Niko njiani kuelekea Moshi kwa ajili ya maandalizi ya kupanda Mlima Kilimanjaro chini ya The Mwalimu Nyerere/Mt. Kilimanjaro Charity Climb.
Nilikusudia kusafiri moja kwa moja hadi Moshi kupitia njia ya Serengeti lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa. Hivi sasa niko Mwanza na natarajia kufika Moshi kesho kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kutokana na maandalizi hafifu ya uchangishaji wa pesa za hisani ambao nafanya kila mwaka ninapokwea Mlima Kilimanjaro, yawezekana kuwa azma ya kuchangisha pesa za hisani haitafana sana mwaka huu. Katika siku chache zijazo na kabla ya kuanza msafara nitafanya uamuzi iwapo itawezekana kufanikisha kuchangisha pesa za hisani au iwapo nitalazimika kuahirisha uchangishaji huu mpaka msafara ujao wa kukwea Mlima Kilimanaro.
Suala lingine katika msafara wa mwaka huu ni kuwa muongozaji mashuhuri wa filamu toka nchini Marekani, Jim Becket, anakusudia kupiga picha za filamu wakati wa msafara huu. Jaffar Amin naye anatarajia kuungana nami katika msafara huu kutokana na makubaliano yetu wakati wa msafara wa mwaka jana kuwa tutaendeleza jitihada za kuchangisha pesa za hisani.
Kwa kuwa Jaffar atakuwa nasi, Jim anakusudia kujumuisha ndani ya filamu yake historia ya mahusiano kati ya Tanzania na Uganda na jinsi gani haya mahusiano yamebadilika, akijikita juu ya malengo ambayo mimi na Jaffar tunayo katika masuala ya hisani.
Mwanadada Andrea Wobmann ambaye amewahi kufanya kazi ya kujitolea jijini Mwanza naye pia anajiunga nasi kuukwea Mlima Kilimanjaro
No comments:
Post a Comment