Sababu moja ya msingi inayonisukuma kuhifadhi jina la 'mtaalamu' huyu ni kuwa shughuli za uchawi haziruhusiwi kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, kwa hiyo ili kutupunguzia yeye na mimi uwezekano wa kujikuta tunasaidia polisi kwenye uchunguzi nimeona ni bora abaki bila jina.
Katika barua pepe hiyo ameorodhesha matatizo 43 ambayo ana uwezo wa kuyamaliza. Nasema anayamaliza kwa sababu siyo yote ni maradhi. Mfano, anaweza “kutatua matatizo ya sehemu yako ya kazi, kama kutoelewana na bosi.” Kama hupandi cheo kazini anao uwezo wa kukupandisha. Jambo la hatari ambalo ana uwezo wa kufanya ni “kulipa kisasi kwa mbaya wako.”
Anaonekana kuwa na uwezo wa kipolisi na wa kimahakama kwa mpigo. Mfano, anaweza kurejesha mali iliyoibiwa. Aidha, anaweza kumaliza kesi mahakamani. Ni mshauri wa mavazi pia: anaweza "kutabiri nyota na nguo za kuvaa kuanzia Jumatatu hadi Jumapili." Mengine ni pamoja na uwezo wa kuwanasa wanga na wachawi, na uwezo wa "kutengeneza jini wa shari na kumtuma katika mambo ya shari."
Pamoja na mambo hayo anajitangaza kuwa na uwezo wa kutibu pia matatizo ya kiafya, mfano, matatizo ya uzazi kwa kina mama, kupungua nguvu za kiume, maradhi ya masikio, pumu, kichwa, tumbo, n.k.
Hivi karibuni, baada ya kuandamwa kwa Babu wa Loliondo kuwa anadanganya na kuwa hatibu ila anadanganya, niliandika makala kumtetea nikeleza jinsi gani watafiti wa nchi moja ya Ulaya walibaini katika utafiti kuwa inawezekana kumdanganya mgonjwa kuwa anapata dawa ya kutibu ugonjwa fulani, naye akapona akiamini kuwa amepewa dawa kumbe kapewa peremende tu inayofanana na dawa halisi. Katika mazingira hayo mgonjwa anapona kwa sababu anamuamini daktari anayempa ile dawa feki, na kuamini kuwa ni kweli anapewa dawa.
Katika makala niliyoandika nilihoji kama ni kweli kuwa Babu wa Loliondo anadanganya lakini watu wanapona kwa imani kuwa wanapewa dawa inayoponyesha basi hilo lisiwe tatizo la mtu yoyote ambaye hana mpango wa kwenda Loliondo. Kwa mantiki hiyo, ningemtetea hata huyu ‘mtaalamu’ wa kutibu zaidi ya 43, lakini nasita.
Labda tofauti ya msingi hapa kati ya huyu mtaalamu na Babu wa Loliondo ni kuwa Babu hakutangaza kama anatumia nguvu za uchawi – ingawa kuna baadhi ya watu wanasema kuwa anafanya hivyo.
No comments:
Post a Comment