Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya tatu kati ya nne
Kuhama
si suluhisho pekee la kukabiliana na maafa. Suluhisho ni kujenga
miundombinu inayoweza kuhimili maafa hayo ingawa naamini nguvu ya Mungu
ndiyo kinga kuu. Zipo nchi kama Japan na New Zealand ziko kwenye ukanda
wa tetemeko la ardhi. Indonesia takriban kila mwaka inakumbwa na
tetemeko la ardhi, milipuko ya volkano na mafuriko. Uturuki, Pakistani
na hata Marekani huwa zinakumbwa na athari za mitetemeko ya ardhi na
mafuriko.
Ujumbe katika nchi hizi si
kuhamisha watu bali ni kujenga miundombinu imara inayoweza kukabiliana
na nguvu hizi za asili na walau kupunguza makali yake. Kwa Dar es Salaam
sijasikia hoja ya kujenga kingo katika mto uliofurika ili kupunguza
makali ya mafuriko siku zijazo. Kwa nini hatuoni hili la miundombinu na
tunakimbilia kuwahamisha waathirika?
Ni ukweli uliowazi kwamba maeneo yalikotokea mafuriko ni
maeneo mazuri kwa biashara na ujenzi wa majumba makubwa ya kisasa. Je,
wakishahama hawa waathirika maeneo haya yatabaki kuwa wazi tu au
yatagawiwa kwa matajiri na "wawekezaji" kujenga vitega uchumi vyao? Kama
serikali au jiji litayagawa haya maeneo kwa wawekezaji kwa nini
tunataka kuwahamisha watu hawa bila kuwapa fidia inayolingana na thamani
ya maeneo yao?
Najua fika kuwa wakati huo
waja, ambao serikali au jiji litasema 'maeneo haya ni mazuri kwa
biashara na kwamba wawekezaji watajenga nyumba imara za kuhimili
mafuriko na kujenga kingo kwenye mto na miundo mbinu ya kuzuia
mafuriko'. Tutaipokea hoja hiyo kwa mikono miwili na kusahau kwamba
ilifanyika dhuluma ya kuwahamisha waathirika bila kuwapa malipo.
Naungana na waathirika kuidai fidia kabla ya kuhamishwa kwa haki katika
maeneo yao. Natoa wito kwa serikali kuwalipa fidia waathirika. Pili
natoa wito kwa Watanzania kuhakikisha kuwa waathirika wanapata haki yao.
Natoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuliangalia suala hili kwa kina na
mapana yake.
Itaendelea.
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment