Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, September 13, 2013

Hatari ya kuamini kila unachoambiwa

Miaka arubaini iliyopita taarifa ya kutua kwenye mwezi kwa chombo cha anga cha Marekani, Apollo 11, na kutembea kwenye mwezi kwa wanaanga wawili kutoka chombo hicho kulizua maswali mengi kutoka kwa mwanafunzi mwenzangu, Richard. Yeye hakuamini iliwezekana kwa binadamu kufika kwenye mwezi. Umri wangu ulikuwa miaka tisa na naamini Richard alikuwa na umri huo huo. Alisema, "Wanatudanganya hao!"

Mimi niliamini kuwa wale wanaanga wawili walifika kwenye mwezi. Sijui kwa sababu ipi sikuwaza kuwa ni uongo, lakini nakumbuka tu kuwa niliamini taarifa tulizosikia na kusoma bila kuhoji. Kwa umri wetu maoni yetu, ya kuamini au kutoamini, hayakutokana na ushahidi wowote tuliokuwa nao lakini ajabu ni kuwa tulikuwa na maoni tofauti.
Mwanaanga Edwin "Buzz" E. Adrin akionekana kwenye mwezi pembeni ya chombo kilichotua kwenye mwezi tarehe 20 Julai 1969. Picha ya National Space Agency (NASA).
Ukweli ni kuwa nilifikia maamuzi ambayo watu wengi hufikia katika mazingira ya aina hiyo. Tunayoambiwa tunaamini. Tatizo ya hali kama hii ni uwezekano wa kupokea taarifa za uongo kutoka mamlaka na serikali mbalimbali na kutumika kwa manufaa ya hao watoa taarifa za uongo.

Niligundua hivi karibuni kuwa wasiwasi wa taarifa zile kwa Richard za mwaka 1969 haukutokea Tanzania tu; hata baadhi ya Wamarekani hadi hii leo hawaamini kuwa Wamarekani wenzao walifika kwenye mwezi na wanasema kuwa mandhari ya mwezi ambayo tunaiona kwenye baadhi ya picha ilibuniwa na kutengenezwa hapa hapa duniani kwenye jengo moja kubwa linalohifadhi ndege kwenye uwanja mmojawapo wa ndege wa nchini Marekani.

Inawezekana kuwa tofauti ya sasa na mwaka 1969 ni kuwa watu wengi zaidi wamejenga desturi ya kutoamini taarifa za serikali na mamlaka mbalimbali. Serikali na mamlaka zimebainika mara nyingi kutoa taarifa za uongo na watu sasa wanaposikia taarifa hizo huanza kwa kutoamini hizo taarifa mpaka pale watakapopata taarifa kutoka vyanzo tofauti zinazothibitisha ukweli wa hizo taarifa za awali.

Taarifa inayofanana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2012/01/ingekuwa-unaishi-kwenye-sayari-ya.html

No comments: