Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, June 20, 2011

Mlima Meru, wa pili kwa urefu Tanzania, wa 72 ulimwenguni

Mlima Meru ni Mlima wa pili kwa urefu Tanzania baada ya Mlima Kilimajaro. Una urefu wa mita 4,565 juu ya usawa wa bahari na unaorodheshwa kushika nafasi ya 72 kwa milima mirefu kuliko yote duniani. Mlima Meru uko mkoa wa Arusha, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
Mlima Meru ukionekana kutoka Arusha.
Watu wengi wanaoparamia milima kama mimi huanza kupanda milima rahisi kwanza kabla ya kwenda kwenye ile yenye kutoa changamoto kubwa zaidi. Wengi hupanda Mlima Meru kabla ya Kilimanjaro, ingawa mimi nimeanza kupanda Mlima Kilimanjaro nikikusudia baadaye kuukabili Mlima Meru. Waliopanda milima yote miwili wanasema kuwa, pamoja na kuwa Meru siyo mrefu kuliko Kilimanjaro (Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari), untoa changamoto kali kwa sababu kupanda kwake ni mpando wa siku 2 mfululizo wakati Mlima Kilimanjaro unahusisha njia zinazovuka mabonde kadhaa na hiyo ina maana kuwa wanaoelekea kileleni hujikuta wakipanda na kushuka na hata wakati mwingine kupita sehemu zenye tambarare.

Tafiti zinathibitisha kuwa miaka bilioni kadhaa iliyopita Mlima Meru ulilipuka kutokana na msukumo wa gesi za volkano na kusababisha sehemu yake ya pembeni kumeguka na kutapakaa kwenye eneo la umbali unaofikia upande wa magharibi ya Mlima Kilimanjaro. Hizo tafiti zimethibitisha kuwepo tabaka ya udongo wa Mlima Meru juu ya sehemu hiyo ya Mlima Kilimanjaro.

Picha hii ya chini ambayo imepigwa na vyombo vinavyoruka juu vya shirika la Marekani NASA inaonyesha vizuri sehemu ya Mlima Meru iliyomeguka kutokana na mlipuko wa volkano. Tofauti ya rangi iliyopo kwenye picha inaakisi tofauti ya umbali kutoka usawa wa bahari wa eneo hilo la Mlima Meru.
Hii picha ya Mlima Meru inatumika kwa hisani ya NASA/JPL-Caltech. [Photo: Courtesy NASA/JPL-Caltech]

Saturday, June 18, 2011

Tarehe za kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka huu ni Septemba 20 hadi 27

Kila mwaka tangu mwaka 2008 nimekuwa napanda Mlima Kilimanjaro kuchangisha pesa za hisani. Mwaka 2008 nilipanda Mlima huo na raia wa Vietnam, Le Hu Dyuong. Mwaka 2009 nilipanda Kilimanjaro na Notburga Maskini, ambaye tulisoma pamoja Shinyanga Commercial Institute (Shycom) miaka iliyopita. Yeye alikuwa pamoja na mtangazaji maarufu wa Clouds FM, Gerald Hando.
Le akiwa kwenye bwawa lenye mamba, baada ya msafara wa kupanda Mlima Kilmanjaro mwaka 2008.
Mwaka jana nilipanda mlima na Jaffar Amin, mtoto wa kiongozi wa zamani wa Uganda, Idi Amin.
Jaffar Amin, akiwa amekaa mbele ya mahema yetu kwenye kambi ya Karanga iliyopo mita 3,963 juu ya usawa wa bahari wakati wa msafar wa mwaka jana wa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Mwaka huu natarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia tarehe 20 hadi 27 Septemba. Natarajia kupanda mlima pamoja na wafuatao. Ambao wamesema watajiunga na mimi mwaka huu ni pamoja na mwanablogu mwashuhuri Muhidini Issa Michuzi, mdau wa Utalii Aysha Boma, raia wa Uswisi Andrea Wobmann, mtengeneza filamu wa Marekani Jim Becket (amewahi kuongoza picha ya Mark Dacascos) pamoja na mpigapicha wake, na raia wa Uganda Barbara Allimadi. Kuna wengine ambao bado hawajathibitisha.

Thursday, June 16, 2011

Tabia ya Tumbili

Kumradhi endapo nitakuwa nimemuudhi yoyote kwa kutumia hii picha hapa chini ya huyu jamaa akiwa kwenye mkao wa kula, pamoja na kwamba nilishwahi kuitumia hapa.
Miaka kadhaa iliyopita nilihudhuria mafunzo ya muda mfupi katika chuo kilichopo Tengeru karibu na Arusha, sehemu ambayo ilikuwa inatembelewa na tumbili mara kwa mara.

Jioni moja baada ya kutoka darasani nilishuhudia baadhi ya wanafunzi wenzangu, wakiwa wamevutiwa na hawa wanyama, na walijaribu kuwasogelea pole pole lakini kila walipowakaribia wale tumbili walisogea mbali.

Cha ajabu ni kuwa mmoja wa wakufunzi wetu alipopita kwenye njia ya mguu karibu kabisa na sehemu ambapo tumbili walikuwa wamekaa, wale tumbili hawakuondoka na walibaki pale pale. Raia wa Zambia ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi alitabiri mapema kuwa wale tumbili wasingemkimbia yule mkufunzi. Yule mkufunzi alikuwa mzungu. Na ndivyo ilivyotokea na akapita pale karibu yao kabisa bila kumkimbia.

Mimi ninao uzoefu wa kuishi karibu na tumbili. Huyo aliye kwenye picha ni mmoja kati wengi wa makundi makubwa ya tumbili yaliyopo hapa Butiama. Niliwaambia wenzangu kuwa inaelekea kuwa tumbili wanatambua sura za watu na hukumbuka na kuzigawanya sura hizo katika makundi mawili – wale ambao wanaweza kuwa hawatishii usalama wao na wale ambao wanatishia usalama wao. Nikiwa Butiama, wakati nafanya mazoezi ya kutembea kujiandaa kupanda Mlima Kilimanjaro hukutana na tumbili mara kwa mara na huwa hawanikimbii ingawa nimeshuhudia wanawakimbia baadhi ya watu wengine, hasa watoto.
Hawa tumbili wa Butiama wanayo sababu nzuri ya kukaa mbali na binadamu. Tumbili wana tabia ya kuiba mazao ya kilimo na wakazi wengi wa Butiama wanalazimika kuwafukuza tumbili wanaojaribu kuiba hayo mazao. Sijawahi kufukuza tumbili, kuacha mara chache wakati mlango uliachwa wazi na nikamkurupusha tumbili aliyekuwa ananyemelea maandazi yangu asubuhi.yemelea ,aribu kuw

Wednesday, June 15, 2011

Leo katika historia ya Kombe la Dunia 2006: Poland, Trinidad & Tobago, na Paraguay zaaga mashindano


Poland, Trinidad & Tobago, na Paraguay ziliaga mashindano ya Kombe la Dunia.

Poland ilipoteza michezo yake yote miwili ya Kundi A, kwanza kwa Ecudaor (0-2), halafu kwa Ujerumani (0-1). Ingawa ilishinda mechi yake dhidi ya Costa Rica (2-1), haikutosha kuivusha na kuingia raundi ya pili. Ni ushindi wa Ecuador wa 3-0 dhidi ya Costa Rica uliyoivusha Ecuador, na kuiondoa Poland kwenye mashindano.

Trinidad & Tobago, katika ilipangwa na England, Sweden, na Paraguay katika Kundi B. Yenyewe ilitoka sare mechi moja tu na Sweden (0-0), na kupoteza mechi mbili. Tarehe ya leo, mwaka 2006, Trinidad & Tobago ililazwa 2-0 na England na kuyaaga mashindano, ikiwa ya mwisho kweye kundi lake.

Paraguay, ilishika nafasi ya pili toka mwisho kwenye kundi lake baada ya kufungwa 1-0 na Sweden, tarehe 15 Machi 2006, na timu ikapanda ndege kurudi Ascuncion.

Kwenye Kundi A Ujerumani na Ecuador ziliingia randi ya pili, wakati ni England na Sweden zilizoingia raundi ya pili toka Kundi B.

Monday, June 13, 2011

Omukama wa Missenyi

Mapema mwaka huu, nikiwa kwenye ziara ya Mkoani Kagera, nilipata fursa ya kutembelea Bunazi, katika Wilaya ya Missenyi na kuzuru makazi ya mtemi wa eneo hilo. Mtemi wa sasa wa Missenyi, tangu mwaka 2001, ni Omukama Paulo Lwamujongo II, aliyemrithi baba yake, Omukama Serapion N.L. Kyamukuma II (1932 – 2001) aliyetawala kati ya mwaka 1955 hadi 2011 alipofariki.

Orodha ya watawala waliyomtangulia Omukama Paulo Lwamujongo II
Na.
Jina
Maelezo
Kipindi cha Utawala (kama ni wazi, miaka haijulikani)
1
Wakara
Bunyoro

2
Kagoro I
Alitoka Bunyoro na akahamia Kyango (Buganda)

3
Nyamutura
Alifia Kyango (Buganda)

4
Lwekika I
Alifia Mayanja (Buganda)

5
Kagoro II
Alliingia Missenyi na kuwa Mwami wa kwanza wa Missenyi

6
Nyamutura II


7
Kagoro III
Hakuwa na mtoto wa kiume; kaka yake mdogo alirithi

8
Kyamukuma I
Kaka yake Kagoro III

9
Lwekika II
Mukama wa kwanza wa Missenyi
1870 – 1903
10
Suleimani Kakoko Wakara II

1913 – 1919
11
Paulo Nyamutura Lwamujongo I

1919 – 1955
12
Serapion N.L. Kyamukuma II

8 Feb 1955 – 22 Machi 2001

Kwa mujibu wa historia iliyotolewa, chimbuko lao ni Unyankole, Uganda. Maelezo zaidi:
Watawala wa Bunyoro walikuwa Wahima. Jamaa zao walikuwa wa ukoo wa Balebeki. Rumonge, mtawala mdogo wa Kihima huko Ankole alipoasi Bunyoro alifukuzwa. Nafasi yake ilichukuliwa na mtu wa ukoo wa Balabeki. Sehemu ya kusini ya Ankole mpakani mwa Mto Kagera ilikuwa Kibumbilo ambako mtawala mdogo wa Kihima, Kakoko, alitawala. Naye pia alikuwa wa ukoo wa Balebeki

Mwisho Kibumbilo ilikuwa sehemu ya Himaya ya Baganda mpaka ilipowekwa mipaka ya Wajerumani na Waingereza. Kwa hiyo historia ya utawala huu kwa Missenyi kabla ya matokeo haya haimo katika kitabu cha historia ya Buhaya.

Mwana ukoo wa Omukama wa Missenyi (kulia) akitoa maelezo ya historia mbele ya sehemu ambapo Omukama Serapion Kyamukuma alipokelea wageni wake.
Kabla ya kutawazwa mwaka 2011 Omukama Lwamujongo II alikuwa Dar es Salaam, ambako alikuwa anafanya kazi.

Saturday, June 11, 2011

Takwimu: Majeshi ya Libya na Syria*

Ukilinganisha majeshi ya Syria na Libya, unaweza kupata picha ni sababu gani moja kuu ambayo inafanya jumuiya ya Kimataifa kuishamblia Libya bila woga lakini kujiumauma meno kuhusu suala la kuichukulia hatua kama hizo Syria kwa shutuma dhidi ya kile kinachoelezwa majeshi ya nchi hizo mbili kushambulia raia wake.


Libya
Syria
Askai wa Miguu


Askari
76,000
325,000
Mgambo na askari wa akiba
40,000
314,000
Vikosi vingine vya kijeshi (kama FFU)
0
108,000
Jumla
116,000
747,000Zana za Kijeshi


Vifaru
1,540
4,600
Mizinga ya kutungua ndege
600
6,385
Ndege za kivita
447
607
Idadi ya wanajeshi na zana peke yake siyo kipimo sahihi cha nguvu ya jeshi, lakini ni dhahiri kuwa kuishambulia nchi yenye askari 108,000 ni rahisi zaidi kuliko kushambulia nchi yenye askari 747,000.

*Taarifa zinatokana na wavuti hii hapa, na hii.

Tuesday, June 7, 2011

'Chanzo' cha Mto Nile


Mwaka jana nilipata fursa ya kutembelea Uganda na kufika kwenye ‘chanzo’ cha Mto Nile unaotokana na Ziwa Viktoria na kupita nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Sudan, na Misri, kabla ya kuingia kwenye Bahari ya Mediterranean.
Kutoka kushoto, Samwel Muganda, mimi, mgeni toka Misri, Francois Lumumba (mwanae marehemu Patrice Lumumba), na wageni wawili kutoka Misri ambao majina yao hayakuweza kupatikana, tulipotembelea Jinja wakati wa sherehe za uhuru wa Uganda.
Tafsiri ya meneno kwenye bango lililopo kwenye picha ni:
KARIBU KWENYE CHANZO CHA MTO NILE  JINJA, UGANDA
Sasa uko kwenye kingo ya mashariki ya Mto Nile, kwenye sehemu ambapo mto unaanza kutiririka kutoka Ziwa Viktoria (chanzo cha Nile) kuelekea kwenye Bahari ya Mediterranean. Inachukuwa miezi mitatu kwa maji kumaliza safari ya maili 4,000 (kilomita 6,400).

Maporomoko ambayo John Hanning Speke aliyaona mwaka 1862 na kuyaita “Maporomoko ya Rippons” ikiwa ni jina la rais wa Royal Geographical Society (Chama cha kifalme cha wanajiografia) cha London yalifunikwa na maji mwaka 1947 kufuatia ujenzi wa bwawa kubwa la Owen Falls. Bwawa lilimalizika kujengwa mwaka 1952 likifanikiwa kutumia kasi ya maji kutoka kwenye Ziwa kufua umeme kwa njia ya maji kwa ajili ya Uganda.

“Omugga Kiyira” ni jina la asili la Mto Nile. Ghuba iliyopo nyuma ya bango hili, sehemu ambapo maji ya Ziwa Viktoria yanajipenyeza ndani ya Mto Nile, inaitwa Ghuba ya Napoleon.

Kwenye kingo ya magharibi ya mto kuna mnara mrefu wenye pango mraba zilizochongwa juu kwenye sehemu ambapo Speke alisimama kwa saa nyingi alipoona chanzo cha Mto Nile, na kufanya pajulikane kwa ulimwengu wa nje.
Mimi najiuliza swali. Ziwa Viktoria linapokea maji kutoka mito mbali mbali ya nchi za Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Mto Mara wa Tanzania, na Mto Kagera unaopita Rwanda, Burundi, na Tanzania. Maji yote haya kutoka mito kadhaa yanachangia maji yanayoingia kwenye Mto Nile. Itakuwaje chanzo kiwe Jinja tu? Labda ingekuwa sahihi kusema kuwa kuna vyanzo vingi vya Mto Nile ambavyo vimetapakaa kwenye nchi za Afrika Mashariki.

Sunday, June 5, 2011

Mada yangu ya leo: Umaskini mbaya

Mojawapo ya habari ambazo zimeandikwa kwa kina sana kwenye kipindi cha hivi karibuni ni nia ya Serikali ya kujenga Barabara ya lami kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara kupitia mbuga ya Serengeti.

Ni habari ambayo pia imeleta mvutano mkubwa baina ya pande mbili. Upande moja ina wale wanaopinga kuwepo kwa barabara hiyo, wakidai kuwa ujenzi wake utaathiri majaliwa ya wanyamapori waliyopo Serengeti. Upande wa pili ni wale ambao wanadai kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wakazi wa mkoa wa Mara na mkoa wa Arusha na kuwa umefika wakati kwao pia kufaidikia ni ujenzi wa barabara kama maeneo mewngine ya Tanzania.

Wanamazingira wa ndani ya nchi na nje ya nchi wameungana kupinga kwa nguvu kabisa ujenzi wa barabara hiyo wakidai kuwa Serikali ya Tanzania imeweka sahihi mikataba ya kimataifa ya kutunza na kulinda mazingira na kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakiuka mikataba hiyo. Aidha hifadhi ya Serengeti imeorodheshwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kama eneo la urithi wa Dunia na ujenzi wa barabara hiyo unaweza kusababisha kufutwa hadhi hiyo na kuleta athari mbalimbali kwa nchi, ikiwa ni pamoja na kupunguka kwa watalii watakaotembelea Serengeti na hivyo kuathiri biashara ya utalii na mapato yanayotokana na utalii. Na vitisho siyo vidogo, ikiwa ni pamoja na tishio la Tanzania kunyimwa misaada mbalimbali kutoka nje.

Hoja ya kwamba kwa kujenga barabara hiyo Tanzania itakuwa inakiuka mikataba ya kimataifa ambayo imeweka sahihi ni hoja yenye nguvu. Lakini tunayo mifano mingi ya nchi ambazo zinafanya maamuzi yanayokiuka sheria za kimataifa kwa misingi ya kulinda maslahi ya nchi hizo. Sisi tunaathirika na tatizo la kuwa omba omba. Maslahi ya nchi yetu tunapangiwa na nchi nyingine kwa hiyo hatuna ubavu wa kujenga hoja kuwa jambo fulani linaathiri maslahi yetu, na hivyo basi kudai mapitio ya vipengele ambavyo vitazingatia mahitaji yetu kwenye mikataba ya Kimataifa ya aina hiyo.

Hoja kuwa barabara ya lami inaweza kufuta misafara ya msimu ya wanyama kuhama kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine nina wasiwasi nayo. Kwamba nyumbu na pundamilia wanaovuka  mbuga zenye wanyama hatari kama simba, na chui, na wanaovuka mto Grumeti uliyojaa mamba watashindwa kuvuka barabara ya lami ni mojawapo ya yale masuala ambayo wengine tunayakubali kwa shingo upande kwa sababu tu wanayoyasema ni watu ambao wanasemekana ni wataalamu wa wanyamapori na mazingira. Lakini ni hoja ya kitoto, kwa maoni yangu. Inawezekana ipo athari ya kiasi fulani itakayosababishwa na barabara ya lami, lakini siamini kuwa athari hiyo itafuta kabisa uwepo wa wanyama hao kwenye sura ya dunia kama inavyodaiwa na hawa wataalamu.

Umaskini ni tatizo, lakini wenye hoja inayounga mkono ujenzi wa barabara ya lami kupita ndani ya mbuga ya Serengeti tungekuwa na uwezo wa kifedha ingewezekana kabisa kupata wataalamu wetu wakatufanyia utafiti utakaoonyesha kuwa athari ya barabara ya lami kwa nyumbu na pundamlia siyo ya kutisha. Huu ndiyo utaratibu uliyopo nchi zilizoendelea pande zinazokinzana zinapotaka kuvunja hoja ya upande mwingine. Umesikia hivi karibuni kuna tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya simu za kiganja yanaweza kuleta ugonjwa wa saratani, wakati miaka yote tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya simu hizo hayana athari zozote?

Barabara zilizopo kwenye hifadhi za wanyama katika mataifa mengi yaliyoendelea kunakotoka shinikizo kubwa dhidi ya ujenzi wa hii barabara zimewekwa lami. Tungekuwa tuna uwezo wa kuweka msimamo tungeomba wale wote wanaopinga barabara za lami kwenye mbuga za wanyama kwanza wafumue lami zilizopo kwenye barabara zinazopita kwenye mbuga zao halafu ndiyo waje tukae meza moja kupanga namna ya kuepusha kuweka lami ndani ya mbuga ya Serengeti.

Sishabikii kumaliza wanyama, lakini naamini mahitaji ya binadamu yanawekwa nyuma ya mahitaji ya wanyama. Tatizo ni kuwa wanaharakati wa mazingira hawaambiliki, na hawana muafaka. Tunaamrishwa kusikiliza wanaosema wao, na hawasikilizi hoja nyingine zozote. Ni baadhi ya hao ambao katika jitihada za kuzuwia kuuwawa kwa baadhi ya wanyama kwa ajili ya kutengeneza makoti ya baridi kwa ajili ya binadamu, wako tayari kuua binadamu hao hao wanaovaa hayo makoti.

Hakuna tusi kubwa kwa Watanzania kama kusema kuwa mnyama ni muhimu kuliko mwanadamu. Ni kweli kwa baadhi ya wenzetu, wanyama ni muhimu sana hata kuliko binadamu. Na tumeshuhudia wanyama kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa kuwatibu maradhi wakati binadamu wenzao wanalala nje bila kufahamu wapi watakula, wacha kupata huduma ya matibabu.

Hoja yangu ya leo ni kuwa umasikini si sifa nzuri, na ina athari kubwa kwa nchi ambayo inajaribu kuwahudumia raia wake lakini inapata shinikizo kutoka kwa wahisani ambao kauli yao ina nguvu kuliko ile ya raia Watanzania.

Wednesday, June 1, 2011

Wageni wa Butiama: Profesa Mbilinyi na Profesa Mbilinyi

Muda si mrefu uliyopita nilipokea simu ikiniarifu kuwa kuna mgeni amefika nyumbani. Nilipouliza ni nani, niliambiwa: "Profesa Mbilinyi."
Profesa Simon Mbilinyi (kulia) akijaza kitabu cha wageni kwenye maktaba ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere, Butiama. Katikati ni Profesa Marjorie Mbilinyi.
Nikielekea kuonana na mgeni nikawa najiuliza: "Huyu atakuwa Profesa Mbilinyi yupi? Hakuwa mmoja, walikuwa wawili: Profesa Marjorie Mbilinyi, na Profesa Simon Mbilinyi (ambaye ni mume wake) ambao walikuwa wamepita Butiama wakielekea Ukiliguru ambapo waliwahi kufanya kazi zamani.

Profesa Marjorie Mbilinyi ni mwanaharakati wa masuala ya jinsia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Profesa Simon Mbilinyi amewahi kuwa waziri wa Serikali ya Tanzania.