Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, June 18, 2012

Ukoo mkubwa kuliko maelezo

Mapema kwaka 2000 nilipewa jukumu la kumtambulisha mgeni kwa kundi la wenyeji waliofika kumpokea huyo mgeni nyumbani Butiama. Kabla ya mgeni kufika nilichukuwa kalamu na karatasi na kumuuliza aliye karibu nami jina lake na akanitajia jina na ubini wake. Cha ajabu, alikuwa na ubini kama wangu. Baadaye niligundua kuwa ni mmoja wa baba zangu wadogo.

Niliona aibu sana, lakini naamini kuwa ninayo sababu nzuri ya kutomfahamu. Marehemu babu yangu, Mtemi Nyerere Burito, alikuwa na wake 22. Aidha alikuwa na kina mama wa nyumba ndogo wanne ambao kwa kabila la Wazanaki wanajulikana kama vitungo. Kutokana na uzao wa babu na wake zake, mimi nina ndugu na jamaa wanaokaribia 6,000 kwa hiyo kumfahamu kila mmoja wao siyo jambo rahisi.

Kwa kawaida, uzao uliyonitangulia ulikuwa na watoto wengi, lakini iwapo nitachukuwa wastani wa watoto sita tu kwa kila mme na mke kwa ajili ya kukadiria idadi ya uzao wa Mtemi Nyerere, nikianza na bibi zangu ishirini na wawili, napata idadi ya baba wadogo/shangazi 132, watoto wa baba wadogo/shangazi 792, na wajukuu wa baba wadogo/shangazi 4,752, ikiwa ni jumla ya ndugu 5,676. Na hii ni kutoka upande wa baba mzazi tu.
Kaburi la Mtemi Nyerere Burito, kulia, pamoja na kaburi la mke wake wa tano, Christina Mgaya wa Nyang'ombe, kushoto, katika eneo la Mwitongo kwenye kijiji cha Butiama.

Hata iwapo watapunguzwa wale waliofariki, bado inaacha idadi kubwa ya majina na sura ambazo si rahisi kuzikumbuka, pamoja na kuzingatia kuwa kukumbuka ndugu ni suala linaloweza kujenga mahusiano mazuri kwenye familia kubwa. Swali moja ambalo naulizwa mara kwa mara ninapokutana na ndugu ambao siwafahamu vizuri ni: "Unanifahamu mimi?" Ninapokuwa namfahamu mambo huenda vizuri lakini pale ninaposhindwa kumtambua nakuwa mtu nisiefaa kabisa, nachukuliwa kama mtu ambaye hafanyi jitihada ya kutosha kuwafahamu ndugu zake.
Sehemu ya wanaukoo wa Burito Nyerere wakiwa 
Hivi karibuni nilikutana na binamu zangu wawili ambao mama yao, marehemu shangazi yangu, ni binti wa tatu wa mke wa saba wa Mtemi Nyerere Burito. Pamoja na kuwa anakaribia miaka 50, mmoja wa wale binamu zangu hakuwa ananifahamu, na alikuwa hajawahi kusikia jina langu. Ilikuwa ni faraja kubwa sana kwangu kwa sababu ilikuwa ni ushahidi tosha kwangu kuwa tatizo la kutoweza kuwatambua ndugu zaidi ya 5,000 halikuwa linawakumba tu wale waliokaa sana jijini Dar es Salaam.

Friday, June 15, 2012

Mwanzo wa msafara wa Mlima Kilimanjaro

Tarehe 10 Juni 2012 nimemaliza msafara mwingine wa kukwea Mlima Kilimanjaro nikiwa pamoja na kundi la watu 14 katika msafara uliyokuwa na madhumuni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya Shule ya Sekondari Nyegina.

Kutegemea na njia inayotumika, msafara wa kwenda kilele cha Mlima Kilimanjaro unachukuwa kati ya siku 5 hadi 10. Msafara wetu ulichukuwa siku 7 kwenye njia ya Lemosho inayoanzia kwenye lango la Londrossi.
Katika siku ya pili ya msafara, kilele cha Kibo kilionekana mbele yetu kwenye uwanda wa juu wa Shira na kumpa kila mmoja shauku ya kufika kileleni. Wawili kati ya ya 14 tulioanza hawakufanikiwa kufika kileleni. Habari kamili zitawekwa hapa hivi karibuni.

Waziri Bernard Membe naye atabiri hali ngumu kwa Chama cha Mapinduzi

Nimewahi kuandika hapa kuwa majaliwa ya Chama cha Mapinduzi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 hayaonekani kuwa mazuri kutokana na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:

1. kuongezeka kwa nguvu ya kisiasa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
2. kuendelea kupoteza majimbo ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na jimbo la Arumeru hivi karibuni
3. kuachana na misingi iliyokitambulisha Chama cha Mapinduzi kama mwakilishi wa maslahi ya Watanzania wanyonge, wakulima na wafanyakazi.

Habari kamili ziko hapa:

http://muhunda.blogspot.com/2012/04/chama-cha-mapinduzi-ukingoni.html

Sasa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, naye anatabiri hali mbaya kwa CCM. Habari zake kamili hizi hapa:

http://swahilivilla.blogspot.com/2012/06/aitabiria-ushindi-chadema-uchaguzi-mkuu.html?spref=fb

Ukiona kiongozi mwandamizi wa chama tawala naye anatoa hoja kama hizi ni vugumu kuendelea kusema kuwa ni hoja za watu wasiokitakia mema Chama cha Mapinduzi. Hazibaki kuwa ni ndoto za wapinzani sasa.

Thursday, June 14, 2012

Francis Cheka kupambana na Joseph Kaseba siku ya Saba Saba

Bingwa wa IBF wa Afrika wa uzito wa Super Middleweight, Francis Cheka, ataingia ulingoni tarehe 7 Julai 2012 kupambana na Joseph Kaseba katika pambano linaloandaliwa na Global na kuratibiwa na Kaike
Francis Cheka, kushoto, na Joseph Kaseba, kulia.
Siraju.

Cheka alitwaa ubingwa wa mabara wa IBF afrika alipomshinda Mada Maugo katika pambano liliofanyika ukumbi wa PTA Dar es Salaam tarehe 28 Aprili 2012.

Pambano hilo litakuwa pambano la kwanza kufanyika katika uwanja mpya wa Taifa wa Dar es Salaam. Baadhi ya mapambano yatakayosindikiza pambano hilo ni pamoja na Adiphoce Mchumia dhidi ya Ramadhani Kido, Amos Mwamakula dhidi ya Rashini Ali, Mkongo Kanda Kabongo dhidi ya  Said Mbelwa, na bondia chipukizi Ibrahimu Class toka kambi ya masumbwi Ilala inayonolewa na kocha Habibi Kinyogoli atapambana na Sadiki Momba.

Picha na habari kwa hisani ya superdboxingcoach.

Sunday, June 3, 2012

Onesmo Ngowi ateuliwa kuandaa mkutano wa mwaka wa IBF 2012

Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama cha Ngumi cha Marekani (IBF/USBA) limemteua Rais wa Shirikisho hilo katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi,  Mtanzania Onesmo Ngowi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuandaa mkutano wa 30 wa Shirikisho hilo mwakani. Mkutano wa 30 wa IBF/USBA unatarajiwa kufanyika katika jiji la Berlin nchini Ujerumani kuanzia tarehe 24 hadi 30 Juni mwaka 2013.
Ngowi alichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho la IBF/USBA uliomalizika Hilton Hawaiian Village Resort, jijini Honolulu, Hawaii, Marekani tarehe 2 Juni. Uteuzi wa Ngowi unafuatia juhudi zake alizozifanya kuendeleza shirikisho hilo katika bara la Afrika tangu ateuliwe na Rais wa zamani wa IBF/USBA Robert Lee Sr. mwaka 1999 jijini New Jersey, Marekani. Onesmo Ngowi anakuwa mtu wa kwanza kutoka bara la Afrika kushika nyadhifa kubwa katika taasisi ya ngumi duniani na hii inaisaidia sana Tanzania na bara zima la Afrika kijitangaza vyema katika nyanja mbalimbali kama vile utalii na bishara.

Katika Kamati hiyo ya maandalizi kuna wajumbe sita nao ni ; Louis Priluker  wa Marekani, Roberto Rea wa Italia, Lahcen Oumghar wa Uholanzi na Roberto Ramirez wa  Mexico. Kamati hiyo itafanya shughuli zake katika kipindi cha mwaka mmoja na itakutana mara nne kwa mwaka. Sekretarieti ya Kamati ya Ngowi itakuwa katika jiji la New Jersey nchini Marekani kuliko na makao makuu ya shirikisho hilo duniani.

Mkutano huo wa Honolulu uliazimia kufanya mkutano wa IBF kwaka 2014 katika bara la Asia na mwaka 2015 IBF itafanya mkutano wake katika bara la Afrika mahali ambapo patateuliwa.

Ngowi  anawahimiza Watanzania ambao wako katika uandaaji wa mikutano kuchangamkia nafasi hii ambayo itawaleta watalii zaidi ya 1,000 nchini toka nchi zaidi ya 200 duniani. Hii ni nafasi ya nadra sana katika biashara na watanzania ni muhimu wakachangamka kama wenzao wengine katika nchi zinazokuwa wenyeji wa mikutano kama hii.

Saturday, June 2, 2012

Wadau wa IBF wakiwa Honolulu

Rais wa shirikisho la ngumi la IBF Daryl Peoples, katikati, akiwa amesimama na Rais wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi, Onsemo Ngowi, kulia, pamoja na promota maarufu wa ngumi za kulipwa toka Thailand, Jimmy Chaichotchuang, walipotembelea Pearl Harbour katika kisiwa cha Honolulu.

Wanahudhuria kikao cha mwaka cha IBF ambacho kinafanyika huko Honolulu na kitamalizika leo.