Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, September 13, 2010

John Mnyika wa CHADEMA anajibu hoja dhidi ya sera ya majimbo (sehemu ya pili na ya mwisho)

Hii ni sehemu na pili na ya mwisho ikijibu ya hoja ya Amani Millanga dhidi ya sera ya majimbo.

Katika makala hii, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, anaendelea kutetea sera ya majimbo ya CHADEMA.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------
Sera ya Majimbo: Afrika Kusini, Nigeria na mfumo mpya wa utawala Tanzania


na 

John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje (CHADEMA)

Hivi karibuni niliandika makala yenye [kichwa cha habari] "Sera ya majimbo na siri ya Maisha bora kwa kila Mtanzania'. Wengi wamenipigia jumbe mbalimbali za kunipongeza. Wengine wameniuliza maswali na baadhi wamepingana na hoja zangu. Lengo la makala yangu ya leo ni kujibu baadhi ya maswali hayo na kufafanua dhana na muktadha wa baadhi ya hoja nilizozitoa.

Nafurahi kwamba kuna waliopingana na hoja zangu si kwa sababu tu ya kubisha, ila wameingia katika viatu vya Watanzania wenye hofu kuhusu majimbo ama wanapotoshwa kuhusu majimbo. Na ni kweli kabisa. Na hasa baada ya kuzindua sera 'nzito' (heavy) kwenye uchaguzi na tena kuanzia kuitambulisha Kilimanjaro! Washindani wetu wakaitumia hii fursa kupotosha sera hii na kuwatia hofu wananchi. Uzuri ni kwamba hakukuwa na hoja zilizotolewa, zaidi ya kauli tu ni 'ukabila', italeta vita kama Nigeria, ni Ubaguzi, wengine watakosa rasilimali n.k. 

Sasa tuna miaka mitano ya kubishana kwa hoja. Na niliwahi kusema huko nyuma ukweli ukitamalaki aliyesema uwongo hutamani kujifunika kwa kiganja kama Adili na nduguze. Na hii ndiyo itawakumba viongozi wa juu wa CCM miaka kadhaa toka sasa. Changamoto kwetu sasa ni kuuhamisha mjadala huu kwa wananchi ili wafahamu undani wa mambo haya. Na nonavyoona sasa kuna masuala ambayo tumeanza kuelewana.

Wapo waliotoa hoja kwamba tusifanye kitu kwa kuiga! Ukweli ni kwamba hii haikuwa sera ya kuiga. Ilizuka kama wazo (idea) tu, kwamba kwa kuwa falsafa yetu ni nguvu ya umma, kwa nini tusipeleke mamlaka kwa umma. Tukajiuliza ni kwa njia gani, likaja wazo la kuwa na mfumo mpya wa utawala - ikiwemo suala la muundo mpya wa utawala (majimbo). 

Na kwa kweli ilikuwa ni eneo jipya kabisa kiasi kwamba kulikuwa na mitazamo tofauti kuhusu mfumo uweje. Katika harakati hizo ndio tulipoanza kuangalia pia je nchi nyingine zinafanyaje? (hii inakaribia na kuiga). Lakini hatukuingia kiundani sana kuchota mifano ya nchi nyingine kwa kuwa hata muda huo hatukuwa nao. Kwa hiyo tukafikiria kwa kadiri ya mazingira yetu. Tukaingia kwenye uchaguzi, CCM wakaanza kupotosha kwa kutumia mifano ya nchi mbalimbali. Hapo sasa ikabidi kuingia kiundani hiyo mifano wanayotoa kwa nia ya kuwajibu, hapo ndipo mjadala sasa kwa pande zote ukaanza kutawaliwa na mifano ya nje (hapo ndipo hisia za kwamba tunaiga kujengeka). Lakini nilisema na narudia - sisi tulikuja na dhana ya uliberali/umajimbo wa kiutendaji (functional federalism).

Wapo waliojenga hoja kinzani kwamba nchi nyingi wanachukua ufiderali kwa sababu ya kutafuta UMOJA. Nakubaliana nao. Lakini UMOJA ni sababu moja tu. Hata sisi ni moja ya sababu kama msingi mmojawapo (rejea makala yangu ya awali). Lakini kila nchi ni zaidi ya hapo, pitia misingi ya ufiderali ya nchi mbalimbali utakubaliana na mimi.

Mchambuzi mmoja amechukua muda mrefu kupinga hoja zangu kwa kuzungumzia mfano wa Afrika Kusini na ubaguzi wa rangi (Apartheid). Kwa kufanya hivyo, nami hapa chini nitatota uchambuzi wangu kuhusu Afrika Kusini. Hoja kubwa iliyotolewa ni kwamba Afrika Kusini (SA) wamechukua muundo wa majimbo ili kukabiliana na ubaguzi wa rangi (Apartheid), na kwamba palikuwa na majimbo manne katika nchi hiyo ambayo yamegawanyika. 

Nakubali kuwa palikuwa na majimbo manne (kwa hiyo kama ingekuwa ni kwa lengo la kuunganisha majimbo kuleta umoja na kuondoa unbaguzi pekee kwa nini Afrika Kusini imeamua kuwa na majimbo tisa badala ya hayo manne?). Haya majimbo mengine matano yametoka wapi? Yameundwa kwa vigezo gani? Nitajadili suala hili kiasi hapo chini.

Wengine wamenijia huu [juu?] na kusema hawakubaliani nami katika mipaka yetu, imewekwa kiubaguzi. Kwanza niseme kwamba sijatamka bayana kwamba mipaka yetu imewekwa kiubaguzi. Nilichosema ni kwamba imetokea mara kadhaa watawala wetu kuweka mipaka ya kiwilaya bila kutoa sababu za kina na kuonekana kuwa ni misingi ya ukabila ama makabila. Niliwauliza maswali mawili ambayo kwa kuwa sikupewa majibu ya kina nimeona leo niyaulize rasmi kupitia makala yangu: "Unaweza ukaniambia ni kwanini Rais ameigawa wilaya ya Tarime kuwa wilaya mbili za Tarime na Rorya? Au unaweza kuniambia kwa nini wilaya ya Hai ambayo ni ndogo iligawanywa kuwa wilaya mbili za Hai na Siha (wilaya ambayo kwa idadi wa watu ni ndogo kuliko kata moja yenye watu wengi zaidi katika jimbo la Ubungo)?"

Mchambuzi mmoja ametoa hoja kwamba hatuna sababu ya kuweka mistari ya uwanja wa mpira wa kikapu (basketball) ilihali tunacheza mpira wa miguu (football). Na mchambuzi amehitimisha hoja yake kwa kuuliza kwa lugha ya Kiingereza sera ya majimbo 'for what' ambayo naweza kutafsiri "kwa ajili gani ama kwa nini?" Hii ni njia nzuri ya kujenga hoja kwa kutumia mifano, nami nitautumia mfano huu kufafanua hoja za awali.

Hapa kuna mambo mawili - Mosi, ni kwamba hii mistari tunayoita mistari hivi sasa ilichorwa na watu kama sisi (ila wao tunawaita watawala). Mistari ya nchi ilichorwa na wakoloni. Baadhi ya mistari ya mikoa na wilaya tukairithi toka kwao. Na mistari mingine watawala wakaanza kuichora. Na mingine wanaendelea kuichora. Mwaka juzi wakachora mstari kukatokea mkoa unaitwa Manyara. Na sasa nasikia wanataka kuchora zaidi.

Wasiwasi wetu ni kwamba wanaichora vibaya, bila shabaha (hawajibu swali FOR WHAT). Sisi tunataka ichorwe na wananchi kupitia mchakato wa kuunda katiba mpya. Iwe mistari ya wananchi kwa ujumla wao na kwa matakwa yao. Tunaweka wazi misingi ya ufiderali. Halafu kwa pamoja tuamue uweje na mipaka yake iweje.

Tunapotaja mipaka ya maeneo hivi sasa, mathalani ya Jimbo la Ziwa ama Jimbo la Kaskazini n.k., tunataja kama mawazo yetu tu na ili kurahisisha uelewa. Mipaka itakuwa ipi hili ni suala la wananchi kuamua. Tofauti na sasa ambapo Rais anaweza akalala akaamka akatangaza kugawa mkoa...na akateua anayemtaka kuwa mkuu wa mkoa ama akafanya hivyo kwa wilaya. Hakuna udhibiti, hakuna urari, hakuna ushiriki (No checks, No balance, No participation)....FOR WHAT, anaweza tu kuwajibu kwamba URAIS HAUNA UBIA, AMA NIMEFANYA HIVYO KWA MASLAHI YA UMMA, AMA NIMEFANYA HIVYO KWA MAMLAKA MLIYONIPA!

Mmoja ameandika kulalamika kwamba sera ya majimbo itaibagua "Singida". Nadhani Singida imetumika kama ishara (symbol) ikimaanisha maeneo ambayo hayana rasilimali. Mambo kadhaa yanajitokeza. Mosi, hakuna haja ya kufikiria sana kuhusu Singida - hakutakuwa na Jimbo linaitwa Singida. Singida ni mkoa wa hivi sasa ambao utavunjwa na kuunganishwa na maeneo mengine kuwa JIMBO LA KATI (Central Province). Itajumuisha maeneo gani itategemea idadi ya majimbo nchi nzima kwa mujibu wa uamuzi wa wananci. Lakini kama tukiwa na majimbo 8 au 9 basi Jimbo la Kati linaweza kuwa maeneo ya DODOMA, SINGIDA, MTERA, KILOSA n.k. Sasa wakazi wa maeneo haya watuambie je, kanda hii haitakuwa na rasilimali? Huku kuna Zabibu, mabwawa ya maji, mito, mbuga za wanyama, ardhi ya kilimo n.k.

Lakini nirudie ambacho niliwahi kukisema, na nakirudia tena - duniani kote RASILIMALI ni zaidi ya MALIASILI. Kuna majimbo (states) hazina MALIASILI lakini zinatumia RASLIMALI watu na upekee wake kufanya kwenda mbele. Kadiri Singida inavyoendelea kuwa tegemezi kwa Dar es Salaam (soma - serikali kuu) msitegemee maajabu ya Mussa. Hivi mpaka sasa DODOMA imetumiaje fursa ya kuwa Mji Mkuu wa Bunge kuleta maendeleo? (Hapa namaanisha, Dodoma sio mji mkuu wa Tanzania - huu ni mjadala mwingine tofauti). Ni wapi kwenye katiba pameandikwa kwamba mji mkuu ni Dodoma ama ni lini sheria ya bunge ilipitishwa kubadili makao makuu ya nchi kuwa Dodoma zaidi ya sheria njiti iliyoibuka baadae ya Mamlaka ya Maendeleo ya Mji Mkuu (CDA)?

Nimelalamikiwa kwa kutumia mifano ya nchi zilizofanikiwa. Nadhani ni kitu kizuri kutumia mifano mizuri na kujifunza kutoka katika mifano mibaya. Wachambuzi watupe nchi ambazo zimeshindwa kutokana na kutumia Mfumo wa Ufiderali. Nami nitatoa mifano ya nchi nyingi zaidi zilizofanikiwa kutokana na ufiderali na nchi zilizoshindwa kutokana na serikali kuu kuhodhi kila kitu (unitary).

Yupo aliyesema kwamba Nigeria haiendelei kutokana na majimbo. Wanaojua historia na mwelekeo wa nchi watakubaliana nami kwamba yanayotokea Nigeria si kwa sababu ya majimbo, tena ukweli ni kwamba kuna majimbo ambayo yamepitisha sheria za maendeleo (progressive laws) zinazowapa wananchi wake manufaa ya rasilimali. Kuna majimbo ambayo hayana msalie mtume na rushwa. Harakati (struggle) za Niger Delta si kati ya wananchi kwa wananchi, ni kati ya wananchi na watawala waliofunga ndoa na makampuni ya kinyonyaji. Ni struggle ambayo hata Tanzania inakuja, tuwe na mfumo wa ufiderali, tusiwe nao hatuwezi kuwazuia wananchi kudai raslimali zao.

Njia pekee ni kutambua hili kama tatizo la kiuongozi na kulishughulikia. Na kwa kweli muundo wa sera ya majimbo (in herent) unatambua suala la wananchi kumiliki ama kunufaika na rasilimali kama nilivyodokeza katika makala yangu iliyopita.

Sasa nirudi kwenye mfano wa Afrika Kusini. Nchi hii imepitia mchakato wa kuwashirikisha wananchi katika kuunda katiba yao tofauti na katiba ya Tanzania hivyo uamuzi wa majimbo ni wa wananchi. Nao ndio waliamua kuwa na majimbo tisa badala ya manne. Na ni kwa kuangalia sababu za ukubwa wa kimaeneo, rasilimali, historia, mamlaka n.k. Na hili si suala geni, Canada kwa mfano ilibuni mfumo wake wa majimbo mwaka 1867 (kwa sababu za umoja zaidi), lakini majimbo ya Canada yamekuwa yakibadilika, ama kuongezeka au wajibu wake kubadilika kutokana na mageuzi ya kijamii, ukubwa, dhima ya serikali, na maamuzi ya kimahakama.

Hii inathibitisha kwamba majimbo ya kiutendaji (functional federalism) sio ndoto. Ni kitu kinawezekana kwa lengo la kukidhi matakwa fulani (the FOR WHAT). Matakwa ambayo kwa mimi nimeyaainisha kwenye misingi tisa niliyotoa katika makala yangu iliyopita.

Chama ambacho kilikuwa kinapambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini ni African National Congress (ANC). Kwa hiyo kama nia ya kuunda majimbo ingekuwa ni kupambana na ubaguzi wa rangi, ANC ingekuwa ya kwanza kutaka mfumo wa MAJIMBO/UFIDERALI. Lakini ANC ilikuwa inapinga majimbo (kama walivyo rafiki zao CCM wa Tanzania). Na walikuwa wanasema wanataka Mamlaka ya Serikali Kuu (unitary government) ili serikali kuu ya chama tawala ANC iweze kutoa huduma kwa wananchi kila mahali mathalani hospitali, shule na kuondoa tofauti za kiuchumi (hii ni hoja ambayo kwa kutamkwa ni tamu!).

Na ANC (kama ambavyo CCM inafanya sasa) ilikuwa ikisambaza propaganda kwamba neno FEDERALISM (MAJIMBO) ni la kibaguzi na la kimbari na kwamba linafanana na HOMELANDS, neno ililokuwa linayagawa maeneo kwa mujibu wa ubaguzi wa rangi (Ndio maana haishangazi kwamba kwenye katiba ya Afrika Kusnini hakuna neno FEDERALISM ingawa nchi imeundwa, inatambua na kufuata mfumo wa UFIDERALI).

Lakini nakubaliana na uchambuzi kwamba katika yale majimbo manne ya asili yapo ambayo yalikuwa yakitaka kujitenga mathalani KwaZULU Natal. Lakini mwisho wa siku wananchi waliupenda zaidi mfumo wa ufiderali.

Mwalimu [Nyerere] alitaka Serikali ya Mamlaka (unitary government) - hoja zake zilikuwa hizo hizo za serikali kuu kupeleka huduma kila mahali. Ametimiza wajibu wake katika wakati wake. Kuna mahali amefanikiwa, kuna mahali ameshindwa. Sasa, zimepita nyakati za dola kuhodhi uchumi (state centralized economy).

Sasa ni wakati wa watu (namaanisha wazawa na si wageni) kumiliki uchumi (people centred economy). Na huu ndio msingi wa falsafa ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati. Na hili nimelichambua katika misingi ya ufiderali ambao CHADEMA inapendekeza Tanzania tuufute [tuufuate?] Ndio maana naendelea kusisitiza kuwa pamoja na kuwa kipaumbele ni UONGOZI kuna uhusiano mkubwa baina ya MFUMO/MUUNDO WA UONGOZI na UONGZI wenyewe.

Na hili ndilo nashauri serikali inayoongozwa na CCM ilizingatie. Kama haitalizingatia basi wananchi wanapaswa kujulishwa mapema kwamba wakichagua CHADEMA wanachagua falsafa ya NGUVU YA UMMA kutumika katika utawala na UFIDERALI kuwa muundo - labda kama wananchi (ambao sio wote wanaunga mkono sera CHADEMA) au bunge (ambalo halitakuwa la CHADEMA peke yake) - WAKATAE wakati wa mjadala wa KATIBA MPYA! Wakati huo tutaamua kama tufuate Ufiderali uliogawanika (divided federalism) kama ilivyo Canada ama tufuate Ufiderali uliounganika (integrated federalism) kama ilivyo Ujerumai.

Naamini maoni yangu haya yataibua mjadala zaidi tuendelee kujadili, wananchi wengi zaidi wafahamu ukweli ili tukubaliane ama tukubaliane kutokukubaliana.

Taarifa zinazohusiana na hii:

Sunday, September 12, 2010

Jagwa Music waendeleza rirandi nchini Denmark

Jagwa Music ni kikundi ambacho kinapiga muziki wa Mchiriku, au Mnanda, kama vijana wengi wanavyopenda kuuita. Wasanii hawa sasa hivi wako katika ziara ya maonyesho mawili nchini Denmark.

Jana usiku walianza makamuzi ya kasi kubwa. Leo hii, kuanzia saa mbili usiku watakuwa katika mji wa Roskilde kwa ajli ya makamuzi mengine.

Ziara hii, itayakayohitimishwa tarehe 13 Septemba, ni kwa ajli ya kujitangaza kwa ajili ya maandalizi ya ziara nyingine ndefu hapo mapema mwaka 2011.


Waratibu wa safari hii ni kampuni ya Jahazi Music, na kwa maandalizi yote nchini Tanzania wanashirikiana na kampuni ya Maisha Music.


Mwenyeji wa ziara hii nchini Denmark ni kampuni ya GlobalCPH. Kikundi hiki kinamilikiwa na George Sultani Jolijo, na kusimamiwa na kampuni ya Maisha Music Tanzania Limited.

Saturday, September 11, 2010

John Mnyika wa CHADEMA anajibu hoja dhidi ya sera ya majimbo (sehemu ya kwanza)

Katika taarifa iliyopita, Amani Millanga, akiandika kuhusu uchaguzi mkuu 2010, alitoa hoja dhidi ya sera ya majimbo. Ingawa hakutaja chama moja kwa moja, nilihisi anazungumzia sera ya majimbo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Niliwaomba CHADEMA wajibu hoja.



Kama nilivyoahidi, naleta hapa sehemu ya kwanza ya makala mbili za Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alizowahi kuandika juu ya sera hiyo.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------

John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA
Sera ya Majimbo ni siri ya maisha bora kwa kila Mtanzania

na

John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje

Hivi karibuni pameanza tena mjadala kuhusu 'majimbo' na masuala kadhaa yameibuliwa.


Huu ni wakati muafaka nami nichangie hoja kadhaa katika mjadala huu muhimu.


Nikumbushe tu kwamba mjadala huu ulishika kasi sana wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 kwa vijembe vya majukwaani.


Hoja kuu ya kufahamu ni kwamba chimbuko la sera ya majimbo nchini ni falsafa ya CHADEMA ya nguvu ya umma.


Kwani umma ndio unapaswa kuwa na mamlaka lakini pia umma ndio unapaswa kunufaika na rasilimali za nchi.


Niweke pia bayana kwamba katika uchaguzi CHADEMA haikuwa na ajenda ya majimbo kama ajenda inayosimama peke yake. Ilikuwa ni sehemu ya ajenda nyingine.


Tulisema wazi kwamba tatizo la CCM ni kwamba huwa inakuja na ilani ya kuahidi kila kitu na hatimaye kutofanya chochote.


Sisi tulisema pamoja na kuwa na sera nyingi lakini tutakuwa na vipaumbele vitano tu:

Mosi, mfumo mpya wa utawala, pili; elimu, tatu; kilimo, nne; uchumi; na tano afya. Na hata katika vipaumbele hivi bado tulichagua maeneo machache mahususi.


Mathalani katika uchumi tulilenga kodi (kupunguza ukubwa wa kodi na kuhakikisha kuwa kodi zinakusanywa ipasavyo).


Ajira na rasilimali hususan madini katika mfumo wa utawala.

Hapa tulikuwa na masuala matatu, kwanza, uongozi mpya kwa maana ya wananchi kuwaondoa viongozi walioko madarakani kwa maana wameshiriki ufisadi wa nyuma, hivyo hawawezi kufanya mabadiliko yoyote ya maana.


Pili; kusafisha mfumo wa utawala kwa maana ya kupambana na rushwa na ufisadi, na tatu, kutengeneza muundo mpya wa utawala ikiwamo kuanzisha muundo wa majimbo.


Lakini kwa kuwa suala la majimbo lilipata ladha zaidi na mashambulizi mengi; sera, ajenda, maana ya mfumo mpya wa utawala ikafunikwa kabisa.


Sina nia ya kujadili makala ya leo kwa nini hali hii ilijitokeza.


Kwa kuwa wengi wamezoea kutumia jina "sera ya majimbo' nami katika mjadala huu nitatumia jina hili ili twende pamoja.


Suala la sera ya majimbo ni suala la kikatiba. Chama chochote cha siasa kinauza kwa wananchi matakwa yake kama kikipewa ridhaa na wananchi.


Matakwa hayo yanaweza kutokana na misingi ya chama husika ama matakwa ya wananchi ama matakwa ya viongozi wa chama husika.


Lakini baada ya uchaguzi zipo sera ambazo utekelezaji wake lazima urudi tena kwa wananchi kupata ridhaa ya pamoja, mathalani CCM wamejikuta suala la mahakama ya kadhi linapaswa kurudi kwa wananchi, ingawa liko katika ilani ya chama chao.


Lakini mambo mengi ya chama hutekelezwa kwa kwenda kwa wawakilishi wa wananchi yaani Bunge.


Kadhalika, suala la kuundwa kwa majimbo ni suala la mabadiliko ya katiba hivyo kwa vyovyote vile CHADEMA ingepaswa kurudi kwa wananchi.


Hata ndani ya chama kwenyewe, misingi na sera ilikubaliwa kwa pamoja lakini tafsiri ya kina kila mtu alikuwa anaifanya kwa mujibu wa mahali.


Kwa vyovyote vile, kama tungechukua dola tungepaswa kukubaliana kuhusu masuala kadhaa kwa undani kabisa kabla ya kwenda kwa wananchi kuomba ridhaa.


Je, hii ni ishara ya kutoifanyia kazi sera kwa undani? Hapana. Ni kawaida ya ilani ya uchaguzi. Huwa inatoa ahadi ya ujumla. Mathalani, tutahakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma shule ya msingi - suala la nani atafanya nini kutekeleza ahadi hii linakuwapo kwenye programu ya utekelezaji ambayo inaingia kwa kina kuweka mikakati na shughuli mbalimbali.


Suala la sera ya majimbo siyo geni duniani. Nchi kadhaa za Afrika zinafuata mfumo huu, mathalani Afrika Kusini, Nigeria, Ethiopia na nyinginezo. Ulaya nchi nyingi zinafuata mfumo huu.


Marekani ya Kaskazini, Australia. Kwa kweli dunia kwa ujumla wake inatambua umuhimu wa majimbo.


Wengine wamekuwa na majimbo kutokana na tofauti za kimbari/kinasaba (ethnic federalism), wengine ni sababu tu za kurahisisha utendaji (functional federalism) na wengine ni umbali tu wa jiografia (geographical federalism).


Kwa hiyo, wote wanaochambua majimbo ni vyema wakachambua pia ufiderali unafanyaje kazi katika nchi hizi, faida na hasara zake.


Ukiangalia hata muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni aina ya ufiderali, ingawa ni ufiderali tenge!


Kwa hiyo cha msingi hapa ni kujadili misingi ya Sera ya majimbo ya CHADEMA na kuangalia vipi ni sehemu ya falsafa ya nguvu ya umma na kwa vipi inaendana na misingi ya CHADEMA, kwa vipi inaweza kusaidia utekelezaji wa sera za CHADEMA na kwa ujumla ni namna gani ni silaha ya nyongeza katika kukabiliana na ujinga, umaskini na maradhi na hatimaye kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.


Kwa mtazamo wangu, hii ni misingi ya "Sera ya majimbo".


Msingi wa kwanza ni kujenga uwezo wa kisiasa, uongozi na uwajibikaji. Sera ya majimbo inaelekeza taifa kuwa na viongozi wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika ngazi mbalimbali.


Hii ina maanisha kwamba kwa muktadha wa sera ya majimbo, ofisi na vyeo vya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, katibu tarafa vitafutwa.


Uzoefu unaonyesha kwamba wamekuwa wakiongeza mzigo wa gharama kutokana na mwingiliano kati yao na wakurugenzi, mathalani wa halmashauri ambao ni wataalamu wanaofanya kazi chini ya viongozi wa kuchaguliwa.


Uzoefu unaonyesha kwamba kwa kuwa mikono ya mhimili wa serikali ngazi ya chini viongozi hawa wamekuwa sababu ya serikali kuu kuingilia serikali zingine na kimaamuzi na kimwelekeo.


Matokeo yake ni kuwa nchi nzima inaendeshwa na Ikulu Dar es Salaam hata katika mambo ya kawaida kabisa.


Urasimu huu umekuwa kikwazo kwa maendeleo. Nguvu ambayo viongozi hawa wamepewa toka wakati wa muundo wa kikiloni wa kutawala kwa kutumia mawakala umewafanya wawe miungu watu na wanyanyasaji.


Kwa kifupi ni watu wasiohitajika. Kwa upande mwingine, sera ya majimbo inataka mameya wachaguliwe na wananchi moja kwa moja badala ya mabaraza ya madiwani ili kuongeza uawajibikaji.


Kwa kifupi, msingi huu wa sera unachochea hamasa ya uongozi na kuweka viongozi wenye kuwajibika kwa watu. Hii ndiyo falsafa ya nguvu ya umma katika vitendo.


Msingi wa pili ni kushusha na kugawanya madaraka (Devolving and separation of powers). Kwamba uzoefu unaonyesha kuwa majimbo yanapopewa madaraka nayo yanatoa madaraka kwa ngazi za chini yake mpaka chini kabisa.


Serikali kuu inapohodhi mamlaka kadhalika ngazi za chini zinahodhi mamlaka ya ngazi za chini.


Hoja itatolewa kwamba je, kwa nini njia isingekuwa serikali huru za mitaa? Hiyo ni njia moja lakini mamlaka (mandate) ya serikali ya mtaa huwa katika maeneo machache, tena ya utekelezaji zaidi tofauti na mfumo wa majimbo.


Mfumo wa majimbo unahusisha masuala gani ambayo majimbo yanaweza kuyashughulikia moja kwa moja kama ambavyo masuala yanavyogawanywa kwa misingi ya muungano na yasiyo ya muungano.[?]


Lengo ni kufanya serikali ya fideresheni ishughulike na mambo machache na kila eneo lisimamie mambo yake kwa mujibu wa mazingira ya eneo husika. Hiyo ndiyo nguvu ya umma!


Msingi wa tatu ni kupanua umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania na kuvunja dhana ya ukabila.


Mfumo wa sasa wa kugawa wilaya pamoja na sababu zingine zinazotolewa na serikali umekuwa ukilalamikiwa kuwa umejikita katika kugawa wilaya kwa mujibu wa makabila - mfano Rombo ya Warombo, Ukerewe ya Wakerewe - mifano ni mingi kweli kweli.


Sera ya majimbo imelenga kuvunja mshikamano wa kiwilaya na badala yake kutengeneza fungamano la kimajimbo - mathalani Jimbo la Kaskazini linajumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga - hili ni jimbo la Wamasai, Wairaq, Wabarabaig, Wachaga, Wapare, Wabondei n.k.


Jimbo la Ziwa, ni mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza n.k., hii ina maanisha Wasukuma, Wahaya, Wakurya, n.k.


Lengo ni kutengeneza kizio (unit) kipya cha utambulisho chini ya taifa (Tanzania), yaani wakazi wa jimbo fulani kufanya watu wajinasibishe kabisa na majimbo yao.


Hii ni kwa sababu majimbo yanakuwa na upekee wake ambao mtu anapenda 'kujinasibisha' nao.


Mathalani jimbo moja linaweza kuwa na sheria za ajira zenye kuvutia zaidi, n.k. Hii ndiyo nguvu ya umma!


Msingi wa nne ni kuweka utamaduni wa ushindani na upekee ndani ya nchi. Kama ambavyo nchi zinavyoshindana ndivyo ambavyo majimbo yenye taratibu tofauti za kibisahara, ajira, uwekezaji, makazi na kadhalika yatakavyoshindana.


Serikali ya majimbo inatoa mwanya wa majimbo kujiamulia mwelekeo wake katika masuala fulani fulani.


Mathalani jimbo moja linaweza kupiga marufuku uvutaji sigara; majimbo mengine yanaweza kuiga ama yanaweza kutofuata.


Hata katika michezo na kadhalika, ushindani utaongezeka maradufu. Kila jimbo litataka kujinufaisha na mafanikio fulani fulani.


Dhana ya ushindani na upekee imeshindikana katika mazingira ya sasa ambapo kila halmashauri inaongozwa na maelekezo ya Dar es Salaam na inajivunia mafanikio ya nchi kwa ujumla wake.


Hata binadamu, ukipewa uhuru wa kujiamulia una uwezo wa kufanya vitu vya pekee zaidi kuliko ukiwa sehemu ya mfumo mpana.


Hii ni saikolojia ya maendeneleo. Hii ndiyo falsafa ya nguvu ya umma!


Msingi wa sita ni kupanua vyanzo vya mapato. Pia majimbo yanapopaswa kujitegemea kwa aina fulani, moja kwa moja yanapaswa kuanza kutaufta njia za kujitegemea.


Hii itasaidia vyanzo vya mapato kupatikana. Hii ni kutokana na kanuni ya mwitu (The law of the jungle).


Sasa hivi kila mahali wanaitazama Dar es Salaam ikusanye pesa nchi nzima na kutoka kwa wahisani na kila eneo lina achama mdomo kwa ajili ya kupokea.


Wapinzani wa hoja hii wanatoa hoja kwamba lipo jimbo ambalo halina rasilimali na wanatolea mfano wa jimbo la kusini.


Hawa ni watu ambao pengine hawajui kwamba Tanzania ina rasilimali kila mahali. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mikoa ya kusini haina maendeleo.


Ukweli ni kwamba tafiti zinaonyesha kuwa mikoa ya kusini ina rasilimali na mali asili nyingi sana, tatizo kubwa ni miundo mbinu.


Jimbo la Pwani ya Kusini kwa mfano lina mikoa ya Lindi, Mtwara na wilaya a Kisarawe na Kibiti.


Jimbo hili lina rasilimali kama madini, bandari, uvuvi, nishati ya gesi, kilimo cha korosho, mikoko pamoja na utalii. CHADEMA ina kila sababu ya kuwaeleza wananchi umuhimu wa majimbo kwani kila jimbo lina rasilimali za kutosha, ila kwa kuwa serikali ya CCM imekuwa ikiwahadaa wananchi na kuwafanya wabweteke kisaikolojia ili wasijeletee maendeleo, imekuwa ikipinga vikali serikali ya majimbo.


Hata kama kungekuwa hakuna maliasili: ukweli unabaki kwamba zipo nchi duniani ambazo hazina maliasili lakini zimeneemeka kutokana na kutoa huduma tu!


Lakini kwa upande mwingine kama sehemu ya sera ya majimbo, lipo pato ambalo litakusanywa serikali kuu na kusaidia katika maeneo ambayo yana upungufu.


Msingi wa saba ni wananchi kunufaika kutokana na matunda ya rasilimali za eneo lao.


Mfumo wa sasa ambapo rasilimali zote zinamilikiwa na "Dar es Salaam" kwa maana ya serikali kuu, unafanya wananchi wasinufaike na rasilimali za maeneo yao kikamilifu.


Mathalani kodi za madini, mbuga za wanyama n.k., sehemu kubwa inakuja serikali kuu ama kugawanywa katika mfumo ambao haunufaishi maeneo husika ama kutumika katika matumizi ya anasa ya serikali kuu.


Mathalani, pamoja na kuchimba madini yenye thamani, Geita ni moja ya wilaya maskini kabisa. Wanaofaidi madini ya Geita wako Dar es Salaam.


Serikali ya majimbo itakuwa na sehemu ya mamlaka ya ugawanyaji wa mapato yanayotoka katika eneo husika.


Pamoja na kukusanya mapato ya pamoja ya serikali kuu. Hii ndiyo nguvu ya umma.


Msingi wa nane ni kupunguza ukubwa wa gharama za uendeshaji wa serikali. Serikali ya majimbo haiongezi ngazi yoyote ya utendaji kwa kuwa inavunja ngazi za mkoa (ambayo ni mikoa mingi zaidi - takriban 26) na kutengeneza ngazi ya jimbo (majimbo ni machache, manne mpaka manane, kutegemea na makubaliano ya kikatiba).


Wakati huo huo ukubwa wa serikali kuu utapunguzwa kwa kuwa wizara zitabaki chache za mambo ya federesheni mathalani ulinzi, mambo ya nje, fedha.


Wizara nyingine zote zinakuwa katika ngazi ya majimbo husika kwa mujibu wa utaratibu wa majimbo husika.


Kutokana na ukaribu wa utoaji huduma na utendaji, mwishowe gharama za utendaji zitakuwa ndogo kuliko Dar es Salaam inavyoendesha nchi nzima katika kila jambo.


Mathalani utaoaji wa pasi za kusafiria (passport), vibali vya elimu na mambo mengine mengi.


Serikali ya majimbo itahakikisha mfumo wa utendaji unakuwa mdogo kwa kujenga mifumo iliyokaribu zaidi. Hii ndio nguvu ya umma!


Msingi wa tisa ni muundo mpya unaosaidia utekelezaji wa majukumu. Hapa ni mjadala wa kipi kinaanza - muundo ama majukumu (structure or function).


Sera ya majimbo inachukua mtazamo wa kwamba yote yanakwenda pamoja. Wachambuzi wengi wamekuwa wakitoa hoja kwamba matatizo ya msingi ya mwananchi ni hali mbaya ya maisha, kipato duni, uchumi mbovu, elimu duni n.k. Na wanachotaka wananchi ni suluhisho la haya matatizo ya msingi si 'porojo' za sera ya majimbo.


Lakini ukweli ni kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kimatokeo baina ya masuala haya (direct and causality relationship).


Kwa mfano, asili ya wananchi wa Geita kuwa na uchumi mbovu ni sera mbovu ya madini iliyopitishwa Dar es Salaam lakini pia mfumo mbovu wa mgawanyo wa mapato unaosimamiwa kutoka Dar es Salaam na kwa halalishwa na sheria na mikataba mibovu.


Pengine wananchi wa Geita na jimbo lao wanajua zaidi nini ambacho wanataka; sehemu ya tiba ni kuwapa sehemu ya mamlaka ya kujiamulia mambo yao. Wajikaange kwa mafuta yao! Tatizo la elimu pengine ni maagizo ya waziri kutoka Dar es Salaam ambaye hajui kabisa kuwa hali ya Mwanza ni tofauti na Mtwara.


Sasa, hata elimu aamue waziri Dar es Salaam? Changamoto ya nchi yetu ni wananchi kukosa motisha (motivation) na hisia za umiliki (sense of ownership).


Ujinga, umaskini na maradhi ni matokeo tu, chanzo ni uongozi. Kuweka uongozi bora ni suala moja. Kushughulikia mfumo na muundo wa uongozi/utawala ni sehemu ya suluhisho.


Upo wasiwasi wa kufanya hivi kwamba kuna kutengeneza matabaka. Hata sasa matabaka katika nchi yetu yapo, tena mabaya zaidi.


Maana haya ni ya mtu na mtu.Afadhali utofauti wa kisera kati ya jimbo na jimbo kuliko mtu na jirani yako.


Kuna hofu kwamba yapo majimbo yatakayojitenga. Katika muundo wa Tanzania ya jimbo lenye makabila mbalimbali haliwezi kujitenga, ilhali jeshi, mambo ya nje na masuala kadhaa nyeti yako kwenye kapu moja.


Huku ni kuhofia kivuli. Huku ni kuyaficha majimbo ambayo ni siri ya maisha bora kwa kila Mtanzania.


Ndiyo maana nasisitiza, tunapaswa kukubali mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Hakuna kulala, mpaka kieleweke.

Sunday, September 5, 2010

Amani Millanga atoa maoni yake kuhusu uchaguzi

Sera za Serikali za Majimbo ni Hatari kwa Utaifa Wetu
Na Amani Millanga
-------------------------------------------------------------------------
Amani Millanga ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine ambaye yuko masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Leicester, nchini Uingereza, akisomea shahada ya uzamivu katika mawasiliano ya umma. Tasnifu ya shahada yake ni  Broadcasting for Sustainable People Centred Development in Tanzania: A Case Study of TBC as a Tool for Eradicating Extreme Poverty. Tafsiri isiyo rasmi ya tasnifu ni: Upashaji Habari kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya watu nchini Tanzania: Uchunguzi Kifani wa TBC kama chombo cha Kufuta Umaskini Uliyokithiri.

Nimetuma ombi kwa CHADEMA wajibu hoja za Amani Millanga na mara nitakapopata majibu hayo, nitayaweka hapa. 

--------------------------------------------------------------------------------------------
Amani Millanga, kushoto, akiongea na David Saragana, Afisa Kilimo wa Kijiji cha Butiama kama sehemu ya utafiti anaofanya kwa ajili ya masomo yake ya uzamili.

Hatuzihitaji na Hatuziamini
Tukielekea katika uchaguzi mkuu tutayasikia mengi na ahadi lukuki kutoka kwa wagombea wa urais, ubunge na udiwani kwamba wakichaguliwa Tanzania itajaa neema na kila mmoja wetu atayaona mabadiliko makubwa yakienda sambamba na ukuwaji wa uchumi. 


Wagombea wanawajengea watu matumaini na hamu ya kuiona Tanzania hiyo ya ahadi. Pasina shaka ahadi wanazozitoa wagombea zinatokana na sera za vyama vyao.

Sera ndizo dira na mwelekeo mgombea na chama chake katika kuijenga Tanzania yetu. Hivyo basi sera za kiutawala za chama chochote kinachotuomba ridhaa ya kutuongoza ni lazima ziwe zinalenga kujenga nchi na taifa lenye umoja, udugu, amani na mshikamano.

Ndugu zangu, vipo vyama vinawania kuliongoza taifa letu vyenye sera za kimajimbo. Chama chenye sera kama zino hatukihitaji na wala hatukiamini kukipa dhamana ya kutuongoza kwani kitatupeleka pabaya hata kama zake sera nyingine ni nzuri kiasi gani.

Siku zote ustawi wa taifa na watu wake huanzia kwenye umoja na amani katika taifa husika. Matokeo ya sera za serikali za majimbo ni kuondoa umoja, udugu na hatimaye utaifa mambo ambayo ni muhimu katika kuijenga na kuilinda amani ya nchi, uchumi na ustawi wa watu wake.

Ukaburu
Ukiongelea serikali za majimbo katika Tanzania bila shaka unaongelea umkoa na ukabila. Mambo haya mawili hayasigani na ni hatari kwa umoja wetu, amani yetu, udugu wetu na utaifa wetu kama watanzania. Sera hizi za majimbo ni sera za kupandikiza mbegu chafu ya ukabila itakayoigawa Tanzania. Baadhi yetu
wanaweza kuwa wanazishabikia lakini ukweli unabaki pale pale kuwa zitatumaliza.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alituusia kuwa tuwaogope kama ukoma wale wenye sera za ukabila, umkoa, udini au rangi za ngozi za watu kwani ni wabaguzi na hawana tofauti na makaburu. Bila shaka sera za serikali za majimbo ni za kibaguzi na hazitufai katika nchi yetu.

Tanzania Jimbo Letu
Wapo wanaosema mbona Nigeria au Marekani hata India kuna serikali za majimbo, kwa nini isiwe hapa kwetu Tanzania? Tena watakupa mifano ya mafanikio ya serikali za majimbo katika nchi hizo. Lakini wanasahau kwamba Tanzania kama taifa na nchi inayo historia yake ambayo imejengeka katika misingi imara ya kujiona kuwa sisi sote ni watanzania na kabila letu wote ni watanzania na jimbo letu ni Tanzania.

Utamaduni wetu wa kuulizana kabila au mkoa atokao mtu ni kutaka ujue kama ni mtani wako na mtaniane na si vinginevyo. Lakini tukileta serikali za majimbo tutaanza kuulizana tunatoka mikoa gani ili tubaguane na tuwapendelee wale tunaotoka nao mkoa mmoja na kabila moja. Haya yapo India, Nigeria na hata Marekani. Serikali za majimbo kimsingi zitawaongezea wananchi mzigo wa gharama za kuiendesha serikali kuu na serikali za majimbo zenye mabunge na msululu wa viongozi. Nigeria ni mfano hai.

Tanzania Kuparaganyika
Kwa kuwa sisi ni taifa changa, sera hizi za kimajimbo zitaturudisha kule tulikotoka kabla ya uhuru – Nchi bila Utaifa. Na bila shaka huo ndio mwanzo wa Tanzania kumegeuka na kupasuka vipande vipande. Hakika huo ndio mwanzo wa watu wa jimbo fulani kujiona wao ni bora kuwazidi watu wa jimbo jirani. Huo ndio mwanzo wa jimbo fulani kutangaza kwamba raslimali zote zilizoko kwenye jimbo hilo ni zake na wala zisitumike kwa manufaa ya majimbo mengine. Huo ndio mwanzo wa kusikia siku moja Kagera inatangaza kujitenga na kuwa nchi. Hapo Tanzania kama nchi na taifa haitakuwepo tena. Kama Mwalimu Nyerere angekuwa na fikra hizi za
kimajimbo basi Rukwa, Kigoma, Dodoma au Singida kusingekuwa na kitu au maendeleo yeyote.

Hitimisho
Ndugu zangu, tukielekea kwenye masanduku ya kupigia kura tukumbuke kuwa sera ya serikali za majimbo ni kitanzi cha kuunyonga utaifa wetu, umoja wetu na amani yetu. Tuzikatae sera hizi kwa kuwanyima kura zetu. Kinga ni bora kuliko tiba.

Friday, September 3, 2010

Wageni toka JKT wamtembelea Mama Maria Nyerere

Leo asubuhi, wageni wanne toka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walimtembelea Mama Maria Nyerere kijijini Butiama.
Kutoka kushoto: Col. S.M. Msindo, mwenyeji wao na Mkuu wa Kambi ya JKT Rwamkoma, Lt.Col. Mlawa, Maj. M.M. Kipakulo, Maj. M.P. Kivuyo, na WO2 Daria Malombe.
Lt.Col. Mlawa, Mkuu wa Kambi ya JKT Rwamkoma akiwapa wageni maelezo nje ya kaburi la Mwalimu Julius K. Nyerere, Mwitongo, Butiama.
Baada ya kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere, wageni walitembelea Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere na kabla ya kuondoka walionana na Mama Maria Nyerere, mjane wa Mwalimu Nyerere.

Wageni pamoja na mwenyeji wao wakiwa pamoja na Mama Maria Nyerere, wa pili kutoka kushoto.



Wageni hao toka Dar es Salaam walikuwa kwenye ziara ya kikazi.