Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, December 30, 2016

Hii ndiyo redio ya Mwalimu Nyerere 'enzi za Mwalimu'


Hii ndiyo redio ya Mwalimu Nyerere 'enzi za Mwalimu' (kwenye picha, chini). Ni aina ya National Panasonic, ambayo aliitumia katika miaka ya sitini na sabini.

Mwalimu Nyerere alikuwa msikilizaji makini kabisa wa taarifa za habari, na alikuwa akisikiliza taarifa kutoka vituo vya redio vya nje ya nchi, kama Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), pamoja na vituo vya ndani (wakati huo ikiwa ni Redio Tanzania peke yake).

Uzito wa redio hii ni kilo 20, na wakati wa safari kuna mtu maalum alikuwa akiibeba. Mabadiliko ya teknolojia yalisababisha kupungua kwa ukubwa wa redio, na katika miaka ya baadaye Mwalimu naye alianza kutumia redio ndogo zaidi ambazo uzito ulifikia hata chini ya robo kilo. Redio hii ipo kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere, Butiama.

Wednesday, December 14, 2016

Fidel Castro katoa mchango muhimu Afrika; tuisome historia

Ukisikiliza sehemu kubwa ya maoni ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi juu ya kiongozi wa Cuba Fidel Castro, utaafiki kuwa hana mchango wowote wa maana kwa binadamu wenzake. Inahijati kujikumbusha kidogo sehemu ya historia ya ukombozi wa bara la Afrika ili kupata picha tofauti.

Castro, kiongozi wa Cuba kwa karibia miaka 50, amefariki hivi karibuni na kuzikwa jijini Havana. Ni aina ya kiongozi ambaye anapewa sifa nyingi na kushutumiwa vikali wakati huo huo.

Hatushangai sana kusikia ukosoaji mkubwa dhidi ya Fidel Castro na uongozi wake. Yeye, pamoja na wapiganaji wenzake waliongoza mapambano mwaka 1956, na hatimaye kufanikiwa kufanya mapinduzi mwaka 1958, yaliyong’oa madarakani utawala wa Fulgencio Battista uliokuwa unaungwa mkono na Marekani. Ni kuangushwa kwa Batista ndiyo kuliibua uhasama wa Marekani dhidi ya Cuba.

Kufanikiwa kwa mapinduzi dhidi ya Batista ilikuwa tishio kubwa dhidi ya Marekani katika nyanda nyingi. Lakini hatari kubwa zaidi kwa Marekani ilikuwa kufanikiwa kwa kundi dogo la wapiganaji walioanzisha mapambano wakiwa na bunduki mbili tu, na hatimaye kufanikiwa kuangusha utawala ulioungwa mkono na taifa kubwa. Kwa sera za nchi za nje za Marekani, eneo la Amerika ya Kusini lilikuwa himaya yake na Cuba ya Castro ilikuwa mfano wa kupata jirani mpya mkorofi.

Huu ulikuwa mfano hatarishi kwa maslahi ya Marekani, mfano ambao ungeweza kuigwa na watu kwenye mataifa mengi ya Amerika ya Kusini ambapo Marekani ilikuwa imesimika nguvu zake za kiuchumi na kijeshi.

Wakati huo Ukomunisti ulionekana kama kirusi ambacho kisipodhibitiwa kingeweza kusambaa na kuathiri mawazo ya mamilioni ya watu ulimwenguni. Cuba ya Fidel Castro haikupaswa kufanikiwa kwa hali yoyote. Mwaka 1960 serikali ya Cuba ilipotaifisha mitambo ya kusafisha mafuta ghafi iliyomilikiwa na kampuni za Marekani serikali ya Marekani ilianzisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba, vikwazo ambavyo bado vimekuwepo kwa zaidi ya miaka 55.

Licha ya kuwepo vikwazo hivi vya kiuchumi Cuba imefanikiwa kufikia maendeleo makubwa katika huduma za afya, kuongezeka kwa umri wa kuishi, kufanikiwa kwa mpango wa chanjo kwa watoto, na kuboreshwa kwa mifumo ya elimu ambayo inalingana hata na nchi zinazotajwa kuwa zimeendelea. Tanzania tunatambua mchango wa Cuba katika kuleta madaktari ambao wamefanya kazi maeneo mengi ya nchi. Lakini Cuba haijatoa msaada wa madaktari tu, bali imesomesha maelfu ya madaktari siyo tu kutoka nchi zinazoendelea bali hata kutoka mataifa makubwa ikiwemo Marekani yenyewe.

Kwenye bara la Afrika, pamoja na kuandamwa na Marekani na nchi za Magharibi, Cuba imetoa mchango mkubwa sana katika jitihada za Waafrika za kusaka na kulinda uhuru wa nchi zao. Miaka ya sitini Cuba ilituma wapiganaji wake nchini Algeria, Congo, na Guinea Bissau.

Katika miaka ya themanini tulishuhudia tena utayari wa Cuba kusaidia Waafrika kutetea maslahi ya nchi zao dhidi ya nguvu ya ubepari na ubeberu. Wanajeshi wa Cuba walipigana na wenzao wa Angola kudhibiti mashambulizi ya jeshi la serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini yaliyokuwa yamevamia Angola tangu 1983. Mwaka 1988 kwenye mapambano yaliyofanyika kwenye mji wa Cuito Cuanavale wanajeshi wa Afrika ya Kusini walishindwa kuvuka ngome iliyosimikwa na wanajeshi wa Cuba, Angola, na wapiganaji wa vyama vya ukombozi vya Afrika ya Kusini na hivyo kushindwa kutimiza kusudio lao la kuteka mji mkuu Luanda.

Kuiokoa Afrika ya Kusini aibu ya kushindwa kwenye mapambano ya Cuito Cuanavale, Marekani, ambayo nayo kimaslahi ilikuwa upande wa Afrika Kusini kwa kisingizio cha kupinga kusambaa kwa Ukomunisti nchini Angola na barani Afrika, ilijitokeza kama msuluhishi kati ya Cuba, Angola, na Afrika ya Kusini. Ushindi huu kwa Angola na Cuba ndiyo uliharakisha uhuru wa Namibia chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Aidha, kwa ushindi ule watawala wa serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini wakang’amua kuwa kipo kikomo cha kutumia nguvu za kijeshi kulinda utawala wao wa kibaguzi. Kuendelea kuanguka kwa tawala za kibaguzi kwenye makoloni ya Ureno, pamoja na Zimbabwe kulionekana tishio kwa utawala wa Afrika ya Kusini, na hivyo kuchochea mikakati ya hujuma na vita dhidi ya nchi jirani ambazo zilitoa msaada kwa harakati za ukombozi za Afrika ya Kusini.

Kwa pigo moja la Cuito Cuanavale Cuba ya Fidel Castro ikaweka chachu ya ukombozi kwa Angola, Namibia, na Afrika ya Kusini.

Kama wapo Waafrika ambao watauonea aibu mchango huu mkubwa wa Fidel Castro na Cuba kwa bara la Afrika, basi tukubali kuwa maneno tunayolishwa kila siku yamefanikiwa kutufundisha kusikiliza yale tunayoambiwa tu na kutuzuwia kufanya maamuzi yetu wenyewe juu ya nani ni muhimu katika historia ya bara letu. Cha ajabu ni kuwa baadhi yetu tuko tayari kuyakubali hayo maneno kutoka kwa wale wale ambao wakati wa mapambano walishikamana na kusaidiana na maadui wa ukombozi wa bara la Afrika.


Hawapo viongozi wasiyo na mapungufu, na hata kama Fidel Castro alikuwa na mapungufu katika uongozi wake, haituzuwii Waafrika kutambua mchango wake muhimu katika ukombozi wa bara letu. Hili suala linahitaji kuisoma historia tu, halihitaji hata mjadala.

Tuesday, December 13, 2016

Lugha yetu Kiswahili

Kiswahili lugha nzuri, lakini hutatanisha wengi.

Siku moja nikiwa safarini nilijikuta kwenye mgahawa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Nilikuwa nimewahi asubuhi mapema siku hiyo nikaondoka Arusha bila kupata staftahi, au kifungua kinywa.

Nilipovuka eneo la ukaguzi la maafisa usalama na kuingia kwenye ukumbi wa abiria wanaojiandaa kupanda ndege nikawahi kwenye mgahawa na kuagiza kahawa. Aidha, hupendelea kula mayai asubuhi, kwa hiyo nikamuita mhudumu ili nimuagize mayai kuwahi kabla ya abiria kutangaziwa kuingia ndani ya ndege.

Mazungumzo yakawa hivi:

Mimi: Nitapata mayai?
Yeye: Ndiyo.
Mimi: Naomba jicho la ng'ombe.
Yeye: Hapa hatuna jicho la ng'ombe.

Sikumuelewa. Huyo huyo aliyekubali kuwa mayai yapo akaniambia hawana jicho la ng'ombe. Nilibaini naongea na mtu ambaye Kiswahili kinampiga chenga. Nilihisi alikuwa mwenyeji wa Kenya. Nikamwambia anipeleke kwa mpishi niongee naye, na huko kwa mpishi nikaagiza mayai jicho la ng'ombe na yakakaangwa vizuri tu.
Jicho la ng'ombe.
Nilivyoelewa mimi, mhudumu alidhani nimeagiza nipikiwe jicho hasa la ng'ombe.

Taarifa inayofanana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2013/10/msiofahamu-vyema-kiingereza-zungumzeni.html

Sunday, November 20, 2016

Rais Magufuli na ngoma za Ikulu: utamaduni unadumishwa

Desturi ya kupokea mgeni mashuhuri kwa kupiga ngoma ipo miongoni mwa watawala wa makabila mengi ya Tanzania.

Enzi za tawala za kitemi, hiyo ndiyo ilikuwa desturi. Mgeni, hasa yule ambaye alikuwa na hadhi ya utawala kama mwenyeji wake, alipigiwa ngoma za mwenyeji wake. Ni ngoma ambazo zilisikika kwenye himaya ya mtemi mwenyeji na zilisambaza taarifa ya kuwepo kwa mgeni muhimu.

Baada ya uhuru wa Tanganyika, desturi hiyo ilihamia kwenye Ikulu ya Dar es Salaam na viongozi mbalimbali waliotembelea Ikulu walipokelewa kwa desturi hiyo.
Rais Nyerere akimkaribisha Rais Sekou Toure wa Guinea kupiga ngoma za kumkaribisha Ikulu, Dar es Salaam.
Kumbukumbu yangu inaweza kuwa siyo sahihi, lakini sikumbuki kama baada ya Mwalimu Nyerere desturi hii ilifuatwa sana, ingawa tunaona sasa kuwa Rais wa awamu hii ya tano, John Magufuli, ameichangamkia vyema na huwashirikisha viongozi wanaofika Ikulu kupiga ngoma zilizopo Ikulu.

Inawezekana pia kuwa siyo wageni wote wanaofika Ikulu ambao hukaribishwa kwa kupiga ngoma,

Thursday, November 10, 2016

Mbuga ya Serengeti inavyoonekana juu ya Mlima Balili

Mkoa wa Mara una vivutio vingi vya utalii, na mojawapo ya vivutio hivi ni Mlima Balili uliyopo Wilaya ya Bunda.
Kutoka juu ya Mlima Balili kuna mojawapo ya mandhari nzuri katika eneo hili. Kwenye picha, upande wa kushoto ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Juu kidogo ya picha hii unaoenakana Mto Grumeti ambao ni mojawapo ya mito inayotiririka ndani ya Hifadhi ya Serengeti na kuishia ndani ya Ziwa Victoria.

Ziwa Victoria linaonekana juu kulia. Upande wa kulia ni barabara kuu inayotoka Musoma hadi Mwanza.

Friday, August 12, 2016

Kijijini kama mjini

Wapo wengi ambao hawakupenda uamuzi wa serikali ya awamu ya nne ya kuanzisha kwa wilaya mpya ya Butiama. Mimi ni mmojawapo.

Nimejihusisha na kazi ya kutangaza historia na utamaduni wa eneo la Butiama kwa zaidi ya miaka saba sasa, na natambua ni jinsi gani utamaduni wa eneo unavyoweza kuathirika unapotokea muingiliano wa haraka kati ya maeneo ya mijini na ya vijijini. Mawasiliano mazuri kati ya miji na vijiji yanaweza kuongeza kasi hiyo, na hali kadhalika, uamuzi wa kuanzisha wilaya mpya pia unaweza kuleta matokeo hayo hayo.

Wilaya mpya inakuja na ongezeko kubwa la wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali. Nao siyo kama wanakuja na tamaduni zao za asili tu, ila wanaleta zaidi tamaduni za miji, na hata sheria za miji. Matokeo yake ni kudumazwa kwa tamaduni za asili za maeneo hayo mapya ya wilaya, na hasa kama yalikuwa maeneo ya vijijini.
Mojawapo ya sehemu za burudani na starehe za Butiama zilizoibuka baada ya kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Butiama.
Msimamo wangu haulengi kutetea suala la ukabila, bali unalenga kulinda na kutunza mila na desturi za eneo mahususi kwa madhumuni ya kuendeleza utalii wa utamaduni.

Saturday, July 30, 2016

Mada yangu ya leo: mwizi ni mwizi tu

Sikumbuki niliisoma wapi habari hii, lakini kuna kichwa cha habari cha toleo la gazeti la hivi karibuni liliarifu kuwa yule mtuhumiwa wa kuiba milioni 7 kwa dakika "mwenye asili ya Kiarabu" amefikishwa mahakamani.

Kwanza, nitamke wazi kuwa hili suala liko mahakamani na mimi simhukumu mtuhumiwa. Namtetea kwa kubaguliwa. Akikutwa na hatia, nitazungumzia hilo.

Mwizi ni mwizi tu, hata kama ni kabila yako. Uandishi wa aina hii wa kubainisha kuwa mtuhumiwa ana asili ya Uarabu ni hatua ya wazi ya kubagua mtu kwa rangi yake ya ngozi. Maana inayojitokeza ya makala hii ni kuwa kama angekuwa Mbantu akutwe na hatia ya kuiba milioni 7 kwa dakika, tatizo lingekuwa dogo zaidi. Labda milioni 7 ingekuwa 2 tu kwa sababu tu mwizi alikuwa ana rangi tofauti ya ngozi.

Monday, March 28, 2016

Viongozi wabaguzi ambao wanaendelea kuenziwa

Wapo viongozi wa dunia ambao wamejijengea sifa kubwa, pamoja na ukweli kuwa wanabeba kasoro kubwa za kibaguzi kwenye matamshi au maamuzi yao. Viongozi wawili ambao wanayo sifa hii ni Winston Churchill, na Mahatma Gandhi.
Sir Winston S Churchill.jpg
Winston Churchill (Picha: Wikipedia)

Churchill alikuwa kiongozi wa Uingereza ambaye aliwahi pia kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Katika nyadhifa zake mbalimbali amenukuliwa akitoa matamshi na kuchukua hatua za kibaguzi dhidi ya watu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Waafrika, Wahindi, na Waarabu. Kwa ujumla, alikuwa mbaguzi wa rangi ha kiwango cha Hitler aliyeamini kuwa binadamu mwenye ngozi nyeupe anapaswa kutawala binadamu wengine wote. Pamoja na ukweli huu, Churchill anakumbukwa kwenye historia kama kiongozi aliyefanikiwa kuiongoza Uingereza vyema wakati wa vita vya pili vya dunia.

Gandhi naye haachwi mbali kwa matamshi yake ya kibaguzi. Akiwa anafanya kazi Afrika ya Kusini aliandika kuhusu kupinga kwake kwa wahindi kufananishwa na Waafrika, akiamini kuwa Mwafrika alikuwa na hadhi ya chini kuliko Mhindi. Gandhi ni mmoja wa wanaharakati wa India ambaye anaheshimika sana katika ulimwenguni wa mapambano dhidi ya ukoloni, haki, na usawa.

Wanataaluma wanafahamu kuwa, kwa kutumia mifumo ya habari na mawasiliano ambayo inamilikiwa na kampuni chache sana duniani, inawezekana kujenga taswira juu ya kiongozi ambayo haifanani kabisa na hali halisi. Mwizi anaweza kuonekana ni muadilifu, na mhalifu akaonekana asiye na hatia. Hali kadhalika, muadilifu na asiye kuwa na hatia akatambulishwa kuwa tofauti kabisa na hali halisi.
File:Portrait Gandhi.jpg
Mahatma Gandhi (Picha: Wikipedia)
Haipingiki kuwa historia ya kiongozi inapaswa kuakisi mazuri na mabaya yake, lakini nafikiri inapofikia suala la ubaguzi wa binadamu kwa misingi ya rangi ya ngozi, basi kinga hiyo inapotea kwa viongozi wa aina hiyo. Kiongozi asiye mbaguzi na aliyetumbukia kwenye makosa ya kiutendaji anaweza kuvumiliwa kidogo, lakini kiongozi mbaguzi hasafishiki na hapaswi kuvumiliwa hata kidogo.

Hata hivyo, uandishi wa historia unaoficha mabaya ya viongozi wa aina hii pamoja na mifumo ya habari na mawasiliano ambayo inaendelea kudhibitiwa na wamiliki wachache haitoi fursa ya kuwaanika viongozi wa aina hii pamoja na maovu yao.