Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, July 28, 2013

Maendeleo (na makelele) yameingia Butiama

Butiama bado ni wilaya changa kabisa, lakini tayari mabadiliko yatokanayo na miji (na kero zake) yameanza kuonekana Butiama.

Makelele ni mojawapo ya kero za miji ambayo sehemu kama Butiama haikuwa nayo mpaka hivi karibuni. Butiama haikuwa na huduma ya basi linalosafiri moja kwa moja kwenda Mwanza na hapo awali wasafiri walilazimika kusafiri mpaka njia kuu iendayo Mwanza, sehemu iitwayo Nyamisisi, au kuanzia safari Musoma. Miaka michache iliyopita huduma ya basi la moja kwa moja kutoka Butiama hadi Mwanza ilianzishwa na kuleta kero ninazozungumzia.
Basi la kuelekea Mwanza kwenye stendi ya Butiama.
Basi hilo linapoegeshwa alfajiri kusubiri abiria ni kawaida ya madereva wake kupiga honi mfululizo kwa muda mrefu na kusababisha makelele kwenye eneo kubwa la Butiama. Butiama ni kijiji kidogo kwa hiyo mfululizo wa honi hizo za kila kukicha ni usumbufu mkubwa kwa wakazi wengi wa Butiama.

Sijaelewa mantiki ya kupiga hizo honi ingawa naamini zinakusudiwa kuwaamsha abiria wanaosafiri.Lakini ni vigumu kuelewa utaratibu wa abiria anaekusudia kwenda Mwanza kutegemea kuamshwa na honi ya basi.

Wednesday, July 24, 2013

Kazi ya siasa ni chaguo la mwisho kwa mwanafunzi wa shule ya msingi Ramadhani Alfonsi

Mwanafunzi wa shule ya msingi Ramadhani Alfonsi anakusudia kusomea udaktari au urubani. Lakini asipofanikiwa azma ya kufanya mojawapo ya kazi hizo mbili basi ataingia kwenye siasa.

Nimesikia leo mahojiano yake kwenye redio ya TBC FM na ni chaguo ambalo linaibua maswali. Miaka mingi iliyopita nilitembelea shule moja ya sekondari iliyopo Mufindi, Iringa, na mwanafunzi mmoja alipoulizwa angependa kufanya kazi ipi atakapokuwa mtu mzima alisema anataka kuwa mbunge.

Leo hii mwanafunzi Ramadhani anachagua udaktari kwanza, siasa mwisho. Iwapo wanafunzi wengi zaidi sasa wanachagua kazi nyingine kama chaguo la kwanza badala ya kuingia kwenye siasa basi kwa maoni yangu haya ni maendeleo.

Uongozi na siasa vyote vina umuhimu wake lakini naamini kuwa taaluma kama udaktari na taaluma nyingine za ufundi zinaleta manufaa makubwa zaidi kwa jamii kuliko siasa. Kwa mazingira ya sasa kila mtu anaweza kuwa mwanasiasa lakini siyo kila mtu anaweza kuwa daktari, rubani, au mhandisi.

Taarifa nyingine zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/siasa-ya-tanzania-chama-na-sera-zake-au.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/04/mwalimu-wangu-gordian-mukiza.html

Tuesday, July 16, 2013

Simba Sports Club wakaribishwa Butiama na Mama Maria Nyerere

Mama Maria Nyerere leo amekuwa mwenyeji wa viongozi na wachezaji wa klabu ya soka, Simba Sports Club kijijini Butiama.
Wageni hao wamepita Butiama wakielekea Musoma ambako kesho wanacheza mechi ya kirafiki.

Baadhi ya viongozi walioongozana nao ni kocha mkuu Abdallah Kibadeni na kocha wa walinda mlango (ambaye alikuwa mwanafunzi mwenzangu Shule ya Sekondari Tambaza) James Kisaka.

Wageni walipata fursa ya kuzuru kaburi la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye amezikwa Butiama.

Sunday, July 14, 2013

Mzee Mwinyi alisema kila enzi na kitabu chake?

Alisemaje Mzee Ali Hassan Mwinyi, rais mstaafu wa Tanzania? Kila enzi na kitabu chake?

Sikumbuki vizuri lakini enzi za uongozi wake alitamka maneno yanayofanana na hayo akimaanisha kila rika linafikiwa na matukio au mitazamo ambayo, kwa muda, inachukua umuhimu fulani katika jamii. Halafu baada ya muda yanakuja mengine na yale ya mwanzo yanapoteza umuhimu.
Hili basi la abiria (kwenye picha) lina rangi za timu ya soka ya Uingereza, Manchester United. Na upande wa mbele limeandikwa "Manchester United". Bila shaka mmiliki ni shabiki wa timu hiyo mashuhuri. Linafanya safari zake kati ya Musoma na Bunda.

Nyuma ya basi kuna picha ya mchezaji ambaye sifahamu ni nani na wala simfananishi na mchezaji yeyote mashuhuri ambaye ninamfahamu. Bila shaka wenye enzi zao wanamtambua.

Mimi ingewekwa picha ya Mbaraka Mwinshehe ningemtambua.

Thursday, July 11, 2013

Mandhari mpya ya Mwitongo, Butiama

Mandhari ya eneo la Mwitongo inaendelea kupendeza kutokana na kazi ya mtaalamu wa kutengeneza vihenge, Kisyeri Magese.
Kwa miezi kadhaa sasa, mtaalamu huyu asilia kutoka kijiji cha jirani, Nyamuswa, anakarabati na kujenga upya vihenge vya kuhifadhia nafaka ambavyo viko kwenye makazi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye eneo la Mwitongo, kijijini Butiama na ambavyo Mwalimu Nyerere alivitumia kuhifadhia ulezi aliolima.

Baadhi ya vihenge, kama kinachoonekana kwenye picha (kulia), vimekamilika na kazi yote inatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2013. Hili ni eneo linalotembelewa na wageni wanaofika Butiama.

Sunday, July 7, 2013

Maana ya Mwitongo

Kwa kabila la Wazanaki Mwitongo ni jina la eneo walipoishi watu zamani na kuhama. Ni mahame.
Kwa mila za Wazanaki tukio lililofanya watu wahame eneo ilikuwa kufariki kwa mkuu wa kaya. Baada ya kuzikwa tu mali zake zote (na zama hizo hata wake walikuwa ni mali) zilirithiwa na kuhamishiwa kwa warithi.

Mwitongo kwenye kijiji cha Butiama ni eneo alipoishi na kuzikwa Mtemi Nyerere Burito, baba mzazi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwalimu Nyerere naye amezikwa eneo hilo hilo tarehe 23 Oktoba 1999.

Chief Nyerere alizikwa tarehe 30 Machi 1942.

Wednesday, July 3, 2013

Uchakachuaji mpaka kwenye harusi!

Harusi zimekuwa chanzo cha biashara. Hiyo ni dhahiri. Lakini maharusi wanapokuwa ndiyo watafutaji kwenye harusi yao wenyewe, mipaka ya ustaarabu haipo tena.

Kwa muda mrefu wanakamati kwenye harusi za Tanzania wametumia ushiriki wao kwenye kamati hizo kutoa huduma mbalimbali za kulipiwa zinazohitajika kwenye harusi, kama vile, mapambo, magari, huduma za picha na video, na burudani.

Kwa kawaida kufukuzia huku kwa pesa za sherehe hakuwahusu maharusi wenyewe, wao wakifurahia tu mchango wa ndugu, jamaa, na marafiki wa kwenye kamati kufanikisha sherehe. Leo nimedokezwa kuwa siku hizi baadhi ya maharusi nao wanafanya jitihada kubwa ya kufaidika na harusi zao kwa pesa zinazochangwa.

Bwana harusi mmoja mtarajiwa alimtafuta mtu anayemfahamu na kumwambia afike kwenye kamati ya maandalizi na kutangaza kuwa anatoa huduma ya chakula lakini kwa masharti kuwa faida watagawana na mwenye ndoa. Alisema: "Siwezi kuacha pesa yote hiyo iende kwa watu wengine."

Dada mwingine aliyeolewa hivi karibuni naye inasemekana alipachika watu wake kwenye huduma za mapambo na chakula na kunufaika vizuri baada ya sherehe yake. Naambiwa alikusanya mtaji mzuri wa biashara.