Juzi nilipewa fursa ya kutoa neno la shukurani kijijini Butiama kwenye hafla
ya kuzindua onyesho la noti na sarafu kwenye Makumbusho ya Mwalimu J.K.
Nyerere.
Mgeni rasmi alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Juma Reli. Katika
kumalizia neno la shukurani niliomba uongozi wa Benki Kuu kuangalia uwezekano wa
kubadilisha picha ya Mwalimu Julius Nyerere waliyotumia kwenye noti ya shilingi
elfu moja. Kwa maoni yangu ile picha haifanani kwa karibu sana na sura ya
Mwalimu Nyerere. Sikuamuru wala sikuikataa noti, ila niliomba tena kwa
unyenyekevu mkubwa. Lakini ukifuatilia habari zilizoandikwa juu ya ombi langu
utapata picha tofauti.
ITV walifungua dimba la upotoshaji kwa kusema kuwa nilitamka kuwa picha ile
inamdhalilisha Mwalimu (au familia yake?). Huu ni uongo wa mchana na siyo kweli
kabisa kuwa nilitumia neno “kudhalilisha.” Nikisoma baadhi ya vichwa vya habari
vya baadhi ya magazeti yaliyoandika habari hizo navyo vinapotosha.
The Citizen wameandika kuwa nimeitaka serikali kuiondoa hiyo noti. Huo nao ni
uongo mwingine. Gazeti lingine limeandika kuwa familia ya Mwalimu Nyerere
imeikataa noti ya shilingi elfu moja. Ni uongo juu ya uongo. Naamini orodha ni
ndefu zaidi lakini sijapata fursa ya kufuatilia kwa muda mrefu.
Sikusema kuwa familia imeikataa noti. Nilichosema ni hayo niliyoandika mwanzo
wa taarifa hii.
Ninayo bahati mbaya ya kutungiwa maneno ambayo sijayasema kwenye taarifa
zinazonihusu. Mwanzo nilikuwa napuuzia nikiamini kuwa tatizo hili litaisha
lakini kila muda unavyozidi kupita naona hali ni ile ile.
Nimekuwa nawashauri waandishi wa habari waache kutumia mtindo wa kuandika
“Madaraka alisema….” na badala yake watumie maneno yangu mwenyewe na kuandika
habari kwa njia ya kuninukuu. Naamini njia hii inapunguza kuweka maneno ambayo hayakutamkwa.
Naanza kufikia kuamini kuwa maneno yangu mwenyewe huwa hayauzi magazeti na
inalazimika mwandishi kuweka chumvi kidogo ili magazeti mengi zaidi yatoke. Kama
hii ni kweli basi hali hii inadhirihisha kuwa sifa ya weledi kwenye sekta ya
habari inaanguka, na inahitaji kufanyika jitihada ya kuirekebisha.