Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, March 22, 2013

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya tatu kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya tatu kati ya sehemu nne)


Tasnia ya muziki wa Tanzania katika tafiti mojawapo umeitwa ‘the radio-driven contemporary music industry’. Kwa maneno rahisi, tasnia ambayo imekuwa inaendeshwa na redio. Redio zimekuwa na uwezo wa kumpandisha na kumshusha mwanamuziki, kumtafutia soko, kumzibia soko na kadhalika. Hali hii ikisindikizwa na rushwa ambayo imetapakaa katika jamii yetu, unapata picha kuwa kungeweza kukawa na sura bora au tofauti ya muziki hali isingekuwa ilivyo.

Kuna ripoti za watu kutoa hongo nyimbo za wenzao zisipigwe, hongo ili nyimbo zipigwe, visasi vya kuzuia nyimbo zisipigwe na kadhalika. Na katika jamii ambayo imekuwa na kawaida ya kutegemea vyombo vya habari kujua muziki gani mpya na mzuri, uwanja huu si uwanja ulio tambarare hata kidogo. Bahati mbaya inaonekana wenye vyombo hivi wako mbali na ukweli unaoendelea katika vyombo vyao au kwa kutokujua au kupuuza.

Janga hili limevikumba hata vyombo ambavyo vinaendeshwa na taasisi za dini. Wanamuziki wa muziki wa injili nao pia wanalia kudaiwa rushwa na watangazaji wa radio za injili!.  Nakumbuka siku niliyopata nafasi kuongea na kiongozi mmoja wa dini ambaye kanisa lake linaendesha kituo cha redio, nilipata mshangao baada ya mkuu huyo, kuanza kutetea watangazaji wake badala ya kuamua kufanya uchunguzi wa tuhuma.

Umefika muda wa redio kuanza kujigawa kimuziki. Ni kichekesho mji kuwa na vituo vya redio 30 halafu vyote vinapiga aina hiyohiyo ya muziki, wakati kuna aina mbalimbali za watu. Ajabu ni kuwa wenye redio wanajua kuwa katika nchi nyingine unaweza kukuta redio iliyoamua kupiga aina fulani tu ya muziki, Jazz Radio, Country music Radio, Classic Music Radio, lakini hilo limekuwa gumu kwao kutekeleza hapa. Kuwe na utofauti, wasikilizaji tuko wa aina tofauti.

Vyombo vya habari vijitahidi kupata wataalamu husika wa aina tofauti za muziki, muziki unaviingizia vyombo hivyo mabilioni ya fedha, vyombo vya habari viupe heshima yake. Bila muziki hakuna redio.

Magazeti yamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza aina mbalimbali za wasanii na sanaa. Pamoja na hongera kwa kazi nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ipo tupu, hakuna wataalamu wa uandishi wa habari za muziki. Hivyo habari nyingi za muziki zinaandikwa na waandishi kama wapenzi wa muziki na si wataalam wa uandishi wa muziki, jambo ambalo liko tofauti na uandishi wa michezo, kwa mfano soka. Unaweza ukasoma habari ya soka ambapo mwandish atakueleza nafasi za wachezaji, kama ni faulo, ni nini kilisababisha, na kama ni goli lilikuwa ni la kichwa au kona au penalty. Hili haliko katika muziki. Utaambiwa tu bendi ilipagawisha, au msanii fulani ateka nyoyo za wapenzi, na maelezo ya juu juu kama yale.

Kunahitajika kuanzishwa mafunzo ya elimu ya uandishi wa kazi za sanaa. Hili litapunguza hata vurugu kama zilizotawala mwaka huu za wapiga picha kufikia hata kulala chini ili tu wapate picha ya nguo za ndani za msanii na hayo ndio kuwa maelezo makuu ya onyesho zima la muziki.

(itaendelea)

Taarifa zinazohusiana na hii:

Thursday, March 21, 2013

Mada yangu ya leo: Viongozi wakae maofisini na kupunguza uzinduzi

Kwa maoni yangu, viongozi wetu hawana muda wa kutosha kukaa kwenye ofisi zao na kufanya kazi ambayo walipa kodi wanatarajia zisimamiwe na viongozi wao. Sababu kubwa inayosababisha tatizo hili ni viongozi wetu kukubali mialiko ya uzinduzi wa kila jambo ambalo Watanzania wanaweza kubuni.

Na hapa sizungumzii viongozi wakuu tu wa nchi, nazungumzia viongozi wa ngazi zote kwa sababu nchini Tanzania imekuwa desturi sasa kwa kila jambo kuwa na uzinduzi rasmi, kuanzia kanda mpya ya kwaya mpaka kinywaji kipya.

Lakini ni dhahiri kuwa mifano inayopatikana kwa urahisi inawahusu viongozi wakuu wa nchi kwa kuwa habari zao zinaandikwa zaidi kuliko zile za viongozi wa ngazi za chini.

Angalia mifano ifuatayo ya Rais, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu, na utapata picha ya ukubwa wa tatizo hili:

Rais Jakaya Kikwete
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Bilal
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Ni dhahiri kuwa kwa kila kiongozi kuna sehemu au shughuli fulani ambayo anapaswa kuhudhuria kwa sababu ya umuhimu wa shughuli yenyewe na nafasi yake katika uongozi, lakini ni dhahiri kuwa kuna shughuli nyingine nyingi ambazo hazina umuhimu kwa viongozi wetu kuhudhuria.

Kuna umuhimu kwa sheria kutumika kutamka shughuli rasmi ambazo viongozi wa ngazi ya Taifa wanapaswa kuhudhuria ili kupunguza mlolongo wa shughuli ambazo tunaoona zinazinduliwa na viongozi hawa. Hili likifanyika, litapunguza gharama kwa serikali na pia kuwapa muda mkubwa zaidi viongozi wetu kubaki kwenye sehemu zao za kazi na kusimamia vyema shughuli za serikali.

Kama nilivyosema awali, hapa nimetoa mifano ya viongozi wa kitaifa kwa sababu ndiyo mifano iliyo rahisi kuitoa. Lakini hili ni tatizo lililopo katika ngazi zote, kuanzia mawaziri mpaka watendaji wa vijiji.

Watanzania nao wabadilishe fikra kuwa haiwezekani kuchapa kazi bila kufanya uzinduzi.

Sunday, March 17, 2013

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya pili kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya pili kati ya sehemu nne)

Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio ambao muziki huu unastahili kurekodiwa. Studio nyingi zimejengwa kwa ajili ya muziki wa aina ya Bongoflava tu. Zile studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi gharama yake huwa ni kubwa sana.

Kundi la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa kiasili, kuwa na muziki huo ukifuata taratibu nzuri ya kurekodiwa unauza vizuri sana. Bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha muziki na ngoma zao, vinaiga uchezaji wa Makirikiri.

Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya; sijausahau. Kwa kweli muziki huu umebaki  hasa kwenye muziki wa injili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.

Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini  kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii.

Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndiyo alama ya muziki wa Tanzania. Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, Afrika Kusini; pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao.

Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndiyo unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndiyo wamekuwa waalimu wetu wakuu.

Ushauri kwa ma-producer wa Bongoflava: kuangalia pia muziki wetu wa asili humu ndani ya nchi ili tuje tumalize 2013 na kitu chetu ambacho Wanaigeria, Wakongo nao pia waige toka kwetu. Inawezekana sana maana wimbo wa Weekend wa Afro70 uliwahi kuweko katika  kumi bora 1972, Nigeria.

Muziki wa injili pamoja na kuwa ndiyo unaotegemewa kutufundisha maadili, ulikuwa na kasoro moja kubwa nayo ni kukosa maadili kwa ku-copy na ku-paste. Nyimbo nyingi zilizokuwa maarufu na kuteka hisia za maelfu ya watu zilikuwa ni kuiga moja kwa moja kutoka Afrika ya kusini. Najiuliza je ndiyo kilichopunguza moto wa muziki huu 2012? Kulikuwa hakuna za kukopi? Wanamuziki wa injili kama ilivyo kwa ushauri kuhusu Bongoflava, ni muda wa kurudi nyuma na kutumia rasilimali ya utamaduni iliyoko kuleta mabadiliko na kukuza soko la muziki huo.

(itaendelea)

Taarifa zinazohusiana na hii:

Friday, March 15, 2013

Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012 (sehemu ya kwanza kati ya nne)

Katika makala hii nitakayoitoa katika sehemu nne, mwanamuziki mashuhuri John Kitime, anafanya tathmini ya hali ya muziki Tanzania mwaka 2012.
******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012

makala ya John Kitime

(Sehemu ya kwanza kati ya sehemu nne)

Mwaka 2012 ndiyo huo umetokomea Ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki wa bendi, matarumbeta, muziki wa injili, na muziki wa kiasili.

Si siri kuwa muziki wa Bongoflava ndiyo uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari na sehemu nyingi za maonyesho ukifuatiliwa na muziki wa Taarabu na muziki wa injili. 

Katika muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndiyo waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia hii.  Waimbaji katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndiyo waliotajwa na kupewa sifa kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali.

Hakuna ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndiyo muziki uliopewa muda mchache sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita kufuata mipigo ya Kikongo zilipewa nafasi zaidi ya bendi ambazo zimejichagulia njia nyingine za muziki wao.

Kuna sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa Bongoflava kuchukua nafasi zaidi katika vyombo vya habari. La kwanza ni uwingi wa kazi za Bongoflava zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya aina moja au nyingine, na katika studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea kutawala anga ya vyombo vya habari, na pia ni kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita katika mfumo wa aina fulani tu za muziki.

Kwa mtazamo wangu heka heka za muziki wa injili zilipungua 2012. Yale matamasha makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa nyingi  kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Muziki wa Taarabu haujaleta mabadiliko kimuziki. Mengi yaliyofanywa katika 2012 ni marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show katika taarabu, upigaji wa gitaa na kuliachia peke yake kama ilivyokuwa kwa bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini na zile video za kucheza mbele ya viwanja vya hoteli. Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo tena ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo pia.

Bendi ziko katika wakati mgumu. Wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa muziki wa bendi haupigwi, kumekuweko na jitihada ndogo za bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na  nyimbo zilizoweza kuteka umma wa Watanzania na hivyo kusababisha muziki huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi.

(itaendelea)

Taarifa zinazohisiana na hii:
sehemu ya pili ya makala hii
sehemu ya tatu ya makala hii

Kutotumia reli kunaua uchumi (sehemu ya pili kati ya mbili)


Katika makala hii yenye sehemu mbili, Dk. Amani Millanga anasisitiza umuhimu kwa Taifa wa kuendeleza mfumo wa reli.
*****************************************
KUTOTUMIA RELI KUNAUA UCHUMI (sehemu ya pili kati ya sehemu mbili)

Hapo utaona kwamba katika reli kuna ajira nyingi sana rasmi zenye mafao ya uzeeni kwa vijana wetu. Ajira hizi zitaongeza mapato kwa serikali kwani wafanyakazi watakuwa wanalipa kodi. Reli itatoa chachu ya kukua kwa viwanda vya kufua chuma, kutengeneza vipuri, n.k. na kuifanya Tanzania iingie tena katika mapinduzi ya viwanda na hasa viwanda vizito. Hili litasaidia kukuza ubunifu, uzoefu, utafiti na teknolojia nchini katika nyanja zote za viwanda vinavyogusa reli. Juu ya hayo reli ni usafiri wa uhakika wenye uwezo wa kusafirisha abira wengi zaidi ya mabasi na kwa usalama zaidi na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za mabasi ambavyo vimewaacha watoto wakiwa yatima na wanawake wakiwa ni wajane. 

Nini kifanyike? Mosi, serikali imiliki shirika la reli. Pili, serikali iunde upya shirika la reli na liwe na muundo wa kujiendesha kwa faida kwa mujibu wa kanuni za biashara na menejimenti kwa ufanisi, uaminifu, kiushindani na kutoa huduma bora za kisasa. Tatu, serikali ijenge njia ya pili kwa reli zetu zilizopo hivi sasa ili iwe rahisi kusafirisha bidhaa na abiria kwa usalama zaidi. Ujenzi huu utanguliwe na ujenzi wa ki/viwanda cha/vya kufua chuma ili kuzalisha chuma cha pua ambacho hutumika katika ujenzi wa reli, kutoa ajira kwa vijana na kupunguza gharama za kuagiza vipuri na vifaa vingine nje ya nchi. Pesa ya kujenga njia ya pili ya reli kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma inatosha kabisa kujenga kiwanda cha kufua vyuma na kubakiza mtaji wa kukiendesha kiwanda hicho.
Nchi zilizoendelea zimewekeza kwenye mifumo ya reli na kufanikisha kupunguza gharama za usafirishaji. Picha ya Daniel Steger inatumiwa kwa utaratibu wa Creative Commons, CC:Attribution-ShareAlike.
Hakuna nchi duniani imeendelea bila kuwa na ki/viwanda vya kufua chuma. Hata historia ya mwanadamu inaonyesha mababu zetu waliweza kupiga hatua haraka za kimaendeleo pale tu walipogundua namna ya kufua chuma (nitaliongelea zaidi katika maoni yangu kuhusu viwanda vyetu).

Mkaa wa mawe na chuma huko Mchuchuma vingetusaidia sana katika hili. Nne, serikali kupitia shirika la reli inunue treni ziendazo kwa kasi. Tano, shirika la reli liweke utaratibu mpya wa kusafirisha abiria. Mfano, kwa treni iendayo kwa kasi kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam isimame katika vituo vikubwa tu navyo visiwe zaidi ya kumi (mfano: Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na vituo vingine vitano muhimu hapo katikati) na itumie masaa yasiyozidi 24 kusafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza. Pia baina ya vituo vikubwa ziwepo treni za kuhudumia vituo vidogo vidogo. Kwa mfano treni iendayo kwa kasi ikitoka Mwanza isimame Shinyanga lakini hapo katikati iwepo treni ya kuhudumia vituo vidogo vidogo kati ya Mwanza na Shinyanga. 

Tano, mfumo wa mawasiliano katika treni uboreshwe ili kuepusha ajali na hasa wakati njia moja tu inatumika kabla ya kujenga njia ya pili. Sita, serikali ijenge reli katika maeneo mengine ya nchi. Saba, shirika la reli liwe na ufanisi katika kupakia na kupakua mizigo. Idara hii ihakikishe mizigo haipotei na inafika katika muda uliopangwa.

Nane, tuna nchi sita jirani zinategemea bandari zetu. Reli ingeweza kuzihudumia nchi hizi kwa faida kubwa. Hivyo basi bandari za nchi kavu kama Isaka zingekuwa vituo kikubwa vya ajira na biashara. 

Je, tunashindwa kuyafanya haya? Naamini kwa nia safi na uzalendo tunaweza. Kinyume chake ipo siku tutakuta mwekezaji ameing’oa  reli  na kuiuza kwa vyuma chakavu.

Thursday, March 14, 2013

Kutotumia reli kunaua uchumi (sehemu ya kwanza kati ya mbili)


Katika makala hii yenye sehemu mbili, Dk. Amani Millanga anasisitiza umuhimu kwa Taifa wa kuendeleza mfumo wa reli.
*****************************************
KUTOTUMIA RELI KUNAUA UCHUMI (sehemu ya kwanza kati ya sehemu mbili)
Dk. Amani Millanga
Kwa miaka zaidi ya kumi Tanzania imezungukwa na taswira iliyokomaa ya kudhoofika kwa njia kuu za usafirishaji za reli, meli na ndege kana kwamba hazina umuhimu wowote katika ujenzi na ukuwaji wa uchumi wa taifa letu na ustawi watu wake. Vituo vyote vya treni vimeota magugu. Reli imegeuka kichaka. Sababu kubwa za kudhoofika huku ni serikali  kushinikizwa na wakubwa kujitoa katika kumiliki njia kuu za usafirashaji. Mashirika yetu ya reli, bandari na ndege yamekufa. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa. Athari zake zinatugusa sote na utaziona kwa macho kila pembe ya nchi. Mwaka 2010 niliandika kuhusu Athari za Kutokutumia Reli. Makala haya ni muhtasari yake.

Tanzania inatumia magari mengi sana ambayo yanatugharimu pesa nyingi za mafuta, vipuri na matairi. Matokeo yake ni mfumuko wa bei kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji. Kwa mfano mwaka 2010 mfuko wa sementi ulikuwa unauzwa sh.9,000 katika maduka ya rejareja jijini Dar es Salaam lakini Mwanza ilikuwa sh 18,000. Gharama za kusafirisha tani moja ya sementi ilikuwa ni sh.150,000 ili hali kwa treni ilikuwa sh.103,663. Hapo utaona zingebaki sh.46,337 mfukoni mwa wananchi kwa kila tani ya sementi, mchele, mahindi, sukari, chumvi n.k. kama tungetumia treni au sh.2,316.85 kwa kila kilo 50.

Kama nchi nzima tungesafirisha kwa kiwango cha chini kabisa tani milioni tano tu kwa treni utapata hesabu hii: sh.46,337 zidisha kwa tani 5,000,000 utapata sh 231,685,000,000 (sh bilioni 231.685) ambazo zingebaki mfukoni mwa wananchi. Hali hii inagusa kila sehemu ya Tanzania. Huko Muleba bei ya sementi ilikuwa ni sh.23,000 mpaka 25,000. Kumbe behewa la sementi lingekuwa linafika Mwanza na kuwekwa kwenye meli ya mizigo hadi Kemondo bila shaka unafuu wa maisha ungekuwa mkubwa kwa mkazi wa Muleba ambaye kipato chake kwa mwaka ni kati ya sh.100,000 na sh.150,000 kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Usafiri wa treni pia ni nafuu sana kwa abiria. Mfano nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza daraja la tatu ilikuwa ni sh.19,000 ili hali kwa nauli ya basi ilikuwa sh.50,000. Hii ina maana sh.21,000 zingebaki mfukoni kwake. Kama watu milioni moja wangetumia treni kwa mwaka 2010 ina maana sh.21,000,000,000 zingebaki mfukoni mwao.

Kampuni ya reli kwa sasa ilikuwa na wafanyakazi 3,220 mwaka 2010 baada ya kupunguzwa kutoka 6,500. Kama shirika la reli litasimamiwa vizuri na serikali litatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa malaki ya Watanzania. Miongoni mwa ajira rasmi ni pamoja na wahandisi wa ujenzi na ukarabati wa treni na reli, madereva wa treni, mafundi katika karakana, wahudumu katika treni za abiria, wakata tiketi katika vituo, watunza takwimu za usafirshaji mizigo, wapakua mizigo kwenye mabehewa na hata wafanyabiashara kama kina mama lishe na baba lishe katika vituo vya treni.

Kwa mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuna vituo 68, na kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kuna vituo 85. Fikiria reli ya kwenda Mpanda na ile reli ya Tanga, Moshi na Arusha, ile ya Mtwara na Lindi, na TAZARA kuanzia Mbeya hadi Dar es Salaam. Fikiria ajira za wasomi wetu waliosomea usimamizi wa biashara, takwimu, uhasibu n.k. ambao wangepata ajira katika kila kituo cha treni. Fikiria ajira katika viwanda vitakavyokuwa vinafua chuma kwa ajili ya kutengenezea mataluma, kupasua kokoto, karakana, sementi, rangi, ufyatuaji matofali, vioo, upasuaji mbao n.k kwa ajili ya kujenga reli mpya na vituo vipya.

(itaendelea)

sehemu ya pili ya makala hii

Saturday, March 9, 2013

Mwenyekiti wa ABETO atembelea Butiama

Moses Musana, mwenyekiti wa Always Be Tolerant Organisation (ABETO), azaki ya nchini Uganda, amefanya ziara kijijini Butiama hivi karibuni.

ABETO iliundwa mwaka 1966 ikiwa na madhumuni ya kuhimiza jamii katika bara la Afrika kutumia njia za amani kutatua migogoro, kuishi kwa amani, kudumisha uvumilivu, demokrasia, na utawala bora.
Mwenyekiti wa ABETO, Moses Musana (kushoto), akisalimiana na Mama Maria Nyerere wakati wa ziara aliyofanya kijijini Butiama hivi karibuni
Katika hafla iliyofanyika jijini Kampala tarehe 11 Agosti 2012, ABETO ilitoa tuzo ya amani kwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo ilipokelewa na Mama Maria Nyerere.

Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2012/12/mkutano-wangu-na-jaffar-idi-amin.html
http://muhunda.blogspot.com/2011/07/wageni-wa-butiama-ujumbe-wa-veta.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/09/wageni-toka-jkt-wamtembelea-mama-maria.html

Wahisani wachangia mabati 33 kwa ujenzi wa shule Kichalikani

Agnes Mambo anaarifu kuwa mabati 33 yamepokelewa hivi karibuni kuchangia ujenzi wa shule ya Msingi Kichalikani iliyopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.

Katika jitihada za kuchangia shule hiyo, mimi natarajia kukwea Mlima mwezi Juni 2013 kuchangisha pesa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo. Msafara wangu ulipangwa mwezi huu lakini nimelazimika kuahirisha mpaka mwezi Juni.
****************************************
Na Agnes Mambo,MKINGA.
MKUU wa wilaya ya Rufiji mkoani Mwapwani, Nurdini Babu, na Mkurugenzi wa idara ya Teknolojia ya Habari IT, katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) la jijini Dar es salaam, Said Masimango, wametoa msaada wa bati 33 zenye thamani ya Shilingi 760,000/- katika shule ya Msingi Kichalikani wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Jengo la Shule ya Msingi Kichalikani.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani mwenyekiti wa Tanga Village Support, Hassani Kibhondah, amesema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kusogeza huduma ya elimu karibu kutokana na wanafunzi wa eneo hilo kutembea umbali wa kilometa tatu kutoka Kichalikani hadi Shule ya Msingi Mongavyeru.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa wadau hao wameguswa na kuchangia ujenzi wa shule hiyo ambayo ilianza kujengwa tangu mwaka 2009 kwa nguvu za wananchi wenyewe ambapo hadi sasa kuna vyumba viwili vya madarasa na ofisi mbili ,hivyo ameomba wapenda maendeleo kuguswa na suala hilo ili ujenzi uweze kukamilika.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule ya msingi Kichalikani, Jambia Ally Kubo, amesema kuwa watoto wanapata adha kubwa kutokana na maji ya bahari kujaa katika kisiwa hivyo kushindwa kuvuka ambapo wameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuchangia ujenzi wa shule hiyo.

Naye Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Kichalikani, Amina Muhaji, awameshukuru wadau hao waliotoa vifaa hivyo ambapo amesema kuwa wanafunzi wanachapwa kutokana na kuchelewa kufika shule. Aliongeza kusema kuwa baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuendelea na masomo wakihofia maisha yao kwa sababu ya kupita katika jangwa na kisiwa na kushindwa kuvuka.

Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2012/06/mwanzo-wa-msafara-wa-mlima-kilimanjaro.html