Siku kama ya leo, miaka 55 iliyopita, Apollo Milton Obote,
Waziri Mkuu wa Uganda alifunga ndoa na Bi Maria Kalule kwenye sherehe
iliyohudhuriwa na wageni 20,000.
Bibi harusi alikuwa ni katibu muhtasi kwenye ubalozi wa
Uganda kwenye Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Harusi yao ilifungwa na Askofu wa Uganda, Dk. Leslie Brown
kwenye Kanisa la Namirembe. Wakati wa ibada ya ndoa, Askofu alimwambia Bi
Kalule:
“Hufungi ndoa na Waziri Mkuu. Unafunga ndoa na mtu
unayempenda. Lakini kwa sababu yeye pia ni Waziri Mkuu basi ndoa hii ina
umuhimu mkubwa kwa maisha ya taifa la Uganda.”
Maharusi walipokuwa wanaondoka kanisani mamia kadhaa ya
waliohudhuria walishuhudia wakielekea kwenye sherehe iliyofanyika kwenye uwanja
wa Michezo wa Lugogo, sehemu pia zilipofanyika sherehe za uhuru Oktoba 1962
wakati Uganda ilipopata uhuru wake.
Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga ni miongoni mwa
waalikwa waliohudhuria kutoka Kenya.
Baadaye usiku huo, maharusi walisafiri kutoka Entebbe
kuelekea London kuelekea kwenye fungate yao.
No comments:
Post a Comment