Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, July 28, 2017

Afrika tunaibiwa sana, tena sana

Hii ni makala yangu ya tarehe 18 Julai 2017 kwenye safu yangu inayoitwa Ujumbe toka Muhunda ndani ya gazeti la Jamhuri linalochapishwa kila Jumanne.

******************************

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali Global Justice Now inaeleza jinsi gani bara la Afrika linavyoibiwa rasilimali yake.

Ripoti hiyo, inayoitwa Honest Accounts 2017, inaeleza kuwa kwa mwaka 2015 mali na pesa za thamani ya Dola za Marekani bilioni 203 zimetoka Afrika kwa njia ya faida ambazo mashirika ya kimataifa yamepata kutokana na shughuli za biashara na uzalishaji barani Afrika, na kwa mianya haramu ya pesa zinazotumwa nje. Wakati huo huo ni kiasi cha Dola bilioni 161.6 tu ambazo kwa mwaka huo ziliingia barani Afrika kwa njia ya mikopo, kutuma pesa kwa watu binafsi kutoka nje ya bara la Afrika, na misaada.

Huu utafiti unatukumbusha tu kuwa bara la Afrika ni tajiri, lakini kwa bahati mbaya Waafrika tunakubali, au kwa kutokujua au kwa kudanganywa, kuwa sisi ni maskini. Hali hii inatufanya sisi na serikali zetu kuwa na mawazo ya ombaomba ambaye badala ya kutumia uwezo aliojaliwa kutafuta riziki, anazunguka mitaani kuomba watu pesa za kuendesha maisha yake.

Taarifa inaendelea kufafanua jinsi bara la Afrika linavyoibiwa na mashirika ya biashara ya kimataifa. Wakati bara la Afrika linapokea kiasi cha Dola bilioni 19 kwa njia ya misaada kutoka nje, kiasi cha Dola bilioni 68 zinahamishwa kwenda nje na mashirika haya ambayo, kwa kawaida na kwa makusudi, hayataji thamani halisi za bidhaa wanazoingiza barani Afrika na mali inayoondoshwa kwenda nje. Ni hitimisho ambalo linafanana na hitimisho lililofikiwa na taarifa ya kwanza ya makinikia. Tofauti ni kuwa taarifa hii haitolewi na wataalamu waliyotumwa na Rais John Magufuli ila na shirika lililopo Ulaya ambalo linamulika kiwango cha wizi dhidi ya Afrika.

Pamoja na shutuma hizi dhidi ya wizi unaoendelea kudhoofisha maisha ya Waafrika, ni muhimu kutofautisha aina ya wizi huu. Kwanza, upo wizi ambao lazima tukubali kuwa ni wizi halali ambao unalindwa na sera na sheria mbovu zilizopitishwa na mabunge ya nchi za Afrika kulinda mifumo inayonyima Waafrika fursa ya kufaidika na utajiri wao.

Tutakuwa tunajidanganya kama hatutakubali kuwa rushwa ni mojawapo ya vichocheo vikubwa ambavyo vilisababisha baadhi ya nchi hizi kuweka sera na sheria ambazo, kwa ujumla wake, hazilindi maslahi ya Waafrika bali zinalinda maslahi ya mashirika ya nje kufuja rasilimali za bara letu na kuwaacha wananchi wake kuwa watumwa wa mali yao wenyewe.

Hata hivyo yapo mazingira ambayo hayasukumwi na rushwa ambapo inaziweka nchi za Afrika wakati kwenye shida kubwa za kiuchumi zinazowalazimisha kuweka mazingira yasiyo na manufaa kwa wananchi wake.

Madai ya kutaka kubadilisha mifumo hii ambayo yamejitokeza sasa nchini Tanzania yamewahi kujitokeza kwenye sekta ya madini nchini Zambia. Ilipobinafsisha migodi yake ya kuchimba shaba, Serikali ya Zambia ilikuwa inakabiliwa na uzalishaji mdogo na gharama kubwa ya kugharimia uzalishaji iliyokadiriwa kufikia Dola milioni moja kwa siku.

Ilipotafuta msaada kutoka mashirika ya fedha ya nje ikaambiwa dawa ni moja tu: ubinafsishaji. Kwa usiri ule ule ambao tuna uzoefu nao hata sisi, serikali ya Zambia ilifanya majadiliano ya ubinafsishaji na wawekezaji ambao, ingawa sheria ya madini ilitaka walipe mrahaba wa asilimia 3 kwa serikali kwa mauzo ya shaba nje ya nchi, mkataba wa siri uliwaruhusu kulipa asilimia 0.6. Aidha, makampuni ya kuchimba madini yakapunguziwa kodi ya mapato kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba wafanyakazi waliowaajiri wakawa wanalipa kodi kubwa zaidi kuliko makampuni hayo.

Huu nauita wizi halali, kwa sababu kimantiki ni wizi tu hata kama unalindwa na sheria za nchi. Pili, upo wizi ambao unakatazwa kwa mujibu wa sheria. Inakadiriwa kuwa kiasi cha Dola bilioni 29 zinafujwa barani Afrika kutokana na biashara haramu ya magogo, uvuvi, na biashara za wanyamapori na mimea. Biashara haramu ya pembe za ndovu inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola bilioni 10.

Njia nyingine ambayo inainyima Afrika manufaa inayotokana na mali yake ni kukosekana kwa viwanda vinavyochakata malighafi zake. Tunauza pamba nje ya nchi halafu tunanunua nguo zinazotokana na pamba hiyo. Tofauti ya thamani ya malighafi na bidhaa iliyotengenezwa inabaki nje.

Tunaruhusu utaratibu wa kupeleka nje makinikia badala ya kuweka mitambo barani Afrika ya kuchakata madini, na kwa hali hiyo kukosa ongezeko la thamani ya mali inayopelekwa nje na mapato kwa serikali zetu.

Kwa kifupi ripoti iliyotolewa inatukumbusha tu kuwa sehemu kubwa ya nchi zinaozoendelea zinanufaika na utajiri wa Afrika kuliko sehemu kubwa ya Waafrika wenyewe. Zile porojo kuwa nchi tajiri zinasaidia bara la Afrika hazina ukweli wowote. Ni bara la Afrika ambalo linasaidia nchi tajiri.

Kuna hotuba nzuri sana ya Mwalimu Nyerere inayotuasa tusikubali kusikia kelele tunazopigiwa tunapoazimia kufanya jambo lenye manufaa. Kwenye hotuba anasema kuwa tunapozidi kukaribia lengo, na kelele zitazidi kuwa kubwa.


Vita vya kurudisha mikononi mwa Waafrika utajiri wao inahitaji kutumia uzoefu mkubwa na maarifa. Lakini ni vita ambayo inahitaji kuiendesha huku tukiwa tumeziba masikio kuepuka kuyumbishwa na kelele ambazo zinazidi kuongezeka ili kutuondoa kwenye safari ya kurejesha na kuimarisha hadhi na heshima ya bara la Afrika.

No comments: