Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, March 31, 2012

Gumzo za Nyamisisi

Muda si mrefu uliopita nilikuwa Nyamisisi kwenye barabara kuu inayounganisha Manispaa ya Musoma na jiji la Mwanza.

Wakati nikisubiri basi la kuelekea Mwanza nilisikia mazungumzo ya baadhi ya wakazi wa eneo lile.

Kwanza mmoja wao alianza kuwaarifu wenzake kuhusu mtu ambaye wanamfahamu ambaye alikuwa amehamia Urusi na ambaye kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo mtu alikuwa anapata kipato kikubwa huko Urusi.

Nilitafakari sababu ya kumhamisha mtu kutoka Nyamisisi hadi Urusi na sikuipata. Hata hivyo nilivyoendelea kusikiliza yale mazungumzo nikagundua sikuwa nimeelewa vizuri. Aliyekuwa akizungumziwa alikuwa Malouda, mcheza kandanda maarufu ambaye anacheza soka ya kulipwa nchini Urusi.

Mazungumzo yalihamia kuhusu malipo makubwa ya wacheza mpira na wanamuziki. Mchangiaji mmoja alisisitiza kuwa wanamuziki wanalipwa pesa nyingi zaidi kuliko wacheza mpira na katika kusisitiza hoja yake alisimulia yaliyomkuta David Beckham.

Alieleza Beckham, akiwa Marekani, aliingia kwenye duka la nguo kwa madhumuni ya kununua nguo na akamwambia mwenye duka afunge duka kwa sababu sehemu ile haikuwa salama, na yeye alikusudia kununua nguo zenye thamani iliyo sawa na shilingi milioni 50.

Mwenye duka akamuuliza Beckham: "Wewe ni nani mpaka nifunge duka?"
Beckham: "Mimi ni David Beckham."
Mwenye duka: "Unafanya shughuli gani?"
David Beckham: "Ni mchezaji wa mpira."

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa Nyamisisi, yule mmiliki wa duka alimwambia Beckham: "toka hapa!" na akamfukuza dukani kwake.

Mtoa maelezo aliendelea kuwahadithia wenzake kuwa wasanii maarufu ulimwenguni ni matajiri zaidi kuliko wachaeza mpira wa miguu ingawa kuna baadhi ya waliyomsikiliza walipinga hiyo hoja.

Baada ya muda basi la Mwanza likafika na kuninyima fursa ya kuendelea kusikiliza gumzo za Nyamisisi.
posted from Bloggeroid

Tuesday, March 27, 2012

Kambi ya Barafu ya Mlima Kilimanjaro

Kambi ya Barafu ya Mlima Kilimanjaro iko usawa wa Mita 4,800 juu ya usawa wa bahari. Ni kutokea kambi hii ndipo wengi wanaoelekea kilele cha Uhuru huanza safari yao saa 5 usiku.

Safari ya kufika kileleni hukamilika kati ya saa 12:00 alfajiri hadi saa tatu asubuhi, ikitegemea kasi ya mwendo.
Vibanda vya mviringo vya wahifadhi vilivyopo Kambi ya Barafu.
Vibanda vya mviringo katikati ni vya wahifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, sehemu ambapo kila mgeni hujisajili anapowasili kambini.

Monday, March 26, 2012

Amani Millanga azungumzia maandamano ya Songea (sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)

Vijana na Maandamano, Polisi na Mauwaji: Tunaelekea Wapi? (Sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)

Na Amani Millanga

Wengi watakubaliana nami kuwa kiini hasa cha watu kuandamana ni kukithiri kwa umaskini nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana, uonevu, kutokuthaminiwa kwa UTU wa watu na kuheshimiwa HAKI zao, maisha kuwa ghali, unyonyaji na dhuluma.

Katika hotuba yake ya “Wasia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM” Hayati Baba wa Taifa aliyachambua vema mambo haya aliposema hivi:

“Tanzania isikosee ikaacha msimamo wake wa kuhakikisha kwamba uko usawa wa binadamu, kuna usawa wa msingi katika hali ya maisha ya kila mtu, na kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania. Tukifanya kosa kama hilo tutavuruga msingi wote wa utulivu na amani katika nchi yetu. Maana yake ni kwamba tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za ‘Sisi’na ‘Wao’. Tutaacha watu wachache wawe na mali nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; watu wengi wawe ni maskini na wanyonge; na wana maning’uniko na ghadhabu za umaskini na unyonge. Mgawanyiko wa namna hiyo ni hatari sana. Utaratibu wa vyama vingi katika mazingira na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauiti kubwa sana za mapato na hali ya maisha au hata matumaini tu ya maisha mema ya baadaye haziwezi kuzaa utulivu. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga amani na utulivu wa kudumu katika nchi masikini bila kuheshimu misingi ya haki na usawa. Na ‘unyang’au’ kwa hulka yake hauheshimu misingi ya haki na usawa.”

Suluhisho
Hatima ya maisha ya vijana si suala dogo la kuacha lijimalize lenyewe. Linataka kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Suluhisho la kweli ni kurudi katika miongozo ya Mwalimu Nyerere ya kuthamini UTU na USAWA wa watu na kuheshimu HAKI zao. Tuonyeshe kwa vitendo kwamba kweli tunazijua, tunazitambua na kuguswa na shida za watu. Na kwamba kwa uhakika kabisa kabisa tunazifanyia kazi. Na matunda au matokeo ya kazi hiyo yanaonekana. Shaaban Robert aliandika, “Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.”

Vijana wanataka matendo. Wanataka ajira. Wanataka huduma bora ya afya. Wanataka elimu bora kwao na vizazi vyao. Wanataka kunufaika na utajiri wa raslimali za nchi. Wanataka rushwa idhibitiwe. Dhuluma, uonevu na unyonyaji vikomeshwe. Kazi hizi zinafanywa na serikali. Lakini serikali ina wajibu wa kuyafanyia kazi mambo haya na kuleta majibu ya kuwaridhisha vijana na wananchi. Matokeo yake imani ya vijana na wananchi kwa CCM na serikali yake itarudi.

Nayasema haya kwa upendo na moyo mweupe kabisa kama mfuasi wa siasa na mafunzo ya Mwalimu Nyerere na kada wa CCM (nje ya chama ndani ya umma) – chama kilichoijengea Tanzania heshima katika Afrika na kote duniani. Chama kilichosimamia na kutetea haki za wanyonge ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Wakati umefika sasa wa kuirejesha hadhi ya CCM. Kinyume chake basi kauli aliyoitoa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Bila CCM Madhubuti Nchi Itayumba” itatimia siku si nyingi. Pia nitumie fursa kuwasihi vijana na wananchi kwa ujumla kuepuka matumizi ya nguvu, jazba na hasira pale wanapoandamana kwani hasira haimalizi hasira. Amani ikishapotea ni vigumu sana kuirejesha.

Hitimisho
Nimalizie kwa kusema kwamba kuiuwa nafsi isiyo na hatia ni dhambi kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi. Katika Quran Mwenyezi Mungu anasema katika SURAT AL MAIDA (Sura ya 5: Aya 32) kwamba:

“Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi (ufisadi) katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.”

Pia katika Biblia Mwenyezi Mungu katika Amri ya sita anasema “USIUWE”. Iweje leo tunaanza kuuwana? Tutaiua Tanzania.

Namuomba Mungu azidi kuibariki Tanzania. Adumishe Uhuru na Umoja kati ya wanawake, wanaume na watoto wa Tanzania kwani Uhuru na Umoja wetu ndizo ngao zetu za kuilinda na kuikinga amani yetu isitoweke.

Friday, March 23, 2012

Amani Millanga azungumzia maandamano ya Songea (sehemu ya pili kati ya sehemu tatu)

Vijana na Maandamano, Polisi na Mauwaji: Tunaelekea Wapi? (Sehemu ya pili kati ya sehemu tatu)

Na Amani Millanga

Vijana hawa wanazijua haki zao na mahitaji yao ya msingi ya kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao, ya chakula, malazi na mavazi. Kama ilivyo kwa binadamu yeyote awaye, vijana hawa hawataki kuishi katika maisha duni ya kimaskini. Wanataka ustawi na maisha bora kwao na vizazi vyao.

Pia tufahamu kwamba vijana hawa, kwa jitihada zao binafsi, ni wajuzi katika fani mbalimbali kuanzia ufundi mekanika hadi ujenzi wa nyumba. Wana maarifa ya kuendesha biashara tena kwa faida. Wanajua fika wafanye nini ili wastawi. Ni wafanyakazi hodari ndio maana wanaweza kujilisha na si wezi. Lakini ni bahati mbaya sana katika safari yao ya maisha, njia yao imejaa vikwazo vya kila namna - dhuluma na uonevu; rushwa na ufisadi. Kutokana na hali hii vijana hawa wamekata tamaa. Wengi wao hawana tena tumaini la maisha bora. Ndoto zao zimekufa.

Sasa wanazivuta hisia na wameanza kuandamana wakiungwa mkono na wazee, wafanyakazi maofisini na jamii inayowazunguka wanawake kwa wanaume. Nilifuatilia maandamano ya Mwanza na taarifa nilizozipata zinasema kwamba wanawake katika maeneo ya jiji hilo walikuwa na ndoo za maji tayari kuwapatia vijana wanawe nyuso zao pindi mabomu ya machozi yakipigwa.

Mapambano ya Mbeya nasikia yalikuwa ni makali kweli. Katika maandamano ya vijana kudai haki zao tumeiona ‘NGUVU YA VIJANA’ ikitembea. NGUVU hii ya vijana ikiachwa bila kupewa majibu na suluhisho la matatizo yao ITAUMA NA TAIFA LITAUMIA. Tumeiona mifano kila pembe duniani na hivi karibuni katika nchi za Kiarabu. Tusifike huko.

Kuwauwa Waandamanaji ni Kuitia Amani Kitanzi
Kuwauwa waandamanaji ni sawa na kuiwekea kitanzi amani. Hali hii inaweza kusababisha maandamano yenye ghasia kuibuka nchi nzima. Nayo serikali ikajikuta inatumia mabavu zaidi kuyazima maandamano haya. Katika kuyazima maandamano ipo nafsi kubwa sana ya watu wengi kupoteza maisha. Watu wakipoteza maisha chuki itaongezeka na damu nyingi zaidi itazidi kumwagika kutokana na mapambano kati ya raia na vyombo vya dola.

Huo ndio wakati ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wasioitakia mema Tanzania. Hapo litatolewa tamko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu umwagaji damu huo na ukiukwaji wa haki za binadamu. Serikali itaingia katika mgogoro mkubwa ndani na nje katika jumuiya ya kimataifa. Matamko yatatolewa na wananchi ndani ya nchi na pia mataifa makubwa ya nje kwamba serikali ijiuzulu na Chama cha Mapinduzi (CCM) kama chama tawala kiachie ngazi.

Hatujui nini itakuwa ni hatima ya hali hii. Lakini ukweli ni kwamba amani haitakuwepo tena. Watu wengi wasio na hatia watauwawa na wengine watakuwa wakimbizi. Uchumi na ustawi utavurugika. Kwa hiyo basi Polisi ijitahidi sana kuepuka kuuwa raia wasio na hatia. Itumike busara zaidi na nguvu za kadri na kadri za “piga lakini chunga usiuwe” na si risasi za moto. Tukumbuke kuwa Tanzania ni katika nchi chache sana Afrika ambayo haijaingia katika machafuko. Na yapo mataifa yanataka siku moja Tanzania itikiswe ili waone nini kitatokea. Mungu atuepushe balaa hili.

Wednesday, March 21, 2012

Lugha yetu Kiswahili

Hii ni sehemu ya hotuba niliyotoa kwenye mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto, Mwanza, tarehe 18 Februrai 2012.
***********************************
Napenda kugusia pia matumizi sahihi ya lugha kwa sababu kama tukirejea kwenye ile nukuu ya Mwalimu Nyerere kuwa shabaha ya elimu ni:

 “...kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine maarifa na mila za taifa, na kuwaandaa vijana wawe tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza taifa.”

basi utakuta kuwa lugha ni kipengele muhimu sana cha mila za Taifa. Lakini kinachotokea kwenye lugha siku hizi kinatisha. Mifano ni mingi lakini nitataja mfano toka kwenye sanaa.

Kuna msanii mmoja wa siku hizi anaimba wimbo mmoja na kutumia neno “hakunaga”. Sasa sitaki kuanzisha ubishi kati yangu na nyinyi kuhusu kama huyu ni msanii mzuri au siyo kwa sababu tunaweza tusifikie muafaka. Lakini kuna mtu nimesikia akisema kuwa katika masuala ya sanaa siyo muhimu kuzungumza lugha sahihi kwa sababu ukilazimisha hivyo unaua kipaji cha ubunifu, au utunzi.

Inawezekana haya ninayosema yanapingana na mliyofundishwa na walimu zenu, lakini kwa maoni yangu ni afadhali tuache kusikia nyimbo kama “hakunaga” lakini tuzungumze lugha ambayo ni sahihi. Huyu msanii anasikilizwa na watoto ambao baada ya miaka ishirini wataamini kuwa “hakunaga” ni neno sahihi la lugha ya Kiswahili.

Hapa sizungumzii Kiswahili tu, ila lugha yoyote ile ambayo wewe umejifunza au ambayo utajifunza. Hakuna lugha ambayo ni muhimu kuliko lugha nyingine. Mimi naongea Kiswahili, Kiingereza, na Kitaliani, lakini nafahamu Kizanaki kidogo sana. Kwa wazee wa Kizanaki ambao hawaongei Kiswahili hizo lugha nyingine hazinisaidii kitu chochote. Kwanza ni aibu kuwa kuna wakati mwingine nalazimika kutumia mkalimani kuongea na mzee wa Kizanaki.

Kwa hiyo ushauri wangu ni kuwa jiufunzeni lugha kwa kadiri inavyowezekana lakini jifunzeni hizo lugha vizuri.

Labda ni vyema kuanza kuzungumza Kiswahili vizuri kwanza, halafu kuendelea na lugha nyingine. Nyie ndiyo wazazi wa kesho, ndiyo viongozi wa kesho. Na mnao wajibu wa kulinda na kuhifadhi Kiswahili kama urithi wetu.

Siku hizi, kwa bahati mbaya, wale wanoongea Kiswahili kwa kuchanganya na maneno ya Kiingereza ndiyo wanaonekana wafahamu zaidi kuliko wale wanaoongea Kiswahili peke yake. Wengine wanachanganya lugha kwa kufikiria wataonekana bora zaidi ya wengine, lakini kuna wengine wanafanya hivyo kwa sababu baadhi ya maneno wamejifunza kwa Kiingereza halafu ndiyo wanatafuta maana yake katika Kiswahili.

Ninawaomba nyinyi mjifunze lugha vizuri kwa sababu nyinyi ndiyo mtakuwa mnaotazamwa na watoto wenu kama walimu wao. Msipojifunza vizuri lugha yenu mtachangia kupoteza kabisa lugha yetu au kuibadilisha.

Naomba niwape mfano mmoja. Zamani wakati Watanzania tukisafiri kwenda Kenya tulikuwa tunaagiza “nyama ya kuchoma” ; Wakenya walivyokuja Tanzania waliagiza “nyama choma”. Sasa naogopa kuanza mjadala na Sr. Judy kuhusu usemi upi ni sahihi lakini ukweli ni kuwa naamini sasa hivi ni Watanzania wachache sana wanaotumia msemo “nyama ya kuchoma”. Karibu kila mtu anasema ”nyama choma”, na hii naamini imechochewa na matumizi na hasa matangazo kwenye vyombo vya habari.

Maana yake ni kuwa jambo linalorudiwa mara kwa mara linaweza kubadilisha matumizi kwenye lugha.

Na huu ndiyo aina ya mfano wa mabadiliko ya matumizi ambayo tunaweza kuona baada ya miaka kadhaa kwa watoto wanaoendelea  kusikiliza “hakunaga”.

Friday, March 16, 2012

Amani Millanga azungumzia maandamano ya Songea (sehemu ya kwanza kati ya sehemu tatu)

Vijana na Maandamano, Polisi na Mauwaji: Tunaelekea Wapi? (Sehemu ya kwanza kati ya sehemu tatu)

Na Amani Millanga

Naomba nitwae fursa hii kuwapa pole wale waliofiwa na ndugu zao waliouwawa na Polisi huko Songea. Poleni sana.

Tunaelekea wapi?
Amani ya Tanzania sasa inatikiswa na hali si shwari nchini. Hali hii inatia hofu na mashaka makubwa kwa Mtanzania mzalendo kwani matukio ya mauwaji yanayotokana na wananchi kuandamana na kuuwawa na polisi yanazidi kuongezeka. Polisi wamewaua raia wasiokuwa na hatia katika sehemu mbalimbali nchini zikiwemo Arusha, Mbeya, na sasa Songea.

Mauwaji haya ni kinyume na maadili na wajibu wa Polisi kwani kazi zao siku zote ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Iweje leo Polisi wanawaua raia na kuharibu mali zao? Chuki inayopandikizwa na ukiukwaji huu wa haki za binadamu ni kubwa dhidi ya Serikali na pia kwa Chama cha Mapinduzi. Chuki hii ni kubwa sana miongoni mwa vijana na hata watu wazima, na jambo la hatari zaidi ni kwamba inasambaa kwa kasi zaidi kile pembe ya nchi - mijini na vijijini. Katika makala haya nitawaongelea vijana kwani hawa ndio wamekuwa wakipambana na Polisi.

Wasifu wa Vijana
Vijana ninaowaongelea hapa wana umri kati ya miaka 16 na 40 (ingawa ujana unaanzia miaka 18) na ndiyo walio wengi katika nchi yetu. Pili, ndiyo nguvu kazi ya taifa. Tatu, wengi wao hawana hata elimu ya msingi, na wale waliobahatika kupata elimu ya sekondari wengi wao wamesomea katika sekondari za kata ambazo zimewakata. Nne, wengi wao hawana ajira rasmi yenye pensheni na mafao mengine. Tano, wamekulia katika mazingira ya ulimwengu wa utandawazi (Profesa Shivji anauita UTANDAWIZI) na Tanzania inayokumbatia sana siasa za uliberali mamboleo zilizojaa unyonyaji, dhuluma na uonevu. Sita, ni wahanga wa soko huria ambalo limewaacha wanalia. Saba, wengi wao hawaijui kwa dhati historia ya nchi yetu na siasa yake ya kuthamini UTU na HAKI ilivyokuwa. Nane, wengi wao si waoga pale wanapokuwa wanadai haki zao. Tisa, wengi wao wamekulia katika familia zenye hali ngumu ya maisha inayozungukwa na umaskini uliokithiri na magonjwa katika mitaa ya miji yetu na vijiji vyetu. Kumi, wengi wao wana afya zilizodhoofika kutokana na kutokupata lishe ya kutosha na matibabu ya uhakika lakini wanafanya kazi ngumu sana tena kwa muda mrefu na kulipwa ujira mdogo.

Mtu anaweza kuwadharau vijana hawa kwamba kwa kuwa wengi wao si wasomi na wana dhiki, basi ni rahisi kuwadanganya au kuwatisha wakanyamaza kwa dhana kwamba: hawazijui haki zao za msingi; hawajui mfumo wa uchumi wa dunia unavyofanya kazi na unavyowaathiri; hawajui athari za kupanda kwa bei ya mafuta; hawajui athari za mfumuko wa bei; na hawajui maana halisi ya demokrasia kwani zipo tuhuma kwamba wengi wao hawapigi kura au wanauza shahada zao. Na kwamba wanachojua ni kupata mlo wao na siku inapita. Lakini si hivyo hata kidogo.

Itaendelea

Sunday, March 11, 2012

Tatizo la matandao Butiama linaelekea ukingoni

Watumiaji wa mtandao wa Internet Butiama si wengi lakini wachache tuliopo hupata shida kubwa sana kupata mawasiliano ya uhakika.
Kasi ya mtandao kwa kutumia huduma za mtandao za kampuni za simu za kiganjani ni ghali na aghalabu kasi ni ndogo sana. Kampuni nyingine hazitaki hata kuleta hiyo huduma. Nimekuwa nawabembeleza Zantel kwa zaidi ya miaka mitatu kuanzisha hiyo huduma Butiama lakini hawajaamua kuianzisha mpaka sasa.

Sasa nimepata taarifa kuwa mbunge wa Musoma Vijijini, Mhe. Nimrod Mkono, amewasilisha maombi serikalini ili mkongo wa Taifa wa mtandao uletwe pia Butiama. Katika maelezo yake Mhe. Mkono ameeleza kuwa Butiama sasa ni wilaya rasmi ya Serikali ambapo kuna shule kadhaa na kwa sababu hiyo anaona umuhimu wa kupata huduma hii muhimu.

Sent from Samsung Mobile

Friday, March 9, 2012

"Asilimia 98 ya Watanzania hawaheshimu sheria"

Kuna wakati mmoja, nadhani imepita miaka mitatu sasa, nilisikia mahojiano kwenye kipindi cha redio ambapo kamanda mmoja wa polisi wa mkoa alisema kuwa asilimia 98 ya Watanzania hawaheshimu sheria. Sikumbuki alikuwa ni nani na alikuwa wa mkoa upi.

Siamini kama alifanya utafiti wowote kabla ya kutamka hivyo, lakini kwa kuwa ni kamanda wa polisi tunaweza kuamini kuwa uzoefu wake unampa nafasi ya kutamka jambo ambalo linaweza kuwa sahihi kwa kiasi kikubwa.

Kwa hesabu za wakati ule ilikuwa ni kasi cha Watanzania laki saba tu ndiyo walibaki kuheshimu sheria za nchi yetu.

Ingefaa pia kuamini kuwa viongozi wetu, wale ambao wanapaswa kuongoza wananchi kuheshimu na kutii sheria, nao pia ni miongoni mwa hao laki saba. Kama si hivyo, hatufiki huko tuendako.

Tuesday, March 6, 2012

Selemani Galile kupambana na Thomas Mashali kuwania ubingwa wa TPBO Aprili 9

Mkanda wa ubingwa wa ngumi za kulipwa wa TPBO (Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania) katika uzito wa "middleweight" unatarajia kuwaniwa April 9 mwaka huu Dar es Salaam. Bado haijafahamika sehemu ambapo pambano hilo litafanyika.
Mkanda huo ambao upo wazi utawaniwa na bondia Thomas Mashali na Selemani Galile.

Galile amesema amejiandaa vyema kwa ajili ya kunyakua mkanda huo:
"Naendelea kufanya mazoezi yangu kwa ajili ya kuwania mkanda huu ambao ninaamini utaweza kunitambulisha ubora wangu katika tasnia hii ya masumbwi,"alisema Galile.

Alisema mpinzani wake Mashali hana hofu naye kwa kuwa mchezo huo huamua nani mkali atakayetwaa ubingwa wakati wakiwa ulingoni na si nje ya hapo na kwa sasa anasema amepata staili mpya za mabondia wa dunia.

Picha na taarifa kwa hisani ya superboxingcoach.

Saturday, March 3, 2012

Matumla amsambaratisha Maneno Oswald

Katika mpambano wa marudiano kati ya Rashidi Matumla na Maneno Oswald uliyofanyika tarehe 25 Februari 2012 katika ukumbi wa PTA Dar es Salaam, Matumla alimshinda Oswald kwa pointi.
Rashidi Matunla (kushoto) akimaliza ubishi kati yake na Maneno Oswald (kulia) katika pambano lao la tarehe 25 Februari 2012. 
Katika pambano hilo la raundi 10 katika uzito wa "Super Middleweight" matokeo ya waamuzi yalikuwa kama ifuatavyo: Anthony Ruta 97 - 93; Pemba Ndava 95 - 95; na Ramadhani Basta 97 - 95.

Kwa matokeo haya Matumla ameshinda mapambano matatu kati yao na kutoka sare pambano moja, wakati Maneno ameshinda pambano moja na kutoka sare moja.

Thursday, March 1, 2012

Nyoka wa kumwaga

Wale ambao wamepata fursa ya kusoma makala zangu za Kiingereza kwenye gazeti la Sunday News watagundua kuwa, mara kwa mara, naandika kuhusu nyoka. Nakutana na nyoka mara kwa mara kiasi ambapo inakuwa vigumu kukwepa hii mada. Wapo kila mahali. Natazama nje ya dirisha langu na naona nyoka anatambaa ukutani (picha ya hapa chini). Kuna mmoja aliingia chumbani kwangu usiku, na nikamkuta sehemu ambapo ninakanyaga niamkapo kitandani.
Kuna safari moja, wakati natoka chumbani kwangu, ikiwa kuna giza kidogo, nilimruka nyoka bila kutambua na nikafunga mlango wa chumba na kumbana nyoka mlangoni. Nilivyorudi chumbani nikamkuta yuko hai, sehemu ya kiwiliwili chake kikiwa nje ya chumba na sehemu ikiwa chumbani kwangu, ingawa alikuwa bado hai. Nilimchota na mti mrefu nikamtoa nje ya nyumba na kumuachia. Kuna mtu aliniuliza: "Kwa nini hukumuua?" Jibu nililipata kwenye asili ya kabila langu: Wazanaki.

Kwanza, angeweza kuwa Muhunda, nilimuarifu, mzimu wa Kizanaki (sisi tunaita musambwa) unaolinda kabila la Wazanaki wa Butiama (kila eneo kati ya maeneo nane ya Uzanaki lina musambwa wake). Tunaamini kuwa Muhunda anaweza kujibadilisha na kuwa nyoka, au chui, au nyani dume. Kwa imani za Wazanaki Muhunda siyo Muumba; Wazanaki wana imani kuwa yupo Muumba na mbingu.

Mimi najiita Mzanaki, japokuwa sina uwezo wa kuongea Kizanaki. Aidha, kwa mujibu wa mila zetu, mimi ni mmoja wa walinzi au wasimamizi wa msitu wa mitambiko ambao nao unaitwa Muhunda, sehemu ambayo Muhunda anaaminika kutembelea mara kwa mara. Kwa hali siyo siwezi kuua kiumbe ambacho napaswa kukilinda, hasa ukizingatia kuwa jukumu kubwa la Muhunda ni kulinda jamii nzima ya wakazi wa Butiama, Watyama.

Mimi naungana na wale wanaoamini kuwa kuna viumbe wachache sana ambao wananaweza kushambulia viumbe wengine bila kuwa na hisia kuwa usalama wao uko hatarini. Ni binadamu pekee ndiyo mwenye hulka ya kushambulia binadamu mwenzake, hata pale ambapo usalama wake hauko hatarini. Nyoka wengi hawashambulii binadamu isipokuwa tu pale wanapohisi kuwa usalama wao unatishiwa, kwa hiyo naamini kuwa sina sababu ya kuua kila nyoka ninayemuona.

Ni nyoka aina ya Mamba Mweusi tu ambaye inasemekana anaweza kumshambulia binadamu pasipo sababu ya msingi.