Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, December 31, 2011

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya pili kati ya nne

Maoni ya Amani Millanga kuhusu mafuriko ya Dar: sehemu ya pili kati ya nne

Kuhamisha bila viwanja na fidia ni dhuluma
Serikali imetoa mwezi mmoja kwa waathirika kuwa wamehama. Jambo hili si sawa kwa sababu: kwanza, nyumba ya kuishi haijengwi ndani ya mwezi mmoja kutokana na waathirika kutokuwa na pesa za kununulia vifaa vya ujenzi katika hali ya mfuko wa bei na ughali wa maisha ulioko nchini. Pili, tukumbuke kwamba waathirika tunaowaongelea hapa ni kina mama lishe, wafagia barabara, walinzi korokoroni, wachimba mitaro, machinga na watu wenye hali duni. Kipato chao ni kidogo mno hata hawawezi kupata milo mitatu kwa siku. Ni watu wasio na akiba benki. Ni watu ambao hawawezi kupata mikopo benki kwani benki haimkopeshi maskini hata siku moja. Na hata kama wanayo akiba benki lakini ni ndogo sana, haiwezi kujenga nyumba ndani ya mwezi mmoja ukizingatia ughali wa vifaa vya ujenzi.

Iweje leo tuwaambie waondoke wakajenge nyumba ili hali tunajua fika kwamba hawana uwezo wa kujenga nyumba? Tatu, ipo hoja kwamba waathirika waliwahi kupewa viwanja wakati Mzee Makamba akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nao wakaviuza. Hawakuhama. Na sasa tunawalaumu kwa kuacha kuhama wakati ule. Lakini tusisahau kwamba waathirika hawa wameishi katika maeneo haya kwa miaka mingi sana. Hawakuhamia jana wala juzi. Wana historia ya vizazi na vizazi. Mtu kazaliwa pale, kakulia pale, kaoa au kuolewa pale na sasa ana wajukuu tunamwambia ahame eti aepuke mafuriko (ambayo hayatokei kila mwaka) bila kulipwa fidia. Hivi hoja hii itakuingia akilini hata kama ni wewe? Kama ni mimi sihami ng'o.

Waathirika walipaswa kulipwa fidia ya nyumba zao ili kupitia hapo wapate nguvu ya kifedha ya kuwawezesha kwenda kujenga huko waendako. Naamini hakuna mwathirika hata mmoja aliyewahi kulipwa fidia enzi za Makamba akiwa mkuu wa mkoa ili ahame.  Sasa kama hawakulipwa fidia kwa nini leo  tunawalaumu? Uko wapi utu katika suala hili? Iko wapi sheria inayolinda haki na utu wa waathirika hawa?

Nafahamu kabisa kuwa serikali au jiji litatumia mabavu kuwahamisha waathirika kwani limewahi kufanya hivi mara nyingi tu na kuwahamisha watu. Niseme wazi kabisa, kwamba, kitendo cha kuzibomoa nyumba za waathirika bila fidia inayolingana na thamani ya eneo hilo lililoko katika jiji, na bila kuwapa viwanja, kitakuwa ni kitendo cha dhuluma. Na pia kuwapa viwanja tu, au kuwalipa fidia tu, ni dhuluma vilevile. Tutakuwa tumefanya uonevu. Tutakuwa tumekiuka haki za binadamu. Tutakuwa tumeudhalilisha utu wa waathirika. Baya zaidi tutakuwa tumewafanya waathirika kuwa maskini zaidi na zaidi.

Tukumbuke kuwa wakati wanajenga serikali ilikuwepo. Mbona haikuwazuia? Bomoabomoa ikifanyika bila kuwatendea haki itakuwa ni udhalimu. Katika hali sasa upo uwezekano wa kutolewa hoja kwamba serikali haiwezi kuwalipa fidia waathirika wanaoishi mabondeni. Swali hapa ni kama ni halali kuilipa Dowans zaidi ya shilingi bilioni 94, iweje haramu kuwalipa waathirika?

Kimsingi huenda pesa watakayolipwa waathirika isifikie hata robo ya malipo ya Dowans. Kivipi? Wako waathirika takriban 5,000. Ukiwa na wastani wa watu watano kwa familia moja ina maana una familia 1,000 za waathirika ambazo ni kaya au nyumba 1,000. Tuseme tunawalipa shilingi milioni 20 kila familia. Unapata jibu kwamba ni shilingi milioni 20 zidisha kwa familia 1,000 ambazo ni jumla ya shilingi bilioni 20.

Pesa hizi zitabaki nchini hazitakwenda nje kama Dowans. Pesa hizi zitaondoa umaskini kwa waathirika kinyume na zile za Dowans zitakazoongeza umaskini kwa kila mtanzania. Shilingi bilioni 94 ukizigawa kwa watu milioni 43 tulionao sasa utapata kila mmoja wetu analipa shilingi 2,186.05. Asilimia 50 ya Watanzania kwa mujibu wa takwimu zetu ni maskini wanaoishi chini ya dola moja kwa siku. Dola moja ni sawa na shilingi 1,583.50 leo hii tunawataka kila mmoja alipe dola 1.38 sawa na shilingi 2,186.05 kwa Dowans. Kama mlo wa Mtanzania maskini ni shilingi 1,000 kwa siku basi hii ina maana kwamba maskini wasile siku mbili ili tukawalipe Dowans. Ajabu sana hii.

Itaendelea.

No comments: