Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, July 14, 2017

Simulizi za Jaffar Idi Amin

Hii simulizi nilipewa na Jaffar Idi Amin, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Uganda kati ya mwaka 1971 hadi 1979, Idi Amin Dada.

Anasema kuna siku alikuwa kwenye matembezi kwenye jiji la Kampala akakuta gari aina ya Volkswagen imeegeshwa na akasimama kwa muda mrefu akiiangalia kwa sababu aliitambua kuwa ilikuwa gari ya zamani ya baba yake.

Akiwa anaiangalia akatokea mtu na kumsalimia na kumuuliza sababu za kukaa muda pale akiangalia ile gari. Mazungumzo yakawa hivi:

"Mbona unaishangaa sana hiyo gari?"
"Ilikuwa gari ya baba yangu."
"Baba yako nani?"
"Idi Amin."

Anasema alivyotamka jina la baba yake yule aliyekuwa anamhoji akashangaa sana na kusema: "Baba yako ndiyo alimuondoa baba yangu nchini!"

Aliyekuwa anaongea naye alikuwa mmoja wa watoto wa Milton Obote, Eddy Engena-Maitum. Serikali ya Rais Obote ilipinduliwa na Idi Amin, wakati huo akiwa kamanda wa jeshi la Uganda, tarehe 25 Januari 1971 wakati Obote akiwa nchini Singapore kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Madola.

Idi Amin alishika madaraka mpaka mwaka 1979 baada ya Rais Nyerere kutangaza vita dhidi ya Uganda kufuatia uvamizi wa eneo la Kagera na majeshi ya Idi Amin. Baada ya kukomboa eneo lililovamiwa vita iliendelea ndani ya ardhi ya Uganda na kuhitimishwa kwa kuangushwa kwa serikali ya Amin.

Jaffar akamwambia Eddy: "Mimi nitakutambulisha kwa mtu ambaye baba yake alimuondoa baba yangu hapa Uganda." Alimaanisha mimi.

Mwalimu Nyerere akiwa na mwenyeji wake, Rais Milton Obote, wakati wa moja ya ziara zake nchini Uganda. Wa pili kutoka kulia ni Idi Amin, na kulia ni Philemon Mgaya, aliyekuwa mpambe wa Rais Nyerere.
Kabla ya siku hiyo Jaffar alipokutana na Eddy jijini Kampala, mimi na Jaffar tulikwa tumeonana kijijini Butiama katika tukio lililoandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuadhimisha miaka 30 ya vita vya Kagera, vita vilivomuondoa Idi Amin nchini Uganda.

***********************************
Bofya hapo chini kusoma maelezo yangu (kwa lugha ya Kiingereza) juu ya ziara ya Butiama ya Jaffar:

***********************************

Idi Amin na familia yake walikimbilia nchini Libya, na baadaye kuhamia Saudia Arabia. Milton Obote na familia yake walihamia Tanzania na wakawa majirani zetu Msasani kwa muda mrefu.

No comments: