Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, March 2, 2018

Hii ndiyo mila ya Kizananki ya kurudisha mahari

Miaka ya hivi karibuni baada ya kufariki mmoja wa shangazi zangu, nilipigiwa simu na baba yangu mdogo kunipa taarifa ya msiba na kunitaka nifike kwenye msiba.

Nilichelewa kidogo kufika kwenye msiba na aliendelea kunipigia simu mara kwa mara kunihimiza nifike mapema kwenye msiba. Alisema: "huu ni msiba wenu, njoo haraka!"

Sikuelewa maana ya ule kuwa "msiba wetu" mpaka baadaye.

Katika mila ambayo ilifuatwa miongoni mwa Wazanaki, mume anaweza kurudishiwa mahari na ndugu wa mke ili kuhalalisha wanandoa wawili kuachana na mke kurudi kwa ndugu zake.

Hili hutokea kwa sababu za kutoelewana kwa wanandoa, na hasa kama ndugu wa mke wanaamini kuwa dada yao anateswa au kudhalilishwa na mume wake.

Nilichojifunza kwenye msiba ni kuwa Mwalimu Nyerere alirudisha mahari kwa mume wa shangazi yangu na shangazi akarudi kuishi miongoni mwa ndugu zake.

Kwa desturi ya enzi hizo mke anayerudi nyumbani anatunzwa na ndugu zake. Kwa huyo shangazi, Mwalimu Nyerere alimjengea nyumba na aliendelea kuishi kwenye kijiji cha Butiama mpaka alipofariki.

Kwa mila hii mahitaji yake yote makubwa pamoja na ya watoto wake yatatimizwa  na ndugu zake. Aidha, inapotokea binti zake kuolewa basi mahari yao inachukuliwa na hao waliomrudisha nyumbani. Kwa mantiki hiyo, hata unapotokea msiba gharama za msiba zinabebwa na waliomtoa kwa mume wake.

Na ndiyo hapo nikaelewa kauli ya baba yangu mdogo: "huu ni msiba wenu!" Mwalimu Nyerere ana warithi wake ambao wanapaswa kurithi pia majukumu yake.

Lakini mila na desturi zinabadilika. Wakati wa msiba uliibuka ubishi mkali kati ya wazee juu ya mila hiyo. Baadhi yao waliona kuwa haipaswi kufuatwa kwa sasa.

No comments: