Siku chache zilizopita nimehudhuria sherehe ya kupokea mahari ya kitukuu wa Mtemi Edward Wanzagi wa Butiama.
|
Wageni wanajitambulisha. |
|
Wageni (waliosimama), wanawasalimia wenyeji. |
Desturi inaelekeza kuwa mahari lazima ipokelewe kabla ya saa sita mchana, yaani kabla jua halijavuka na kuwa upande wa magharibi.
|
Kukagua mahari. |
Kuna mlolongo mfupi wa matukio yanayohusiana na sherehe hiyo. Wageni wanaoleta mahari wanatambulishwa kwa wenyeji wao, na wao wanatambulisha upande wao. Halafu, wageni wanajongea walipoketi wenyeji na "kuwaamkia." Na kama ishara ya heshima wageni wote wanaamkia "shimakoo" hata kwa wale wageni ambao wanaostahili "shikamoo" zao kutoka kwa baadhi ya wenyeji. Wakati wa kusalimia wenyeji huketi wakati wageni wanasimama mbele ya wenyeji.
|
Kukagua mahari. |
Baada ya salamu ndiyo unawadia wakati wa kukabidhiwa mahari. Mahari iliyoafikiwa ni ng'ombe sita, na mbuzi wanne. Wenyeji hukagua mahari kuhakikisha kuwa ng'ombe na mbuzi wako kwenye hali nzuri. Na hapo ilitokea mmoja wa wazee kwa upande wa wenyeji kutamka kuwa mmoja wa ng'ombe alikuwa na homa, hakuwa mzima. Na desturi ingelazimisha yule ng'ombe kurudishwa na kuletwa mwingine ambaye hana tatizo. Lakini ikaamuliwa kuwa pengine hali hiyo ya ng'ombe ilisababishwa na safari ndefu ya kuwafikisha pale Butiama na kuwa baada ya muda hali ya kawaida ya ng'ombe yule itarejea.
|
"Ng'ombe mmoja ana homa," alisema mzee mmoja baada ya kuwakagua ng'ombe. |
Baada ya hapo msemaji wa wenyeji anatamka kuwa mahari imekamilika na kina mama wanapiga vigelegele. Inafuata hatua ya kukabidhi zawadi ndogo kwa wazee (blanketi), na kwa mama wa bibi harusi (kitenge na sufuria). Mwisho kwenye ratiba ni chakula na baadaye wageni kuondoka.
|
Mzee Joseph Muhunda Nyerere anapokea blanketi kutoka kwa mwakilishi wa Bwana Harusi. |
Baada ya hapo inasubiriwa siku ya kufunga ndoa. Kwa mila na destru za zamani, ndoa ingekuwa imekamilika baada ya kupokelewa mahari.
Maharusi watarajiwa hawahudhurii sherehe hii.
No comments:
Post a Comment