Kuna maeneo mengi ya Tanzania, kama hii hapa kwenye picha iliyopo karibu na kijiji cha Butiama, unapoweza kuona alama ambazo hazijulikani ni za nini. Maelezo yasiyo na uthibitisho yatolewayo na baadhi ya watu ni kuwa hizi ni alama ambazo ziliwekwa na Wakoloni wa Kijerumani waliokuwa nchini kati ya mwaka 1891 na 1919. Inasemekana waliweka hizi alama maeneo ambako walichimbia madini yenye thamani.
Alama hizi zilizopo Butiama zinaonekana ni za muda mrefu sana uliyopita. Ni alama zenye msalaba, na zinakaribiana kwa futi chache tu. Miaka michache iliyopita kwenye sehemu inayofanana na hii, ndani ya pango, watu kadhaa walikufa wakijaribu kuchimba ndani ya hilo pango baada ya kufukiwa na mawe na kifusi.
Nakumbuka kuonana na mtu mmoja jijini Dar es Salaam miaka mingi iliyopita aliyeniomba nigharamie ununuzi wa baruti kwa ajili ya kwenda kulipua eneo lililopo Kondoa ambalo yeye aliamini lilikuwa na shehena ya madini ya Wajerumani. Kama ambavyo huwa sipendi kucheza bahati nasibu, mimi sikukubali ombi lake.
No comments:
Post a Comment