Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Wednesday, February 29, 2012

Wizi wa mitihani ni janga la Taifa

Picha hii (hapa chini) ni ya tangazo lililobandikwa kwenye chuo kimojawapo mashuhuri cha Tanzania kwenye moja ya majiji ya Tanzania.
Nimefuta majina ya walioorodheshwa ili kuhifadhi majina ya wahusika.

Tangazo linaashiria kuwa walioorodheshwa wanatuhumiwa kuibia kwenye mitihani. Mwalimu mmoja ambaye alizisikia taarifa hizi alisema kuwa anaamini kuwa hawa walionaswa ni asilimia ndogo sana ikilinganishwa na wale ambao waliibia lakini hawakunaswa, ambao baada ya muda watahitimu masomo yao.

Kwa nini wizi wa mitihani ni janga la Taifa? Mwalimu Nyerere, katika moja ya hotuba zake, alisema:
"...[shabaha ya elimu ni] kurithisha kutoka kizazi kimoja had kizazi kingine maarifa na mila za taifa, na kuwaandaa vijana wawe tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza taifa."
Kwa mtindo huu, tunarithisha majukumu ya kulitumikia na kuliendeleza taifa kwa wahitimu ambao hawana elimu inayolingana na shahada wanazotoka nazo vyuoni. Ni sawa sawa na kujenga nyumba kwenye msingi hafifu. Kuna siku moja nyumba itaporomoka na tutajikuta tunaongozwa na watu wa mataifa mengine ambapo ipo elimu ya kweli, na wako wasomi wa kweli.

Kuna mtaalamu mmoja anasema kuwa tayari tunaongozwa na watu hao.

posted from Bloggeroid

Tuesday, February 21, 2012

Salim Mkalekwa kupambana na Abdallah Mohamed (Prince Naseem)

Bingwa wa ndondi za kelipwa wa walterweight (kilo 67) wa Pugilistic Syndicate of Tanzania (PST), Abdallah "Prince Naseem" Mohamed, anatarajia kupanda ulingoni tarehe 24 Februari 2012, katika pambano la ubingwa dhidi ya bondia Salehe Mkalekwa.
Bondia Salehe Mkalekwa (kushoto), mratibu wa pambano Shabani "Mwayamwaya" Adiosi (katikati), na bondia Abdallah "Prince Naseem" Mohamed (kulia).
Mapambano ya utangulizi yatawahusisha mabondia Shaaban Zungu dhidi ya Hassan Debe (kilo 55); Safari Mbeyu dhidi ya Ibrahim Maokolo (kilo 67); Geoffrey Pacho dhidi ya Dickson Kawiani, na Kulwa Kindondi dhidi ya Khaji Hamisi. Uzito wa mabondia katika mapambano haya mawili ya mwisho haukupatikana.

Pambano hilo linaratibiwa na Shabani "Mwayamwaya" Adiosi na litafanyika kwenye ukumbi wa New Kibeta, Mbagala Kuu, Dar es Salaam.

Picha na taarifa kwa hisani ya Super D Boxing Coach.

Thursday, February 16, 2012

Wengine wanakufa kwa njaa, wengine hawataki kula

Zaidi ya mwaka mmoja uliyopita niliona takwimu kwenye wavuti moja inayatoa takwimu za dakika kwa dakika kwa mwaka mzima. Takwimu zilainisha kuwa kwa wakati ule watu 22,000 tayari walikuwa wamekufa kwa njaa duniani na wakati huo huo kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 22.6 zilikuwa zimeshatumika duniani kote na watu wanaotafuta huduma na dawa za kupunguza uzito.

Hizo pesa zingegawanywa kwa idadi ya watu waliyokufa, kila mmoja angepata zaidi ya Dola milioni moja na kuepusha mtu yoyote kufa kwa njaa.

Tatizo la uzito wa kupindukia ni kubwa kwenye nchi tajiri, lakini haliwezi kuzidi tatizo la kufa kwa njaa linalokabili wakazi wa nchi maskini duniani.

Friday, February 3, 2012

Francis Cheka amshinda Karama Nyilawila kwa pointi

Katika pambano lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro tarehe 28 Januari 2012 bondia Francis Cheka alimshinda Karama Nyilawila kwa pointi katika pambano la uzito wa "Super Middleweight" lisilokuwa la ubingwa.

Katika pambano hilo kali mabondia wote wawili walitupiana makonde ya kujibizana lakini kwa mujibu wa majaji wa mchezo huo, Cheka aliibuka mshindi. Majaji walitoa pointi zifuatazo: John Chagu 100 - 96, Mark Hatia 96 - 97, na Boniface Wambura 99 - 97. Refa wa mchezo alikuwa Nemes Kavishe.
Karama Nyilawila (kushoto) akiinama kukwepa kombora la Francis Cheka katika pambano la hivi karibuni liliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. (Picha kwa hisani ya superboxingcoach)
Pambano hilo lilisimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), na promota wa pambano alikuwa Philemon Kyando.