Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, December 19, 2017

Hili sijalielewa hata kidogo

Imefika wakati Jeshi la Polisi libadilike kidogo.

Kuna umuhimu wa polisi kuboresha huduma kwa tunaofika kwenye vituo vya polisi ili tupate huduma inayoridhisha. Nazungumzia wahalifu na wasiyo wahalifu. Wote tunastahili kupewa huduma ya kuridhisha.

Hivi karibuni, nikiwa naendesha gari, nilisimamishwa Singida mjini na afisa usalama barabarani kwa kosa la kutosimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu.

Nilikiri kosa haraka na kukubali kulipa faini ili niendelee na safari. Suala ambalo lingechukua dakika tano lilichukua saa nzima.

Nilielekezwa kwenda kituoni na afisa aliyenikamata akafika baada ya dakika kumi kunijazia hati ya malipo. Nilipodai risiti nikaambiwa mhasibu ameshaondoka, nirudi asubuhi kuchukua risiti. Ilikuwa saa kumi jioni.

Nilimfahamisha kuwa niko safarini na isingewezekana kurudi asubuhi. Ilikuwa naambiwa nirudi asubuhi kama vile naishi Singida.

Ni mpaka mhasibu alipopigiwa simu na afande ndipo aliporudi na kuniandikia risiti. Alikuwa kanuna sana kwa kurudishwa ofisini. Mdomoni alikuwa na kijiti cha kuondoa nyama zinazobaki kati ya meno baada ya kula nyama ya kuchoma.

Maoni yangu ni kuwa wakati wowote mhalifu anapotozwa faini anapaswa kupewa risiti wakati huo huo anapotozwa faini. Siyo sawa polisi wakatumia sheria kutoza faini halafu wakapuuzia kutoa risiti wakati huo huo.

Ama sivyo mhasibu anapofunga ofisi na faini zisitozwe.

Halafu, si tumeshapewa somo kuwa tusilipie kitu chochote bila kudai risiti? Au hilo somo haliwahusu polisi?

Mimi naamini linawahusu. Kupewa risiti baada ya kulipa faini si hisani. Ni haki.

Saturday, November 18, 2017

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao

Njia kuu mbili za kuumbuliwa na matusi ya mtandao ni adhabu ya sheria, na kukutana uso kwa uso na unayemtukana.

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ni sheria ambayo inaainisha matusi kama mojawapo ya makosa ambayo yanaweza kumtia mtu hatiani kwa yale anayoyaandika au kwa picha anazoweka mtandaoni. Kuna baadhi ya watu, au kwa kutokujua sheria au kwa makusudi, tayari wametiwa hatiani na maandiko ambayo yanaainishwa kuwa makosa kwenye sheria hii.

Na sina shaka kuna wengi wengine watakumbwa na tatizo hilo kwa sababu inaelekea kuna watu wanaamini kuwa akiwa kajibanza pembezoni mwa nchi akarusha matusi kwenye mtandao basi siyo rahisi kupatikana.

Tatizo la kuonana uso kwa uso limenitokea leo baada ya kutembelewa Butiama na Fabian Zegge, "rafiki" wa mtandao ambaye sikutarajia kuonana naye hata siku moja. Alifika Musoma kwenye shughuli zake na akaamua kunitembelea Butiama.

Mara baada ya kusalimiana naye nilimwambia kuwa angekuwa ni mtu ambaye tulirushiana maneno yasiyo na ustaarabu katika mawasiliano yetu kwenye mtandano, leo hii ningeona aibu kujitokeza kusalimiana naye. Ningemwambia amekosea namba ya simu aliponipigia awali kutaka kufahamu iwapo nipo nyumbani.
Kutoka kushoto kwenda kulia: mimi, Fabian Zegge, na mwenyeji wake.
Nimejifunza mambo mawili ya msingi leo: kwanza, hawa "marafiki" wa ndani ya mtandao ambao wengi wetu tunaamini hatutaonana nao hata siku moja ni watu ambao tunaweza kuonana nao wakati wowote. Sikutarajia kuonana na Fabian Butiama.

Pili, na kwa kutambua ukweli huo, nimeone umuhimu kwamba tunapowasiliana na watu mbalimbali kwenye majukwaa kwenye mtandao tunapaswa kuongozwa na ustaarabu kwenye kauli zetu.

Bila kuzingatia hayo tutaumbuliwa na sheria au aibu ya kukutana na tunaowatukana.

Saturday, November 11, 2017

Mimba zisizoisha za Chausiku Suleiman

Zaidi ya miaka sita iliyopita nilipata fursa ya kumtembelea mama mmoja, Chausiku Suleiman, anayeishi Maji Chai, jirani na Tengeru kwenye barabara kuu ya kutoka Moshi kwenda Arusha. Alinipa simulizi za ajabu. Yeye anapata ujauzito kila anapojifungua, bila hata kukutana na mume wake.

Nilipoonana naye alikuwa na umri wa miaka 47 na alikuwa na watoto 16 aliyewazaa ndani ya kipindi cha miaka 30. Tatizo lake lilianza alipopata ujauzito wa mtoto wa tano. Majuma matatu baada kujifungua alihisi kuwa alikuwa mjamzito tena. Nilipoonana naye mwaka 2011 alisema kuwa mimba yake wakati huo ilikuwa ina zaidi ya miaka mitatu.

Chausiku Suleiman akiwa na baadhi ya watoto wake, Maji Chai, Arusha.
Nilipomuuliza iwapo ametafuta ushauri wa daktari aliniambia kuwa madaktari wameshindwa kubaini tatizo lake na wameshindwa kuona kama ana kichanga tumboni.

Alisema anahisi kuwa madaktari wanaamini kuwa ana imani kuwa na tatizo ambalo halipo.

Saturday, September 2, 2017

Hivi Mwalimu Nyerere alikuwa Yanga au Simba?

Hivi Mwalimu Nyerere alikuwa Yanga au Simba? Hili ni swali ambalo nimewahi kuulizwa sehemu ambayo sikutarajia kabisa kuulizwa.

Mwaka 2012, nikiwa kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro nikiongozana na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto ya Mwanza, nilipokea simu wakati tukitembea kati ya kambi ya Horombo na kambi ya Kibo.

Aliyenipigia simu alijitambulisha akisema mimi hununua vocha za simu kwenye kibanda chake mjini Musoma.

Alinisimulia kuwa alikuwa anabishana na wenzake, baadhi yao wakisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, wengine wakipinga na kusema siyo kweli. Akaniomba mimi nimalize ubishi wao.

Kwanza, ingawa nilikuwa kwenye njia ya Marangu kuelekea kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, njia ambayo inasemekana kuwa ni moja ya njia rahisi za kufika kileleni, ukweaji Mlima Kilimanjaro wakati wote unampa mtu changamoto za kila aina.

Mawasiliano ya simu za kiganja huwa ni ya kubahatisha kutegemea na sehemu ulipo na kutegemea na hali ya hewa. Mlimani kwenyewe pumzi inavutika kwa kutumia nguvu na jitihada ya ziada. Aidha, kwa sababu ya baridi chaji ya betri ya simu haikai kwa muda mrefu.

Kwa sababu hizo, unapopigiwa simu, unategemea itahusiana na suala la dharura au linalohusiana na kazi au suala lingine la aina hiyo.

Lakini nilielewa kuwa, kwa aliyenipigia simu, kufahamu kama Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga au la ilikuwa muhimu kwake kwa wakati ule.

Nilimwambia kuwa hata mimi husikia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa Yanga, na wakati fulani wazee wa Yanga walitembelea Butiama nikawauliza swali hilo lakini kwa wakati ule aliponiuliza sikukumbuka walinijibu nini.

Ninachokumbuka ni kusikia mtu akisema kuwa kadi namba 1 ya Dar es Salaam Young Africans huwa haijulikani kapewa nani, na ndiyo hiyo watu wanasema ilikuwa kadi ya Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere mwenyewe aliposimulia kuhusu kuhudhuria mechi za soka alisema ilikuwa muhimu kuwa asikae mtu mbele yake, kwa sababu kila wakati mchezaji alipokaribia kufunga goli naye alikuwa akirusha mguu mbele kupiga mpira hewa.

Bofya kwenye picha hapo chini kusoma taarifa juu ya mechi chache za mpira ambazo Mwalimu Nyerere alihudhuria:
Mwaka 1972, Rais Jaffar El Nimeiry wa Sudan akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwenye mechi ya soka dhidi ya timu ya taifa ya Sudan.
Taarifa nyingine kama hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/07/simba-sports-club-wakaribishwa-butiama.html

Friday, August 25, 2017

Umuhimu wa wagombea huru sasa umejidhihirisha

Hii ni makala yangu ya tarehe 11 Agosti 2015 kwenye safu yangu inayoitwa Ujumbe toka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri linalochapishwa kila Jumanne.
******************************************
Kama unahitajika ushahidi kuwa upo umuhimu wa kuruhusiwa kwa wagombea huru ndani ya Katiba ya Tanzania, basi huo ushahidi umejitokeza baada ya matukio ya hii karibuni yaliyomo ndani ya siasa za Tanzania.

Tukio lililohitimisha ukweli huo ni kuhama kwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Kwa maelezo yake, amehama kutoka CCM kwenda CHADEMA kwa sababu “…mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjifu wa Katiba, na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM.”

Aliendelea kusema: “Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo zaidi na chuki iliyokithiri dhidi yangu.” Kilichotokea Dodoma, kwa mujibu wa maelezo yake, ni kubaka Demokrasia.

Amehamia CHADEMA akiamini kuwa yale yaliyomkuta ndani ya CCM hayawezi kutokea ndani ya CHADEMA. Na dalili ni nzuri kwake mpaka sasa kwa sababu CHADEMA hawakuchukua muda mrefu na walimpa nafasi ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nafasi ambayo CCM haikumpa. Hatimaye amepitishwa kuwa ni mgombea urais wa muungano wa vyama vya siasa vinavyojulikana kama UKAWA.

Mwalimu Nyerere amenukuliwa na Lowassa akitamka kuwa Chama cha Mapinduzi siyo baba yake [Mzee Nyerere Burito], wala mama yake [Mugaya wa Nyang’ombe] na kuwa akikosa mabadiliko ndani ya chama hicho, basi atayatafuta nje ya chama hicho. Mheshimiwa Lowassa amekosa mabadiliko ndani ya CCM na anaamini atayapata ndani ya CHADEMA na UKAWA. Swali ambalo halijaulizwa ni hili: asiyeona mabadiliko ndani na nje ya CCM anakuwa mtoto wa nani?

Kwangu mimi haipo sababu ya msingi ya kuwepo yatima wa kisiasa nchini. Jawabu ni kuwepo kwa mfumo wa kikatiba unaoruhusu wagombea huru kama nguzo ya tatu kwenye siasa. Wagombea huru watatoa fursa kwa wanachama waliokosa macho ya kuona na masikio ya kusikia fursa za mabadiliko zilizomo ndani ya chama tawala na ndani ya vyama vya upinzani kutafuta mabadiliko hayo kwingineko kama wagombea huru, au kama watetezi wa wagombea huru.

Kuna mengi ambayo mtu anaweza kuunga mkono ndani ya sera za vyama tofauti vya siasa, lakini akawa pia hakubaliani na kipengele cha sera kwenye vyama hivyo hivyo. Aidha, kuna maamuzi ambayo yanaweza kupitishwa na chama anachokiunga mkono ambayo hayaafiki. Mtu wa aina hii anapaswa kupewa fursa ya kikatiba ya kupenyeza mawazo yake bila kulazimika kuchukua uamuzi ambao tunaousikia kwa baadhi ya watu wa kustaafu siasa au kuachia wadhifa wake ndani ya chama cha siasa, kwa sababu tu haoni chama ambacho kinawakilisha matakwa yake kwa wakati huo.

Kinadharia, chama kinachotawala au chama cha upinzani kinachobaini hali hiyo kitatambua ukomo wa kile ambacho mimi naita jeuri ya chama, au uhakika wa chama cha siasa kuwa kile kinachoidhinishwa na maamuzi rasmi au yasiyo rasmi ya chama ndiyo mwisho wa mjadala na kufungwa kwa kikao. Mfumo wa wagombea huru unaweza kuwa kama sehemu ya mwisho ya kukata rufaa kwa wananchi kwa sababu hiyo ya uwepo wa kukinzana kwa mitazamo baina ya mtu na mienendo ya chama alichokiunga mkono.

Woga mkubwa wa washiriki wa siasa za siku hizi ni kushindwa uchaguzi, siyo kung’ang'ania misimamo ambayo nyakati hizi inaitwa imepitwa na wakati.

Kwenye nadharia ya siasa chama cha siasa kinapaswa kuwa tayari kushindwa kwenye uchaguzi kwa sababu ya kushikilia misimamo mbalimbali ambayo kimekuwa kikiunga mkono kwa mujibu wa sera zake. Kwenye miaka ya mwanzo baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mwalimu Nyerere, akiwa Waziri mkuu wa wakati ule, alipingana na baadhi ya wawakilishi wa chama cha TANU bungeni na wa serikali yake, ambao wakati wa kujadili muswada wa uraia wa Tanganyika walidai kuwa uraia wa Tanganyika uwe haki ya Watanganyika wenye ngozi nyeusi tu. Katika kupinga msimamo wa wenzake na akiwa anatetea hoja kuwa kila Mtanganyika anayo haki ya kuwa raia bila kubaguliwa kwa rangi ya ngozi yake, Mwalimu Nyerere alisema kuwa serikali yake itakuwa tayari kushindwa kwenye kura bungeni na kuondoshwa madarakani lakini haiwezi kukiuka misingi ya haki na usawa ambayo yenyewe iliipigania na kuitetea.

Leo hii ndani ya siasa tunashuhudia kuwa misimamo ni kama mashati ambayo hubadilishwa kwa mujibu wa mahitaji yanayojitokeza.

Kwa mtazamo wangu, vyama vyote siasa vinaweka mikakati ya kufika Ikulu tu, kwa kushinda uchaguzi mkuu ujao. Kwa CCM ni kupigana kufa na kupona kuhakikisha kuwa Edward Lowassa hawi rais wa tano wa Tanzania.

Kwa UKAWA hali hii ni dhahiri kuliko kwa CCM. Hatutarajii kuwa jambo rahisi kwa vyama vinne vya siasa kukubaliana kwa yote yaliyomo kwenye sera zao. Kwao jambo la msingi itakuwa “Rais wetu akishaapishwa tutajua la kufanya.”

Ukweli haupingiki kuwa lipo pengo ndani ya siasa ambalo linalazimisha sehemu fulani ya wapiga kura ya Watanzania kuwepo kwenye siasa za vyama ambazo haziwakilishi kikamilifu matakwa yao. Suluhisho ni wagombea huru. Wagombea huru hawatamaliza hitilafu zilizopo lakini watazipunguza kwa kiasi kikubwa.

Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2017/07/afrika-tunaibiwa-sana-tena-sana.html

Saturday, August 19, 2017

Simulizi za Samora Machel, rais wa kwanza wa Msumbiji

Miaka kadhaa iliyopita nilihudhuria mkutano uliyoandaliwa jijini Maputo Msumbiji na muungano wa vyama vya wanajeshi na wapiganaji wa zamani walioshiriki vita mbalimbali duniani. Chama chao kinaitwa Worlds Veterans Federation.

Katika moja ya hafla zilizoandaliwa na Rais wa Msumbiji wa wakati huo Armando Guebuza, nilipata fursa ya kukaa na mzee mmoja mpiganaji wa zamani wa jeshi la ukombozi la FRELIMO ambaye alishiriki kwenye vita ya ukombozi ya Msumbiji.

Alinisimulia mengi juu ya maisha yao walivyokuwa kwenye kambi za FRELIMO zilizokuwa Tanzania, na baadhi ya matukio katika vita iliyoshiriki.

Alisema kuna wakati Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ilitembelea baadhi ya maeneo yaliyokombolewa ndani ya Msumbiji na kupokelewa na Samora Machel, wakati huo akiwa rais wa FRELIMO aliyeshiriki mwenyewe katika mapambano.

Waliandaa chakula kwa ujumbe ulioyoongozwa na Katibu Mtendaji wa kamati, Hashim Mbita. Lakini walipokuwa tayari kuanza kula tu, hapo hapo ndege za jeshi la Ureno zilianza kushambulia kambi ile na chakula kikaachwa ili kunusuru maisha yao.

Inaelekea jeshi la Ureno lilipata taarifa ya ziara ile.

Mwalimu Nyerere na Samora Machel kwenye moja ya mikutano ya hadhara.

Niliambiwa kuwa Samora mwenyewe aliongoza mikakati ya kulinda usalama wa ule ujumbe, akiwatanguliza wageni wakikimbia mbele na wakiwa wamezungukwa na ulinzi mkali wa wapiganaji wa FRELIMO. Nikaambiwa Samora mwenyewe alikuwa wa mwisho, nyuma ya kila mtu, akiwa ameshika bastola yake mkononi.

Ni kielelezo cha ushujaa wa baadhi ya viongozi wetu wa zamani. Yule mzee alinitolea simulizi hii huku akicheka kuwa wageni hawakuweza kula siku ile.

Taarifa nyingine ambazo unaweza kupendelea kusoma:
https://muhunda.blogspot.com/2016/12/redio-ya-Mwalimu-Nyerere.html
https://muhunda.blogspot.com/2012/09/wageni-wa-butiama.html

Saturday, August 5, 2017

Baraka Elias, Mtanzania mrefu kuliko Watanzania wote

Nimewahi kuonana na Baraka Elias, Mtanzania mrefu kuliko Watanzania wote, alipotembelea Butiama mwaka 2012. Ana urefu wa mita 2.20 na umri wa miaka 27.
Kwenye picha juu ni yeye pamoja na Notburga Maskini anayeongea naye, kushoto. Notburga tumewahi kuongozana naye kwenye moja ya misafara yangu ya kukwea Mlima Kilimanjaro.

Taarifa nyingine za Baraka Elias hizi hapa (kwa Kiingereza):

Taarifa nyingine za Notburga Maskini hizi hapa (kwa Kiingereza):

Friday, July 28, 2017

Afrika tunaibiwa sana, tena sana

Hii ni makala yangu ya tarehe 18 Julai 2017 kwenye safu yangu inayoitwa Ujumbe toka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri linalochapishwa kila Jumanne.

******************************

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali Global Justice Now inaeleza jinsi gani bara la Afrika linavyoibiwa rasilimali yake.

Ripoti hiyo, inayoitwa Honest Accounts 2017, inaeleza kuwa kwa mwaka 2015 mali na pesa za thamani ya Dola za Marekani bilioni 203 zimetoka Afrika kwa njia ya faida ambazo mashirika ya kimataifa yamepata kutokana na shughuli za biashara na uzalishaji barani Afrika, na kwa mianya haramu ya pesa zinazotumwa nje. Wakati huo huo ni kiasi cha Dola bilioni 161.6 tu ambazo kwa mwaka huo ziliingia barani Afrika kwa njia ya mikopo, kutuma pesa kwa watu binafsi kutoka nje ya bara la Afrika, na misaada.

Huu utafiti unatukumbusha tu kuwa bara la Afrika ni tajiri, lakini kwa bahati mbaya Waafrika tunakubali, au kwa kutokujua au kwa kudanganywa, kuwa sisi ni maskini. Hali hii inatufanya sisi na serikali zetu kuwa na mawazo ya ombaomba ambaye badala ya kutumia uwezo aliojaliwa kutafuta riziki, anazunguka mitaani kuomba watu pesa za kuendesha maisha yake.

Taarifa inaendelea kufafanua jinsi bara la Afrika linavyoibiwa na mashirika ya biashara ya kimataifa. Wakati bara la Afrika linapokea kiasi cha Dola bilioni 19 kwa njia ya misaada kutoka nje, kiasi cha Dola bilioni 68 zinahamishwa kwenda nje na mashirika haya ambayo, kwa kawaida na kwa makusudi, hayataji thamani halisi za bidhaa wanazoingiza barani Afrika na mali inayoondoshwa kwenda nje. Ni hitimisho ambalo linafanana na hitimisho lililofikiwa na taarifa ya kwanza ya makinikia. Tofauti ni kuwa taarifa hii haitolewi na wataalamu waliyotumwa na Rais John Magufuli ila na shirika lililopo Ulaya ambalo linamulika kiwango cha wizi dhidi ya Afrika.

Pamoja na shutuma hizi dhidi ya wizi unaoendelea kudhoofisha maisha ya Waafrika, ni muhimu kutofautisha aina ya wizi huu. Kwanza, upo wizi ambao lazima tukubali kuwa ni wizi halali ambao unalindwa na sera na sheria mbovu zilizopitishwa na mabunge ya nchi za Afrika kulinda mifumo inayonyima Waafrika fursa ya kufaidika na utajiri wao.

Tutakuwa tunajidanganya kama hatutakubali kuwa rushwa ni mojawapo ya vichocheo vikubwa ambavyo vilisababisha baadhi ya nchi hizi kuweka sera na sheria ambazo, kwa ujumla wake, hazilindi maslahi ya Waafrika bali zinalinda maslahi ya mashirika ya nje kufuja rasilimali za bara letu na kuwaacha wananchi wake kuwa watumwa wa mali yao wenyewe.

Hata hivyo yapo mazingira ambayo hayasukumwi na rushwa ambapo inaziweka nchi za Afrika wakati kwenye shida kubwa za kiuchumi zinazowalazimisha kuweka mazingira yasiyo na manufaa kwa wananchi wake.

Madai ya kutaka kubadilisha mifumo hii ambayo yamejitokeza sasa nchini Tanzania yamewahi kujitokeza kwenye sekta ya madini nchini Zambia. Ilipobinafsisha migodi yake ya kuchimba shaba, Serikali ya Zambia ilikuwa inakabiliwa na uzalishaji mdogo na gharama kubwa ya kugharimia uzalishaji iliyokadiriwa kufikia Dola milioni moja kwa siku.

Ilipotafuta msaada kutoka mashirika ya fedha ya nje ikaambiwa dawa ni moja tu: ubinafsishaji. Kwa usiri ule ule ambao tuna uzoefu nao hata sisi, serikali ya Zambia ilifanya majadiliano ya ubinafsishaji na wawekezaji ambao, ingawa sheria ya madini ilitaka walipe mrahaba wa asilimia 3 kwa serikali kwa mauzo ya shaba nje ya nchi, mkataba wa siri uliwaruhusu kulipa asilimia 0.6. Aidha, makampuni ya kuchimba madini yakapunguziwa kodi ya mapato kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba wafanyakazi waliowaajiri wakawa wanalipa kodi kubwa zaidi kuliko makampuni hayo.

Huu nauita wizi halali, kwa sababu kimantiki ni wizi tu hata kama unalindwa na sheria za nchi. Pili, upo wizi ambao unakatazwa kwa mujibu wa sheria. Inakadiriwa kuwa kiasi cha Dola bilioni 29 zinafujwa barani Afrika kutokana na biashara haramu ya magogo, uvuvi, na biashara za wanyamapori na mimea. Biashara haramu ya pembe za ndovu inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola bilioni 10.

Njia nyingine ambayo inainyima Afrika manufaa inayotokana na mali yake ni kukosekana kwa viwanda vinavyochakata malighafi zake. Tunauza pamba nje ya nchi halafu tunanunua nguo zinazotokana na pamba hiyo. Tofauti ya thamani ya malighafi na bidhaa iliyotengenezwa inabaki nje.

Tunaruhusu utaratibu wa kupeleka nje makinikia badala ya kuweka mitambo barani Afrika ya kuchakata madini, na kwa hali hiyo kukosa ongezeko la thamani ya mali inayopelekwa nje na mapato kwa serikali zetu.

Kwa kifupi ripoti iliyotolewa inatukumbusha tu kuwa sehemu kubwa ya nchi zinaozoendelea zinanufaika na utajiri wa Afrika kuliko sehemu kubwa ya Waafrika wenyewe. Zile porojo kuwa nchi tajiri zinasaidia bara la Afrika hazina ukweli wowote. Ni bara la Afrika ambalo linasaidia nchi tajiri.

Kuna hotuba nzuri sana ya Mwalimu Nyerere inayotuasa tusikubali kusikia kelele tunazopigiwa tunapoazimia kufanya jambo lenye manufaa. Kwenye hotuba anasema kuwa tunapozidi kukaribia lengo, na kelele zitazidi kuwa kubwa.


Vita vya kurudisha mikononi mwa Waafrika utajiri wao inahitaji kutumia uzoefu mkubwa na maarifa. Lakini ni vita ambayo inahitaji kuiendesha huku tukiwa tumeziba masikio kuepuka kuyumbishwa na kelele ambazo zinazidi kuongezeka ili kutuondoa kwenye safari ya kurejesha na kuimarisha hadhi na heshima ya bara la Afrika.

Friday, July 21, 2017

Mamlaka ya Mapato Tanzania yawageukia wauza spea

Nimesikia taarifa ya habari asubuhi hii kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania wameanza kukagua maduka ya wauza spea za magari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mamlaka inachunguza bidhaa hizo zilizopo madukani ili kupata uthibitisho wa wenye maduka kuwa wamepata hizo bidhaa kwa njia za halali.

Kwa muda mrefu inaaminika kuwa baadhi ya wenye maduka yanayouza spea za magari wananunua spea hizo kutoka kwa wezi wa magari, au wezi wanaoiba spea kutoka kwenye magari.

Hizi hatua zikiendelea kwa muda mrefu zinaweza kupunguza wizi wa spea za magari, na hata wizi wa magari.

Miaka mingi iliyopita nilipoishi Dar es Salaam niliwahi kuibiwa kioo cha mbele cha gari. Nilipotoa taarifa kituo cha polisi niliambiwa na polisi kuwa wana hakika kuwa kioo changu kitapatikana Gerezani, eneo la Dar es Salaam ambalo huuza bidhaa mbalimbali zilizotumika, nyingi ya hizo zikiwa bidhaa za wizi.

Wezi watapungua
Askari wa upelelezi wawili nilioambatana nao kuelekea Gerezani walinushauri kubaki mbali kidogo na eneo wakati wao walipoingia Gerezani na wakarudi baada ya muda na kuniambia kuwa kioo changu, ambacho kilikuwa na namba ya gari yangu, wamekiona. Hawakutaka niongozane nao kwa sababu walisema nafanana sana na polisi na tungekuwa pamoja tusingepata ukweli.

Cha ajabu ni kuwa wale polisi walinishauri ninunue kioo changu. Bila hivyo walisema sitakipata. Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa kupata mali ya wizi wakati huo.

Bila shaka hizi jitihada mpya za Mamlaka ya Mapato zitapunguza kasi ya wizi, na zitaleta mabadiliko chanya kwa wamiliki wa magari.

Taarifa nyingine kama hii:
https://muhunda.blogspot.com/2016/07/mada-yangu-ya-leo-mwizi-ni-mwizi-tu.html
https://muhunda.blogspot.com/2011/07/maana-sahihi-ya-neno-fisadi.html

Friday, July 14, 2017

Simulizi za Jaffar Idi Amin

Hii simulizi nilipewa na Jaffar Idi Amin, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Uganda kati ya mwaka 1971 hadi 1979, Idi Amin Dada.

Anasema kuna siku alikuwa kwenye matembezi kwenye jiji la Kampala akakuta gari aina ya Volkswagen imeegeshwa na akasimama kwa muda mrefu akiiangalia kwa sababu aliitambua kuwa ilikuwa gari ya zamani ya baba yake.

Akiwa anaiangalia akatokea mtu na kumsalimia na kumuuliza sababu za kukaa muda pale akiangalia ile gari. Mazungumzo yakawa hivi:

"Mbona unaishangaa sana hiyo gari?"
"Ilikuwa gari ya baba yangu."
"Baba yako nani?"
"Idi Amin."

Anasema alivyotamka jina la baba yake yule aliyekuwa anamhoji akashangaa sana na kusema: "Baba yako ndiyo alimuondoa baba yangu nchini!"

Aliyekuwa anaongea naye alikuwa mmoja wa watoto wa Milton Obote, Eddy Engena-Maitum. Serikali ya Rais Obote ilipinduliwa na Idi Amin, wakati huo akiwa kamanda wa jeshi la Uganda, tarehe 25 Januari 1971 wakati Obote akiwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Idi Amin alishika madaraka mpaka mwaka 1979 baada ya Rais Nyerere kutangaza vita dhidi ya Uganda kufuatia uvamizi wa eneo la Kagera na majeshi ya Idi Amin. Baada ya kukomboa eneo lililovamiwa vita iliendelea ndani ya ardhi ya Uganda na kuhitimishwa kwa kuangushwa kwa serikali ya Amin.

Jaffar akamwambia Eddy: "Mimi nitakutambulisha kwa mtu ambaye baba yake alimuondoa baba yangu hapa Uganda." Alimaanisha mimi.

Mwalimu Nyerere akiwa na mwenyeji wake, Rais Milton Obote, wakati wa moja ya ziara zake nchini Uganda. Wa pili kutoka kulia ni Idi Amin, na kulia ni Philemon Mgaya, aliyekuwa mpambe wa Rais Nyerere.
Kabla ya siku hiyo Jaffar alipokutana na Eddy jijini Kampala, mimi na Jaffar tulikwa tumeonana kijijini Butiama katika tukio lililoandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuadhimisha miaka 30 ya vita vya Kagera, vita vilivomuondoa Idi Amin nchini Uganda.

***********************************
Bofya hapo chini kusoma maelezo yangu (kwa lugha ya Kiingereza) juu ya ziara ya Butiama ya Jaffar:

***********************************

Idi Amin na familia yake walikimbilia nchini Libya, na baadaye kuhamia Saudia Arabia. Milton Obote na familia yake walihamia Tanzania na wakawa majirani zetu Msasani kwa muda mrefu.

Saturday, July 1, 2017

Watoto wa mjini nimewakubali

Nimejifunza siku chache zilizopita kuwa mtoto anayeishi mjini ni tofauti sana na yule anayeishi kijijini. Wa mjini wajanja.

Nilikuwa kwenye mitaa ya Kariakoo hivi karibuni nikaamkiwa na binti mdogo aliyevaa baibui niliyemkadiria kuwa na umri usiozidi miaka saba. Aliniomba msaada wa pesa kwa ajili ya mama mlemavu aliyekuwa kwenye kiti cha walemavu upande wa pili wa barabara.

Nilitoa shilingi 5,000 nikamkabidhi na kumuuliza kama nimsaidie kuvuka barabara ya Livingstone ambayo wakati huo ilikuwa na msululu wa magari. Alinihakikishia atamudu kuvuka mwenyewe. Nikaendelea na kununua miwani kwa machinga na yeye akaondoka.

Dakika 20 baadaye nikamkuta yule mama mlemavu kwenye mtaa wa jirani nikamuuliza kama alipokea zile pesa nilizotoa.

"Pesa gani?"
"Zile elfu tano nilizompa yule binti akuletee?
"Hata sijazipata. Ngoja tumsubiri."

Wakati huo binti alikuwa kwenye duka moja akiendelea kuomba msaada kwa watu mbalimbali.

Binti alivyoniona akatabasamu kwa aibu na kukabidhi zile pesa kwa yule mama, ambaye alinijulisha kuwa ni mjukuu wake.

Nilitafakari kuwa inawezekana wanapozunguka kuomba pesa mjukuu anabaki na pesa nyingi kuliko anazokabidhi kwa bibi yake.

Friday, April 7, 2017

Bila Karume hakuna Tanzania

Bila yeye hakuna Tanzania. Ni maneno ambayo Mwalimu Nyerere aliyatamka akizungumiza juu ya masuala mbalimbali, pamoja na chimbuko la muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Nachapisha tena makala iliyochapishwa tarehe 26 Aprili 2016 kwenye safu yangu "Ujumbe toka Muhunda" ndani ya gazeti la Jamhuri. Katika makala hiyo narudia ukweli ambao unasahauliwa, ya kuwa wazo la muungano ni wazo la Sheikh Abedi Amani Karume. Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuuwawa kwake.

********************************

Muungano ni pendekezo la Sheikh Karume
Na G. Madaraka Nyerere

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo unatimiza miaka 52. Kwa binadamu miaka 52 siyo haba, na aliyoitimiza tunamuita mzee. Kudumu kwa muda mrefu kiasi hiki kunapaswa kupongezwa, ingawa si wakati wote wanaostahili pongezi wanaipata.

Tarehe ya leo, miaka 52 iliyopita, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliweka sahihi hati ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini wengi wanapoandika au kuzungumzia Muungano huweka msisitizo wa mchango wa Mwalimu Nyerere na imani yake kubwa juu ya umuhimu wa kuungana. Kwa maoni yangu, Sheikh Karume hapati sifa anayostahili kama muasisi wa Tanzania.

Kwenye mahojiano ndani ya filamu iliyoandaliwa na M-Net, Mzee Rashidi Kawawa alifafanua kuwa wazo la kuunganisha Tanganyika na Zanzibar lilitolewa na Mzee Karume, halikuwa wazo la Mwalimu Nyerere. Ni kweli kuwa Mzee Karume alitoa wazo kwa mtu ambaye tayari alikuwa anaamini juu ya umuhimu wa umoja, na bila shaka ndiyo sababu ya kukubaliwa.

Naye Mama Maria Nyerere amesimulia kuwepo Ikulu Dar es salaam siku Karume alipotoa wazo hilo. Mzee Karume alikuwa Dar kwa shughuli za kikazi, na ni katika mazungumzo na Mwalimu baada ya mazungumzo yake rasmi ya kikazi ndipo mazungumzo ya muungano yalianza. Mwalimu alianza kulalamika juu ya kasi ndogo ya mchakato wa kuunganisha nchi tatu za Afrika Mashariki ili kuunda shirikisho. Hapo hapo Karume alimwambia Mwalimu kuwa kama mchakato huo unachelewa, basi yeye yuko tayari Zanzibar iungane na Tanganyika. Na kuongeza: “Wewe utakuwa rais, mimi nitakuwa makamu wako.”

Wazo la kujenga umoja halikuwa geni kwa Mwalimu Nyerere, kwa hiyo haihitaji utafiti wa kina kubaini sababu ya kulikubali mara moja na kulivalia njuga wazo la Mzee Karume. Agenda ya kuleta umoja wa nchi za bara la Afrika ilikuwa ni mojawapo ya mikakati ya chama cha TANU wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika.
 Kwa namna fulani, Mzee Karume ni kama alikuwa anamwambia Mwalimu Nyerere kuwa hiyo safari ya umoja tuianze kwa hatua hii ndogo baina ya Tanganyika na Zanzibar, hizo hatua kubwa zitafuata.

Wataalamu wengi wa kikatiba wamekosoa taratibu zilizofuata kukamilisha wazo la Mzee Karume mpaka kufikia kuwekwa sahihi hati ya Muungano kati yake na Mwalimu Nyerere tarehe 26 Aprili 1964. Na hapa lawama kubwa inamuangukia mpokea wazo, Mwalimu Nyerere.

Pamoja na kwamba ziko hoja nzuri za kukosoa mchakato wenyewe, zipo pia hoja kinzani ambazo hazikubali kuwa Muungano ni batili. Malumbano haya, miaka 52 baadaye, bado yanaendelea. Lakini yasituyumbishe tukasahau kuwa ni Mzee Karume ndiyo alianzisha hoja ya muungano.

Zipo taratibu za kugeuza simulizi za wazee kuwa historia rasmi, na pengine wakati umefika sasa wa wanahistoria kufanyia utafiti kipengele hiki cha historia ambacho hakipewi uzito unaostahili.

Kuna wakati baadhi ya wasomi wetu, katika kutafuta sababu zinazowaridhisha wao juu ya historia ya Muungano, walisisitiza kuwa wazo la Muungano liliibuliwa na afisa mmoja wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA. Kwa mawazo yao sisi hatuna uwezo wa kufikiri kuwa Muungano ni muhimu kwetu, tunahitaji Wamarekani kutufundisha. Miaka hiyo ya sitini, kila tukio liliwekwa kwenye mizani ya vita kati ya itikadi za nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani, na itikadi za nchi za mashariki zikiongozwa na Urusi.

Kama siyo imani ya kuona kuwa kila jema na lenye manufaa hutoka nje tu, basi inakuwa ni jitihada pia ya kupuuza mchango wa viongozi wetu katika kujenga na kuimarisha Muungano kwa kushawishi kuwa mawazo yao yalipandikizwa na wale ambao tunaamini hawana nia njema bali wanalinda masilahi yao.

Bahati nzuri, kama vile alifahamu mapema kuwa haya maneno yatasemwa Mwalimu Nyerere aliwajibu mapema watu hawa. Katika chapisho la chama cha TANU la Juni 1960 lililosisitiza haja ya kuwepo kwa shirikisho la Afrika Mashariki, Mwalimu aliweka msimamo wake na wa TANU juu ya shirikisho kwa kusema (siyo tafsiri rasmi):

“Katika watu wanaounga shirikisho watapatikana watu ambao wanasukumwa na sababu tofauti….watakuwepo wafanyabiashara…kutakuwa na kila aina ya watu upande wa shirikisho na watakuwa na kila sababu. Lakini hoja ya shirikisho inajitosheleza kwa uhalali wake yenyewe. Thamani ya almasi haitegemei tabia ya wale wanaoichimba. Madini ni almasi, au siyo almasi. Iwapo shetani mwenyewe atajitokeza na kuunga mkono huu mpango wa shirikisho, ujio wake hautabadilisha mawazo yangu juu ya shirikisho au juu ya shetani mwenyewe.”

Mawazo ya Sheikh Abeid Amani Karume ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika yalitua kwa muumini mkubwa wa umoja wa watu, na hasa umoja wa nchi za Afrika, Mwalimu Nyerere. Lakini tukubali kuwa bila Mzee Karume upo uwezekano kuwa hadi sasa tungekuwa hatuna Tanzania.


Miaka 52 baadaye, kwenye mazingira ya vijana wetu kutumia muda wao mwingi kutumiana ujumbe kwenye Twitter, Facebook, na Instagram kuliko kufukua yaliyojichimbia kwenye vitabu pamoja na kutafiti yale ambayo hayapendi kusemwa, ipo hatari kuwa yale ya CIA yataendelea kuwekewa uzito zaidi kuliko yale ambayo hayakidhi malengo ya mada za wasomi.

Taarifa nyingine inayohusiana na hii:

Sunday, April 2, 2017

Tumbili wa Mwitongo

Baadhi ya wanyama wanaopatikana kwa wingi eneo la Mwitongo, kijijini Butiama, ni tumbili. Ni wanyama wanaosumbua binadamu kwa kushambulia mazao ya kilimo, au baadhi ya vyakula vinavyohifadhiwa na binadamu iwapo tahadhari hazichukuliwi kulinda vyakula hivyo.

Kwa kawaida huogopa binadamu, lakini wanayo hulka ya kuzowea binadamu iwapo hawatishiwi usalama wao. Kwenye video, chini, ni mmoja wa tumbili ambao amepunguza woga kabisa akiniona kiasi cha kuchukua karanga mkononi mwangu.


Wanyama wengine wanaopatikana kwa wingi eneo la Mwitongo ni pimbi,

Tuesday, March 21, 2017

Tanzania ni nchi nzuri sana

Tanzania ni nchi nzuri sana. Hakuna ubishi juu ya hoja hii.

Lakini inahitaji fursa ya kutoka sehemu moja na kuzunguka maeneo mbalimbali ya Tanzania ambayo yanavutia kwa mandhari na vivutio mbalimbali vya asili. Ukibaki sehemu moja tu huwezi kufahamu juu ya ukweli huu.

Kama huna hiyo fursa siyo kosa lako, lakini kama unayo fursa na uwezo basi huna budi kuzunguka na kuifahamu vyema nchi yako. Utalii wa ndani unajenga uchumi, na wale ambao tunao uwezo wa kutembelea maeneo ya Tanzania tunapaswa kuchangia kwa kadiri tunavyoweza.Moja ya sehemu ambazo zinavutia nchini Tanzania ni maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria. Video hii imechukuliwa kwenye kivuko cha Busisi kwenye njia kuu inayotumika na wasafiri kati ya Mwanza na Geita, Chato, hadi Kagera.

Sunday, March 19, 2017

Unafahamu masuala haya 5 kuhusu Mwitongo?

Unafahamu masuala haya 5 kuhusu Mwitongo?

Mwitongo ni eneo la kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania tarehe 13 Aprili 1922. Aidha, ni eneo alipozikwa tarehe 23 Novemba 1999.

Yafuatayo ni masuala matano ya Mwitongo ambayo pengine huyafahamu.

1. Ajali ya ndege
Mwaka 1978, baada ya majeshi ya Idi Amin Dada kiongozi wa kijeshi wa Uganda kuvamia eneo la mkoa wa Kagera, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianza kampeni ya kuondoa majeshi ya Idi Amin kwenye ardhi ya Tanzania.

Katika harakati za kujiandaa na vita hivyo, kikosi cha anga cha JWTZ kilihamisha baadhi ya ndege zake za kivita kutoka kituo cha Ngerengere na kuzipeleka kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza.

Kwa sababu ya kasi ya hizo ndege, marubani wawili waliorusha hizo ndege walipitiliza Mwanza na kulazimika kuzunguka kuelekea upande wa kaskazini mashariki ili warudi tena kutua Mwanza. Uamuzi huo ukasababisha waruke juu ya anga ya mji wa Musoma.

Askari wa kikosi cha mizinga kilichokuwa kinalinda eneo la Musoma, kwa kukosa taarifa juu ya ndege hizo na kudhania kuwa ni ndege za adui, walizishambulia. Moja ya ndege hizo ilianguka Musoma, na nyingine iliangukia Mwitongo, kwenye msitu wa Muhunda.

Eneo la Mwitongo ilipoanguka ndege ya pili umejengwa mnara wa kumbukumbu.
Mnara wa kumbukumbu ya ajali ya ndege kwenye msitu wa Muhunda.
2. Msitu wa Muhunda
Msitu wa Muhunda ni sehemu ya eneo la Mwitongo. Ni msitu ambao, kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, ndiyo makazi ya mzimu wao, Muhunda. Msitu una ukubwa wa ekari 5.

Ni marufuku kukata miti iliyopo ndani ya msitu huo. Inaruhusiwa kukusanya kuni za matawi yaliyoanguka chini tu. Wazee wa kimila hufanya mitambiko ndani ya msitu huo.

Inaaminika kuwa mzimu huo hujibadilisha kuwa mojawapo ya viumbe vifuatavyo: nyani mkubwa, chui, mbuzi mkubwa, au nyoka mkubwa.

3. Mamba Mweusi (Black Mamba)
Mwinuko wa Mwitongo upo ndani ya eneo lililozungukwa na vichaka misitu, na majabali makubwa.

Ni eneo ambalo lina viumbe wadogo wadogo, pamoja na nyoka wa aina mbalimbali. Mojawapo wa nyoka hawa ni mamba mweusi.
Picha ya Mamba Mweusi. Jina lake la kisayansi ni Dendroaspis polylepis. Picha inatumika kwa idhini ya Creative Commons License. Taarifa kamili zipo hapa: http://creativecommons.org/licenses/by-sa/3.0/deed.en
Huyu ni moingoni mwa nyoka wenye sumu kali kabisa duniani, na inasemekana kuwa nyoka pekee ambaye hushambulia binadamu kwa makusudi, tofauti na aina nyingine ya nyoka ambao hushambulia tu wanapotishiwa usalama wao.

4. Ziwa Viktoria
Mwitongo ni eneo la mwinuko wa mita 1,405 juu ya usawa wa bahari. Kwa sababu ya mwinuko huo mtu anayesimama Mwitongo anaweza kuona kingo za Ziwa Viktoria zilizopo umbali wa kilomita 40 magharibi mwa Butiama.
Ziwa Viktoria.

5. Nelson Mandela
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitembelea Mwitongo mwezi Novemba 1999. Alifika Mwitongo kuhani kifo cha Mwalimu Nyerere aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999.

Mzee Mandela aliandaliwa chumba maalum cha kulala wakati wa ziara yake. Kitanda maalum kiliwekwa kwenye chumba hicho. Hata hivyo, ratiba yake haikuruhusu kulala, na akaondoka siku hiyo hiyo kurudi Afrika Kusini. Kitanda kile hakijaondolewa kwenye chumba kile hadi hii leo.