Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, February 26, 2013

Lugha yetu Kiswahili

Hivi majuzi katika sherehe mojawapo niliandaa mtiririko wa nyimbo mbalimbali za muziki wa dansi za kusikiliza kwenye sherehe hiyo kwa kutumia kompyuta yangu ambayo inahifadhi mkusanyiko wa nyimbo nyingi ambazo nimezikusanya kwa miaka mingi. Baada ya hapo kompyuta inaunganishwa na vipaza sauti na nyimbo zilizochaguliwa zinaanza kusikika moja baada ya nyingine kwa muda mrefu tu.

Nyingi ya nyimbo hizo ni za wanamuziki wa zamani, wengi ambao hawako hai kwa sasa. Baadhi ya hizo Watanzania tunaziita "zilipendwa" au nyimbo za zamani ambazo vijana wengi wa siku hizi hawasikilizi.

Mmoja wa waliohudhuria sherehe hiyo alizipenda nyimbo zile sana na hakutulia sana kwenye kiti chake, akiinuka mara kwa mara kwenda kucheza muziki mmoja baada ya mwingine.

Nilivyotambua jinsi nilivyomsumbua huyo mtu nikajisifia kwa kumuuliza: Umenikubali? Na hapo nikazua mjadala na mtu mwingine aliyehudhuria sherehe hiyo akihoji iwapo ilikuwa sahihi kwangu kutumia neno hilo. Alisisitiza kuwa hawezi kunikubali mimi bali anaweza kukubali nyimbo ambazo nilizichagua kusikilizwa kwenye sherehe hiyo.

Mimi nilisisitiza kuwa "kunikubali" ulikuwa ni msemo tu lakini ukimaanisha alikubali uwezo wangu wa kuchagua nyimbo nzuri na siyo kunikubali mimi binafsi. Hoja yangu ilikuwa hata asingefahamu ni nani aliyechagua zile nyimbo angeweza kusema: "namkubali aliyepanga hizo nyimbo."

Ni kweli kuwa msemo wa "kumkubali" mtu umeibuka kwenye matumizi yasiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili, hasa kwa vijana wa Tanzania, ukimaanisha kutoa sifa isiyo ya kawaida kwa mtu kwa uwezo wake wa kufanya jambo fulani.

Lakini siyo kweli pia kuwa tunaweza kuzungumzia kuwa wapiga kura "wamemkubali" mgombea mmoja na kumchagua kuwa kiongozi wao na kwa maana hiyo matumizi hayo yakaleta maana rasmi?

Wewe unasemaje?

Sunday, February 17, 2013

Wageni wa Butiama: mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC

Hizi ni habari za zamani kidogo ambazo nilizitoa kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza. Nazirudia hapa kwa manufaa ya wale ambao hawakuzisoma.
******************************************
Kabla ya kufika kwa Jaffar Amin kijijini Butiama mwezi Aprili [2009] ziara yake, ambayo iliandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya shirika la utangazaji la BBC, ilitanguliwa na kufika Butiama kwa baadhi ya miamba ya utangazaji ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikiwa ni pamoja na Solomon Mugera, mkuu wa Idhaa hiyo, na Vicky Ntetema, kiongozi wa ofisi ya BBC iliyopo Tanzania.
Wengine toka BBC waliyofika Butiama walikuwa ni muongozaji vipindi Charles Hilary ambaye kwa desturi hutangaza akiwa London, Caroline Karobia anayefanya kazi kutokea Nairobi, na jina lenye kufahamika na wengi wa wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Eric David Nampesya, mtangazaji wa BBC wa eneo la Maziwa Makuu, ambaye anaonekana hapo juu, kulia, pamoja na Solomon Mugera. 

Nikiwa mmoja wa wasikilizaji wa mara kwa mara wa BBC nilijisikia mwenye furaha kuwa miongoni mwa watu mashuhuri kama hawa toka Idhaa ya Kiswahili ya BBC.

Friday, February 15, 2013

Wazanaki na mirathi

Kwa desturi ya kabila la Wazanaki, wapwa ndiyo walirithi mali za marehemu. Baadhi ya sababu zinazotajwa kwa jamii ya Wazanaki kufuata mila hii ni kuwa baba wa familia hakuwa na uhakika kuwa watoto waliozaliwa na mke (wake) zake walikuwa ni wa kwake.

Kwa sababu hiyo urithi walipewa wapwa kwa sababu, kupitia kwa dada yake, baba huyo alikuwa na uhakika kuwa anapofariki mali zake zinabaki kwa ndugu ambao ana uhusiano nao wa damu.

Mila hii ilianza kupungua nguvu kwenye msiba wa mmoja wa wadogo zake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Joseph Kizurira Nyerere aliyefariki tarehe 8 Agosti 1994.
Mzee Joseph Kizurira Nyerere, kushoto, alikuwa shabiki mkubwa wa Vijana Jazz Orchestra.
Akizungumza baada ya mazishi ya mdogo wake, Mwalimu Nyerere alisema umefika wakati kwa Wazanaki kuachana na hiyo desturi na kurudisha mirathi kwa mke na watoto wa marehemu.

Wednesday, February 13, 2013

Francis Cheka kutetea ubingwa wa Afrika dhidi ya Thomas Mashali Mei Mosi


Taarifa kwa vyombo vya habari toka Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Afrika (IBF/Africa) linaarifu kuidhinishwa kwa pambano la utetezi la ubingwa wa IBF Africa unaoashikiliwa na Mtanzania Francis Cheka. Habari kamili hizi hapa:
********************************************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
FEBRUARY 13, 2013
   Francis Cheka (kushoto) akiwa na Adam Tanaka (katikatia) na Thomas Mashali (kulia)
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Afrika (IBF/Africa) limetoa kibali kwa bondia Francis Cheka ambaye ni bingwa wa Afrika katika uzito wa Super Middle kutetea ubingwa wake dhidi ya bondia Thomas Mashali wa Tanzania. 

Mabondia hao wawili leo tarehe 13 February walikutana katika hoteli ya Ndekha, iliyoko Magomeni Kondoa na kutia sahihi mkataba wa kupigana pambano hilo ambalo limepangwa kufanyika siku ya Mei Mosi katika ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam.

Thomas Mashali ambaye ndiye bingwa wa Afrika ya Mashariki na Kati (ECAPBF) katika uzito wa Middle ana kiwango kizuri cha kushindana na Francis Cheka katika pambalo hilo.

Hii itakuwa mara ya pili kwa bondia Francis Cheka kutetea mkanda alioushinda tarehe 29 April 2012 dhidi ya bondia machachari Mada Maugo wa Tanzania. Cheka aliutetea vyema mkanda wa ubingwa wa IBF/Afrika dhidi ya bondia Chiotcha Chimwemwe ambaye ni Afisa katika jeshi la Malawi siku ya Boxing Day (26 Decewmber 2012) katika jiji la Arusha.

Kama Francis Cheka atashinda tena pambano hili, atapewa nafasi ya kupigana kugombea mkanda wa IBF wa mabara (IBF I/C) .

Pambano hili linaandaliwa na kampuni ya Mumask Investment and Gebby Pressure ya jijini Dar es Salaam chini ya uratibu wa Adam Tanaka.

Imetumwa na:

UONGOZI
Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Africa (IBF/Africa)
Dar-Es-Salaam, Tanzania 

Taarifa nyingine inayohusiana na hii
http://muhunda.blogspot.com/2012/05/ngowi-kusamamia-pambano-la-ubingwa-wa.html

Monday, February 11, 2013

Mapigano kati ya Wakristu na Waislamu Katoro, Geita, 7 wafa

Kuna taarifa nimepata kuwa watu saba wamekufa kutokana na mapigano kati ya Wakristu na Waislamu huko Katoro, Geita.

Kwa mujibu wa mtoa habari vurugu zilianza kutokana na mmiliki wa bucha kuuza nyama ya ng'ombe aliyechinjwa na Mkristu.

Baadhi ya Waislamu walifika kwenye bucha hiyo na kuichoma moto na kusababisha kuzuka hayo mapigano.

Taarifa zinasema pia kuwa raia wa kigeni ambaye alipita kwenye eneo la vurugu kwa gari alishambuliwa na kuchinjwa.

Hivi karibuni Serikali mkoani Mwanza iliagiza kuwa Waislamu pekee ndiyo waruhusiwe kuchinja wanyama ambao nyama yao inauzwa kwenye bucha.

Friday, February 8, 2013

Mtanzania apata nafasi ya kugombea ubingwa wa Dunia IBFTAARIFA KWA UMMA
FEBRUARY 6, 2013
DAR-ES-SALAAM, TANZANIA

Bingwa wa IBF katika bara la Afrika uzito wa unyoya (Featherweight) Ramadhani Shauri amepewa nafasi ya kugombea ubingwa wa dunia wa IBF kwa vijana walio chini ya miaka 25 katika uzito wa Lightweight. Shauri ambaye alishinda taji la ubingwa wa IBF katika bara la Afrika mwaka jana baada ya kumpiga bondia Sunday Kizito wa Uganda ana rekodi ya mapambano 17.


IBF imeamua kumpatia Shauri nafasi ya kugombea ubingwa huo wa dunia kwa vijana baada ya kuangalia mkanda wa video wa pambano lake la ubingwa wa Afrika na kuridhika kuwa anaweza kushindania ubingwa huo wa vijana,

Mabondia wengi wa Marekani ambao walikuja kuwa mabingwa wa dunia na kuweza kupata pesa nyingi walianza kuwa mabingwa wa dunia kwa vijana na hivyo kuweza kupanda chati kwenye viwango vya IBF. Mbondia hao ni kama Bernard Hopkins, Floyd Mayweather na Oscar De la Hoya.
Ramadhani shauri akiwa na mkanda wa ubingwa wa IBF Afrika.
Kama Shauri atashinda na kuwa bingwa wa dunia upande wa vijana atakuwa kwenye macho ya mapromota wakubwa duniani kama kina Dong King, Bob Arum na wengine wengi. Nafasi kama hii inaipa nchi ya Tanzania nafasi nzuri sana ya kujitangaza kibiashara na utalii kwani dunia inaiona kuwa kati ya nchi zinazotoa mabingwa wa dunia.

Kama Shauri atashinda taji hili atakuwa Mtanzania wa kwanza tangu historia ya ngumi nchini kuweza kushinda taji la shirikisho kubwa kati ya manne duniani ambayo ni IBF, WBA, WBO na WBA.

Shirikisho la Ngumi la Kimatafia Afrika (IBF/Africa) ambalo lina makao yake makuu ya kuhudumia bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati ndilo lililomtafutia Shauri nafasi aliyopata.

IBF/Africa inawahamasisha Watanzania walio na mapenzi mema na nchi yao pamoja na makampuni mbalimbali binafsi ya umma yajitokeze kwa wingi kumpatia Shauri ufadhili wa kuweza kuligombea taji hili.
Mungu mbariki bondia Ramadhani Shauri, Mungu ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amen.

Imetolewa na:
UTAWALA
Shiriklisho la Ngumi la Kimataifa Afrika (IBF/Africa)
Dar-Es-Salaam, Tanzania

Tuesday, February 5, 2013

Mada yangu ya leo: Tulipie gazeti na kupanga kurasa?

Mara kwa mara hununua gazeti na ninapoanza kusoma nakuta kuwa kurasa za ndani hazijapangwa kwa mtiririko wa kawaida, namba za mwisho zikiwa zimetangulia. Mathalani, unaweza kusoma kurasa ya tano na ukiendelea unakuta inafuata kurasa ya 19.

Hii inatokana na mpangilio mbaya wa karatasi zilizomo ndani zenye kurasa nne kila moja. Ni rahisi kurekebisha huu mkanganyiko kwa kupanga vyema tu hizo kurasa na kuendelea kusoma gazeti kwa mtiririko uliyokusudiwa na wahariri.

Kwa hiyo mara kwa mara hujikuta najaribu kurekebisha huo mpangilio uliokusudiwa na naamini wasomaji wengine wengi hufanya hivyo. Hii ni kazi ambayo inapaswa kufanywa na wachapishaji lakini ni dhahiri kuwa hawaifanyi, au kwa kuona haina umuhimu, au yawezekana kuwa mashine ambazo zinapaswa kufanya kazi hii ya kupanga kurasa hazifanyi kazi vizuri.

Kwa sababu yoyote iliyopo ni suala ambalo halipaswi kuendelea. Mteja alipie gazeti, halafu apange kurasa za gazeti? Hii ni bidhaa ambayo haijakamilika. Haina tofauti na kwenda kwa kinyozi halafu akukabidhi mashine ya kunyolea nywele na kukwambia ukate nywele zako mwenyewe halafu ukimaliza akudai hela.

Monday, February 4, 2013

Amani Millanga ahoji ukodishwaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji (sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)


Katika sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala yake hii ambayo nimeitoa katika sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.

**********************************************************
Mali ya Taifa (sehemu ya tatu)

Na Amani Millanga

Tanzania ya leo imejaa watoto wengi wa mitaani. Katika kusherehekea miaka 100 ya uhuru mwaka 2061 kizazi hiki cha maskini hohehahe wasio na ardhi kitakuwa kimeongezeka sana kwani hakuna jitihada za makusudi za kupambana na ongezeko la watoto wa mitaani. Hawa watakuwa ni watumwa katika Tanzania iliyojaa walowezi. Lakini historia ya wanadamu inaonyesha kwamba binadamu hudai haki zao. Kizazi hiki kitadai ardhi. Itapatikana wapi ardhi ya kuwapa? Katika hiyo benki ya ardhi?  

Nchi yetu inapaswa kujifunza kutoka kwenye makosa makubwa yaliyofanyika katika uwekezaji katika uchimbaji madini ambao kimsingi ni UWIZISHAJI. Mali ya taifa inaporwa kwa kutumia sheria za nchi. Tunaachiwa mazingira yaliyoharibiwa na kemikali na mashimo. Nasikia mashimo hayo yatageuzwa kuwa mabwawa ya kufugia samaki. Kichekesho kwelikweli. 

Jambo la kusikitisha ni kwamba fikra bado ni zilezile ,“wanaokodisha ardhi watatoa ajira, watakuza uchumi na kuwasadia wakulima wadogo.” Kwa kutumia hesabu za pato la taifa (GNP) wanatuonyesha kwamba uchumi utakua lakini ukuaji huo utakuwa mikononi mwa walowezi na wala hautawafikia Watanzania wengi vijijini na mijini.

Tufahamu kwamba wanaokodishiwa ardhi wamekuja kuchuma (kunyonya) na kupeleka mali kwao na wala si kuinua uchumi wa Mtanzania au kumlisha Mtanzania. Na huu ni wizi wa ajira na mapato ya Mtanzania. Kwa jembe la mkono Tanzania inajitosheleza kwa chakula na inalisha nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, Somalia, Malawi na hata Zambia. Kama tunaweza kuwalisha jirani basi tunaweza kuwalisha Waarabu, Wakorea, Waingereza, n.k. 

Hivi kuna uharamu gani kwa Mtanzania kuzalisha embe na nanasi zikauzwa Uingereza, mchele ukauzwa Saudi Arabia na Qatar, nyanya zikauzwa Korea na machungwa yakauzwa popote pale duniani? Ni wapi tunashindwa? Je tumeshajiuliza ni kwa nini tunashindwa? Je tumeshatafuta dawa mujarabu ya kutuwezesha kuzalisha kwa ubora wa kimataifa ya kuliteka soko? Kama jibu ni ndiyo, kwa nini tunaendelea kukodisha ardhi tena kwa bei ya chee kwa wageni? Kama jibu ni hapana, kwa nini wenye jukumu la kumuwezesha Mtanzania kuzalisha kwa kiwango kikubwa chenye ubora wa kimataifa hawawajibishwi? Wanapaswa kuwajibishwa kwa sababu wanahujumu uchumi na ustawi wa nchi kwa kuwatelekeza wakulima.    

Hivi kweli tunashindwa kuufufua ushirika? Je tunashindwa kumwezesha mkulima mdogo akawa mkulima mkubwa? Haya yote yanawezekana kikwazo kikubwa kilichopo ni kwamba nia ya dhati ya kuinua maisha mkulima haipo. Hili linatokana na kuendelea kukumbatia sera za Benki ya Dunia na IMF ambazo zinaukomaza zaidi mfumo wa kinyonyaji wa kibeberu na kuwaharibia maisha Watanzania. Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuacha kukodisha ardhi yetu kwa walowezi. Kuendelea kwa zoezi hili kutaiangamiza Tanzania. Hatupaswi kuufumbia macho ukweli huu.

Sunday, February 3, 2013

William Rutta anaandika kuhusu senene katika utamaduni wa Wahaya


William Rutta ni Meneja wa Kiroyera Tours. Hapa anatoa maelezo kuhusu utamdauni wa kabila la Wahaya wa kula senene.
*************************************************
Senene katika utamaduni wa Wahaya
William Rutta
na William Rutta

Senene (Ensenene, kwa Kihaya) ni miongoni mwa wadudu wanaotumiwa sana na kabila la Wahaya mkoani Kagera kama kitoweo, pengine kuliko kabila lolote tangu enzi za mababu.

Pamoja na wadudu hao kuheshimika katika kabila la Wahaya, historia kamili ya asili ya wadudu hao bado haijulikani.

Mwanzoni senene waliliwa na wanaume peke yake. Wanawake walionywa wawe na haya siku zote na wasivunje mwiko kwa kula senene na vitu vyote vilivyokatazwa. Wanawake wote walikuwa na utii wakiheshimu mila na desturi za kabila lao hivyo kutokana na haya hiyo waliitwa “WAHAYA”. 

Wasichana walipeleka zawadi ya senene kwa wachumba wao kama ishara ya kuonyesha upendo na utayari wa kuolewa na mchumba huyo. Msichana ambaye hakufanya hivyo uwezekano wa kuolewa na mchumba wake ulikuwa mdogo, hivyo senene walitumika kama ishara ya upendo na uaminifu.

Zipo aina nyingi za senene lakini wale wanaozungumziwa hapa wamegawanyika katika kundi lijulikanalo kama Orthopterous. Hawa ni jamii ya panzi wapole ambao hawana tabia ya kuharibu na kuteketeza makazi yao kwa chakula kama walivyo nzige wengine. Senene huzaliana kwa wingi katika mwambao wa maziwa makuu baada ya kutaga mayai yao ardhini kipindi cha kiangazi.

Baada ya kutaga mayai na kuangua mzunguko wa maisha yao huishia kati ya mwezi Oktoba na Desemba ambapo kipindi hiki huwa ni msimu wa mvua za vuli zijulikanazo kwa wahaya kama Omusenene. Hiki ni kipindi ambacho senene huruka wakiwa katika makundi wakihitimisha safari ya maisha yao.

Pamoja na kutumika kama kitoweo pia jamii imeanza kufaidika na senene kama chanzo cha kujipatia kipato, jambo ambalo limeufanya mkoa wa Kagera hasa Bukoba kujulikana sana kitaifa na kimataifa, pia kutokana na uchunguzi wa madaktari imeonekana kuwa senene wanaongeza vitamin “C”

Taarifa nyingine inayofanana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2011/09/lugha-yetu-kiswahili.html

Taarifa nyingine inayofanana na hii kutoka kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza
http://madarakanyerere.blogspot.com/2012/10/akamwani-traditional-welcome-gesture-in.html