Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, March 30, 2010

Wageni: Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete azuru Butiama

Picha: Mama Salma Kikwete (kulia) akihutubia kijijini Butiama leo asubuhi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mstaafu Enos Mafuru

Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, leo asubuhi alifanya ziara fupi kijijini Butiama ambapo alitembelea kituo cha afya cha Butiama, pamoja na kutoa msaada wa vifaa vya hospitali.

Akiwa pia Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), alichukuwa fursa katika hotuba yake kuelezea madhumuni ya WAMA kuwa ni pamoja na kuhamasisha uboreshaji wa afya ya wanawake na watoto, kuhimiza maendeleo ya elimu, hasa kwa wasichana, pamoja na kutahadharisha juu ya janga la UKIMWI.

Aliwaasa wanafunzi wa kike waliyohudhuria mkutano wake kutokubali vishawishi vya wavulana, vishawishi ambavyo alisema vikikubaliwa vitaleta athari kwa msichana na maendeleo yake ya elimu.

Wakati wa ziara yake alipewa zawadi ya ng'ombe na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambae alinunuliwa kutoka kwa mfugaji mashuhuri wa ng'ombe wa maziwa wa Butiama, Nashon Jirabi.

Nashon siyo mfugaji mzuri tu wa ng'ombe, bali amenijulisha kuwa ana kuku 200 wa mayai na anavuna zaidi ya trei 4 kila siku. Kwa bei ya Sh.5,000/- kwa trei moja, siyo pesa mbaya ukizingatia kuwa atavuna hayo mayai kwa kipindi cha miaka miwili. Inashinda biashara ya gari kwa mbali na hakuna visingizio vya kukamatwa na askari wa usalama barabarani.

Nashon pia amewahi kufanya kazi kama operata wa magari makubwa katika machimbo ya dhahabu ya Buhemba, pamoja na machimbo yaliyopo karibu na Lubumbashi, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Picha: Mama Kikwete (katikati ya picha) akitoa shukurani baada ya kukabidhiwa zawadi ya ng'ombe wa maziwa.

Picha: Kushoto ni mwanakiji mwenzangu, Nashon Jirabi akiwa na Mbunge wa Musoma Vijijini Mh. Nimrod Mkono (katikati), pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama, Zacharia Mang'ararya Wambura ambaye anajulikana zaidi kama "Debe Tupu" kabla ya kukabidhi zawadi ya ng'ombe kwa Mama Kikwete.
Picha: Nashon Jirabi (kushoto), Mbunge Nimrod Mkono (katikati), na Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama, "Debe Tupu."

Picha: Nashon akizungumza na Mbunge wa Musoma Vijijini Mh. Nimrod Mkono wakati wakisubiri kuwasili kwa Mama Salma Kikwete

Monday, March 29, 2010

Ziarani Uingereza

Picha: Mwenyeji wangu, Anna, Dk. William Shija, na mimi kwenye ofisi ya Dk. Shija.

Picha hii ya zamani kidogo inatokana na ziara niliyofanya nchini Uingereza mwaka 2007 kufuatia mualiko niliyopata toka Global Women's Strike, kikundi cha wanaharakati wa Uingereza wanaotetea haki za wanawake.

Wakati wa ziara hiyo nilipata fursa ya kumtembelea Dk. William Shija, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola kwenye ofisi yake iliyopo jirani na bunge la Uingereza. Dk. Shija alikuwa mmojawapo wa wagombea waliojitokeza ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania uteuzi wa kuwa mgombea urais wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005. Wakati huo alikuwa mbunge wa Jimbo la Sengerema.

Amewahi kuongoza wizara ya Sayansi, Teknolojia, na Elimu ya Juu; Wizara ya Habari na Utangazaji; Wizara ya Nishati na Madini; na Waizara ya Viwanda na Biashara.

Dk. Shija aliteuliwa tarehe 9 Septemba 2009 kushika wadhifa wake wa sasa kwa kipindi cha miaka mitano.

Saturday, March 27, 2010

Mada yangu ya leo: biashara ya fedha za kigeni

Jambo moja ambalo napata shida sana kulielewa ni taratibu za kuendesha biashara ya fedha za kigeni nchini Tanzania.

Unapokwenda kubadliisha fedha za kigeni kwenye mabenki au maduka ya fedha za kigeni baadhi ya sehemu hizo hazipokei fedha za Marekani zenye tarehe kabla ya mwaka fulani (nadhani ni 2003). Hivi karibuni niliposindikiza wageni kubadilisha fedha zao na nilipouliza ni kwanini kuna utaratibu kama huu, niliambiwa na mfanyakazi mmoja wa tawi la benki moja iliyopo Musoma kuwa Benki Kuu ya Tanzana inaelekeza kuwa pesa hizo zisibadilishwe na badala yake zichukuliwa pesa zenye miaka ya hivi karibuni, yaani kuanzia 2004 na kuendelea.

Hili ni jambo la ajabu sana, kwa sababu Tanzania ndiyo inaweza kuwa moja ya nchi chache duniani ambayo inakataa fedha ambazo wenyewe waliyozitengeneza hawana tatizo nazo. Nadhani Wamarekani wanaofika Tanzania na dola zao wakiambiwa kuwa hapa hazina thamani, hubaki kushangaa tu. Hapa Tanzania mteja anapunjwa kwa kupewa thamani ndogo ya fedha anazobadilisha wakati wanaobadilisha wanapata thamani ile ile ya fedha ya kigeni huko nje.

Jambo lingine ambalo linaruhusiwa na taratibu za Benki Kuu ni kuweka viwango taofauti kwa noti zenye thamani kubwa (mfano za mia, na za hamsini), na viwango vya chini kwa noti zenye thamani ya chini (mfano za ishirini, na kwenda chini).

Kwa kuweka viwango viwili tofauti, ni kama vile vile mteja anafanyiwa hisani kubadilishiwa zile noti za thamani ndogo. Aidha ni kama vile huko nje noti hamsini zenye thamani ya dola moja moja zina thamani ndogo zaidi kuliko noti moja ya dola hamsini. Wanaobadilisha noti zenye thamani ndogo kwa kiwango cha chini wanapata thamani ile ile ya pesa ya kigeni wanapoipeleka nje, lakini mteja anapunjwa.

Hivi karibuni nilimsindikiza rafiki yangu Mtanzania anayesoma Uingereza kubadilisha fedha kwenye benki mojawapo ya Musoma na alipopewa viwango tofauti, hakuelewa somo. Aling'ang'ania kiwango cha juu mpaka benki wakakubali yaishe na kumbadilishia paundi zake za Uingereza kwa kiwango kile cha juu.

Kuna wakati nilipolalamika kwa mfanyakazi wa kampuni ya simu na kutaka kufahamu sababu ya kuruhusu mawakala wao kuuza vocha kwa bei inayozidi thamani iliyochapishwa juu ya vocha yenyewe (mfano, kuuza vocha ya sh.1,000/- kwa sh.1,100/-), niliambiwa kuwa hawawezi kuingilia kwa kuwa tuko kwenye mfumo wa biashara huria. Sikuelewa. Naamini pia jibu kama hilo linaweza kutumika kutetea huu utaratibu wa viwango tofauti vya kubadilisha fedha za kigeni.

Maoni yangu: hii siyo biashara huria; ni ujambazi tu uliyoidhinishwa na sheria na taratibu.

Monday, March 22, 2010

CCM yaendeleza rirandi* ughaibuni

Hizi taarifa zilichelewa kunifikia, lakini siyo vibaya kuzitoa.

Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Pius Msekwa alizuru Uingereza hivi karibuni ambapo alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 33 ya CCM zilizoandaliwa na jumuiya ya wana-CCM waliyoko Uingereza.

Katika sherehe hizo alikabidhi kadi za uanachama kwa wanachama wapya pamoja na kutoa vitendea kazi kwa viongozi wa mashina ya CCM yaliyoanzishwa huko.

Baadhi ya mambo aliyozungumzia huko, kwa mujibu wa taarifa niliyopata kutoka kwa waandaaji, ni pamoja na Azimio la CCM la Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa hiyo:
"Alisema Azimio la Zanzibar la Februari 1991 halikuvunja Azimio la Arusha isipokua lilitazama upya masharti ya uanachama wa CCM na hasa ibara ya 8(7) ya katiba ya CCM toleo la 1987. Azimio la Zanzibar liliondoa miiko ya uongozi iliyowabana halaiki ya wanachama walio wakulima na wafanyakazi wa kawaida hasa baada ya mabadiliko ya uchumi na siasa ya vyama vingi. Hivyo alionya kuwa CCM na serikali yake haitawavumilia watovu wa maadili wanaokighilibu Chama na kuhujumu uchumi kwa kutumia mwanya wa CCM kujisahihisha, kujiboresha na kujiiimarisha."

 Picha zote zinaonyesha matukio mbalimbali wakati wa sherehe/mkutano huo.


*Kuhusu Rirandi: Baada ya rafiki yangu DC wa Tegeta kuendeleza libeneke kwa muda mrefu kwenye Michuzi Blog nimeona na mimi sina budi kumuunga mkono kwa mazingira ya eneo ninaloishi hivi sasa. Hivi karibuni nilitembelea blogu ya rafiki yangu John Kitime na kujifunza maana ya neno "libeneke." Inasemekana ni mtindo wa ngoma ya asili ya kabila la Wapogoro kutoka mkoa wa Mororgoro.

Mimi badala ya kutumia "libeneke", naendeleza "Rirandi." Wenyeji wa mkoa wa Mara watafahamu kuwa Rirandi ni ngoma ya asili ya kabila la Wakurya.

Saturday, March 20, 2010

George Marato wa ITV


George Marato ni mwandishi mashuhuri wa kituo cha televisheni cha ITV ambaye hurusha habari kutoka mkoa wa Mara.

Kwa muda niliyomfahamu ni mtu ambaye ni mtafutaji mzuri wa habari. Iwapo habari haijamfikia Marato, hiyo siyo habari. Itakuwa ni uzushi. Pamoja na kazi anayofanya ITV huwa anaandika makala kwa magazeti mbalimbali ya hapa nchini.

Kwenye picha anaonekana akiandaa habari kwa ajili ya kurusha hewani.

Thursday, March 18, 2010

Viongozi wa CCJ watembela Butiama


Viongozi wa Chama cha Jamii (CCJ) wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Mwalimu Nyerere, eneo la Mwitongo katika Kijiji cha Butiama leo asubuhi.

Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho Renatus Muabhi, na kulia ni Mwenyekiti wa CCJ Richard Kiyabo. Kwa mujibu wa maelezo waliyotoa viongozi hao, madhumuni ya kutembelea Butiama yalikuwa kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere, na kusalimia familia ya Mwalimu Nyerere.

CCJ kimeainisha ndani ya katiba yake madhumuni ya kufuata baadhi ya misingi ya sera za Mwalimu Nyerere, Raisi wa kwanza wa Tanzaia, aliyestaafu siasa mwaka 1985 na kufariki mwaka 1999.

Monday, March 15, 2010

Kuhusu Mwitongo

Eneo la Butiama linalojulikana kama Mwitongo ni sehemu yalipokuwa makazi ya Mtemi Nyerere Burito wa kabila la Wazanaki, ambaye alitawala kati ya mwaka 1912 - 1942. Alifariki tarehe 30 Machi 1942 na kuzikwa hapo hapo Mwitongo.

Maana ya Mwitongo ni mahame, au sehemu walipoishi watu na kuhamia sehemu nyingine. Sababu kubwa ya kuhama eneo ilikuwa kufariki kwa kiongozi mkuu wa familia (au ukoo) na kurithiwa kwa mali zake. Warithi walichukuwa mgao na kuhamia kwenye makazi yao. Enzi hizo, wake pia walirithiwa kwa hiyo wengi wa wake 22 wa Mzee Nyerere walirithiwa na kuhamia maeneo mengine.

Picha: Kaburi la Mtemi Nyerere Burito (kushoto), na la mke wake wa tano Mgaya wa Nyang'ombe (kulia). Nyumba ya mviringo ndipo ilipokuwa nyumba ya Mtemi Nyerere

Mgaya wa Nyang'ombe alikuwa mke wa tano wa Mtemi Nyerere, lakini tunaambiwa hakurithiwa kwa sababu mwanae, Julius Kambarage, alitamka angemtunza mama yake. Wageni wanaotembelea Mwitongo huonyeshwa eneo ambapo ilikuwepo nyumba ya Mgaya, au sehemu alipozaliwa Mwalimu Nyerere.

Picha: Sanamu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Mwitongo, sehemu alipozaliwa.

Kabla ya kufariki, Mwalimu Nyerere alielekeza sehemu ambapo angependa kuzikwa, pembeni tu ya sehemu alipozaliwa. Haikuwezekana kumzika alipotamka kwa sababu ni sehemu ambayo ulijengwa mfereji wa maji machafu. Sehemu iliyochaguliwa baadaye haikuwa mbali na eneo aliloelekeza yeye.

 Picha: Nyumba iliyojengwa kuzungukia kaburi la Mwalimu Nyerere, eneo la Mwitongo, Butiama.

Friday, March 12, 2010

Mwanaharakati wa Uingereza - Brian Haw

Wakati wa ziara yangu ya London mwaka 2007 nilipata fursa ya kutembelea Parliament Square, eneo lililopo bunge la Uingereza na sehemu ambapo mwanaharakati Brian Haw ameweka kambi ya kudumu ikiwa ni jitihada yake binafsi ya kupinga vita na sera ya nje ya Serikali ya Uingereza, hususani vita vya Iraq.
Picha: Brian Haw, mimi, na mkewe, Kay.
Amekuwa hapo tangu tarehe 2 Juni 2001, akiishi ndani ya hema. Habanduki hapo isipokuwa tu kuhudhuria kesi mahakamani na hupata msaada wa chakula na vitu muhimu toka kwa washirika wanaomuunga mkono. Nilipomtembelea alikuwa akishika kipaza sauti na kumwaga sera kwa mtu yoyote aliyekuwa tayari kusikiliza, sehemu kubwa ikiwa ni wapita njia na wapitao kwa magari.

Halmashauri ya Jiji la Westminster ilimfungulia kesi kujaribu kumuondoa alipo, lakini alishinda kesi hiyo ya mwaka 2002. Mahakama iliamua kuwa kambi yake haikuwa kizuizi kwa wapita njia kupita eneo hilo.

Alinifahamisha kuwa alikuwa akishirikiana na washirika wengine kujaribu kumuweka Waziri Mkuu wa wakati ule, Tony Blair, chini ya ulinzi na kumfikisha mbele ya sheria kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Saturday, March 6, 2010

Kumbukumbu ya ajali ya ndege

Kabla ya kuanza vita vya Kagera kati ya Tanzania na Uganda mwaka 1979 na wakati wa maandalizi ya kuanza mapambano hayo ilitokea ajali ya ndege ya Jeshi la Wanancnhi wa Tanzania (JWTZ) iliyosababishwa na kutunguliwa kwa makosa kwa ndege mbili zilizokuwa zikihamishwa kutoka kambi ya Ngerengere kwenda Mwanza.

Kutokana na kasi ya hizo ndege marubani wawili walivyofika Mwanza walijikuta wamepitiliza na katika jitihada za kurudi tena kutua Mwanza, ndege hizo zilipita kwenye anga ya Musoma ambapo zilitunguliwa na mizinga ya JWTZ kwa makosa kwa sababu ya kutokuwa na taarifa juu ya kupita kwa ndege hizo kwenye anga ya Musoma na kudhaniwa kuwa ni ndege za jeshi la anga la Uganda.

Baada ya kushambuliwa, ndege moja ilianguka Musoma na nyingine iliangukia Butiama, pembezoni mwa msitu wa Muhunda, na zaidi ya kilomita 40 toka Musoma. Sehemu ilipoanguka ndege hiyo ndiyo imewekwa kumbukumbu hii.
 
 Hii kumbukumbu ilijengwa miaka kadhaa iliyopita, lakini jambo la ajabu ni kuwa hivyo vyuma vinavyoonekana pembeni vilibanduliwa na wafanyabiashara wa vyuma chakavu kwa ajili ya kuuza kwenye viwanda vinavyotengeneza nondo.

Tuesday, March 2, 2010

Kuhusu Muhunda

Muhunda ni eneo la kijiji cha Butiama ambapo kwa kabila la Wazanaki ni msitu ambapo zamani mitambiko mbalimbali ya kimila ilikuwa ikifanyika.

Ni eneo lenye ukubwa wa kiasi cha ekari 15 ambalo limewekewa uzio, na hairuhusiwi kuingia humo kiholelaholela. Ni wazee wa kimila tu, waitwao Wanyikura, wanaoruhusiwa kuingia humo kufanya mitambiko. Kuna kundi lingine dogo la watu maalum ambao nao huruhusiwa kuingia humo. Wengine, kama kina mama wanaotafuta kuni za kupikia, wanaruhusiwa kuingia na kuokota kuni ambazo zinatokana na matawi ya miti yaliyoanguka yenyewe lakini hawaruhusiwi kukata kuni toka kwenye matawi ya miti uliosimama.

Inaaminika kuwa mzimu wa Wazanaki wa eneo la Butiama, unaoitwa Muhunda, ndiyo unaishi katika eneo hili, na ndiyo sababu panaitwa Muhunda. 'Muhunda' ni kama mzimu unaoilinda jamii ya Wazanaki wa Butiama. Wazanaki wa maeneo mengine nao wanayo mizimu yao.

Vilevile, inaaminika kuwa Muhunda hujitokeza kama nyoka, au nyani mkubwa, au wakati mwingine kama chui. Katika kuishi Butiama kwa miaka kumi mfulilizo sasa, nimeshashuhudia nyani mkubwa kuonekana eneo la Muhunda, na baadaye wazee walifunga safari kwenda eneo la mto Mara kwa mpiga ramli kutaka kufahamu maana ya kuonekana kwa 'Muhunda.'

Inasemekena wakati wowote kukitokea tukio kama hilo kuna tatizo ndani ya jamii na ni jukumu la wazee wa mila kuchunguza tatizo ni nini na kufanya mitambiko kuzuia tatizo hilo kuendelea.