Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, March 2, 2010

Kuhusu Muhunda

Muhunda ni eneo la kijiji cha Butiama ambapo kwa kabila la Wazanaki ni msitu ambapo zamani mitambiko mbalimbali ya kimila ilikuwa ikifanyika.

Ni eneo lenye ukubwa wa kiasi cha ekari 15 ambalo limewekewa uzio, na hairuhusiwi kuingia humo kiholelaholela. Ni wazee wa kimila tu, waitwao Wanyikura, wanaoruhusiwa kuingia humo kufanya mitambiko. Kuna kundi lingine dogo la watu maalum ambao nao huruhusiwa kuingia humo. Wengine, kama kina mama wanaotafuta kuni za kupikia, wanaruhusiwa kuingia na kuokota kuni ambazo zinatokana na matawi ya miti yaliyoanguka yenyewe lakini hawaruhusiwi kukata kuni toka kwenye matawi ya miti uliosimama.

Inaaminika kuwa mzimu wa Wazanaki wa eneo la Butiama, unaoitwa Muhunda, ndiyo unaishi katika eneo hili, na ndiyo sababu panaitwa Muhunda. 'Muhunda' ni kama mzimu unaoilinda jamii ya Wazanaki wa Butiama. Wazanaki wa maeneo mengine nao wanayo mizimu yao.

Vilevile, inaaminika kuwa Muhunda hujitokeza kama nyoka, au nyani mkubwa, au wakati mwingine kama chui. Katika kuishi Butiama kwa miaka kumi mfulilizo sasa, nimeshashuhudia nyani mkubwa kuonekana eneo la Muhunda, na baadaye wazee walifunga safari kwenda eneo la mto Mara kwa mpiga ramli kutaka kufahamu maana ya kuonekana kwa 'Muhunda.'

Inasemekena wakati wowote kukitokea tukio kama hilo kuna tatizo ndani ya jamii na ni jukumu la wazee wa mila kuchunguza tatizo ni nini na kufanya mitambiko kuzuia tatizo hilo kuendelea.

1 comment:

Anonymous said...

Mkuu Madaraka,

Ahsante sana kwa kutuletea habari zote hizi katika lugha yetu ya Taifa. Kama nilivyokuahidi nitakuwa ninazisoma makala zako zote kila ukiandika.

Habari kama hizi ni sawa na kutufungulia HAZINA ya historia ambayo wengi wetu hatukuijua na hasa watoto wetu.

Nakuomba usichoke kutumwagia habari unazoona zitakuwa za manufaa kwetu Watanzania kuzijua.
Ahsante sana kwa kuitikia wito wetu na umetimiza ahadi yako kwetu. Mungu Akubariki!

This Is Black=Blackmannen