Hivi karibuni nimemaliza mzunguko wa kazi na mazoezi nikitumia baiskeli wa takriban kilomita 174 ndani ya mikoa ya Mwanza na Mara. Imenipa fursa ya kuthibitisha kuwa utamaduni wa ukarimu miongoni mwa Watanzania bado uko imara.
Jiunge nami kwenye msafara huu...
Agosti 1
Safari yangu ilianzia Mwanza kwa kuvuka na meli iitwayo MV Clarias kuelekea Nansio, Ukerewe. Huko nilipokelewa na muongozaji wageni maarufu wa kisiwa cha Ukerewe, Tumaini Yohana Ladislaus ambaye ni mmiliki wa
Tumaini Tours.
|
Muda mchache kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ukerewe kutokea Mwanza. |
Siku ya kwanza alinipeleka kwenye makazi ya Mtemi Gabriel Ruhumbika, kwenye kijiji cha Bukindo ambako tulipata maelezo mafupi ya historia ya eneo hilo kutoka kwa mmoja wa waongozaji anayepokea wageni katika makazi hayo. Mtemi Ruhumbika ni baba mzazi wa Mtemi Michael Lukumbuzya ambaye alishika nyadhifa kadhaa serikalini ikiwa ni pamoja na kuwa balozi wa Tanzania nchini Canada.
|
Muongozaji wageni akitoa maelezo ya picha mbili za Mtemi Michael Lukumbuzya. |
Tulipotoka hapo tulielekea kwenye kijiji cha Murutunguru. Hapa ilikuwa sawasawa na kufungua kurasa za kitabu cha watu mashuhuri. Niliambiwa hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa mkuu wa walinzi binafsi wa Rais Julius Kambarage Nyerere; hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Gertrude Mongella; hapa ni nyumbani kwa aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania, Pius Msekwa, na kadhalika, na kadhalika. Na ni hivyo hivyo katika sehemu nyingi ya kisiwa cha Ukerewe.
Inasemekana Ukerewe ndiyo eneo lenye mkusanyiko mkubwa zaidi kwa kilomita za mraba za wasomi wa shahada za uzamivu kuliko sehemu yoyote ile Tanzania, na pengine hata Afrika.
Itaendela na: Mjasiriamali wa Ukerewe
sehemu ya pili ya makala hii
1 comment:
Kiukweli nimeipenda sana, Tuletee mambo mazuri zaidi ya kiutalii
Post a Comment