Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, August 29, 2010

Vicent Nyerere: mgombea ubunge wa CHADEMA jimbo la Musoma Mjini

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2010, nitajitahidi kuhudhuria mikutano ya wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea na kuzileta habari hapa.

Jana nilihudhuria mkutano wa uzinduzi wa Vincent Josephat Nyerere wa kuwania kiti cha ubunge, Musoma Mjini, kupitia Chama cha Demokrasia na Mandeleo (CHADEMA).

Katika hotuba yake alisema:
"Nimejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kwa sababu ndiyo chama pekee kinachoweza kumtetea mwananchi mwenye maisha ya chini, na mlalahoi. Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, na mbunge aliyemaliza muda wake, hawaambiliki."
Vincent Nyerere akihutubia mkutano jana mjini Musoma.
Mkutano huo ulifanyika kwenye kiwanja cha Mukendo, Musoma. Aliongeza:
"Nyinyi ni mashahadi wa kutosha kwamba afya ya wakazi wa Musoma Mjini imedorora. Tunayo magari na wagonjwa mengi na mnayaona. Niambie ni nani ambaye ni mgonjwa na akabebwa na gari lile akapelekwa hospitali? ...Gari ya wagonjwa inabeba diwani wa CCM anakwenda kufuata ndizi Tarime."

Vincent Nyerere akihutubia mkutano Musoma mjini.
Aliendelea:
"Shule za kata nyinyi mmezichangia. Lakini huwezi kusema shule ya kata ni maendeleo. Shule inakuwaje maendeleo kama haitowi watoto wanaopasi; kama hakuna watoto waliopasi, siyo maendeleo. Mimi sijaridhika. Chama changu pia hakijaridhika.

Elimu inayotolewa Tanzania haimsaidiii mtoto wa Kitanzania, hasa shule ya msingi....Sisi CHADEMA tunaamini kwamba lazima mtoto huyu asome sekondari. Shule ya msingi iishie kidato cha nne. Ndiyo maana Tarime watoto walikuwa wanasoma mpaka kidato cha nne bila kulipa.* Na Musoma Mjini, inawezekana."

Na kusema:

"Mji huu umezungukwa na ziwa kwa asilimia karibu ya sabini, na kazi kubwa tunazozifanya katika ziwa hili ni uvuvi. Tumemchagua mbunge, anakwenda bungeni hajuwi thamani ya wavuvi na ni wapiga kura wake. Anaacha wabunge wa Morogoro wanachangia hoja za Ziwa Viktoria: wanasema kokoro ni marufuku.

Bila kokoro haiwezekani. Alitakiwa aweke hoja, ajenge hoja na aitetee kwamba kokoro liwepo, tuwe na maendeleo maalum ya kuvua, tuwafundishe vijana wetu wanaovua, wapi ni mazalia ya samaki, na wapi siyo mazalia ya samaki, na uvue kwa kutumia kokoro."
Vincent Nyerere akihutubia mkutano Musoma mjini.
Mengine haya:

"Bungeni nitajenga na kusimamia hoja. Mimi siyo muoga. Ukiona natetemeka, ni baridi. Na mimi nitafanya kazi zangu za ubunge bila chuki, bila uwoga, bila ubaguzi."
.............

"Lazima tutengeneze miradi mipya ya maendeleo, kwa kutumia mfuko wa Jimbo na marafiki tuliyonao, wawasaidie kina mama kwa sababu wakina mama ndiyo jamii inayoteseka kuliko sisi wanaume. Mama wa Musoma mjini ndiyo anakwenda kulala na mtoto hospitali, baba yuko nyumbani. Anaomba mama mwingine amshikie mtoto arudi kumpikia baba."
*Halmashauri ya Tarime Mjini inayomaliza muda wake likuwa inaongozwa na CHADEMA.

1 comment:

Anonymous said...

ni chadema tu mwaka huu.