Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, September 21, 2015

Ushauri kwa wanaopiga kura kwa mara ya kwanza

Nimepiga kura kwa mara ya kwanza mwaka 1985. Ningeweza kupiga kura mwaka 1980 lakini sikuwa nchini wakati huo, nilikuwa masomoni. Naamini kuna vijana wengi ambao watakuwa wanapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka huu na naomba nitoe ushauri mdogo kwao.
Nikiwa na Mwalimu wangu, Godian Muikza (kushoto) ambaye ni diwani anayemaliza muda wake wa Kata ya Ikondo, Wilaya ya Muleba Kusini.

Kwanza lipo suala muhimu la kuchambua ahadi. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1985 nilimpa kura ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi na ya ubunge nilimpa Kapteni Ukiwaona Ditopile Ramadhani Mwinshehe Mzuzuri. Siku zile sikuwahi kuhudhuria mkutano wowote wa kampeni za uchaguzi kwa hiyo kura yangu ya ubunge sikupiga kutumia kigezo kikubwa zaidi ya kufurahishwa na jina la mgombea. Sikumbuki hata alikuwa anagombea nafasi ile dhidi ya nani, lakini nakumbuka ilikuwa wanawania nafasi ya ubunge wa jimbo la Ilala. Mgombea urais, Mzee Mwinyi, alikuwa ana fursa ya kusikika zaidi ya wagombea ubunge kwenye vyombo vya habari kwa hiyo yeye tulimsikia zaidi ya wagombea ubunge.

Hata mwaka huu naamini kuna wapiga kura wengi watajitokeza wa aina yangu, kama nilivyokuwa mimi mwaka 1985 na kupiga kura kwa kufurahishwa na jina la mtu tu bila hata kuchambua kwa makini sera anazowakilisha mgombea huyo. Mwaka 1985 hatukuwa na vyama vingi, lakini sasa vipo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya msingi ya mpiga kura yoyote kuacha kuweka sera za vyama kwenye mizania na kuamua chama kipi kitapata kura yake. Hatuna uhakika kuwa yanayoahidiwa yatatekelezwa, lakini bado ni muhimu kuchambua sera tofauti. Akishinda mtu wako na asipotekeleza ilani yake angalau unayo sehemu ya kuanzia kumhoji. Kama ulimchagua kwa mkumbo tu hutakuwa na kigezo cha kuamua kuwa hajatimiza ahadi zake.
Wapiga kura wa Butiama wakipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010


Pili, nazungumzia wale ambao wana uhakika mkubwa wa matokeo ya ushindi kwa wanaowaunga mkono, ikiwa ni vyama vya siasa au mgombea mmoja mmoja. Kusikiliza na kuamini na kauli kama “ushindi ni lazima” ni mwanzo wa kukaribisha vurugu. Kama kiongozi anatumia kauli hiyo kuhamasisha tu wafuasi wake ili waweke juhudi kubwa kwenye kampeni inaweza kuwa haina madhara. Lakini kauli hiyo inaweza kufasiriwa kuwa “tumeshashinda hata kabla ya kupiga kura na mtu yoyote atakayesema kuwa hatujashinda ni muongo na ametuibia kura.” Hapo tunakaribisha vurugu.

Mwaka 2010 niliteuliwa wakala wa mgombea ubunge na nilijifunza kitu kimoja cha msingi. Kama wakala wa mgombea yuko makini, siyo rahisi kuibiwa kura. Sikulala siku hiyo mpaka matokeo yalipothibitishwa na msimamizi wa uchaguzi alfajiri ya siku iliyofuata. Wanaoibiwa kura ni wale ambao wameweka mawakala ambao siyo waaminifu au ambao hawakuwa makini. Mtu akitaka kuibiwa, ataibiwa.
Kulia ni Mhe. Vincent Nyeerere, Mbunge wa Musoma Vijijini kupita Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) anayemaliza kipindi chake cha ubunge aliyeniteua kusimamia kura zake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kushoto ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kapteni Godfrey Ngatuni.
Tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi tumesikia shutuma kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo wataalamu wa kuiba kura. Kama hizo shutuma ni za kweli, sioni sababu yoyote ya kutoana roho kwa sababu sasa hivi Mhe. Edward Lowassa amehamia upande wa pili. Yeye amekulia na kujifunza siasa ndani ya CCM na, kwa vyovyote vile, atakuwa amehama na uelewa uliobobea wa mbinu zinazotumika kuiba kura na atakuwa anafahamu mbinu za kutumika kuzuwia wizi huo. Mwizi hawezi kumuibia mwizi.
Mwanachama wa Chama cha wananchi (CUF) akielekea kwenye mkutano wa kampeni jijini Mwanza mwaka 2010.

Kwa sababu hii sioni kabisa busara ya mtu yoyote kutamka kuwa kaibiwa kura kama yeye mwenyewe hataki kuibiwa kura. Labda atumie kauli hiyo kama kisingizio cha kupinga matokeo. Tunao wajibu wa kujenga mazingira yenye kulinda amani, lakini tunao pia uwezo wa kuweka mazingira yanayobomoa amani.

Uchaguzi huu umeibua ushindani mkubwa kati ya CCM na vyama vinavyowakilishwa na UKAWA. Kwa bahati mbaya, ushindani unaonyesha dalili za uhasama na muelekeo kuwa kipindi hiki cha kampeni kitaibua matukio ya kuvunjika kwa amani. Lakini amani itavunjika tu iwapo wapiga kura tutakubali ivunjike. Na amani inapovunjika hutasikia hata siku moja kuwa Mhe. John Magufuli au Mhe. Edward Lowassa kavunjika mguu kwa sababu ya vurugu za kisiasa.


Bado sijaona sababu ya msingi ya kuvunjika kwa amani kutokana na uchaguzi. Usikubali kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani.

No comments: