Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, June 10, 2010

Balozi mpya wa Tanzania Afrika ya Kusini

Balozi mpya anayewakilisha Tanzania nchini Afrika ya Kusini, Mhe. Radhia Msuya, hivi karibuni aliwasilisha hati za utambulisho kwa Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini mjini Pretoria.

Picha: Rais Zuma (katikati), na Balozi Msuya (kulia)

Utambulisho huo ulifanyika tarehe 8 Juni 2010 kwenye Makazi ya Rais yaliyopo jijini Pretoria. Rais Jakaya Kikwete alimteua Balozi Musya mwezi Machi mwaka huu kushika nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Emmanuel Mwambulukutu aliyestaafu. Kabla ya uteuzi wake Balozi Msuya aliongoza Idara ya Ulaya na Amerika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Picha (kutoka kushoto kwenda kulia): Robert Kahendaguza (Mkuu wa Utawala na Fedha wa Ubalozi wa Tanzania), Rais Zuma, Balozi Msuya, na Brigedia Jenerali Simon Mumwi (Mwambata Jeshi, Ubalozi wa Tanzania)

Saturday, June 5, 2010

Hii kali

Muda mchache uliopita, Muhidini Michuzi ameripoti kwenye blogu yake kuwa wachawi kumi wanajiandaa 'kuwatengeneza' Brazil kabla ya mpambano na Taifa Stars. Fuatilia hapa:

http://issamichuzi.blogspot.com/2010/06/wachawi-10-wajitokeza-kuiroga-brazil.html


Mimi ushauri wangu huu: bila kushirikisha Muhunda ni kupoteza pesa na muda.

Uchaguzi 2010: Eva Sweet Musiba


Mwandishi wa habari wa magazeti ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Sweet Eva Musiba, ni mmoja wa wagombea ubunge wa viti maalum, Mkoa wa Mara, waliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.Bulleted List
Maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Elimu:
  • Stashahada ya Uandishi wa Habari, Dar es Salaam School of Journalism
  • Masomo ya Awali ya Uhasibu, Business Efficiency (B.E.I.)
  • Darasa la VII, Shule ya Msingi Mwembeni, Musoma

Uzoefu:
  • Mwandishi wa habari, Jarida la Mama na Watoto, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mara
  • Mhasibu Mwandamizi, kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki - Fish Filters Tanzania Limited (Beach Department)
  • Mjumbe, bodi ya uandaaji gazeti la TAA la Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza (MPC)
  • Mteuliwa miongoni mwa waandishi na wapiga picha katika maziko ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mwitongo, Butiama) 1999
  • Mwandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na Msanii Afrika (Mwanza), Radio Free Africa (Mwanza), Mzawa (Mwanza), Hoja (Dar es Salaam), TAA (Mwanza), Jarida la Mazingira (Ubalozi wa Sweden), Mwakilishi wa Radio Uhuru Kanda ya Ziwa (2005-2009), Mwakilishi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo (2005-2010)
Ana mtoto mmoja.

Tuesday, June 1, 2010

Wageni wa Butiama: Walimu toka Canada


Kila mwaka kijiji cha Butiama hupokea wanafunzi wa ualimu toka Chuo Kikuu cha Queen's kilichopo Kingston, Canada. Kwa muda wa majuma kadhaa, wanafunzi hao hushiriki mazoezi yao ya ualimu kwenye Shule ya Sekondari Butiama. Miaka iliyopita walikuwa pia kwenye Shule ya Sekondari ya Machochwe iliyopo Wilaya ya Serengeti.

Pamoja na mazoezi ya kufundisha, wanaleta pia misaada ya vitabu na vifaa vya kufundishia kwenye shule wanazofikia. Chini ya ziara hizi, shule ya Machochwe imepata vifaa vya umeme vinavyotumia nguvu za jua, wakati shule ya Butiama imepokea fedha zilizojenga darasa la wanafunzi.

Kundi la Wakanda la mwaka 2008 (picha ya juu) lilijumuisha wanafunzi waliyotumia muda wao mwingi wa mapumziko wakicheza mpira wa mguu dhidi ya wanafunzi na vijana wa Butiama. Kwenye picha, kutoka kushoto ni Kathleen Bolger, Vicki Bowman, Stacey Copeland, Jennifer Lytle, Jennifer Michel, Shannon Mullins, and Karen Versluys.

Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Canada inashika nafasi ya kumi kwa ubora duniani.