Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, April 7, 2017

Bila Karume hakuna Tanzania

Bila yeye hakuna Tanzania. Ni maneno ambayo Mwalimu Nyerere aliyatamka akizungumiza juu ya masuala mbalimbali, pamoja na chimbuko la muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Nachapisha tena makala iliyochapishwa tarehe 26 Aprili 2016 kwenye safu yangu "Ujumbe toka Muhunda" ndani ya gazeti la Jamhuri. Katika makala hiyo narudia ukweli ambao unasahauliwa, ya kuwa wazo la muungano ni wazo la Sheikh Abedi Amani Karume. Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuuwawa kwake.

********************************

Muungano ni pendekezo la Sheikh Karume
Na G. Madaraka Nyerere

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo unatimiza miaka 52. Kwa binadamu miaka 52 siyo haba, na aliyoitimiza tunamuita mzee. Kudumu kwa muda mrefu kiasi hiki kunapaswa kupongezwa, ingawa si wakati wote wanaostahili pongezi wanaipata.

Tarehe ya leo, miaka 52 iliyopita, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliweka sahihi hati ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini wengi wanapoandika au kuzungumzia Muungano huweka msisitizo wa mchango wa Mwalimu Nyerere na imani yake kubwa juu ya umuhimu wa kuungana. Kwa maoni yangu, Sheikh Karume hapati sifa anayostahili kama muasisi wa Tanzania.

Kwenye mahojiano ndani ya filamu iliyoandaliwa na M-Net, Mzee Rashidi Kawawa alifafanua kuwa wazo la kuunganisha Tanganyika na Zanzibar lilitolewa na Mzee Karume, halikuwa wazo la Mwalimu Nyerere. Ni kweli kuwa Mzee Karume alitoa wazo kwa mtu ambaye tayari alikuwa anaamini juu ya umuhimu wa umoja, na bila shaka ndiyo sababu ya kukubaliwa.

Naye Mama Maria Nyerere amesimulia kuwepo Ikulu Dar es salaam siku Karume alipotoa wazo hilo. Mzee Karume alikuwa Dar kwa shughuli za kikazi, na ni katika mazungumzo na Mwalimu baada ya mazungumzo yake rasmi ya kikazi ndipo mazungumzo ya muungano yalianza. Mwalimu alianza kulalamika juu ya kasi ndogo ya mchakato wa kuunganisha nchi tatu za Afrika Mashariki ili kuunda shirikisho. Hapo hapo Karume alimwambia Mwalimu kuwa kama mchakato huo unachelewa, basi yeye yuko tayari Zanzibar iungane na Tanganyika. Na kuongeza: “Wewe utakuwa rais, mimi nitakuwa makamu wako.”

Wazo la kujenga umoja halikuwa geni kwa Mwalimu Nyerere, kwa hiyo haihitaji utafiti wa kina kubaini sababu ya kulikubali mara moja na kulivalia njuga wazo la Mzee Karume. Agenda ya kuleta umoja wa nchi za bara la Afrika ilikuwa ni mojawapo ya mikakati ya chama cha TANU wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika.
 Kwa namna fulani, Mzee Karume ni kama alikuwa anamwambia Mwalimu Nyerere kuwa hiyo safari ya umoja tuianze kwa hatua hii ndogo baina ya Tanganyika na Zanzibar, hizo hatua kubwa zitafuata.

Wataalamu wengi wa kikatiba wamekosoa taratibu zilizofuata kukamilisha wazo la Mzee Karume mpaka kufikia kuwekwa sahihi hati ya Muungano kati yake na Mwalimu Nyerere tarehe 26 Aprili 1964. Na hapa lawama kubwa inamuangukia mpokea wazo, Mwalimu Nyerere.

Pamoja na kwamba ziko hoja nzuri za kukosoa mchakato wenyewe, zipo pia hoja kinzani ambazo hazikubali kuwa Muungano ni batili. Malumbano haya, miaka 52 baadaye, bado yanaendelea. Lakini yasituyumbishe tukasahau kuwa ni Mzee Karume ndiyo alianzisha hoja ya muungano.

Zipo taratibu za kugeuza simulizi za wazee kuwa historia rasmi, na pengine wakati umefika sasa wa wanahistoria kufanyia utafiti kipengele hiki cha historia ambacho hakipewi uzito unaostahili.

Kuna wakati baadhi ya wasomi wetu, katika kutafuta sababu zinazowaridhisha wao juu ya historia ya Muungano, walisisitiza kuwa wazo la Muungano liliibuliwa na afisa mmoja wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA. Kwa mawazo yao sisi hatuna uwezo wa kufikiri kuwa Muungano ni muhimu kwetu, tunahitaji Wamarekani kutufundisha. Miaka hiyo ya sitini, kila tukio liliwekwa kwenye mizani ya vita kati ya itikadi za nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani, na itikadi za nchi za mashariki zikiongozwa na Urusi.

Kama siyo imani ya kuona kuwa kila jema na lenye manufaa hutoka nje tu, basi inakuwa ni jitihada pia ya kupuuza mchango wa viongozi wetu katika kujenga na kuimarisha Muungano kwa kushawishi kuwa mawazo yao yalipandikizwa na wale ambao tunaamini hawana nia njema bali wanalinda masilahi yao.

Bahati nzuri, kama vile alifahamu mapema kuwa haya maneno yatasemwa Mwalimu Nyerere aliwajibu mapema watu hawa. Katika chapisho la chama cha TANU la Juni 1960 lililosisitiza haja ya kuwepo kwa shirikisho la Afrika Mashariki, Mwalimu aliweka msimamo wake na wa TANU juu ya shirikisho kwa kusema (siyo tafsiri rasmi):

“Katika watu wanaounga shirikisho watapatikana watu ambao wanasukumwa na sababu tofauti….watakuwepo wafanyabiashara…kutakuwa na kila aina ya watu upande wa shirikisho na watakuwa na kila sababu. Lakini hoja ya shirikisho inajitosheleza kwa uhalali wake yenyewe. Thamani ya almasi haitegemei tabia ya wale wanaoichimba. Madini ni almasi, au siyo almasi. Iwapo shetani mwenyewe atajitokeza na kuunga mkono huu mpango wa shirikisho, ujio wake hautabadilisha mawazo yangu juu ya shirikisho au juu ya shetani mwenyewe.”

Mawazo ya Sheikh Abeid Amani Karume ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika yalitua kwa muumini mkubwa wa umoja wa watu, na hasa umoja wa nchi za Afrika, Mwalimu Nyerere. Lakini tukubali kuwa bila Mzee Karume upo uwezekano kuwa hadi sasa tungekuwa hatuna Tanzania.


Miaka 52 baadaye, kwenye mazingira ya vijana wetu kutumia muda wao mwingi kutumiana ujumbe kwenye Twitter, Facebook, na Instagram kuliko kufukua yaliyojichimbia kwenye vitabu pamoja na kutafiti yale ambayo hayapendi kusemwa, ipo hatari kuwa yale ya CIA yataendelea kuwekewa uzito zaidi kuliko yale ambayo hayakidhi malengo ya mada za wasomi.

Taarifa nyingine inayohusiana na hii:

Sunday, April 2, 2017

Tumbili wa Mwitongo

Baadhi ya wanyama wanaopatikana kwa wingi eneo la Mwitongo, kijijini Butiama, ni tumbili. Ni wanyama wanaosumbua binadamu kwa kushambulia mazao ya kilimo, au baadhi ya vyakula vinavyohifadhiwa na binadamu iwapo tahadhari hazichukuliwi kulinda vyakula hivyo.

Kwa kawaida huogopa binadamu, lakini wanayo hulka ya kuzowea binadamu iwapo hawatishiwi usalama wao. Kwenye video, chini, ni mmoja wa tumbili ambao amepunguza woga kabisa akiniona kiasi cha kuchukua karanga mkononi mwangu.


Wanyama wengine wanaopatikana kwa wingi eneo la Mwitongo ni pimbi,

Tuesday, March 21, 2017

Tanzania ni nchi nzuri sana

Tanzania ni nchi nzuri sana. Hakuna ubishi juu ya hoja hii.

Lakini inahitaji fursa ya kutoka sehemu moja na kuzunguka maeneo mbalimbali ya Tanzania ambayo yanavutia kwa mandhari na vivutio mbalimbali vya asili. Ukibaki sehemu moja tu huwezi kufahamu juu ya ukweli huu.

Kama huna hiyo fursa siyo kosa lako, lakini kama unayo fursa na uwezo basi huna budi kuzunguka na kuifahamu vyema nchi yako. Utalii wa ndani unajenga uchumi, na wale ambao tunao uwezo wa kutembelea maeneo ya Tanzania tunapaswa kuchangia kwa kadiri tunavyoweza.Moja ya sehemu ambazo zinavutia nchini Tanzania ni maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria. Video hii imechukuliwa kwenye kivuko cha Busisi kwenye njia kuu inayotumika na wasafiri kati ya Mwanza na Geita, Chato, hadi Kagera.

Sunday, March 19, 2017

Unafahamu masuala haya 5 kuhusu Mwitongo?

Unafahamu masuala haya 5 kuhusu Mwitongo?

Mwitongo ni eneo la kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania tarehe 13 Aprili 1922. Aidha, ni eneo alipozikwa tarehe 23 Novemba 1999.

Yafuatayo ni masuala matano ya Mwitongo ambayo pengine huyafahamu.

1. Ajali ya ndege
Mwaka 1978, baada ya majeshi ya Idi Amin Dada kiongozi wa kijeshi wa Uganda kuvamia eneo la mkoa wa Kagera, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianza kampeni ya kuondoa majeshi ya Idi Amin kwenye ardhi ya Tanzania.

Katika harakati za kujiandaa na vita hivyo, kikosi cha anga cha JWTZ kilihamisha baadhi ya ndege zake za kivita kutoka kituo cha Ngerengere na kuzipeleka kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza.

Kwa sababu ya kasi ya hizo ndege, marubani wawili waliorusha hizo ndege walipitiliza Mwanza na kulazimika kuzunguka kuelekea upande wa kaskazini mashariki ili warudi tena kutua Mwanza. Uamuzi huo ukasababisha waruke juu ya anga ya mji wa Musoma.

Askari wa kikosi cha mizinga kilichokuwa kinalinda eneo la Musoma, kwa kukosa taarifa juu ya ndege hizo na kudhania kuwa ni ndege za adui, walizishambulia. Moja ya ndege hizo ilianguka Musoma, na nyingine iliangukia Mwitongo, kwenye msitu wa Muhunda.

Eneo la Mwitongo ilipoanguka ndege ya pili umejengwa mnara wa kumbukumbu.
Mnara wa kumbukumbu ya ajali ya ndege kwenye msitu wa Muhunda.
2. Msitu wa Muhunda
Msitu wa Muhunda ni sehemu ya eneo la Mwitongo. Ni msitu ambao, kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, ndiyo makazi ya mzimu wao, Muhunda. Msitu una ukubwa wa ekari 5.

Ni marufuku kukata miti iliyopo ndani ya msitu huo. Inaruhusiwa kukusanya kuni za matawi yaliyoanguka chini tu. Wazee wa kimila hufanya mitambiko ndani ya msitu huo.

Inaaminika kuwa mzimu huo hujibadilisha kuwa mojawapo ya viumbe vifuatavyo: nyani mkubwa, chui, mbuzi mkubwa, au nyoka mkubwa.

3. Mamba Mweusi (Black Mamba)
Mwinuko wa Mwitongo upo ndani ya eneo lililozungukwa na vichaka misitu, na majabali makubwa.

Ni eneo ambalo lina viumbe wadogo wadogo, pamoja na nyoka wa aina mbalimbali. Mojawapo wa nyoka hawa ni mamba mweusi.
Picha ya Mamba Mweusi. Jina lake la kisayansi ni Dendroaspis polylepis. Picha inatumika kwa idhini ya Creative Commons License. Taarifa kamili zipo hapa: http://creativecommons.org/licenses/by-sa/3.0/deed.en
Huyu ni moingoni mwa nyoka wenye sumu kali kabisa duniani, na inasemekana kuwa nyoka pekee ambaye hushambulia binadamu kwa makusudi, tofauti na aina nyingine ya nyoka ambao hushambulia tu wanapotishiwa usalama wao.

4. Ziwa Viktoria
Mwitongo ni eneo la mwinuko wa mita 1,405 juu ya usawa wa bahari. Kwa sababu ya mwinuko huo mtu anayesimama Mwitongo anaweza kuona kingo za Ziwa Viktoria zilizopo umbali wa kilomita 40 magharibi mwa Butiama.
Ziwa Viktoria.

5. Nelson Mandela
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitembelea Mwitongo mwezi Novemba 1999. Alifika Mwitongo kuhani kifo cha Mwalimu Nyerere aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999.

Mzee Mandela aliandaliwa chumba maalum cha kulala wakati wa ziara yake. Kitanda maalum kiliwekwa kwenye chumba hicho. Hata hivyo, ratiba yake haikuruhusu kulala, na akaondoka siku hiyo hiyo kurudi Afrika Kusini. Kitanda kile hakijaondolewa kwenye chumba kile hadi hii leo.

Friday, December 30, 2016

Hii ndiyo redio ya Mwalimu Nyerere 'enzi za Mwalimu'


Hii ndiyo redio ya Mwalimu Nyerere 'enzi za Mwalimu' (kwenye picha, chini). Ni aina ya National Panasonic, ambayo aliitumia katika miaka ya sitini na sabini.

Mwalimu Nyerere alikuwa msikilizaji makini kabisa wa taarifa za habari, na alikuwa akisikiliza taarifa kutoka vituo vya redio vya nje ya nchi, kama Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), pamoja na vituo vya ndani (wakati huo ikiwa ni Redio Tanzania peke yake).

Uzito wa redio hii ni kilo 20, na wakati wa safari kuna mtu maalum alikuwa akiibeba. Mabadiliko ya teknolojia yalisababisha kupungua kwa ukubwa wa redio, na katika miaka ya baadaye Mwalimu naye alianza kutumia redio ndogo zaidi ambazo uzito ulifikia hata chini ya robo kilo. Redio hii ipo kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere, Butiama.