kina Kirefu cha Bahari (Deep Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%) kuliko mikoa yote    ikiwekwa pamoja!         Kwa          hiyo,       hakukuwa  na               haja         ya   kufanya maandamano kwa sababu Gesi Asilia nyingi inapatikana kwenye bahari ya kina kirefu ambayo iko  ndani ya mipaka ya nchi yetu bila kujali mipaka ya mikoa yetu. Isitoshe Gesi Asilia imegundiliwa kwenye miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa Miaka kati ya Milioni 199.6 hadi 23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa yetu haikuwepo wakati huo!

Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia pia unaendelea tukiwa wa mategemeo makubwa  ya  upatikanaji  wa  raslimali  hizi  katika  Mikoa  ya  Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe,  Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia  mpaka  wetu  na  Msumbiji  hadmpaka     wetu  na   Kenya. Hatutarajii  mikoa  hii  nayo  ifanye  maandamano  ya  kutaka  kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na Mafuta zitakapogunduliwa mikoani mwao.

3.0   MATUMIZI   YA   GESI   ASILIA   YA   MNAZI   BAY   (MTWARA)   NA SONGO SONGO (LINDI)

Mpaka hivi sasa Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka
Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi

3

Bay kwa sasa huzalisha umeme kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu. Mitambo ya kufua  umeme kutokana na Gesi Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao uwezo wa kuzalisha MW 18 lakini  matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na Lindi haijavuka MW 12. Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni za Wentworth na Maurel & Prom zikizalisha Gesi Asilia            (inayotumiwa na TANESCO) kiasi cha Futi za Ujazo Milioni 2 kwa siku. Ikumbukwe kwamba  ufuaji wa umeme wa hapo    Mtwara          Mjini      ulikuwa mikononi         mwa   Kampuni ya  Artumas iliyofilisika.  Tangu   Desemba   2006   hadi   leo   hii   kiasi   cha   gesi kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya mikoa hiyo miwili ni chini ya asilimia 1 ya gesi yote iliyogundulika  Mnazi Bay (Mtwara Vijijini). Vilevile  ikumbukwe kwamba  kuna  visima  vinne  vya  Gesi  Asilia  pale Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na kinachotumika kwa sasa na tena kwa kiwango cha chini kabisa ni kimoja tu!

Aidha ni vizuri ndugu zangu Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii  inatafutwa  na  kuchimbwa na  wawekezaji  wenye  mitaji  mikubwa, wataalamu na teknolojia ya utafutaji na uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa kurejesha mitaji yao. Uchorangaji wa kisima kimoja  cha utafutaji wa Gesi Asilia nchi kavu unahitaji Dola za Marekani Milioni
40, na kwenye kina kirefu cha maji baharini zinahitajika zaidi ya Dola za       Marekani    Milioni    100.    Ikumbukwe       kwamba, Serikali    kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Tanzania (TPDC), inatumia fedha za walipa  kodwa   nchi nzima  kwa  shughuli     za   kuvutia,            kuratibu       na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia nchini kote ikiwemo Mikoa            ya  Mtwara    na             Lindi.         Walipa   kodi            Wa-Tanzania        bado hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai            fedha zao za kodi zisitumike huko Mtwara!

Ni muhimu pia tukaelewa kwamba Gesi Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) inazalisha umeme  peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi.  Gesi  Asilia  ya  Songo  Songo  (Kilwa,  Lindi)  ndiyo  inayotumika kuzalisha                 umemkwa  ajili  ya  Gridi  ya  Taifa,  na  pia  kwa  ajili  ya
wananchi  wa  Kisiwa  cha  Songo  Songo  (Lindi),  maeneo  ya  Somanga

4

Fungu  (Lindi)  na  viwandani  (Dar  Es  Salaam)TangOktob2004 ambapo mitambo ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha Gesi Asilia ya Songo Songo kilichotumika ni asilimia 7 tu ya Gesi Asilia yote iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba hata uchumi wa Jiji la Dar Es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha Gesi Asilia  (7%)  iliyopo  Songo  Songo  (Kilwa,  Lindi).  Ikumbukwe  kwamba waajiriwa kwenye viwanda vya Dar Es Salaam wamo wanyeji wa kutoka Mtwara       Mjini    ambako     maandamano     yalifanyika     na       vilevile   wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa Vyama vya Siasa  vya Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.

4.0   MIPANGO YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5 HADI 10

(a)  Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam:

Kuuza Gesi Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80% ya  mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa ki-uchumi. Tayari kuna viwanda
34 vinatumia Gesi Asilia  ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo gesi zaidi  itapatikana. Soko kubwa la Gesi Asilia lipo        tayari  Dar   es  Salaam  (na  siyo   Mtwara),  ambapo  ipo mitambo  ya   kufuumeme   kwa   kutumia         mafuta. Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia kila siku. Takribani   Dola za Marekani Bilioni  Moja  (sawna   ShilingTrilioni    1.6)   kwa  mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini ikifua umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei  kubwa  sana.  Bei  ya  umeme  kwa  uniti  moja  (KWh)  ya umeme unaofuliwa kutumia dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya Senti za Marekani 30 hadi 45 na huku bei ya      uniti moja hiyo hiyo ni Senti za Marekani 6-8 kwa umeme utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi.

Vilevile, takribani Dola za Marekani millioni 202 kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji  la  Dar Es Salaam litatumia Gesi Asilia badala ya mafuta katika magari, taasisi na majumbani. Fedha

5

hizi zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa manufaa  ya Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale walioratibu maandamo ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.

(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na Gesi Asilia:

Bomba la Gesi Asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es Salaam) kufua umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia  Somanga  Fungu  (Lindi)  wa  kiasi  kisichopungua  MW
520.

(c) Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu:

Dar   es   Salaam   ndiko      kuna   miundombinu  mikubwa   ya usafirishaji  na  usambazaji  wa  umeme  kuliko  mikoa  mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi unaotulazimisha kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka Dar Es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa moja viwandani, majumbani na kwenye magari.

(d) Kwa  kuzingatia  mahitaji  ya  Gesi  Asilia  yatakayojitokeza: Bomba  la kusafirisha  gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off) katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji hii inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika. Kwa hiyo kuweka mitandao ya usambazaji        wa gesi   kutoka              kwenyBomba           la           Gesi       Asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya Gesi Asilia viwandani na majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine kwa siku za baadae.

(e)Serikali   imetenga   maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini (Lindi na           Mtwara)         kwa  ajili  ya   uanzishwaji      wa           maeneo             ya viwanda    (Industrial Parks/Estates)   vikiwemo      viwanda vya mbolea,  Liquefied    Natural    Gas   (LNG)   na   Petrochemicals. Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko katika hatua za mwisho za maandalizi.
(f) Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya Gesi Asilia na Mafuta kwa kampuni za  huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo maalumu Mtwara,  ambalo  litawekewa

6

miundombinya   msingi   ili   kutoa   vivutio  mbalimbali  kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone).

Ni lazima shughuli za kusafisha na kusafirisha Gesi Asilia zitatoa ajira katika  maeneo  husika.  Kwa  mfano  kwa  mitambo  ya  kusafishia  gesi inayojengwa Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi), kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Watanzania  wanakumbushwa  kuwa  raslimali  zilizopo  nchini  ikiwemo gesi asilia, madini, makaa  ya mawe, wanyama pori, misitu, milima ya utalii, mito, maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote kwa mujibu wa Katiba ya             Jamhuri          ya    Muungano   wa   Tanzania.   Raslimali   hizi zinapatikana,  zinatunzwa  nkuzalishwmaeneo  mbalimbali  nchini mwetu na mapato yake yanatumika kwa maendeleo ya Wa-Tanzania wote bila kujali maeneo raslimali hizo zilipo.


Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani  mwetu. Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu    kwa          kisingizio             cha   raslimali   zilipo    kwenye    wilaya   zetu. Tusikubali kuvunjavunja  wilaya zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu. Tusikubali  kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye kata zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU 
Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)
WAZIRI YA NISHATI NA MADINI JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


7