Hii ni moja ya makala zangu zinazochapishwa kwenye safu yangu iitwayo Ujumbe Kutoka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri. Ilichapishwa tarehe 14 Aprili 2015.
*************************************
Nilipata fursa ya
kushuhudia kwenye runinga majadiliano ya muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao
2015. Kwa mtazamo wangu sheria ikianza kutumika kutakuwa na ongezeko kubwa la watumiaji
wa mawasiliano, hasa ya simu, kubebeshwa makosa, kulipa faini, na kutumikia
vifungo gerezani.
Kusudio la itakayokuwa
Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015, kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa bungeni
na serikali, ni: “...kutunga sheria ambayo itaainisha makosa yanayohusiana na
matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kuweka
utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki.”
Ni kweli kuwa vipo vipengele
ndani ya muswada vinavyoainisha makosa ambayo yanastahili adhabu. Mfano, wahalifu
wengi leo wanatumia mtandao kuiba pesa kutoka kwenye akaunti za benki, pamoja
na kutumia majina ya watu wasiyokuwa na hatia kufanya uhalifu huo ili kuficha
utambulisho halisi wa wahalifu hao. Aidha, kutoa taarifa zinazolinda ulinzi na
usalama wa taifa bila shaka kunastahili adhabu kali.
Hakuna ubishi pia kuwa kushirikisha
watoto kwenye vitendo vya ngono na kutumia picha au taarifa hizo kwenye mitandao
ya kompyuta na simu ni makosa ambayo hayapaswi kuvumiliwa. Wanaoshiriki vitendo
vya aina hii wanastahili kuhamishiwa gerezani na kubaki huko maisha yao yote.
Aidha, nimewahi kuandika kwenye
safu hii kuwa wanaotumia mtandao wa habari na mawasiliano kusambaza uongo
hawatumii vyema wajibu wao kama wanajamii. Hawa, kwa maoni yangu, wanastahili
adhabu iliyoainishwa kwenye kifungu cha 16 cha muswada wa sheria hii.
Lakini pamoja na yale ambayo
wengi tutakubaliana ni makosa dhahiri, kuna makosa yaliyoainishwa kwenye
muswada ambavyo yatawakumba wasiokusudiwa. Kifungu 7(2)(b), ambacho
kinabainisha kuwa anayepokea data kompyuta ambayo haijaidhinishwa atakuwa
ametenda kosa mwa mujibu wa sheria hii, kinampa mwanya mtu yoyote mwenye nia
mbaya uwezo wa kutuma data hizo kwa mtu mwingine bila anayepokea taarifa hizo
kuziomba, na hizo taarifa zilizopokelewa zitakuwa ushahidi wa kumtia hatiani
anayekutwa nazo. Pamoja na kuwa muswada unatambua kuwa ni kosa kwa mtu kutuma
taarifa kwa mwingine bila ya ridhaa ya anayezipokea, teknolojia iliyopo
inaruhusu kutotambuliwa kwa aliyezituma. Sheria hii inaacha mwanya kwa watu
kukutwa na hatia na kulipa faini au kutumikia vifungo kutokana na vitendo vya
makusudi vya watu wengine.
Sheria hii itasababisha umiliki
wa simu kuwa sawa na ule wa silaha. Inakuwaje pale mtu
anapoiba simu yangu na kutuma ujumbe ambao maudhui yake, kwa mujibu wa sheria
hii, ni kosa la jinai? Mtu anaweza kujibu kuwa ni wajibu wangu kuhakikisha
naichunga simu yangu, kama ambavyo mmiliki wa silaha anavyowajibika kuchunga
silaha yake isitumike kwenye matukio ya uhalifu. Tayari wanadamu hatuaminiani
kwa mengi, na hali hii itatuongezea sababu nyingine ya kutoaminiana.
Katika muswada huu
ipo dhamira ya kuzuwia uhalifu, lakini yawezekana pia kuna kusudio la kudhibiti
harakati za kijamii na za kisiasa. Kipengele 20(1) kinachoelekeza kwamba ni
hatia kutuma ujumbe bila ya ridhaa ya anayeupokea una sura mbili. Kwanza upo
ujumbe tunaopokea kila siku wa kampuni za simu ambazo zinaleta usumbufu mkubwa
kwa baadhi ya wateja kutokana na kuwa siyo kila anayezipokea anazihitaji.
Naafiki kuzuwia taarifa za aina hii. Mtumiaji wa simu anapaswa kupewa uwezo wa
kuchaguwa iwapo anataka kupokea taarifa za kibiashara kupitia kwenye kampuni za
simu.
Lakini kuna sura ya
pili inayoibuliwa. Zipo taarifa za kijamii na kisiasa ambazo pia tunapokea. Siku
kadhaa zilizopita nimepokea ujumbe wa mgombea mtarajiwa wa jimbo mojawapo la
ubunge ambaye anajiandaa kugombea ubunge, akiomba kuungwa mkono kwenye harakati
zake. Sheria ikipitishwa huyu naye anapaswa kwenda na maji, kwa kunitumia
ujumbe bila ridhaa yangu. Hapa naona kuna kasoro kidogo.
Ni kweli kuwa naye ni
msumbufu kwa watumiaji wa mtandao wa simu, lakini kuna umuhimu wa kulinda haki
ya raia kupokea taarifa zenye madhumuni ya kupanua ufahamu wao na uwezo wao wa
kushiriki kwenye michakato inayojenga demokrasia. Kwa mtazamo wangu, hizi
taarifa ni muhimu kuliko taarifa za kila siku ambazo tunapokea kutoka kwenye
kampuni za simu.
Kampeni za uchaguzi zikipamba
moto huyu mgombea angeweza kutumia simu yake kutuma taarifa kuwaelimisha wapiga
kura wake kuhusu masuala muhimu ya harakati zake lakini sheria inatishia
kudhibiti fursa hiyo, na itawanyima wapiga kura wake fursa ya kupata taarifa
hizo kwa urahisi. Baya zaidi, sheria inawapa fursa wapinzani wake kulalamika
kupokea bila ridhaa yao ujumbe wake na hivyo kuhatarisha yeye kukutwa hatiani. Ni
kipengele kinachodhibiti uhuru wa kupata habari.
Mpaka leo hii ninayo
nafasi ya kupokea ujumbe wa harakati mbalimbali za kijamii na kisiasa kutoka
kila pembe ya Tanzania, lakini ikishapitishwa sheria hii nitategema taarifa za vyombo
vya habari pekee. Siamini kama demokrasia inalindwa kwa kutegemea taarifa za
waandishi wa habari tu. Wakati mwingine tatizo la baadhi ya vyombo vya habari
ni kuelemea na kuwa na misimamo ambayo inaunga mkono upande mmoja dhidi ya
mwingine. Siyo vibaya kuwa na misimamo ya aina hiyo, lakini ni muhimu pia
kuwepo fursa kwa wapokea taarifa kuunganishwa moja kwa moja na watoa taarifa
bila kuwekewa chujio wala chumvi. Anayeamini kuathirika na taarifa za uongo kwa
njia hii bado anabaki na fursa ya kutumia sheria kupata haki dhidi ya mtoa
taarifa.
Hii itakuwa sheria
inayodhibiti maovu kadhaa katika matumizi ya kompyuta na teknolojia ya habari
na mawasiliano, lakini ni sheria ambayo pia itatishia uhuru wa kupokea habari
na kubadilishana mawazo.
Taarifa nyingine kama hii: