Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, July 1, 2017

Watoto wa mjini nimewakubali

Nimejifunza siku chache zilizopita kuwa mtoto anayeishi mjini ni tofauti sana na yule anayeishi kijijini. Wa mjini wajanja.

Nilikuwa kwenye mitaa ya Kariakoo hivi karibuni nikaamkiwa na binti mdogo aliyevaa baibui niliyemkadiria kuwa na umri usiozidi miaka saba. Aliniomba msaada wa pesa kwa ajili ya mama mlemavu aliyekuwa kwenye kiti cha walemavu upande wa pili wa barabara.

Nilitoa shilingi 5,000 nikamkabidhi na kumuuliza kama nimsaidie kuvuka barabara ya Livingstone ambayo wakati huo ilikuwa na msululu wa magari. Alinihakikishia atamudu kuvuka mwenyewe. Nikaendelea na kununua miwani kwa machinga na yeye akaondoka.

Dakika 20 baadaye nikamkuta yule mama mlemavu kwenye mtaa wa jirani nikamuuliza kama alipokea zile pesa nilizotoa.

"Pesa gani?"
"Zile elfu tano nilizompa yule binti akuletee?
"Hata sijazipata. Ngoja tumsubiri."

Wakati huo binti alikuwa kwenye duka moja akiendelea kuomba msaada kwa watu mbalimbali.

Binti alivyoniona akatabasamu kwa aibu na kukabidhi zile pesa kwa yule mama, ambaye alinijulisha kuwa ni mjukuu wake.

Nilitafakari kuwa inawezekana wanapozunguka kuomba pesa mjukuu anabaki na pesa nyingi kuliko anazokabidhi kwa bibi yake.

No comments: