Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, December 31, 2011

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya pili kati ya nne

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya pili kati ya nne

Kuhamisha bila viwanja na fidia ni dhuluma
Serikali imetoa mwezi mmoja kwa waathirika kuwa wamehama. Jambo hili si sawa kwa sababu: kwanza, nyumba ya kuishi haijengwi ndani ya mwezi mmoja kutokana na waathirika kutokuwa na pesa za kununulia vifaa vya ujenzi katika hali ya mfuko wa bei na ughali wa maisha ulioko nchini. Pili, tukumbuke kwamba waathirika tunaowaongelea hapa ni kina mama lishe, wafagia barabara, walinzi korokoroni, wachimba mitaro, machinga na watu wenye hali duni. Kipato chao ni kidogo mno hata hawawezi kupata milo mitatu kwa siku. Ni watu wasio na akiba benki. Ni watu ambao hawawezi kupata mikopo benki kwani benki haimkopeshi maskini hata siku moja. Na hata kama wanayo akiba benki lakini ni ndogo sana, haiwezi kujenga nyumba ndani ya mwezi mmoja ukizingatia ughali wa vifaa vya ujenzi.

Iweje leo tuwaambie waondoke wakajenge nyumba ili hali tunajua fika kwamba hawana uwezo wa kujenga nyumba? Tatu, ipo hoja kwamba waathirika waliwahi kupewa viwanja wakati Mzee Makamba akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nao wakaviuza. Hawakuhama. Na sasa tunawalaumu kwa kuacha kuhama wakati ule. Lakini tusisahau kwamba waathirika hawa wameishi katika maeneo haya kwa miaka mingi sana. Hawakuhamia jana wala juzi. Wana historia ya vizazi na vizazi. Mtu kazaliwa pale, kakulia pale, kaoa au kuolewa pale na sasa ana wajukuu tunamwambia ahame eti aepuke mafuriko (ambayo hayatokei kila mwaka) bila kulipwa fidia. Hivi hoja hii itakuingia akilini hata kama ni wewe? Kama ni mimi sihami ng'o.

Waathirika walipaswa kulipwa fidia ya nyumba zao ili kupitia hapo wapate nguvu ya kifedha ya kuwawezesha kwenda kujenga huko waendako. Naamini hakuna mwathirika hata mmoja aliyewahi kulipwa fidia enzi za Makamba akiwa mkuu wa mkoa ili ahame.  Sasa kama hawakulipwa fidia kwa nini leo  tunawalaumu? Uko wapi utu katika suala hili? Iko wapi sheria inayolinda haki na utu wa waathirika hawa?

Nafahamu kabisa kuwa serikali au jiji litatumia mabavu kuwahamisha waathirika kwani limewahi kufanya hivi mara nyingi tu na kuwahamisha watu. Niseme wazi kabisa, kwamba, kitendo cha kuzibomoa nyumba za waathirika bila fidia inayolingana na thamani ya eneo hilo lililoko katika jiji, na bila kuwapa viwanja, kitakuwa ni kitendo cha dhuluma. Na pia kuwapa viwanja tu, au kuwalipa fidia tu, ni dhuluma vilevile. Tutakuwa tumefanya uonevu. Tutakuwa tumekiuka haki za binadamu. Tutakuwa tumeudhalilisha utu wa waathirika. Baya zaidi tutakuwa tumewafanya waathirika kuwa maskini zaidi na zaidi.

Tukumbuke kuwa wakati wanajenga serikali ilikuwepo. Mbona haikuwazuia? Bomoabomoa ikifanyika bila kuwatendea haki itakuwa ni udhalimu. Katika hali sasa upo uwezekano wa kutolewa hoja kwamba serikali haiwezi kuwalipa fidia waathirika wanaoishi mabondeni. Swali hapa ni kama ni halali kuilipa Dowans zaidi ya shilingi bilioni 94, iweje haramu kuwalipa waathirika?

Kimsingi huenda pesa watakayolipwa waathirika isifikie hata robo ya malipo ya Dowans. Kivipi? Wako waathirika takriban 5,000. Ukiwa na wastani wa watu watano kwa familia moja ina maana una familia 1,000 za waathirika ambazo ni kaya au nyumba 1,000. Tuseme tunawalipa shilingi milioni 20 kila familia. Unapata jibu kwamba ni shilingi milioni 20 zidisha kwa familia 1,000 ambazo ni jumla ya shilingi bilioni 20.

Pesa hizi zitabaki nchini hazitakwenda nje kama Dowans. Pesa hizi zitaondoa umaskini kwa waathirika kinyume na zile za Dowans zitakazoongeza umaskini kwa kila mtanzania. Shilingi bilioni 94 ukizigawa kwa watu milioni 43 tulionao sasa utapata kila mmoja wetu analipa shilingi 2,186.05. Asilimia 50 ya Watanzania kwa mujibu wa takwimu zetu ni maskini wanaoishi chini ya dola moja kwa siku. Dola moja ni sawa na shilingi 1,583.50 leo hii tunawataka kila mmoja alipe dola 1.38 sawa na shilingi 2,186.05 kwa Dowans. Kama mlo wa Mtanzania maskini ni shilingi 1,000 kwa siku basi hii ina maana kwamba maskini wasile siku mbili ili tukawalipe Dowans. Ajabu sana hii.

Itaendelea.

Tuesday, December 27, 2011

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu kwa kwanza kati ya nne

Waathirika wa mafuriko wahame: sehemy ya kwanza kati ya nne
Na Amani Millanga

Ndugu zangu Watanzania, naungana nanyi kutoa mkono wa pole kwa waathirika wote wa mafuriko. Poleni sana kwa kupoteza ndugu, jamaa, na marafiki waliofariki katika mafuriko haya. Pia poleni sana kwa kupoteza mali zenu na vitu vyenu vyote kama nyaraka za umiliki wa nyumba zenu, vtambulisho na hata picha za familia n.k. ambavyo ni sehemu ya historia ya maisha yenu. Poleni sana na inshaallah Mungu atawasaidia. Anauona unyonge wenu. Auona umaskini wenu. Anauona udhalili wenu. Na kubwa zaidi Mungu muumba anauthamini sana utu wenu enyi waja wake mlioathirika na mafuriko. Naamuomba Mola Karima aziweke roho za marehemu pema peponi, inshallah. Nazipongeza jitihada zilizofanywa na watu binafsi, mwashirika binafsi pamoja na serikali za kutoa msaada wa kila hali na mali katika kuwafariji waathirika. Inshallah Mungu atakulipeni kwa sadaka zenu.

Wahame Mara Ngapi?
Haya si mafuriko ya kwanza kwa jiji la Dar es Salaam lakini n mafuriko ya kwaanza kufanya uharibifu mkubwa kama tulivyoshuhudia. Mafuriko yamefika hadi Ikulu, ofisi za UN na UNDP. Athari za mafuriko haya zimesababisha kuwepo kwa hoja nyingi kuhusiana na waathirika. Hoja inayotawala sana kwa baadhi ya watu na vyombo vya habari ni ile inayosema "waathirika wahame". Hoja hii haina mantiki wala mashiko yoyote. Hivi kweli hatuoni kwamba tayari waathirika wamekwishahamishwa na mafuriko? Hawako tena majumbani mwao. wanalala nje. Hivi tunataka wahame mara ngapi ili hali mvua imeishawahamisha? Kwa kweli hoja hii ya "wahame" tumeitoa katika wakati usiofaa kabisa. Huu si wakati wa kuwalaumu na kuwatia hofu ya kuwahamisha waathirika. Huu ni wakato wa maombolezo, huruma na huduma. Waathirika wanawalilia watoto zao, ndugu zao na jamaa zao waliofariki. wanalilia mali zao na historia yao. Kusema "wahame" si uungwana na si utu. Tukumbuke kwamba waathirika hawakuomba mafuriko. Lakini nitaitumia hoja hii ya "wahame" katika makala haya kutoa mchango wangu wa nini kifanyike katika wakati huu mgumu kwa taifa ambalo limesherehekea miaka 50 ya uhuru wake hivi karibuni.

Hoja za msingi kwa wakati huu: ni namna gani waathirika wanapata chakula na maji safi na salama; ni namna gani waathirika wanapata vyoo na bafu; ni namna gani waathirika wanalala; na ni namna gani waathirika wanapata nguo za kujisitiri; na tumejipanga vipi kuwakinga waathririka na magonjwa ya kuambukiza ya kipindupindu, malaria, kuhara, minyoo, n.k. Haya ndiyo mambo muhimu ya kufanywa kwanza. Ingawa baadhi yanafanyika basi tuongeze juhudi zaidi ya kutoa huduma zaidi. Pili, ni suala la wapi wanahamia waathirika hawa baada ya Mchikichini. Suala hili linaibua maswali mengi, lakini baadhi yake ni: Je, wahamishiwe wapi? Je, tumeishayatenga au kuyapima maeneo hayo ya kuwahamishia waathirika? Je, tutawalipa fidia za nyumba na ardhi yao? Je, fidia hiyo itachukua muda gani kumfikia muathirika? Je, wwanza kuhamishwa huko kwenye maeneo mapya lini? Maswali ni mengi yanayohusu huduma za afya, elimu na jamii huko wanakohamishiwa maana watu takribani 5,000 si wachache.

Itaendelea.

Monday, December 26, 2011

Matumla na Maneno nguvu sawa

Mabondia Rashidi 'Snake Man' Matumla, na Oswald 'Mtambo wa Gongo' Maneno wametoka sare katika pambano lao la jana lisilo la ibingwa kwa kugawana pointi 99 kwa 99.
Rashidi Matumla, kushoto, anakwepa ngumi ya Maneno Oswald katika pambano la jana.
Rashidi Matumla akiamka baada ya kuteleza kwenye pambano la jana.
Pambano lilifanyika jana katika Ukumbi wa Heineken, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam. Kwa matokeo haya Matumla ameshinda mapambano mawili kati yao na kutoka sare pambano moja, wakati Maneno ameshinda pambano moja na kutoka sare moja.

Bila shaka tutasikia mpambano mwingine kati ya hawa mabondia wawili.

Picha na baadhi ya taarifa kwa hisani ya www.superdboxingcoach.blogspot.com

Saturday, December 24, 2011

Mabondia Rashidi Matumla na Oswald Maneno wapima uzito tayari kwa pambano lao kesho

Mratibu wa pambano za ngumi za kulipwa Shabani Adios "Mwayamwaya', katikati, akishuhudia mabondia Maneno Oswald "Mtambo wa Gongo", kushoto, na Rashidi 'Snake Man' Matumla kulia, wakitunishiana misuli mara baada ya kupima uzito leo kabla ya pambano lao lisilo la ubingwa litakalofanyika Dar es Salaam siku ya Noeli kwenye ukumbi wa Heineken, Mtoni Kijichi.
Picha na habari kwa hisani ya www.superdboxingcoach.blogspot.com